MAANA TATU ZA UBATIZO NA MASHARITI MATATU YA UBATIZO WA KIBIBLIA.

 

Na Mwl Peter Mabula

Bwana YESU KRISTO asifiwe.
Karibu tujifunze jambo muhimu yaani UBATIZO.

 Yohana 3:5 '' YESU akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa ROHO, hawezi kuuingia ufalme wa MUNGU. '' 


Jemimah Mabula na Mchungaji John Malambo wakibatiza 


●Neno ''ubatizo'' linatokana na Neno la kigiriki  ''Baptizo'' ambalo katika kiingeleza ni ''Baptism'' Lenye maana ya Zamisha kwenye maji,Osha.

●Kubatizwa sio kuokoka kama watu wengine wanavyodhani bali mtu anaokoka kwanza ndipo anabatizwa.

 Kulingana na Bwana YESU kwenye andiko hapo juu ni lazima sisi tuzaliwe " kwa maji na kwa ROHO" Katika maisha mapya kupitia katika badiliko la mawazo na moyo. 

Kwa kuwa kuingia katika ufalme wa MUNGU kunataka maisha mapya kabisa, si yale maisha ya zamani yaliyotiwa viraka na yenye dhambi na uovu, ndiyo maana maisha haya mapya yanaitwa kuzaliwa upya. 

■Ubatizo wa maji ni ishara ya nje inayoonyesha badiliko  la ndani.

Ubatizo ni muhimu  sana.

Bwana YESU KRISTO hapo juu amejulisha kwamba kuna batizo mbili.

Ubatizo wa maji ambao ndio mimi leo nauzungumzia  pamoja na ubatizo wa ROHO MTAKATIFU ambao ni muhimu sana.

Kama hujazaliwa kwa maji na kwa ROHO MTAKATIFU huwezi kuingia ufalme wa MUNGU.

Maana yake kama roho yako haijazaliwa upya kwa kufinyangwa upya, kutengenezwa upya kuondolewa  kiburi na ushetani ndani yako huwezi kushinda dhambi hata ukawa na Tiketi ya uzima wa milele. 

Hadi moyo wa jiwe uondolewe ndani yako ndipo utaweza kushinda ya dunia, Ezekieli 36:26-27 MUNGU Mwenyezi  anasema   ''  Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.   ''

Kumbe Anayeweza kutufanya upya roho zetu ni MUNGU kupitia ROHO wake tu. 

Na ROHO MTAKATIFU hapatikana nje na KRISTO bali anapatikana ndani ya KRISTO YESU tu.

●Batizo hizi mbili ndizo zinamkamilisha mtu kwamba amezaliwa mara ya pili.

Ulizaliwa mara ya kwanza na wazazi wako na kimwili lakini sasa unaweza kuzaliwa mara ya pili kwa kuzaliwa na MUNGU kiroho kupitia YESU KRISTO. 

1 Yohana 5:1 "Kila mtu aaminiye kwamba YESU ni KRISTO amezaliwa na MUNGU. Na kila mtu ampendaye mwenye kuzaa, ampenda hata yeye aliyezaliwa na yeye."

Na uthibitisho wa kuzaliwa na MUNGU ni pale ambapo ROHO wake MUNGU atakutengeneza upya.

Kama kuna kitu cha muhimu kwa mtu yule ambaye ameshampokea YESU KRISTO basi ni kuenenda kwa ROHO na kuongozwa na ROHO(Wagalatia 5:2-25)

 Maana 3 za ubatizo ni hizi.

  1.   KUBATIZWA NI KUITIMIZA HAKI YOTE YA MUNGU :

Mathayo 3:14-15 '' Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?  YESU akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa NDIVYO ITUPASAVYO KUITIMIZA HAKI YOTE. Basi akamkubali.''

●Inatupasa kuitimiza Haki yote ya MUNGU kupitia ubatizo kama BWANA YESU aliposema hapo juu.

●Ukikataa kubatizwa maana yake unampinga MUNGU.

