MAOMBI YA KUOMBEA MAONO YAKO YA MWAKA HUU.

 

Na  Mtumishi Peter Mabula


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU kisha tuombe Maombi ya ushindi mkuu.

Kuna makundi mawili ya neno “Maono”

✓✓Kundi kwanza la Maono ni mambo ambayo unayoyaona kutoka ulimwengu wa roho kwa kutumia macho yako ya rohoni ukiwa hujasinzia.

Mfano hai ni huu katika andiko hili

Matendo  18:9 "BWANA akamwambia Paulo KWA MAONO usiku, Usiogope, bali nena, wala usinyamaze,"

✓✓Kundi la pili la  Maono  ni mipango yako unayotaka itokee baadaye kwenye maisha yako.


1 Wafalme 5:5 "Nami, tazama, NAKUSUDIA  KUJENGA NYUMBA kwa jina la BWANA, Mungu wangu, kama BWANA alivyomwambia Daudi baba yangu, akisema, Mwana wako, nitakayemweka katika kiti chake cha enzi mahali pako, ndiye atakayeijenga nyumba kwa jina langu."


◼️Mimi leo nazungumzia maono katika kundi la pili ambapo maono hayo ni mipango unayojipangia ili itokee baadae kwenye maisha yako. 

Haya maono ya Kundi la pili yana  maana gani?


1. Maono haya ni uwezo wa kuyaona maisha ya baadae katika wakati uliopo


1. Maono haya ni picha inayomwonesha mtu anavyotakiwa kuwa kwa kiwango chake halisi cha maisha yake kulingana na kusudi la MUNGU au kulingana na mtazamo wake.

3. Maono haya ni picha ya maisha ya baadae ya mtu. 

Mithali 23:7 "Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo. Akuambia, Haya, kula, kunywa; Lakini moyo wake hauwi pamoja nawe."

4. Maono haya ni mpango wa muda mrefu wa maisha ambayo mtu anapanga kuyafikia.

✓✓Je wewe una maono gani?

Kama huna maono ombea jambo hilo kisha panga maono yako. 

Kuna siku Mtume Paulo Maono yake yalikuwa kupita Efeso.
Matendo  20:16 "Kwa sababu Paulo AMEKUSUDIA KUPITA Efeso merikebuni, asije akakawia katika Asia; kwa maana alikuwa na haraka, akitaka kuwahi Yerusalemu siku ya Pentekoste, kama ikiwezekana."

Je Wewe Maono yako ni Nini mwaka huu?

Mimi Peter Mabula kipindi nikiwa mtoto mdogo siku moja nikiwa na watoto wenzangu wengi tunacheza kuna mtu  mmoja ambaye ni mtu mzima alikuja mahali tulipo na kuanza kutuuliza kila mmoja mmoja wetu mambo haya  “Je wewe unataka kuwa nani baadae?” 

Mimi nilijibu kwamba nataka kuwa katika kazi ambayo ninayo sasa, nilitamka kazi hiyo bila uhakika kama nitakuja kuifanya, siwezi jua kama ni maono yangu ambayo MUNGU aliyahifadhi na akayatimiza nikiwa katika umri mkubwa.

Ayubu 22:28 "Nawe utakusudia neno, nalo litathibitika kwako; Na mwanga utaziangazia njia zako."

Baadae nikiwa shule ya sekondari nikajikuta napitia mazingira magumu sana kwa muda fulani nikakosa tumaini nikajikuta nafanya nadhili mbele za MUNGU maana sikudhani kama hayo yatatokea. Nikasema “MUNGU ukinipa mke na watoto, ukanipa kazi na ukanipa nyumba ya kuishi nitakayoijenga mimi mwenyewe,  ukinipa hayo matatu nitakutumikia kama kichaa, yaani watu watanishangaa ninavyokutumikia kwa juhudi kubwa.

Namshukuru MUNGU aliyatimiza hayo kwenye maisha yangu ndiyo maana Biblia inasema utakusudia jambo nalo litathibitika na mwanga utaziangazia njia zako – Ayubu 22:28 

Ndio maana hata natamani kila ninachokifanya katika kazi ya MUNGU nikirekodi, nina audio nyingi sana za maombi na mafundisho hiyo yote ni katika kumtumikia MUNGU katika KRISTO YESU sawasawa na nadhiri niliyoweka.

 Siku moja kuna rafiki yangu aliniambia hivi “Mtumishi Peter Mabula hivi huwa unaandika masomo saa ngapi maana kila siku uko bize na majukumu na tunaona na uko bize na huduma na tunaona lakini kila siku una uwezo wa kupost masomo mawili, je huwa unayaandika saa ngapi hayo masomo? Maana mengine ni marefu yana ufafanuzi mkubwa” 

Baada ya swali hilo rohoni mwangu mimi nilifurahi baada ya rafiki yangu huyo tunayeabudu naye Kanisani kunieleza hivyo, nikakumbuka nilivyosema zamani mbele za MUNGU kwamba “Nitakutumikia MUNGU kama kichaa hadi watu watanishangaa” kwangu mimi rafiki huyo alikuwa anatimiza unabii wa nadhiri yangu kwamba nitamtumikia MUNGU hadi watu wanishangae kwa namna ninayotumika sana.


Je wewe una maono gani?

Je una maono gani juu ya maisha ya baadae?
Je una Maono gani Kwa ajili ya mwaka huu ambao MUNGU amekupa kuishi.

