MAOMBI YA KUZIFUNGA KAZI ZA SHETANI ZILIZOANZISHWA KATIKA MAENEO YAKO.

 

Na Mwl Peter Mabula


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.!
Karibu sana  tujifunze Neno la MUNGU la uzima na kisha tuombe maombi ya ushindi mkuu..

Wateule wa KRISTO tumepewa mamlaka na MUNGU ya kuzifunga kazi za shetani na tumepewa mamlaka ya kufungulia ushindi kwetu.

Mathayo 18:18 '' Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni. ''

Shetani ana mbinu  nyingi sana za kutaka kuwadhuru kiroho watu wa MUNGU lakini MUNGU siku zote ni Mshindi.

Shetani walio wake hasumbuani nao sana maana alishawafunga ila hutafuta nafasi ya kuwafuata wale ambao walishamkimbia siku walipompokea YESU KRISTO kama Mwokozi.

Kwa sasa shetani anafanya kazi kwa wana wa kuasi yaani wanamkataa YESU KRISTO kama Mwokozi wao.

Wakolosai 2:2 '' ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi; ''

Sasa shetani kwa sababu anawawinda wateule wa MUNGU hujaribu kuanzisha kazi  zake katika maeneo yao ili tu awavute au awafunge vifungo.

Kuna aina mbili za kazi za shetani zinazoweza kuanzishwa katika maeneo ya watu wa MUNGU ili tu kulidhoofisha kundi la watu wa MUNGU ambao ndio wateule wa KRISTO YESU.

Kazi hizo ni
 (a) Kazi za kishetani zinazoonekana.

  Kazi za kishetani zinazoonekana ni kama Bar kuanzishwa pembeni ya nyumba yako mteule au bar kuanzishwa pembeni ya Kanisa, kuanzishwa nyumba za ibada ya kishetani, kuanzishwa kijiwe cha bangi pembeni yako, Mkeo au mumeo kukusaliti, kuwepo kituo cha ukahaba jirani na unapokaa,vilabu vya pombe, kuwekwa kituo cha kutibu watu kipepo n.k

(b) Kazi za kishetani zisizoonekana.

=Kuwepo wachawi katika eneo lako.

=Watu wabaya kufanya vikao vya siri ili wakuharibie wewe.

= maroho ya ukoo yaani mizimu ya ukoo unapokufuatilia.

=Watu wako wa karibu kutumika kishirikina kwa siri  dhidi yako

=Majini kutumwa kwako.

Kazi hizo zote anazifanya shetani kupitia maroho wa kuzimu aliowatuma au kupitia watu walioingia mkataba nae, lakini nguvu zote hizo hutoka kwa shetani maana shetani ndio hutoa nguvu za ki pepo kwa walio upande wake.

Ufunuo 13:2 ''Na yule mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba, yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi.''

Kazi za shetani zisizoonekana ni kama vifungo vya siri ambavyo mtu anafungwa na majini, mizimu au wachawi.

Leo tunazifunga kazi za shetani zilizoanzishwa katika maeneo yako yote.

Kazi ya shetani inaweza kuanzishwa katika ndoa yako, katika uchumba wako, katika ardhi yako, katika eneo la jirani na kanisa, katika familia yako, katika ukoo wako, katika shule unayosoma n.k

Mchungaji mmoja siku moja alituambia kwamba mpinga Kristo mmoja alifungua bar pembeni ya Kanisa na akanunua Spika kubwa na  za gharama kubwa kisha kila jumapili ibada ikitaka kuanza anafungulia mziki katika bar yake na siku zote spika zake alikuwa anazielekeza kanisani, hiyo ni kazi ya  shetani iliyoanzishwa pembeni ya Kanisa ili kuliua Kanisa.

Kwa muda kadhaa ibada Kanisani pale zilivurugika sana, baadae kanisa ikabidi liingine katika maombi ya kufunga ya siku kadhaa.

Baada ya maombi yale siku ya ibada yule mtu akafungulia tena mziki wake wa kiduniani huku spika kaelekeza Kanisani ili tu ibada isifanyike, akafungulia mziki kwa sauti baadae akaanza kuongeza sauti, alipoongeza tu sauti kidogo  spika zake zililipuka kama bomu na vyombo vyote vya mziki alivyokuwa navyo vilianza kuungua kwa moto na vikateketea akiangalia. Alipata hasara kubwa sana na akaanza kutangaza na kudai mitaani kwamba Kanisa lile ni wachawi eti wameroga vyombo vyake vya mziki.

