MWAMINI MUNGU ILI AKUTOE KATIKA VIFUNGO VYA GIZA.

 

Na Mwl Peter Mabula



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.


Karibuni tujifunze Neno la MUNGU Aliye hai.


Mwamini MUNGU ili akutoe katika vifungo vya kipepo.



Kutoka 6:6-7 " Basi waambie wana wa Israeli, Mimi ni YEHOVA, nami nitawatoa ninyi mtoke chini ya mizigo ya Wamisri, nami nitawaokoa na utumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyoshwa, na kwa hukumu kubwa; nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nitakuwa MUNGU kwenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ni YEHOVA, MUNGU wenu, niwatoaye mtoke chini ya mizigo ya Wamisri."



Ukisoma maandiko hayo unaona mambo 4 ambayo MUNGU anasema atayafanya ili kuhakikisha watu wake wako huru mbali na uonevu.



Mambo hayo aliyoyasema MUNGU ili kuwafanya watu wake wawe huru ni haya.



1. Nitawatoa mtoke chini ya mizigo ya wamisri.



Kutoka 6:6 "Basi waambie wana wa Israeli, Mimi ni YEHOVA, nami NITAWATOA NINYI MTOKE CHINI YA MIZIGO YA WAMISRI, nami nitawaokoa na utumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyoshwa, na kwa hukumu kubwa;"



Inawezekana hata wewe kuna  watenda kazi wa shetani wanakutumikisha na kukuonea.


Inawezekana waganga wa kienyeji wamekufunga kipepo ili usifanikiwe mambo fulani maishani mwako, uko chini ya mizigo yao.


Inawezekana Wachawi wamekutesa Sana, uko chini ya Mizigo yao.


Leo katika jina la YESU KRISTO mwambie MUNGU ambaye anaweza kukutoa katika Mizigo  ya maadui wanaokutumikisha kipepo.



Inawezekana kila mara unaota unanyonyesha Mtoto  na maana mojawapo ya ndoto ya namna hiyo kwamba kuna watu wananufaika kupitia wewe.


Ndoto hiyo ni taarifa ya kiroho kwamba Kuna wanaonufaika kupitia wewe, wanakutumikisha kipepo ili wafaidi wao na wanafaidika Sana kupitia wewe huku wewe huna Mafanikio yeyote.


Leo katika jina la YESU KRISTO omba huku ukimwamini MUNGU hakika utatoka katika utumwa wa wanaokutumikisha kipepo.


Leo omba katika jina la YESU KRISTO na utatoka chini ya Mizigo ya wanaokutumikisha kipepo.



2. Nami nitawaokoa na utumwa wao



Kutoka 6:6 "Basi waambie wana wa Israeli, Mimi ni YEHOVA, nami nitawatoa ninyi mtoke chini ya mizigo ya Wamisri, NAMI NITAWAOKOA NA UTUMWA WAO, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyoshwa, na kwa hukumu kubwa;"



Inawezekana uko katika utumwa wa madhabahu za giza.


Inawezekana uko katika utumwa wa Mawakala mbalimbali wa shetani.


MUNGU anao uwezo wa kukutoa katika utumwa  huo, mwamini tu na omba katika jina la YESU KRISTO utatoka katika utumwa huo.



Wako watu wanateseka Sana lakini ndugu ukimwamini MUNGU katika KRISTO YESU anaweza kukutoa katika utumwa wa kila nguvu za giza.



Wako watu ni watumwa kwa sababu ya magonjwa, pombe na tabia chafu.


Wako watu ni watumwa kwa sababu ya vifungo vya giza.


Wako watu ni watumwa kwa sababu wamenyang'anywa kipepo baraka zao n.k.


Leo katika Maombi yako Mwamini MUNGU na omba akutoe katika utumwa wa Nguvu za giza na Mawakala wa shetani hakika katika jina la YESU KRISTO utatoka katika utumwa huo.




3. Nitawakomboa kwa mkono ulionyooshwa  na kwa hukumu kubwa.




Kutoka 6:6 "Basi waambie wana wa Israeli, Mimi ni YEHOVA, nami nitawatoa ninyi mtoke chini ya mizigo ya Wamisri, nami nitawaokoa na utumwa wao, NAMI NITAWAKOMBOA KWA MKONO ULIONYOOSHWA, NA KWA HUKUMU KUBWA;"



MUNGU kukukomboa kwa hukumu kubwa maana yake atawaadhibu vibaya mawakala wa shetani waliokuwa wanakutesa.


MUNGU alifanya hivyo kwa Farao na jeshi lake ambao walikuwa wanawatesa Waisraeli, hukumu kubwa ya MUNGU ilipita Misri na hukumu kubwa zaidi kwa majeshi ya Misri ilifanyika Bahari ya shamu walipomezwa na Bahari baada ya muujiza wa MUNGU kwa Waisraeli.


MUNGU anaweza kukukomboa kwa mkono ulionyooshwa na ukawa huru kabisa.


MUNGU anaweza kukukomboa kwa hukumu kubwa ya kuaadhibu Nguvu za giza waliokutesa.


Ndugu, mwamini MUNGU tu na mtegemee kwa Maombi katika jina la YESU KRISTO na atakutoa katika mikono ya maadui zako katika ulimwengu wa roho.


Mwamini MUNGU kwa Maombi yako ma atakulipizia kisasi kwa Nguvu za giza waliokutesa.



4. Nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nitakuwa MUNGU wenu.



Kutoka 6:7 "NAMI NITAWATWAENI KUWA WATU WANGU, nitakuwa Mungu kwenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ni YEHOVA, MUNGU wenu


, niwatoaye mtoke chini ya mizigo ya Wamisri."



Unapoamua kumuomba MUNGU ili akutoe katika utumwa wa shetani hakikisha kuanzia saa hiyo wewe pia unaamua kuambatana na MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.


MUNGU akikutoa katika Mizigo ya Nguvu za giza hakika utakuwa huru na salama.



Ndugu, amua Sasa kufanyika mtoto wa MUNGU  kwa kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako.


Ndugu, amua Sasa kwamba MUNGU aliyeumba Mbingu na Dunia awe ndio MUNGU wako.


Ndugu, amua leo kwamba MUNGU wa Israeli awe ndiye MUNGU wako unayemwabudu daima na kumtegemea.


Ndugu, Mpokee YESU KRISTO kama Mwokozi wako maana ni katika KRISTO YESU pekee ndiko MUNGU amejifunua kwa Wanadamu.


Acha dhambi na uovu, fuata Neno la MUNGU la injili na MUNGU atakuwa upande wako Siku zote.



Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri. 


Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.



Bwana YESU Amekaribia Kurudi.


Je, Umejiandaaje?


Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?


Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.


Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.


Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.


Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.


Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.


Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.


+255714252292(Ni namba hii  kupiga,  meseji, whatsapp na chochote).

Comments