Kama huna maono ndugu yangu nakuomba umwombe MUNGU ili uwe na maono yako binafsi kwa ajili ya maisha yako baadae. 

Wakolosai 3:17 "Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye."

Nini ufanye juu ya maono yako?   

1. Ombea maono yako ili yaendane na kusudi la MUNGU, omba ROHO MTAKATIFU akufundishe namna ya kuwaza maono yanayoendana na kusudi la MUNGU.

 Zaburi 32:8 "Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama."

Ndugu kumbuka wewe unawaza na MUNGU anawaza hivyo panga maono yako katika MUNGU maana anakuwazia mema.
 Ukipanga maono ya dhambi au maono mabaya ni hasara kwako. 


Mhubiri 11:9 "Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote MUNGU atakuleta hukumuni."

2. Ombea maono yako ili yatimie.

 
Wafilipi 4:6-7 " Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na MUNGU. Na amani ya MUNGU, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika KRISTO YESU."

3. Yajue mambo ambayo yanahitajika ili maono  yako yatimie. 

1 Wafalme 8:17-18 " Basi ilikuwa moyoni mwake Daudi, baba yangu, kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli. Lakini BWANA akamwambia Daudi baba yangu, Kwa kuwa ilikuwa moyoni mwako kujenga nyumba kwa jina langu, ulifanya vema kuwaza hivi moyoni mwako."

Maono ya Daudi yalikuwa kujenga nyumba ya kumwabudia MUNGU.
Maono hayo ya Daudi yakaendelezwa na Suleimani.
Sasa wakati Solomon akitaka kukamilisha Maono yake alitakiwa ajue mambo ambayo yanahitajika ili Maono hayo yatimie.

Mambo gani yalihitajika ili Maono ya Solomon yatimie?
Ni miti ya kujengea,mafundi, mawe makubwa ya thamani na mawe yaliyochongwa.

 1 Wafalme 5:6, 17 " Basi uamuru wanikatie mierezi ya Lebanoni; na watumishi wangu watafuatana na watumishi wako; na ujira wa watumishi wako nitakupa kama utakavyosema; kwa kuwa wajua ya kwamba hakuna kwetu mtu ajuaye kukata miti kama Wasidoni ....... Mfalme akaamuru, nao wakaleta mawe makubwa, mawe ya thamani, ili wauweke msingi wa nyumba kwa mawe yaliyochongwa."

Ndugu Hakikisha unajua vinavyohitajika ili Maono yako yatimie.


4. Vunja vikwazo vinavyoweza kufuta maono yako.

 Mithali 29:18 "Pasipo maono, watu huacha kujizuia; Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria."

Maana yake jizuie mahali panapohitaji kujizuia ili Maono yako yatimie.

 Mfano wa watu walikosa Maono wakajikwaa kwenye Dhambi ni Hawa
Isaya 28:7 "Lakini hawa nao wamekosa kwa divai, wamepotea kwa kileo; kuhani na nabii wamekosa kwa kileo, wamemezwa kwa divai, wamepotea kwa kileo; hukosa katika maono, hujikwaa katika hukumu."

Ndugu usikosee katika Maono yako Bali vunja na jitenge mbali na mambo yanayoweza kuharibu Maono yako ili yasitimie.


5. Pambana na nguvu za giza ili wasizuie maono yako kutimia. 

Waefeso 6:12 "Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho."

Unaweza kujifunza kwa mfano huu wa

Kumbukumbu 2:24  "Ondokeni, mshike safari yenu, mvuke bonde la Arnoni; tazama, nimemtia Sihoni Mwamori mfalme wa Heshboni mkononi mwako, na nchi yake; anzeni kuimiliki, mshindane naye katika mapigano."

  Ambapo Biblia inaonyesha Waisrael ingawa walikuwa wamepewa nchi ya Kananni iwe yao lakini MUNGU aliwaambia wapambane na aliyeishikilia Kanani wakati huo, hivyo na wewe pambana na nguvu za giza wanaojaribu kuzuia maono yako.

6. Andika maono yako utatunza na kuwa unakumbuka, hata Musa aliambiwa na MUNGU aandike.
Kutoka 17:14 "BWANA akamwambia Musa, Andika habari hii katika kitabu iwe ukumbusho, kisha ihubiri masikioni mwa Yoshua; ya kuwa nitaufuta ukumbusho wa Amaleki kabisa, usiwe tena chini ya mbingu."

Andika maono yako kwenye Notebook au daftari ili iwe rahisi kusoma na kuombea maono hayo au kuyakumbuka tu ili ubaki ukitarajia kufikia maono yako mazuri.


7. Tolea sadaka maono yako maana sadaka hubeba mahitaji ya mtu mbele za MUNGU. 

Zaburi 20:3-4 " Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako.  Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako yote."

Sadaka zingine hutengeneza agano la Mungu, hivyo maono yako yanaweza kuwa ndani ya agano lako na MUNGU ndio Maana ni vizuri kutolea sadaka Maono yako kama moyoni mwako unasikia msukumo huo.

8. Endelea kujifunza kwa watu wa MUNGU wema waliofanikiwa katika maono kama 
Omba ndugu katika jina la YESU KRISTO Mwokozi na utamuona MUNGU aliyeziumba mbingu na nchi.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO wetu aliye hai.
+255714252292
Ubarikiwe.

Comments