Aliifunga bar yake bila kupenda na ibada Kanisani zikaendelea kama kawaida.

Kazi za shetani ni nyingi sana lakini inakupasa kwa maombi uzifunge kazi hizo ili zisifanye kazi kwenye maeneo yako maana ni kazi  za shetani.

Kazi sha shetani zinaweza kuwekwa pembeni ya nyumba yako ili tu kukuvuruga na kukuondolea ustawi wako kiroho kama mtu uliyeokolewa na Bwana YESU, lazima kazi hizo za shetani zifungwe kwa maombi.

Waefeso 6:11  '' Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.''

Inawezekana hujaelewa vyema, ngoja nikujulishe kwa lugha rahisi.

=Ni kwamba mganga wa kienyeji kuhamia mtaani kwenu  ujue hapo mkuu wa giza amehamia mtaani kwenu, anaweza akaifunga ardhi kipepo na ninyi mkapata madhara kiroho msipojua namna ya kujinasua kimaombi.

=Wafanyakazi wenzako kazini kuanza kutumika kipepo  au kukusema vibaya ujue hiyo ni kazi shetani imeanzishwa katika eneo lako ili kukuharibia. 

 =Wakala wa shetani kuwa mkuu wako wa kazi au kuwa kiongozi wenu kazini, ujue hiyo ni kazi ya shetani imeingia.

=Watu wanaoiwinda ndoa yako, au wanawinda uchumba wako, wanawinda biashara yako kipepo, ujue hapo kazi ya shetani imeingia

=Ardhi mliyopo inaweza kushikiliwa kipepo na nguvu za giza hata mkashindwa kufanikiwa kamwe.

Jiulize mfano ni wewe au familia yako mnaishi katika eneo hili unategemea nini?

Eneo hili, Isaya 13:21 '' Lakini huko watalala hayawani wakali wa nyikani; na nyumba zao zitajaa bundi; mbuni watakaa huko; na majini watacheza huko.  ''

Yaani unakaa mtaa uliojaa waganga wa kienyeji, na hao huambatana na majini na bundi, itakulazimu ujitambue kiroho na ujue kupigana vita ya kiroho sawasawa ndipo utashinda.

Vipi kama wakuu wa giza wamejaa katika ukoo wenu, yaani wakitoa kafara na wewe wanakutaja jina, yaani jina lako linakuwakilisha huko kwenye madhabahu za giza, vipi kama ni katika eneo lako la biashara au kazini kwako kumejaa watumia tunguri na hirizi?

Utajisikiaje mfano mmepanga kufanya mkutano mkubwa wa injili, kwa miezi kadhaa mmejiandaa na mmetangaza na kuombea sana mkutano huo, lakini unashangaa siku ya mkutano wa injili kuanza, katika mtaa huo huo  ni siku hiyo hiyo kuna tamasha la mziki wa kidunia?  yaani mtaa ule ule, ndugu kama hujui kwamba kazi za shetani zinaweza kuanzishwa basi elewa leo na ziharibu kazi hizo kwa maombi.

Ndugu jifunze kuomba na anza kuomba ili kuharibu kazo zote za shetani, wewe una nguvu sana kama YESU KRISTO ni Mwokozi wako na unamtii.

2 Kor 10:4-5 '' (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika MUNGU hata kuangusha ngome;)  tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya MUNGU; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii KRISTO; ''

Unaweza ukapata mchumba na mambo yakaenda vizuri tu lakini siku chache kabla mfunge ndoa unashangaa mzazi kutoka upande mmoja anakataa msifunge ndoa, kwa sababu ambazo hazina kichwa wala miguu. Mwanaume mmoja siku moja alinipigia simu akilia, akisema kwamba alikuwa na Mchumba wake na walipanga kufunga ndoa na ziku zilipokaribia tu ndugu wa mwanamke walikaa kikao na kupitisha maamuzi kwamba binti yao ataolewa na kijana tajiri aliyetoka nje ya nchi hivyo wakalazimisha mwanaume huyu aachwe. Binti alikuwa hataki kumwacha lakini ndugu zake wote wakamsusia hadi akaamua kumwacha Mchumba wake, hizo ni kazi za shetani zimeingia ghafla ili kuharibu hata kusudi jema la wateule.

