SIMAMA UKAUONE WOKOVU WA BWANA MUNGU KWAKO.

 

Bwana YESU atukuzwe Ndugu yangu.

Karibu tujifunze Neno la MUNGU. 

Somo hili ni la muhimu sana wewe kujifunza.


Karibu nikujuze mambo niliyopewa  ili nikujuze wewe mteule wa MUNGU unayemwabudu katika ROHO na kweli.

Na Mwl Peter Mabula


Kutoka 14:14 "BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya."

Msaada wa MUNGU anapokusaidia kwa jina lingine unaitwa wokovu.

Mwanzo 49:18 "Wokovu wako nimeungoja, Ee BWANA."

Kutoka 15:2 "BWANA ni nguvu zangu, na wimbo wangu; Naye amekuwa wokovu wangu. Yeye ni MUNGU wangu, nami nitamsifu; Ni MUNGU wa baba yangu, nami nitamtukuza."


2 Samweli 22:47 "BWANA ndiye aliye hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe MUNGU wa mwamba wa wokovu wangu;"

Maana ya Neno wokovu ni msaada unaotoka mbinguni kwa ajili ya mwanadamu aliye tayari kwa Wokovu huo.


Tunaweza tukasema kama ifuatavyo Maana ya Neno ''Wokovu.''


1. Wokovu ni hali ya kusalimika na adhabu.


2. Wokovu ni nguvu ya MUNGU ya kutuokoa wanadamu.


3. Wokovu ni mpango wa MUNGU wa kumwokoa Mwanadamu kutoka kwenye mabaya na kumweka kwenye mema aliyoaandaa MUNGU.


4. Wokovu ni hali ya kuokoka.


5. Wokovu ni msaada utokao mbinguni kwa MUNGU kuja kwa wanadamu.


6. Wokovu ni ushindi auletao MUNGU kwa watu wake waaminifu.

Biblia inaposema hapo juu kwamba MUNGU atawapigania ninyi maana yake "MUNGU atawaletea msaada au Wokovu."

Leo Simameni mkauone Wokovu wa Bwana YESU KRISTO ambao atawapa baada ya maombi yenu na utakatifu.

●Simama ukauone ushindi wa MUNGU kwako.

Ukimtegemea Bwana YESU kwa maombi hakika utaona ushindi.


●Ukimtegemea Bwana YESU kwa maombi hakika utaona baraka za MUNGU.


Bwana YESU anasema '' Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba(MUNGU) atukuzwe ndani ya Mwana(YESU). Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya. Mkinipenda, mtazishika amri zangu-Yohana 14:13-15''


●Ukimtegemea Bwana YESU kwa maombi hakika utaona uponyaji wake kwako.


Kumtegemea Bwana YESU ni kumtegemea MUNGU muumbaji wako.


●Ukimtegemea Bwana YESU kwa maombi hakika utaona matendo yake makuu maishani mwako.


●Ukimtegemea Bwana YESU kwa maombi hakika utaona muujiza wa Bwana YESU kwako.


■Ni muhimu sana kujua nguvu za unayemtegemea .

Tunaomtegemea YESU KRISTO tunajua hakika uwezo wake kwamba anaweza yote na hakuna anayeweza kushindana naye.


Mathayo 28:18-20 ''YESU akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la BABA, na MWANA, na ROHO MTAKATIFU; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari. ''


●YESU KRISTO ana mamlaka yote mbinguni na duniani.


Hakuna mchawi wala jini anayeweza kushindana naye.

Ndugu Ukimtegemea Bwana YESU kwa maombi hakika utaona ushindi mkuu.

Ndugu simama ukauone Wokovu wa MUNGU maishani mwako maana hayo matatizo unayoyaona Leo hutayaona tena.

Hiyo huzuni inayokutesa hutaiona tena, endelea tu na YESU KRISTO kwa kumtii na kulitii Neno lake.

Kuna faida kubwa sana katika kumtegemea Bwana YESU.


Ngoja nikupe ushuhuda mfupi.

Mwana 2010 December 27 saa Nne usiku nilipata ajali mbaya ya gari nikiwa Zanzibar. Ajali ile nilipata nikiwa peke yangu na nilianguka katikati ya barabara baada tu ya kushuka kwenye gari na kurushwa juu, wenye gari ile walikimbia wakijua nimekufa. Nilikaaa katikati ya barabara masaa mawili na kwa Neema ya MUNGU nilikuja kupata fahamu masaa 15 baadae nikiwa Hospitalini.


 Baada ya kupata fahamu nilimkuta daktari akiwaambia walionizunguka kwamba kwa majeraha yale siwezi kupona maana alisema kwamba vipimo vinaonyesha kwamba damu imechanganyikana na ubongo maana kichwa kiliumia sana.

