BAADA YA JARIBU ZITO.

 

Peter na Jemimah Mabula



Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe ndugu yangu.


Karibu tujifunze Neno la MUNGU.


Wakati mwingine anayejaribiwa sana huinuliwa sana.


Lakini pia kabla sijaendelea ngoja nikuambie jambo hili muhimu kwamba sio kila jaribu unalopitia limeletwa na MUNGU, kuna majaribu unapitia kwa sababu huombi, kuna majaribu ya shetani ili usiende mbinguni na kuna majaribu yanayotokana na hila za wanadamu wanaokuonea wivu.


Majaribu mengine yote isipokuwa jaribu la MUNGU, hayo Pambana kimaombi na yatafutika.



Mimi leo nazungumzia jaribu la MUNGU kama kipimo kwako.


Wakati mwingine anayejaribiwa jaribu zito akivuka hapo huvuka na ushindi mkubwa mpya,neema kubwa mpya na imani kubwa.


Mkumbuke Ibrahimu aliyeingia kwenye jaribu gumu kuliko jaribu lako wewe, Ibrahimu alikuwa mzee na mke wake alikuwa kikongwe aliyezaa mtoto kwa Neema ya MUNGU lakini wakati wa furaha yao jaribu likaja kwamba Ibrahimu amtoe Isaka sadaka mbele za MUNGU.



Mwanzo 22:1-2 " Ikawa baada ya mambo hayo MUNGU alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia."



Hili lilikuwa ni jaribu gumu sana na zito sana, Ibrahimu hakujua kama alikuwa anajaribiwa, yeye alidhani anapoteza kitu chake cha thamani alichokitafuta kwa miaka mingi sana bila kukipata,kakipata uzeeni sana.


Lakini licha ya kitu hicho kuwa cha thamani sana lakini kwa sababu ni MUNGU amesema basi Ibrahimu alitii ila hakujua kama ni jaribu.



Mwanzo 22:11-12 " Ndipo malaika wa BWANA akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa.  Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha MUNGU, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee."



Hili lilikuwa ni jaribu gumu sana lakini baada ya jaribu Ibrahimu akawa sio yule Ibrahimu wa kwanza.



Mwanzo 22:15-18 " Malaika wa BWANA akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu."



Majaribu kama ya Ibrahimu yapo sana hata leo.


Unaweza kutunza pesa yako muda mrefu ili ujenge nyumba lakini wakati umekamilisha malengo baada ya pesa kutimia MUNGU anakuambia mjengee nyumba yake yaani jenga Kanisa, wakati huo unaweza kuchanganyikiwa, hutajua kama ni jaribu, utaona unaonewa, utajiuliza "kwanini MUNGU hujawafuata wale matajiri wenye nyumba nyingi  na pesa"


Huwezi kujua kwanini MUNGU amekujaribu wewe na katika wakati huo. Ukitii unaweza kushangaa ndani ya miaka 3 unajenga nyumba 3 kubwa zaidi kwa sababu MUNGU amesema "Kama kukubariki nitakubariki"



■Wakati mwingine MUNGU hukujaribu kule ambako moyo wako uko.



●Kama moyo wako uko kwenye gari yako unaweza kujaribiwa huko huko.


Mtu mmoja aliambiwa amgawie Mtumishi fulani gari lake, hata familia yake hawakumuelewa.



●Kama moyo wako uko kwenye pesa,unaweza kujaribiwa huko.



●Kama moyo wako uko kwa watoto unaweza kujaribiwa huko.



Kumbuka tu kama ni jaribu la MUNGU ukishinda hutabaki kama ulivyokuwa.



Akina Hana walikuwa katika jaribu la uzao kwa muda mrefu, kilichofuata ni kumzaa Mtumishi wa MUNGU aliyebeba taifa zima na akapata na watoto wengine watano zaidi.



Wewe umejaribiwa katika mini?



Yakobo 1:2-4 " Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi.


Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa na neno."



Ndugu ukiwa majaribuni usilalamike bali omba tu.


Ukiwa Katika jaribu usijihesabie haki bali endelea kunyenyekea kwa MUNGU.


MUNGU Baba wa mbinguni akutunze na kukubariki.


By Peter Mabula.


Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.

Comments