Kwa jinsi ambavyo ulimwengu umeharibika basi usishangae unaweza hata kwenda safari na wenyeji wako wakakupangia mabaya siku ukifika tu. 

Ni hatari sana pia kuhamia eneo ambalo madhabahu za kishetani ni nyingi kuliko Makanisa.

Ni hatari sana mume wako au mke wako kwenda kwa waganga, ndugu haribu hizo kazi za shetani maana shetani kazi yake anaweza hata akawinda uhai wako kupitia mwenzi wako wa ndoa kwa maelekezo ya mganga, ni hatari sana.

Leo katika jina la YESU KRISTO  Mwana wa MUNGU aliye hai haribu kila kazi za shetani zilizoanzishwa katika maeneo yako yote.

Bwana YESU anakuhakikishia ushindi kwamba ukiomba ushindi katika jina lake hakika utaupata huo ushindi.

Mathayo 7:7 '' Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; ''

Mtu mmoja alinunua kiwanja, kesho yake alipokwenda katika kiwanja chake alikuta watu wabaya wamechimbia vitu vya kichawi, neema ya MUNGU ni kwamba wakati wanachimbia vitu hivyo ilikuwa jioni giza ndio linaanza na kuna mtoto mdogo aliwaona hivyo alipokuja mwenye kiwanja  yule mtoto akampa siri na walipofukua ardhini walikuta vitu vya ajabu, hiyo ni kazi ya shetani iliyoanzishwa katika kiwanja cha mtu kumfunga au kumzuilia  ujenzi au kumfanyia tu kitu kibaya kulingana na watu hao wabaya walivyokusudia.

Mtu mmoja alipoteza pete yake ya ndoa katika mazingira  ya kutatanisha, tangu apoteze hiyo pete na uzao wake ulipotea na vitu vingi vinavyohusika na ndoa vilipotea.

Hakupata uzao tangu siku hiyo, ndugu unayo sababu kubwa ya kuziharibu kila kazi za shetani zilizoanzishwa katika maeneo yako, ukiziacha kazi hizo madhara yatakupata wewe, pambana tu kiroho na sio kimwili.

Ukienda kimwili MUNGU atakuacha na hivyo adui atakutesa zaidi na kukuonea zaidi.

Familia moja baba wa familia hiyo siku moja alimleta mganga wa kienyeji na kulazimisha familia nzima wachanjwe chale na walishwe kitu fulani alichokuwa nacho mganga. Baada ya tukio hilo ilipita miezi kadhaa familia ile ilipata madhara mabaya sana na majanga yasiyo ya kawaida. Binti kutoka familia hiyo aliyekuwa ananisimulia habari hii alisema kwamba kile kitu alicholishwa na mganga kilisababisha tangu siku hiyo kila akilala usiku yanakuja majini na jini moja linanyoosha mkono kuelekea kwenye tumbo la binti huyo, na kile kitu alicholishwa na mganga kinatoka kwa kupitia kitovu kisha kinaenda mkononi mwa jini, kisha majini yanamwingilia na yakimaliza yanakielekeza tumboni kile kidude na kinarudi kwa kupitia kitovu. Dada yule siku ananiambia hayo ilikuwa katika kumwombea maana alikuwa akiumwa tumbo anaweza hata kuzimia siku nyingine, kumbe maumivu yanatokana na majini kupitisha kitu kitovuni na alisema kwamba wakati kitu hicho kinatoka tumboni au kinaingia alikuwa anasikia maumivu kama anakatwa na wembe tumboni na ndio maana alikuwa na  maumivu ya tumbo ya kudumu na yasiyo ya kawaida.

Siri hiyo ya kuingiliwa kila siku na jini aliifanya siri sana kwa miaka mingi hadi alipozidiwa kwa ugonjwa na ndipo aliniambia ili tumuombee, namshukuru MUNGU tulimuombea na kitu kile kikatoka na akapona.

Ni hatari sana yaani kazi za shetani zilipokaribishwa kwenye familia zilisababisha majini yamuoe yule dada bila kupenda.

Ndugu, mimi naamini unayo sababu kabisa ya kuomba ukizifunga kazi zote za shetani zilizoanzishwa au zinazotaka kuanzishwa katika maeneo yako.

