MAMBO MACHACHE KUHUSU VITABU VYA AGANO JIPYA.

 

Na Mwl Peter Mabula

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.

Naamini kila mmoja ambaye ni msomaji wa Biblia anavijua vitabu vya agano jipya, viko 27


Naomba tujifunze machache kuhusu hivi vitabu vya agano jipya.


Tuanze na Agano ni nini?


■Neno agano maana yake ni patano kati ya pande mbili.


✓✓Sasa kuna maagano ya MUNGU na wanadamu.


✓✓Kuna maagano ya wanadamu na wanadamu.


✓✓Na yapo pia maagano kati ya wanadamu na nguvu za giza.


Maagano kati ya wanadamu na nguvu za giza ni maagano yaliyoleta vifungo vya kipepo kwa wanadamu na maagano makubwa zaidi ya wanadamu na nguvu za giza ni pale baadhi ya wanadamu walipofanya agano na shetani ili kuanzisha dini za kinyume, dini hizi ni zile zote zinazokataza watu kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi.


Sasa kwa leo Mimi Peter Mabula sizungumzii maagano kati ya wanadamu na wanadamu au wanadamu na nguvu za giza ila nimedokeza tu, lakini leo nazungumzia vitabu vya agano jipya ambapo hili agano jipya ni agano la milele na la mwisho kati ya MUNGU na wanadamu.


✓✓Agano jipya ni patano la MUNGU kwa wanadamu ili wanadamu watakaotii waupate uzima wa milele.


◼️Ukisikia Agano jipya ndani ya Biblia maana yake ni mapatano mapya ya mwisho kati ya MUNGU na wanadamu.


✓✓Sasa agano jipya linaambatana na vitabu 27  vinavyolifafanua hilo agano na vinavyoonyesha uhusiano kati ya hilo agani jipya na agano la kale.


Ngoja sasa niseme machache kuhusu vitabu vya agano jipya na naamini kuna vitu vingi utajifunza.


◼️Agano jipya lina vitabu 27 vinavyoungana na vitabu 39 vya agano la kale ili kutengeneza Biblia takatifu.


Sisi Wakristo tunatumia vitabu  vyote vya agano jipya na vitabu vyote vya agano la kale, ila kwa sababu tunaishi katika wakati wa agano jipya basi tunavitumia vitabu vya agano la kale kwa jinsi ya KRISTO.


✓✓Ninaposema agano jipya na agano la kale sina tu na maana ya vitabu 39 vya agano la kale na vitabu 27 vya agano jipya bali mapatano ya kwanza kupitia Musa na Mapatano  ya pili kupitia YESU KRISTO.


Kila patano au agano lina kanuni zake  hivyo sisi kwa sasa tunatembea kwenye kanuni mpya ambayo ni ya KRISTO ila tunajifunza pia kanuniza zamani kwa jinsi ya KRISTO ambaye ndiye mwenye agano jipya la milele.


Kumbuka pia  vitabu vya agano la kale vina mambo mengi  nje na aliyopewa Musa hivyo ni muhimu sana sisi tuhusike pia vitabu vyote vya agano la kale maana ni kwa ajili yetu.


Ndani ya agano la kale ambalo sio vitabu kuna torati na ndani ya agano jipya kuna Injili ya YESU KRISTO.


Agano la kale nje na torati lina vitabu vya historia, vitabu vya manabii na Zaburi, ndio maana ni vyema sana kutofautisha torati na agano la kale, torati sio vitabu fulani  bali ni maelekezo ya torati yaliyo ndani ya baadhi ya vitabu vya Biblia, hivyo Biblia nzima inatuhusu sisi wote.


Sasa kwa sababu agano jipya lina taratibu zake ambazo zimeandikwa katika vitabu 27 vya agano jipya leo nazungumzia kwa uchache kuhusu tu hivi vitabu 27 vya gano jipya.


1.       Vitabu vya agano jipya vimetofautiana kwa namna mbalimbali lakini vyote vinamhusu MUNGU ambaye amejifunua katika KRISTO YESU ili kuleta uzima wa milele kwa watakaomwamini.


