MAOMBI YA TOBA, KUUNGAMA NA KUTUBU.


Na Mtumishi Peter Mabula


Bwana YESU KRISTO  atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU linalotuongoza kuingia katika Maombi.

Kuungama ni nini?

✓✓Kuungama ni kukubali ukweli wa ulichokifanya ambacho hakistahili mbele za MUNGU ili sasa usamehewe.

Ni muhimu Sana katika maombi yako ya toba husisha na Kuungama pia.
Uwe Kama Ezra ambaye katika maombi yake alihusika pia na Kuungama.

Ezra 10:1 "Basi hapo Ezra alipokuwa akiomba na kuungama, akilia, na kujiangusha kifudifudi mbele ya nyumba ya MUNGU, wakamkusanyikia katika Israeli wote kusanyiko kubwa sana la wanaume, na wanawake, na watoto; maana watu hao walikuwa wakilia sana."

 ✓✓Kuungama ni kuisema dhambi  yako kwa kuitaja ili usamehewe dhambi hiyo.

Zaburi 38:18 "Kwa maana nitaungama uovu wangu, Na kusikitika kwa dhambi zangu."

 Kuna faida katika Kuungama  dhambi zako mbele za MUNGU Kisha unazitubia na kuziacha.

Hosea 5:15 "Nitakwenda zangu niparudie mahali pangu, hata watakapoungama makosa yao na kunitafuta uso wangu; katika taabu yao watanitafuta kwa bidii."

Katika maombi yako ya kutubu penda kuanza na Kuungama Kisha mwambie MUNGU akusamehe.
Mbele za MUNGU haitakiwi kuleta ujanja ujanja  maana hakuna tunachomficha MUNGU hata kimoja.
Mfano mtu amefanya dhambi ya uongo au uonevu  lakini katika maombi yake ya kutubu anasema tu " Ninatubu BWANA nisamehe" hasemi anatubu kwa ajili ya nini, analijua kosa lake ila hataki kulitaja kosa hilo mbele za MUNGU akiwaogopa wanadamu.
Ndugu ni vyema sana kukubali makosa yako  Kisha mwambie MUNGU unatubu kwa ajili ya makosa hayo.
Huhitaji kuificha dhambi yako bali iweke wazi mbele za MUNGU Kisha itubie na kuiacha.
Kumbuka huwezi kufanikiwa ukificha dhambi yako.
Mithali 28:13 "Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema."

 Ni heri Kuungama dhambi zako yaani kuzitaja mbele za MUNGU Kisha unazitubia.
Wanaomwamini Bwana YESU KRISTO kama Mwokozi wao huungama makosa yao ya kuyaacha.

Matendo 19:17-18 " Habari hii ikajulikana na Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawaingia wote, na jina la Bwana YESU likatukuzwa. Na wengi wa wale walioamini WAKAJA WAKAUNGAMA, WAKIDHIHIRISHA MATENDO YAO."

Ndugu yangu, ni muhimu Sana katika maombi haya ya toba ukaanza na Kuungama mbele za MUNGU juu ya dhambi zako au makosa yao au maovu yako.

Kumbuka dhambi zinaweza zimkazuia MUNGU kukutendea muujiza unaouhitaji.
Isaya 59:1-2 " Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia."

Hivyo kutubu kwanza  na kuacha dhambi ni muhimu Sana Kama unahitaji MUNGU akutendea muujiza.
Sasa katika Maombi yako ya toba anza na Kuungama mbele za MUNGU.

 ✓✓Ndugu, inawezekana wakati mwingine changamoto uliyonayo inatokana na dhambi, tubu kwanza ndugu.

✓✓Wakati mwingine kutokuisikiliza sauti ya MUNGU ndiko kulikoleta tatizo kwako, tubu kwanza ndugu.

✓✓Wakati mwingine familia yenu iliingizwa katika mikataba ya kishetani na Baba wa familia au Mama wa familia hivyo kupelekea familia yote kumilikiwa na nguvu za giza au kuteswa na nguvu za giza, ndugu ukitaka MUNGU akusaidie tubu kwanza kwa ajili ya chanzo hicho kibaya kilicholeta mateso katika familia yenu.

Yeremia 3:13 "Ungama uovu wako tu; ya kwamba umemwasi BWANA, Mungu wako, na njia zako zimekuwa nyingi kuwaendea wageni chini ya kila mti wenye majani mabichi, wala hamkuitii sauti yangu, asema BWANA."

✓✓Ndugu, Wakati mwingine ni wewe umetenda dhambi ndio maana matatizo yakaanza kukuandama, ungama na kutubu kwanza Kama unahitaji msaada wa MUNGU.

✓✓Wakati mwingine wala hukutenda dhambi ila ni uonevu tu wa shetani, tubu kwa ajili ya chanzo hicho Cha tatizo.

Kuna vyanzo vingi vinavyoweza kumpa mtu  Sababu ya Kuungama na kutubu m mbele za MUNGU.
Muhimu tu baada ya kutubu usikubali kurudia dhambi hiyo iliyopelekea utubu.

 Kutubu ni Nini?

✓✓Kutubu ni kuomba Msamaha kwa MUNGU katika KRISTO YESU.

Matendo  3:19 "Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;"

Hivyo ndugu ungama na kutubia dhambi zote na kuziacha.

Ungama na kutubia makosa yako yote na kiyaacha.

Ungama na kutubia uovu wako wote na uache sasa.

Tubu kwa ajili ya familia, kazi yako,eneo lako n.k kulingana na ufunuo unaopewa moyoni mwako katika maombi ya toba.
Toba ndio mlango wa kukutoa katika tatizo ili sasa mema yaje kwako.
MUNGU akubariki.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO.
+255714252292
Ubarikiwe sana

Comments