MUNGU anataka uziharibu kazi hizo za shetani, uzivunje na jina la mawakala wa shetani ulifute katika maeneo yako ndipo utakuwa huru.

Kumb 12:3 ''nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo.''

Zipo kazi nyingi za kishetani hivyo hakikisha unazifunga kazi hizo kwa maombi.

Wengine wamejikuta ni mashoga kwa sababu kazi za shetani zilipoingia katika familia zao wao hawakuchukua hatua.

Kuna wengine ni vichaa leo kwa sababu hawakushughulikia kimaombi kazi za shetani zilizoanzishwa katika maeneo yao.

Kuna watu leo wameugua magonjwa ya ajabu ya kurogwa kwa sababu tu hawakushughulikia kazi hizo za shetani.

Nini ufanye ili kuzifunga kazi za shetani na zikatoweka?

1. Kama hujaokoka okoka, kisha tubu kwa ajili kilichosababisha hizo kazi za shetani kupata nafasi.

2 Nyakati 7:14 '' ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.'' 

2.  Haribu madhabahu za giza zinazotuma kazi za shetani  kwenye maeneo uliyopo.

Kutoka 23:24 '' Usiisujudie miungu yao, wala kuitumikia; wala usitende mfano wa matendo yao; bali utaiangamiza kabisa, na nguzo zao utazivunja vipande vipande. ''

3. Zifunge kwa damu ya YESU KRISTO kazi zote za kishetani  ili zisifanye kaze tena.

Mathayo 16:19 '' Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni. ''

 4. Nyunyuzia damu ya YESU KRISTO kwenye eneo zilipokuwa hizo kazi za shetani na futa maagano ya giza yote kwa kutumia damu ya YESU KRISTO.

Ufunuo 12:11 '' Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao   ........... ''

5. Teketeza hizo kazi za shetani kwa moto wa MUNGU.

Yeremia 5:14 '' Kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wa majeshi, asema hivi, Kwa sababu mnasema neno hili, tazama, nitafanya maneno yangu katika kinywa chako kuwa moto, na watu hawa kuwa kuni, nao moto utawala.''

6. Miliki eneo hilo kiroho na panda mambo ya ufalme wa MUNGU katika ardhi ya eneo hilo.

Walawi 20:24 '' Lakini mimi nimewaambia ninyi, Mtairithi nchi yao, nami nitawapa ninyi kuimiliki; nchi iliyojaa maziwa na asali; mimi ni BWANA, Mungu wenu, niliyewatenga ninyi na mataifa.'' 

7. Mshukuru MUNGU maana amekupa ushindi.

Zaburi 27:6 '' Na sasa kichwa changu kitainuka Juu ya adui zangu wanaonizunguka. Nami nitatoa dhabihu za shangwe hemani mwake; Nitaimba, naam, nitamhimidi BWANA.''

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa na somo hili kuna wakati  nitalifafanua zaidi ndani ya kitabu.

MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu 

Hapa chini ni MAOMBI YA KUZIFUNGA KAZI ZA SHETANI ZILIZOANZISHWA KATIKA MAENEO YAKO.

Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba,

Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea. Kumbuka pia fundisho ni muhimu kuliko maombi hivyo wewe ambaye huwa unahusika na maombi  hakikisha unajifunza kwanza somo lote ndipo utapata nguvu za kuomba na kushinda. Ukipata pia msukumo wa kuambatanisha maombi yako na sadaka unaweza kufanya hivyo kwa utukufu wa MUNGU.

MAOMBI YA KUZIFUNGA KAZI ZA SHETANI ZILIZOANZISHWA KATIKA MAENEO YAKO.

 MUNGU Baba yetu wa mbinguni jina lako litukuzwe.

Ninakushukuru kwa neema yako na ulinzi wako kwangu na kwa familia yangu.

Neno lako katika 2 Nyakati 7:14 Linasema  '' ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.''

Hivyo BWANA niko hapa ninanyenyekea mbele zako MUNGU uliyeniumba na sasa nimeziacha njia zangu zote mbaya hivyo naomba unisamehe dhambi zangu zote, maovu yangu yote na makosa yangu yote.

