MAMBO 12 YANAYOTOKEA BAADA YA MTU KUOKOKA.

 

Na Mwl Peter Mabula

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu. 
Karibuni tujifunze Neno la MUNGU. 
Leo tunajifunza kuhusu mambo yanayotokea baada ya mtu kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wake. 

Mambo hayo 12  yanayotokea baada ya mtu kumpokea YESU KRISTO  kama Mwokozi wake ni haya. 

1. Mtu huyo anasamehewa dhambi zake, maovu yake na makosa yake. 

Yeremia 33:8 "Nami nitawasafisha na uovu wao wote, ambao kwa huo wamenitenda dhambi; nami nitawasamehe maovu yao yote, ambayo kwayo wamenitenda dhambi, na kukosa juu yangu."

Msamaha huo wa dhambi hutokea katika KRISTO YESU pekee. 

Wakolosai 2:13 "Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote;"

 2. Mtu huyo anatakaswa dhambi na uchafu wa rohoni. 

1 Yohana 1:9 "Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote."

3.  Mtu huyo anahamishwa kutoka ufalme wa shetani  na sasa anakuwa ndani ya ufalme wa MUNGU. 

Wakolosai 1:13" Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;"

4. Mtu huyo anaanza safari ya kwenda uzima wa milele. 

Isaya 35:8 "Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo."

5. Mtu huyo anakuwa amepata kibali cha ROHO MTAKATIFU kuingia ndani yake. 

Yohana 14:17 "ndiye ROHO wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu."

6. Jina la mtu huyo linaandikwa katika kitabu cha uzima mbinguni. 

Ufunuo 3:5 "Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake."

7. Mtu huyo anapata kibali cha MUNGU cha kuhudumiwa na Malaika wa MUNGU. 

Waebrania 1:14 "Je! Hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?"

8. Mtu huyo anafanyika mtoto wa MUNGU. 

Yohana 1:12-13 "Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake;
 waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU."

9.  Mtu huyo anafutiwa dhambi zake zote. 

Warumi 4:7-8 " Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao. Heri mtu yule ambaye BWANA hamhesabii dhambi."

Muujiza wa kutubu na kufutiwa dhambi hufanyika katika KRISTO YESU pekee. 

1 Yohana 1:7 "bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote."

10. Mtu huyo anakuwa Mtumishi wa KRISTO  na wakili wa siri za MUNGU. 

1 Wakorintho 4:1-2 "Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa KRISTO, na mawakili wa siri za MUNGU.  Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu."

11. Mtu huyo anakuwa ameokoka. 

Waefeso 2:8 "Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU;"

12. mtu huyo anakuwa mwanafunzi wa YESU KRISTO. 

Yohana 8:31-32 " Basi YESU akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru."

Siku hii YESU KRISTO aliwaambia Wayahudi kwamba wakikaa kwenye Neno lake watakuwa wanafunzi wake,  na leo Bwana YESU KRISTO anawaambia Watanzania wote na Waarabu wote na Wahindi wote na watu wa mataifa yote duniani kwamba kama wakiamua kukaa katika Neno lake hakika watakuwa Wanafunzi wake. 
Bwana YESU KRISTO anakuambia pia na wewe unayesoma ujumbe huu haijalishi wewe ni kabila gani au unatoka nchi gani, muhimu ni kumtii tu.
Kwa mtu kulitii Neno la KRISTO hakika  unafanyika mwanafunzi wa KRISTO. 
Ni heshima kubwa sana mtu kufanyika mwanafunzi wa YESU KRISTO. 

Kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako ni jambo la thamani sana na usikubali likupite kamwe maisha

ni mwako. 
Mimi naamini mwenye sikio la kusikia leo amesikia na ataamua leo kuokoka. 

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO.
+255714252292(Hadi whatsapp).

Comments