Mfano ni Yohana 3:16 "Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele."


2.       Vitabu vya agano jipya vyote vinahusu injili ya KRISTO.


Neno injili linatokana na neno “Euangelion’’ la kigiriki ambalo kwa kiswahili lina maana ya ‘’HABARI NJEMA ZA UFALME WA MUNGU’’


 Mathayo 24:14 "Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja."


◼️Hivyo injili ni habari njema za ufalme wa MUNGU zilizoletwa na YESU KRISTO Mwokozi.


✓✓Wahubiri wote wa leo inawapasa kujua kwamba huu ni wakati wa injili ya KRISTO hivyo kazi yao kama watumishi wa MUNGU ni kuipeleka mbele injili ya KRISTO ya Wokovu.


2 Wakorintho 4:5" Kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali KRISTO YESU ya kuwa ni Bwana; na sisi wenyewe kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya YESU."


3.       Agano jipya  linaanzia na vitabu 4 vya injili ambavyo vinazungumzia maisha halisi ya Bwana YESU alipokuja duniani.


Marko 1:14-15 " Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, YESU akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya MUNGU, akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa MUNGU umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili."


4.       Kitabu cha Matendo ya mitume kinaonyesha namna injili ya YESU KRISTO ilivyoenea maeneo mbalimbali duniani.


Mfano hai.


Matendo 6:7 "Neno la MUNGU likaenea; na hesabu ya wanafunzi ikazidi sana katika Yerusalemu; jamii kubwa ya makuhani wakaitii ile Imani."


Mfano hai mwingine.


Matendo 12:24 "Neno la BWANA likazidi na kuenea."


Mfano hai mwingine.


Matendo  13:49 "Neno la BWANA likaenea katika nchi ile yote."


Hata sisi leo inatupasa kuendelea kuieneza injili ya YESU KRISTO duniani.


5.       Baada ya kitabu cha matendo ya Mitume katika mpangalio wa vitabu vya agano jipya zinafuata nyaraka(Barua) 13 za Mtume Paulo kwa maeneo mbalimbali alikokuwa amehubiri  injili ya YESU KRISTO.


Nyaraka hizo ni Warumi, Wakorintho wa kwanza, Wakorintho wa pili, Wagalatia, Waefeso,Wafilipi, Wakolosai, Wathesalonike wa kwanza, Wathesalonike wa pili, Timotheo wa kwanza, Timotheo wa pili, Tito, Filemoni,


Barua hizi zinafundisha, zinaelekeza, zinafafanua, zina maonyo, zinatia moyo n.k ili tu sisi tulio Kanisa la KRISTO tuwe safi na tusiishie njiani bali tufike uzima wa milele.


Wagalatia 5:16 "Basi nasema, Enendeni kwa ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili."


6.       Baada ya Nyaraka 13 za Mtume Paulo kinafuata kitabu cha Waebrania, hiki ni kitabu cha kipekee sana ambacho kinazungumzia uhusiano uliopo kati ya YESU KRISTO na agano la kale.


Kitabu cha Waebrania kinaanzia na kujulisha kuwa katika agano la kale MUNGU alikuwa anasema na watu mara nyingi zaidi akitumia Manabii lakini wakati huu MUNGU anazungumza na sisi kupitia YESU KRISTO.


Waebrania 1:1-2 " MUNGU, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana(YESU KRISTO), aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu."


Hiyo tu inaonyesha kwamba kitabu cha Waebrania kinazungumzia uhusiano uliopo kati ya Agano la kale na Agano jipya.


Ndio maana ni kitabu hiki pia kinalizungumzia Agano la kale na Agano jipya.


Kinazungumzia damu ya wanyama ambayo Agano la kale waliitumia lakini sisi Sasa tunatumia damu ya YESU.