Ninaomba damu ya YESU KRISTO ya agano  inifutie dhambi zangu zote na initakase niwe safi sawasawa na Zaburi 51:1-2 inavyosema kwamba ''Ee MUNGU, unirehemu, Sawasawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu. Unioshe kabisa na uovu wangu, Unitakase dhambi zangu.''

Eee MUNGU Baba ninashukuru maana Neno lako katika 2 Nyakati 7:14 linasema nikiomba utanisamehe dhambi zangu na kuiponya ardhi yangu.

Ninatubu pia mbele zako MUNGU Baba kwa ajili ya chanzo cha kazi za shetani kufanya kazi katika maeneo yangu, ninatubu kwa ajili ya chanzo hicho na  naomba kuanzia sasa hizo kazi za shetani hazitakuwa na kibali cha kuwepo katika eneo linalonihusu.

Katika jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai, Neno la MUNGU katika Kutoka 23:24 '' linanitaka  kuangamiza miungu na nguvu za giza na kuvunja madhabahu za giza, Neno la MUNGU hapo  linasema '' bali utaiangamiza kabisa, na nguzo zao utazivunja vipande vipande.''

Hivyo navunja kila nguzo na kila eneo kiroho  ambalo lilikuwa makazi za nguvu za giza katika eneo langu.

Naharibu  kila madhabahu  inayotuma kazi za shetani katika maeneo yangu, naibomoa madhabahu hiyo kwa jina la YESU KRISTO.

Kila madhabahu ya wachawi au waganga inayotuma kazi za shetani, hiyo madhabahu naibomoa na kuivunja katika jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai.

Kila madhabahu ya majini au mizimu inayotuma kazi za shetani katika ndoa au Biashara au uchumba au kazi au ardhi yangu, hiyo madhabahu naibomoa na kuivunja katika jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai. 

Kila madhabahu ya kuzimu inayotuma kazi za shetani katika maisha yangu au mtaa wangu au eneo langu, hiyo madhabahu naibomoa na kuivunja katika jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai.

Sasa katika jina la YESU KRISTO nazifunga kila kazi za shetani zilizoanzishwa katika maisha yangu,  katika  jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai nazifunga kazi hizo za shetani zote. Imeandika katika Mathayo 16:19 kwamba ''na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.''

 Sasa katika jina la YESU KRISTO nazifunga kila kazi za shetani zilizoanzishwa katika ndoa yangu au uchumba wangu, katika  jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai nazifunga kazi hizo za shetani zote.

 Sasa katika jina la YESU KRISTO nazifunga kila kazi za shetani zilizoanzishwa katika biashara yangu au kazi yangu, katika  jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai nazifunga kazi hizo za shetani zote.

 Sasa katika jina la YESU KRISTO nazifunga kila kazi za shetani zilizoanzishwa katika ukoo wangu au eneo langu la biashara, katika  jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai nazifunga kazi hizo za shetani zote.

 Sasa katika jina la YESU KRISTO nazifunga kila kazi za shetani zilizoanzishwa katika kiwanja changu au ardhi yangu, katika  jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai nazifunga kazi hizo za shetani zote.

 Sasa katika jina la YESU KRISTO nazifunga kila kazi za shetani zilizoanzishwa katika mtaa wangu au mji ninaoishi, katika  jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai nazifunga kazi hizo za shetani zote.

 Sasa katika jina la YESU KRISTO nazifunga kila kazi za shetani zilizoanzishwa katika kijiji ninachokaa au kata au wilaya au mkoa, katika  jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai nazifunga kazi hizo za shetani zote.

 Sasa katika jina la YESU KRISTO nazifunga kila kazi za shetani zilizoanzishwa katika katika eneo lolote la maisha yangu, liwe ni eneo ninalolifamu au ni eneo nisilofahamu, katika  jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai nazifunga kazi hizo za shetani zote.

Kila kazi za shetani zinazoonekana au zisizoonekana, mimi leo hizo kazi zote nazifunga na kuzifuta kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai milele.

 Sasa naachilia damu ya YESU KRISTO kwenye kila eneo la ardhi yangu au biashara yangu au mtaa wangu ili kazi za shetani zitambue kwamba eneo hilo sasa kiroho limemilikiwa na mteule wa MUNGU.

Katika jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai ninateketeza kazi zote za shetani katika maeneo yangu.

