JITENGE NA MWENENDO MBAYA ULIOPOKEA KUTOKA KWA WAZAZI WAKO.

 

Na Mwl Peter Mabula

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote. 

Karibuni tujifunze Neno la MUNGU. 


Wazazi ndio walimu wa kwanza kwa watoto wao. 

Iko mienendo mibaya wazazi wanaweza kuwa nayo na wakawafundisha na watoto wao.

Ziko mila na desturi mbaya za wazazi ambazo mtoto anaweza kujifunza kwa wazazi wake. 


1 Petro 1:18-23 " Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; MPATE KUTOKA KATIKA MWENENDO WENU USIOFAA MLIOUPOKEA  KWA BABA ZENU; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya KRISTO. Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa mwisho wa zamani kwa ajili yenu; ambao kwa yeye mmekuwa wenye kumwamini MUNGU, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata imani yenu na tumaini lenu liwe kwa MUNGU.  Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo. Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la MUNGU lenye uzima, lidumulo hata milele."


Unapookolewa na Bwana YESU KRISTO ni vyema sana ukachunguza mienendo mibaya uliyoipokea kutoka kwa wazazi wako ili usienende tena katika mienendo hiyo mibaya. 

Biblia hapo juu inasema "MPATE KUTOKA KATIKA MWENENDO WENU USIOFAA MLIOUPOKEA KWA BABA ZENU;" na sasa ufuate mwenendo mpya uwapasao waenda mbinguni waliokombolewa kwa damu ya YESU KRISTO. 


Nimesema mtoto hujifunza zaidi kwa wazazi wake maana wazazi ndio walimu wa kwanza kabisa wa watoto wao. 

Mtoto anapozaliwa huwa anaanza kujifunza kwa kuiga kwa watu anaoishi nao hasa wazazi maana muda mwingi zaidi yuko na wao. 


Kwa mtoto kujifunza kwa wazazi anaweza kujifunza mema na anaweza kujifunza mabaya pia kama anaona wakifanya mabaya. 


Mithali 22:6 "Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee."


Sasa Inawezekana kuna Watu walipokea mienendo mibaya kutoka kwa wazazi wao, Biblia inasema tutoke katika mienendo mibaya tuliyoipokea kutoka kwa wazazi.  


Mama au Baba anaweza kumfundisha mtoto wake mambo mabaya yatakayomtesa mtoto badae. 

Wazazi kama walimu muhimu zaidi   kwa watoto wao inapaswa sana kuwafundisha watoto mambo yanayofundishwa na Biblia, ndipo watoto wao hawatajikwaa katika maisha yao. 


Baadhi ya mienendo mibaya ambayo baadhi ya wazazi wamewafundisha watoto wao ni  hii. 


1. Kutumia uganga, mizimu na kuziabudu miungu.


Wako watu akili zao muda wote zinawaza kwenda kwa waganga wa kienyeji kwa sababu tu walijifunza kutegemea waganga wa kienyeji na waliowafundisha ushetani huo ni wazazi wao,  maana utotoni watoto walikuwa wanaona kila mara waganga wakipishana nyumbani kwao. 


Kuna Watu leo hutimiza matakwa ya mizimu,  ni hatari sana maana ni kutengeneza vifungo vya giza vitakavyowatesa sana baadae. 


Kuna Watu leo wanaabudu miungu kwa sababu wamejifunza  kwa wazazi wake,  ni hatari sana maana ni kufundishwa njia ya jehanamu. 


Kama wewe umefundishwa kwenda kwa waganga ujue umefundishwa mwenendo mbaya sana unaofungulia mashetani kukutesa katika maisha yako. 


Walawi 19:31 "Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu."


2. Ulevi, sigara, bangi n.k


Wagalatia 5:21 "husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa MUNGU."


Hata usipomfundisha mtoto wako pombe au sigara au bangi lakini akikuona tu unatumia uchafu huo ujue ataiga hivyo utakuwa umemfundisha mwenendo mbaya Sana.

Kuna Watu pombe na ulevi vimewafanya kubakwa na kuna hadi Watu wamekuwa mashoga kwa sababu ya ulevi uliopelekea kuingiliwa kinyume na maumbile. 


Ndugu mmoja siku moja aliniambia mambo ya ajabu sana,  alisema kabila lao walevi ni wengi sana na pombe zinawaletea madhara mengi sana na wameshindwa kuacha pombe kwa sababu mkoani kwao mtoto hufundishwa kunywa pombe toka akiwa mchanga.


Wanawake wengi mkoani kwao huwa wakienda shambani kulima na watoto wao wadogo,  huwa wanawapa pombe watoto ili walewe   wasisumbue na wasilie  na kuzuia kazi. 