Maneno yale wala hayakunitisha maana nilipokuwa nimezimia masaa 15 nilikuwa katika ulimwengu mwingine nikionyeshwa mambo mengi mbalimbali ambayo katika utumishi nilitakiwa kuyapitia. Wakati Daktari anawaambia watu huku wengine wanalia kwamba sitapona nilisikia sauti ikisema kwamba ''Daktari wa duniani anasema hutapona lakini Daktari wa mbinguni YESU KRISTO anasema umepona"


Nini kilifuata?

Nilipona katika mazingira ambayo hata daktari wa kidunia hakuelewa. Nilikaa siku 6 Hospitalini pale na siku ya saba nikaruhusiwa kuondoka nikiwa mzima wa afya. Daktari yule wa kibinadamu ambaye ni mwislamu alipokuwa ananiaga alisema kwamba Hakika wewe umeokoka na mshike sana huyo YESU wako maana amekuponya kiajabu sana.


Baada ya Mwezi mmoja sikuwa hata na alama moja ya ajali, nilienda Mwanza nyumbani baada ya wiki mbili baada ya ajali na ndugu zangu walinishangaa sana maana walivyoelezwa hali yangu baada ya ajali ni ni tofauti na walivyoniona nilipofika Mwanza.

 Ni kweli kabisa nilikuwa mahututi na katika hali mbaya sana lakini maombi ya Kanisa la MUNGU Chukwani Zanzibar yalimfanya MUNGU kunitendea muujiza mkuu wa uponyaji.

Ni kweli kabisa katika taaluma ya udakitari walithibitisha kwamba ni vigumu kupona lakini YESU anaweza yote maana kwa kumtegemea aliniponya.


Ndio maana nakuambia mngoje Bwana YESU KRISTO maana atakupigania wewe 

Nini basi naweza kusema?


''Naye YESU alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na KUPONYA MAGONJWA YOTE na UDHAIFU wa kila aina.-Mathayo 9:35''

●Biblia inathibitisha kwamba YESU KRISTO anaponya magonjwa yote na madhaifu yote.

Wewe una ugonjwa gani hata YESU KRISTO asiweze kukuponya?


Ndugu kama hujapona sio kwa sababu MUNGU hawezi kukuponya bali ni kwa sababu hujamwendea akuponye au hujaomba katika usahihi kwamba akuponye.

Au hujapona kwa sababu ya dhambi zako unazoendelea nazo.

Au kwa sababu kuna mambo mabaya hujaamua kujitenga nayo.


Au hujapona kwa sababu ya kuendekeza uganga wa kienyeji na kuiruhusu mizimu ya ukoo au kabila au mji ikutawale.


Niseme nini basi?

 Yeremia 33:6 '' Tazama, nitauletea afya na kupona, nami nitawaponya; nami nitawafunulia wingi wa amani na kweli. ''

MUNGU atauletea afya mji maana yake atawaletea afya watu wakaao Yerusalemu.


Kwa ufunuo siku moja nilipewa andiko hili ili nilitumie katika kuwaombea watu wanaoumwa na watapona.

Ndugu yangu Nakuomba ulione Neno la MUNGU kama lako na sio la watu fulani tu. Hata kama kuna mtumishi alifunuliwa na ROHO wa MUNGU juu ya andiko fulani, hiyo haina maana kwamba andiko hilo wengine haliwahusu.

Kumbuka Neno la MUNGU ni la MUNGU na hilo Neno la MUNGU ROHO MTAKATIFU hulitumia ili kutusaidia na kwa njia ya maombi katika Neno hilo Tunapona kwa jina la YESU KRISTO.


Leo Muombe MUNGU mambo matatu yaliyo katika andiko hilo la Yeremia 33:6 MUNGU Baba katika jina la YESU KRISTO akutendee.


1. Kwa maombi yako yaliyoambatana na utakatifu wa kweli mwambie MUNGU akupe Afya kama Neno lake linavyosema katika Yeremia 33:6


2. Mwambie MUNGU akupe kupona katika kila majanga na magonjwa yaliyokufuatilia, akupe kupona sawasawa na Yeremia 33:6.


3 Mwambie MUNGU akuponye katika jina la YESU KRISTO sawasawa na Yeremia 33:6.


Baada ya maombi yako katika kweli na jina la YESU KRISTO hakika simama ukauone Wokovu wa MUNGU Baba kwako.

MUNGU akubariki sana.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU KRISTO Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.

Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.

Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.

Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU KRISTO Kwako.

By Peter Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

+255714252292.

Nakutia moyo ndugu yangu simama ukauone Wokovu wa MUNGU kwako.

Ndugu hata kama ulikuwa huzai utazaa, ulikuwa unaumwa YESU anaweza kukuponya.

Kwa tatizo lako hilo hilo au changamoto yako hiyo hiyo endelea kumwamini MUNGU Baba maana Wokovu wake utakuja kwako, atakupigania na wewe utakaa kimya kwa furaha.

Comments