Imeandikwa katika Yeremia 5:14  kwamba '' Kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wa majeshi, asema hivi, Kwa sababu mnasema neno hili, tazama, nitafanya maneno yangu katika kinywa chako kuwa moto, na watu hawa kuwa kuni, nao moto utawala.''

Sasa kwa moto wa MUNGU  ninateketeza kazi zote za wachawi na majini katika maeneo yangu, ndoa yangu, biashara yangu na kila .

Kwa moto wa MUNGU nataeketeza kazi zote za laana za wanadamu.

Kwa moto wa MUNGU ninateketeza kazi zote za shetani za mizimu na unajimu katika maeneo yangu.

Ninateketeza kila nguvu za giza, naziteketeza kwa moto wa MUNGU katika jina la YESU KRISTO.

Sasa kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO naachilia damu ya YESU KRISTO kwenye ardhi yangu ili kuitakasa na kuitenga mbali na nguvu za giza.

Naachilia damu ya YESU KRISTO ya agano katika kazi yangu na eneo langu la biashara hivyo kuanzia sana hakuna kazi ya shetani itasimama katika eneo hilo.

Naachilia damu ya YESU KRISTO ya agano kwenye mwili wangu wote, na sasa nguvu za  giza ziachie mwili wangu, kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.

 Naachilia damu ya YESU KRISTO ya agano kwenye kiwanja changu, nafuta kila uchawi uliofanyika hapo.

 Naachilia damu ya YESU KRISTO ya agano katika eneo la kanisa letu, kuanzia sasa hakuna wakala wa shetani atapachezea.

 Naachilia damu ya YESU KRISTO ya agano katika kila eneo ambako kulikuwa na madhabahu za giza na naachilia damu ya YESU KRISTO katika kila eneo linalonihusu ambao kazi za shetani ziliweka makao.

Sasa namiliki ndoa yangu kwenye ulimwengu wa roho, wakala wa shetani hataifuruga, katika jina la YESU KRISTO imekuwa kama nilivyoomba.

 Sasa namiliki ardhi yangu na kiwanja changu na nyumba yangu    yangu kwenye ulimwengu wa roho, wakala wa shetani  hatavamia hapo tena , katika jina la YESU KRISTO imekuwa kama nilivyoomba.

 Sasa namiliki  Biashara yangu na eneo la biashara yangu kwenye ulimwengu wa roho, wakala wa shetani  hatagusa ardhi yangu na eneo langu la biashara, katika jina la YESU KRISTO imekuwa kama nilivyoomba.

 Sasa nalimiliki eneo langu la kazi  kwenye ulimwengu wa roho, wakala wa shetani  hataweza kamwe kuweka mtego katika eneo hilo , katika jina la YESU KRISTO imekuwa kama nilivyoomba.

 Sasa naimiliki ardhi ya mtaa wangu kwenye ulimwengu wa roho, wakala wa shetani hatautumia mtaa huo kamwe kwa ajili ya kuanzisha kazi zake , katika jina la YESU KRISTO imekuwa kama nilivyoomba.

 Sasa namiliki  ukoo wangu na  familia   yangu kwenye ulimwengu wa roho, wakala wa shetani  hataweka kazi zake katika ukoo wangu wala katika familia yangu, katika jina la YESU KRISTO imekuwa kama nilivyoomba.

Eee MUNGU Baba wa mbinguni ninakushukuru  sana maana umejibu maombi yangu, '' Na sasa kichwa changu kitainuka Juu ya adui zangu wanaonizunguka. Nami nitatoa dhabihu za shangwe hemani mwake; Nitaimba, naam, nitamhimidi BWANA.'' kama Zaburi 27:6

Ni katika jina la YESU KRISTO nimeomba na sasa ninapokea ushindi.

 Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.

Hakika umeshinda. Ukiweza hata kuwa na maombi ya kufunga unaweza, pia baada ya maombi yako unaweza  kufanya tendo la imani kwa MUNGU kwa kutoa sadaka  itakayoambatana na maombi juu ya ukomo wa kuteswa na maadui zako katika ulimwengu wa roho, huo ni utashi wako na sio agizo.

Nawaonya pia wanaotumia masomo yangu vibaya na kwa manufaa yao waache tabia hiyo.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By  Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.
+255714252292(mawasiliano, sadaka na whatsap).
MUNGU akubariki sana.

Comments