Niliogopa sana,  yaani mama anampa mtoto pombe ili mtoto asilie,  hivyo mtoto huyo anapolewa anakuwa wa kucheka cheka akiwa kawekwa chini mbali,  huu ni ushetani wa hali ya juu.  Ndugu huyu alisema tangu anaanza kupata akili alikuwa anakunywa pombe hadi leo,  amekuwa mtu wa madeni tu na mambo mabaya yote ameshafanyiwa akiwa amelewa,  ni hatari sana. 

Yaani mtoto amepokea mwenendo mbaya kutoka kwa wazazi wake waliomfundisha. 

Ndugu,  kama una mwenendo mbaya wowote ulioupokea kwa wazazi wako,  huo mwenendo mbaya uache haraka sana.

Biblia inasema " mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya MUNGU katika haki na utakatifu wa kweli.-Waefeso 4:22-24


3. Ndoa za mitaala. 


Ndoa za mitaala ni  Ndoa za wake wengi. 

Wapo Watu wamefundishwa na Baba zao kuoa wake wengi, ni hatari sana. 

Inawezekana ni wewe umepokea mwenendo mbaya kutoka Kwa Baba yako maana Baba yako alioa wake wengi hivyo na wewe unamuiga Baba yako kuoa wake wengi. 


Kuoa wake wengi sio mpango wa MUNGU kamwe bali ni mipango ya shetani. 

Ndio maana MUNGU alimuumba Adamu mmoja tu kwa Eva mmoja tu,  mpango wa MUNGU ni Mume mmoja tu kwa mke mmoja tu. 

Mwanzo 2:23-24 " Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja."


Kuna Watu husema mbona akina Daudi walioa wengi lakini ukweli ni kwamba hakuna andiko hata Moja Katika Biblia ambapo MUNGU alimsifu mtu yeyote aliyeoa wake wengi maana sio mpango wake. 

Kama umejifunza mwenendo wa kuoa wake wengi tambua leo kwamba umeshika mwenendo wa waenda jehanamu, ondoka kwenye huo mwenendo mbaya ulioupokea kutoka kwa wazazi wako. 


4. Kuwafundisha watoto kutokuamini YESU KRISTO Mwokozi. 


Kazi kuu ya shetani ni kuwafanya Watu wasimwamini YESU KRISTO kama Mwokozi wao,  hivyo wapo Baadhi ya wazazi hutumiwa na shetani ili kuwafundisha watoto wao ili wasimwamini YESU KRISTO. 

Ndugu kama ulipokea mwenendo huo ujue ulipokea mwenendo wa kuzimu na sio mbinguni. 

Kwa sasa kwa sababu unajitambua na una YESU KRISTO basi usifuate kamwe mwenendo mbaya uliojifunza zamani kwa wazazi wako. 

Biblia inasema  "Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?- 2 Kor 6:14"


5. Ukali, ukaidi, kiburi


Kuna Watu walijifunza ukali kutoka kwa wazazi wao,  ndugu kataa mwenendo huo mbaya. 

Kuna Watu walijifunza ukaidi na kiburi kutoka kwa wazazi wao hivyo kwa sasa wanaenda katika mwenendo huo mbaya wa ukaidi na kiburi. 

Ndugu hakikisha wewe hufuati mwenendo huo mbaya uliojifunza Kwa wazazi wako. 

MUNGU hataki uwe na kiburi na ukaidi kama wazazi wako. 


 Zaburi 78:8" Naam, wasiwe kama baba zao, Kizazi cha ukaidi na uasi. Kizazi kisichojitengeneza moyo, Wala roho yake haikuwa amini kwa MUNGU."


6. Uzinzi na uasherati 


Waefeso 5:3" Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu;"


Moja ya janga kubwa kwa sasa ni dhambi ya uzinzi na uasherati. 

Moja ya dhambi zinazowapeleka Watu wengi jehanamu ni pamoja na uzinzi na uasherati. 

Ndugu,  kama ulipokea mwenendo wa uzinzi na uasherati kutoka kwa wazazi wako basi hakikisha wewe unajitenga mbali na mwenendo huo mchafu.


7. Ibada za sanamu.


Kuna Watu wanaabudu Sanamu kwa sababu walifundishwa na wazazi wao. 

Ndugu,  Biblia inasema hivi juu ya ibada ya Sanamu kwamba  "Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu. Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo.-1  Wakorintho 10:14-15


Ndugu jitenge mbali na mwenendo wa kuabudu Sanamu uliojifunza kwa wazazi wako. 

Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri. 

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.


Bwana YESU Amekaribia Kurudi.


Je, Umejiandaaje?


Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?


Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.


Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.


Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.


Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.

By Peter Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.

+255714252292(Ni namba hii  kupiga,  kuandika meseji na hadi whatsapp).

Comments