EPUKA SANA MAPATANO MABAYA.

 

Na Mwl Peter Mabula



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.

Karibu tujifunze Neno la MUNGU.


Watu wengi wamejikuta kwenye mapatano mabaya na hayo mapatano yakaleta madhara makubwa  kwao.


Labda tu ngoja nikuambie mambo machache kuhusu mapatano.


1. Watu wawili au kundi hawawezi kufanya jambo likafanikiwa kama hawajapatana.


Amosi 3:3 "Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana?"


Sasa kama ni mtu ameingia katika mapatano mabaya ujue hayo mapatano yatatengeneza uharibifu.

Wako watu hupatana kufanya dhambi mfano ya uzinzi na baada ya hapo shetani anaingilia kati na hivyo kuwafunga vifungo vingi ambayo baadae watashindwa kuving'oa.


Kwa sababu kitu chochote kinachofanyika kati ya mtu na wengine au kati ya kundi la kundi, ili kitu hicho husika kifanikiwe basi lazima yawepo mapatano, sasa kama ni mapatano ya kishetani ujue hiyo ni hatari sana kwao.


Wapo watu walishapatana na shetani siku nyingi tu hivyo wewe unaweza kudhani ni watu wazuri kwako hivyo unaamua kupatana nao, kumbe ni njia ya wao kukupatanisha na shetani wanayemtumikia hivyo kuwa madhara makubwa kwako.

Ndugu, epuka sana mapatano mabaya ya namna yeyote.



 2. Ukipatana na watu wabaya katika kutenda mabaya unaweza kuachwa na MUNGU au MUNGU anaweza kuziharibu kazi zako.

Mfano hai ni Yehoshafati.


2  Nyakati 20:35-37 " Baada ya hayo Yehoshafati mfalme wa Yuda akapatana na Ahazia mfalme wa Israeli; naye huyo ndiye aliyefanya mabaya mno; akapatana naye kufanya merikebu za kuendea Tarshishi; wakazifanya merikebu zile huko Esion-geberi. Ndipo Eliezeri mwana wa Dodavahu wa Maresha akatoa unabii juu ya Yehoshafati, akasema, Kwa sababu umepatana na Ahazia, BWANA amezivunja-vunja kazi zako. Zikavunjika merikebu, zisiweze kufika Tarshishi."


Hata wewe, japokuwa wewe ni Mkristo na unaishi maisha matakatifu lakini MUNGU anaweza kukuacha au anaweza kuziharibu kazi zako kwa sababu tu umekubali kuingia katika mapatano na watu wabaya.

Hivyo ndugu uwe makini sana ili usiingie katika mapatano mabaya yeyote yanayoletwa kwako na watu wabaya.



 3. Unaweza ukaingia patano na baadhi ya watu na kumbe umeingia patano na kuzimu, maana hao ulioingia nao patano ni mawakala wa shetani.


Isaya 28:15 " Kwa sababu mmesema, Tumefanya agano na mauti, tumepatana na kuzimu; pigo lifurikalo litakapopita, halitatufikia sisi; kwa maana tumefanya maneno ya uongo kuwa kimbilio letu, tumejificha chini ya maneno yasiyo kweli;"


Unaweza ukafanya patano na watu kumbe umefanya agano na mauti.


Unaweza kuingia patano na watu na kumbe hapo unakaribisha mapigo kwako.


Unaweza ukaingia patano na watu na kumbe umeingia patano na kuzimu.

Ndugu, uwe makini sana sana ili tu usiingie patano na kuzimu.


Bwana YESU Mwokozi anakupenda sana na hataki kamwe uingie patano lolote na shetani ndio maana anaagiza ujumbe kama huu ukufikie wakati huu na sio wakati mwingine wowote, ndugu fanyia kazi ujumbe huu wa Neno la MUNGU na itakuwa heri kwako.

Usikubali kuingia agano lolote na mawakala wa shetani.



 4. Ukiingia patano la dhambi ni kwa uangamivu wako mwenyewe.


1 Wakorintho 6:9-10 " Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi."


Ndugu, mapatano yote yaliyo kinyume na MUNGU ni mapatano mabaya.

Mapatano ya dhambi yote huleta uangamivu.


Wako watu kwa sababu ya mapatano ya dhambi waliyoyafanya zamani  wamejikuta kwa sasa  wakiteseka, wakipata mapigo, wakifungwa vifungo vibaya na wengine wengi wamekufa katika dhambi hizo hivyo kukosa uzima wa milele.

Ndugu, uwe makini sana na usikubali kuingia patano lolote la dhambi.


Je umeingia patano na mtu ili kumuua mtu  au kuzini?


Je umepatana na nani ili kuharibu kazi ya MUNGU?


Je  umepatana na nani ili kuiba au kutapeli?


Je umepatana na akina nani ili watu wengine wapate madhara?


Ndugu, kama uko katika mapatano mabaya jiondoe  Leo katika hayo mapatano mabaya.

Kama unapanga kuingia patano la kishetani nakuomb

a sana usiingie katika patano hilo.

Kama uliingizwa katika patano baya jiondoe leo, tubu mbele za MUNGU katika KRISTO YESU na usikubali tena kuingia katika mapatano mabaya.

MUNGU akubariki Sana ukizingatia ujumbe.

By Peter Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la MUNGU.

+255714252292

Comments