      2.   KUBATIZWA NI ISHARA YA KUFA NA KUFUFUKA NA YESU KRISTO: 

Wakolosai 2:12 ''  MKAZIKWA PAMOJA NAYE KATIKA UBATIZO; NA KATIKA HUO MKAFUFULIWA PAMOJA NAYE, kwa kuziamini nguvu za MUNGU aliyemfufua katika wafu. ''

●Lazima tuzike matendo yetu mabaya na tufufuke pamoja na KRISTO tukiwa safi, jambo hilo linafanyika tukiwa hapa hapa duniani sio baada ya kufa.

Tukifa tutakufa lakini kwasababu tumekufa na KRISTO tutafufuka naye vile vile.

3.KUBATIZWA NI KUTII USHAURI WA MUNGU: 

Luka 7:29-30  '' Na watu wote na watoza ushuru waliposikia hayo, waliikiri haki ya MUNGU, kwa kuwa wamebatizwa kwa ubatizo wa Yohana. LAKINI, MAFARISAYO NA WANA-SHERIA WALILIPINGA SHAURI LA MUNGU JUU YAO, KWA KUWA HAWAKUBATIZWA NAYE. ''

Mafalisayo walilipinga shauri la MUNGU yaani ubatizo.

●Kumbe kupinga ubatizo au kukataa kubatizwa ni kulikataa shauri la MUNGU.

●Kubatizwa ni kulitii shauri la MUNGU. Ni kuutii ushauri wa MUNGU.

Warumi 6:3-4 '' Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika KRISTO YESU tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama KRISTO alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa BABA, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima. '' 

MASHARITI MATATU YA UBATIZO WA KIBIBLIA.

      1.  Lazima uwe ubatizo wa maji Mengi. 

Yohana 3:23 ''Yohana naye alikuwa akibatiza huko Ainoni, karibu na Salimu, KWA SABABU HUKO KULIKUWA NA MAJI TELE; na watu wakamwendea, wakabatizwa.''

●Huu ndio ubatizo wa kibiblia yaani ubatizo wa maji mengi.

●Ni lazima tuzame mwili mzima ili tukiibuka tuibuke  tukiwa wapya mwili wote. 

Kuna watu wamezamisha macho yao tu ila midomo haijazama ndio maana uongo kwao ni jambo la kawaida, na sema kwa jinsi ya rohoni.

 Kuna watu wamezamisha migongo tu ila sehemu zingine bado ndio maana ni wazinzi kila siku, hao wamebatizwa nusu tu katika roho zao. 

Na ROHO MTAKATIFU habatizi nusu bali wao ndio wameshinda kutimizwa wajibu wao kwa MUNGU.

●Hakuna mtu yeyote kwenye Biblia aliyebatizwa ubatizo wa maji machache ya namna yeyote.

●Wakristo tumeamuriwa na neno la MUNGU kwamba lazima tuwe na ubatizo mmoja ambao ni ubatizo wa Kibiblia, Waefeso 4:5-6 '' BWANA mmoja, imani moja, UBATIZO MMOJA. MUNGU mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote. ''

Lazima uwe ni ubatizo mmoja tu kwa wateule wa MUNGU na ubatizo huo ni ubatizo wa ROHO wa MUNGU ambaye ni mmoja tu na pia ubatizo wa maji ambao hata Bwana YESU KRISTO alibatizwa kwa huo. 

        2.   Anayebatizwa lazima amwamini kwanza YESU KRISTO ya Kuwa ni BWANA na Mwokozi wake na atubu ndipo anabatizwa.

Marko 16:16 '' Aaminiye NA KUBATIZWA ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.''

●Biblia hapa inathibitisha kwamba mtu anamwamini kwanza YESU ndio anabatizwa. hivyo kumbe kuwabatiza watoto wachanga ni matokeo ya kushindwa kuijua na kuielewa Biblia inavyotaka yenyewe.

Watoto wachanga hubarikiwa tu na sio kubatizwa, kama unafanya ishara ya maji na maombi kwa watoto kulingana na ufunuo wako  mwenyewe  hapo unawabariki tu na sio kuwabatiza.