Kinazungumzia sadaka za kuteketezwa zilivyokoma na sasa hatuna sadaka za kuteketezwa na ni kitabu hiki pia ndicho kinafunua kwetu kwamba torati ilikuwa ni kivuli tu kilichoutangulia mwili halisi ambao ni KRISTO YESU.


Waebrania 10:1 "Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao."


Kwa hiyo ukitaka uone uhusiano wa YESU KRISTO na Agano la kale basi sehemu mojawapo ya kusoma ndani ya Biblia ni kitabu cha Waebrania.


Ukitaka uone uhusiano kati ya Agano jipya na Agano la kale basi sehemu mojawapo muhimu ya kusoma ndani ya Biblia ni kitabu cha Waebrania.

 

7.       Baada ya kitabu cha waebrania zinafuata nyaraka(Barua) 7 kwa watu wote.


 Mfano ni  2 Petro 1:1-2 "Simoni Petro, mtumwa na mtume wa YESU KRISTO, KWA WALE WALIOPATA IMANI MOJA NA SISI, YENYE THAMANI, katika hali ya MUNGU wetu, na Mwokozi YESU KRISTO. Neema na iwe kwenu na amani iongezwe katika kumjua MUNGU na YESU Bwana wetu."


Nyaraka za mtume Paulo katika vitabu vyake 13 zinaelekezwa kwa Kanisa la eneo fulani lakini hizi nyaraka 7 za  baada ya kitabu cha Waebrania  kwenye mpangilio wa Biblia , hizi nyaraka ziliandikiwa kwa maeneo mengi na sio eleo moja tu.


Mfano ukisoma Waraka wa kwanza wa Yohana unaanza kwa kusema ‘’WARAKA WA KWANZA WA YOHANA KWA WATU WOTE’’ hii  tofautisha na Nyaraka za Paulo mfano Waefeso  inaanza kwa kusema hivi ‘’WARAKA WA PAULO MTUME KWA WAEFESO’’  hapa najaribu tu kukupa tofauti ili ujue na uongeze maarifa kuhusu vitabu vya agano jipya ambavyo vyote ni vyetu na vinatuhusu sisi vyote hivyo tuvisome vyote na kuvizingatie vyote.


8.       Kitabu cha mwisho cha agano jipya katika mpangilio ni kitabu cha UFUNUO.


Hiki ni kitabu kianachozungumzia  mambo yaliyopo, mambo yajayo na kinazungumzia pia kurudi kwa Bwana YESU KRISTO na kinazungumzia pia Uzima wa milele kwa wateule wa KRISTO walioshinda duniani.


Ufunuo  1:19 "Basi, uyaandike mambo hayo uliyoyaona, nayo yaliyopo, na yale yatakayokuwa baada ya hayo."


Ufunuo wa Yohana 20:11-15 " Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana. Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao. Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto."


Ufunuo 21:1-7 " Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena. Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa MUNGU, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe. Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya MUNGU ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye MUNGU mwenyewe atakuwa pamoja nao. Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita. Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli. Akaniambia, Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure. Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa MUNGU wake, naye atakuwa mwanangu."


Hayo ndiyo mambo machachde kuhusu vitabu vya agano jipya nimependa kukushirikisha leo, siku moja nitazungumzia kitabu kimoja kimoja ikiwezekana kama MUNGU akinipa neema hiyo, pia siku moja nitazungumzia vitabu vya agano la kale.


✓✓Ndugu, nakuomba endelea kujifunza Biblia, endelea kusoma Biblia, endelea kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO kama ambavyo Biblia inafundisha.


✓✓Endelea kumpenda MUNGU na kumtolea zaka na sadaka kama ambavyo Biblia inafundisha.


✓✓Endelea kumtumikia Bwana YESU KRISTO na ambavyo  Biblia inafundisha na endelea kuongozwa na ROHO MTAKATIFU kama ambavyo Biblia inafundisha.


Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri. 

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.

Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.

Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.

Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.

ByPeter Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.

+255714252292(Ni namba hii  kupiga,  meseji, whatsapp na chochote).

MUNGU akubariki sana.

Comments