●Yohana hakumbatiza mtu ambaye hajatubu, ndio maana aliwahubiria kwanza wakatubu ndipo akawabatiza.

Hata mitume waliwahubiria kwanza watu, walipotubu waliwabatiza.

 Matendo 2:38 ''Petro akawaambia, TUBUNI MKABATIZWE kila mmoja kwa jina lake YESU KRISTO, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha ROHO MTAKATIFU.'' 

Hata hapo Biblia inathibitisha kwamba mtu anamwamini kwanza YESU na kutubu ndipo anabatizwa. kwa andiko hili mtoto mchanga asiye elewa maana ya wokovu hana sifa za kubatizwa maana mtoto huyo hawezi kutubu na hajui atubu nini.

Ona mfano mwingine huu.

Matendo 8:12 '' Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa MUNGU, na jina lake YESU KRISTO, wakabatizwa, wanaume na wanawake. ''

          3.   Lazima ubatizwe katika jina la MUNGU BABA, MUNGU MWANA na MUNGU ROHO MTAKATIFU.

Mathayo 28:19  '' Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la BABA, na MWANA, na ROHO MTAKATIFU;''.

Hii ina maana kwamba tunapookoka na kubatizwa tunakuwa watoto wa MUNGU (Yohana 1:12-13), tunakuwa tuna YESU KRISTO kama Mwokozi wetu(2 Petro 2:1) na tunakuwa na ushirika na ROHO MTAKATIFU wa MUNGU.

2 Wakorintho 13:14 "Neema ya Bwana YESU KRISTO, na pendo la MUNGU, na ushirika wa ROHO MTAKATIFU ukae nanyi nyote."

Baadhi ya Mambo muhimu mengine yampasayo anayestahili kubatizwa ni haya hapa chini.

Wewe unayetaka kubatizwa au wewe ambaye tayari ulishabatizwa siku nyingi au miaka mingi unatakiwa uwe na sifa zifuatazo ambazo zinamthibitisha mtu kwamba amebatizwa kwa ROHO na kwa maji.

            1.   Unatakiwa uwe mtii na myenyekevu kwa MUNGU: 

Kumb 28:1'' Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, MUNGU wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, MUNGU wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; '"

Kuhusu unyenyekevu Isaya 66:2'' Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema BWANA; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu. ''

           2.  Unatakiwa uwe mtii kwa viongozi wako wa kiroho.

 Warumi 13:1-2 '' Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa MUNGU; na ile iliyopo umeamriwa na MUNGU. Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la MUNGU; nao washindanao watajipatia hukumu. ''

          3.   Unatakiwa ujue kumtafuta MUNGU kwa maombi. 

1 Yohana 3:22 ''Na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake. ''

         4.   Unatakiwa uichukie dhambi:  

Warumi 4:7-8. '' Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao. Heri mtu yule ambaye BWANA hamhesabii dhambi. ''

      5.    Unatakiwa kujajua na kuyazingatia maeneo muhimu ya kibiblia yanayotakiwa kuzingatiwa ya utoaji ambayo ni 

        a. Fungu la kumi(Zaka)
        b. dhabihu.
        c. Sadaka.

Malaki 3:8-9 ''Je! Mwanadamu atamwibia MUNGU? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu. Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. ''

         6. Unayebatizwa lazima awe na imani kwa KRISTO YESU asilimia mia moja(100%)

 Matendo 4:12 ''  Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. ''.

 Waebrania 11:6 '' Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye MUNGU lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao. ''.

         7. Unayebatizwa anatakiwa awe tayari kuisimamia Imani ya KRISTO muda wote.

Yuda 1:3 '' Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu. '', 

1 Kor 16:13 '' Kesheni, simameni imara katika Imani, fanyeni kiume, mkawe hodari. ''

MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.
+255714252292(whatsapp).
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu. Share kama ulivyo bila kubadili chochote.
Ubarikiwe

Comments