MAOMBI YA KUIFUNGA MILANGO YA KIPEPO NA KUIFUNGUA MILANGO YA KI MUNGU KWENYE MAISHA YAKO.

    

Na Mwl Peter Mabula


Shalom Mteule wa KRISTO upendwae sana na MUNGU Baba.

Karibu tujifunze kisha tuombe maombi muhimu sana.


Siku moja kwenye ndoto niliona  mlango wa uzinzi umefunguliwa  kwa watu wa kazi fulani kwenye kituo chao cha kazi.


Mtu mmoja mwajiriwa katika ile kazi alikuwa ameokoka na kwenye ndoto hiyo niliambiwa nimwambie aombe maombi ya kufunga mlango ule wa uzinzi uliokuwa umefunguliwa na shetani kwao.


 Kwenye ndoto hiyo niliona wanaume na wanawake wakifanya uzinzi na mbele yao  niliona ziwa la moto liko karibu sana nao, na kadri walivyokuwa wanaendelea kuzini ndivyo ziwa la moto lilikuwa linawasogelea sana. Yule Mteule wa KRISTO aliyekuwa ameokoka katika hicho kituo cha kazi yao nikamwambia aombe ili kuufunga ule Mlango wa uzinzi ambao shetani alikuwa ameufungua kwao. baada ya maombi ule Mlango ulijifunga katika eneo lao la kazi. Yule ndugu aliomba na yeye aliishinda ile dhambi maana alikuja kunithibitishia kwamba katika eneo lao la kazi ni jambo la kawaida sana uzinzi kufanyika, tena hata waume za watu na wake za watu  uzinzi ni jambo la kawaida sana na hata yeye mawazo ya kujumuika na wenzake yalikuwa yanamujia ila baada ya ufunuo akakaa sawa kwa MUNGU.


Kwa siku kazaa nilikuwa naomba juu ya milango na nilijifunza mambo mengi juu ya Milango.


Katika Biblia niliona ni MUNGU alizungumza kwa mara ya kwanza  kuhusu Milango pale alipomwambia Kaini kuwa dhambi iko Mlangoni inamuotea. Maana yake Kaini alikuwa amefungua mlango wa dhambi kwa matendo yake.


Mwanzo 4:7 '' Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.''


Baada ya Kaini kuonywa na MUNGU juu ya mlango wa dhambi ambao Kaini aliufungua, ndipo tunaona Kaini akimwambia ndugu yake Habili waende uwandani na huko Kaini kwa sababu hakuufunga Mlango ule basi tunaona akimwua ndugu yake.


Kuna mambo mabaya yakimpata mtu  utasikia watu wa MUNGU wanasema ''Kuna mlango ameufungua ndio maana hayo yamempata'' Wakati mwingine hayo ni kweli kabisa kuna mlango ameufungua huyo ndugu ndio maana yamempata.


Adui akitaka kumdhuru mtu katika nyumba hupitia Mlangoni, ukilala umeufungua mlango wa nyumba yako katika eneo lenye wanyama wakali au wezi hakika adui anaweza kuingia hapo na kukudhuru.


Ukweli ni kwamba ili baraka ije kwako ni lazima Mlango wako wa baraka hiyo uwe umefunguliwa kwako ili hiyo baraka ipate kukufikia.


Wafunguaji wa mlango wa baraka yako wanaweza kuwa ni;


✓✓ MUNGU anaweza kuufunga mlango wako wa baraka Kama utaliasi Neno lake, hutatembea kwenye Kanuni za Neno lake au kwa Sababu ya dhambi zako.


Kwa maombi yako na kukaa kwenye utakatifu na kuliishi kusudi la MUNGU na kumtolea MUNGU zaka na sadaka kwa usahihi na upendo, MUNGU atafungua milango ya baraka kwako.


Kumb 28:8 ''BWANA ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako.''


MUNGU anapoiamuru baraka fulani ije kwako hufungua mlango wa baraka hiyo kuja kwako. Ona Mfano hapa ambapo MUNGU aliamuru baraka ya chakula cha mbinguni ishuke kwa wana wa Israeli. Biblia inasema


Zaburi 78:23-25 '' Lakini aliyaamuru mawingu juu; Akaifungua milango ya mbinguni; Akawanyeshea mana ili wale; Akawapa nafaka ya mbinguni. Mwanadamu akala chakula cha mashujaa; Aliwapelekea chakula cha kuwashibisha.''


MUNGU anaweza kufungua mlango wa baraka fulani kwako, mtii tu na msikilize ROHO MTAKATIFU.


✓✓ Wewe mwenyewe unaweza kuufunga mlango wa baraka yako.


Kwa Sababu makosa yako mbele za MUNGU na ukaidi wako wakuzipinga Kanuni za MUNGU.


Lakini kujitambua kwako kiroho, kuomba, kuzijua haki zako kwa MUNGU, maisha matakatifu na ya haki na kubaki katika Eneo ambalo MUNGU amekufungulia mlango wa baraka yako kutafungua mlango kwako.


 Mwanzo 22:17-18 '' katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote na dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.''


Ibrahimu kama mwanadamu alipomtii MUNGU alibarikiwa, kwa sababu milango ya baraka ilifunguliwa kwake. Milango ya baraka ambayo adui walikuwa wameikalia MUNGU alisema uzao wa Ibrahimu utaimiliki hiyo milango ambayo adui walikuwa wameichukua.


Hata wewe adui zako wanaweza kuifunga milango yako ya baraka, adui zako wanaweza kuichukua milango yako ya baraka. Kazi yako ni kumtii MUNGU sasa na kumcha yeye pekee, Kuishi maisha matakatifu ya Wokovu na kuomba katika KRISTO YESU ili uimiliki tena hiyo Milango ambayo adui zako waliichukua.


✓✓ Wazazi wako wanaweza kuifunga milango ya baraka zako.


Kwa malezi mabaya wanauokulea Wazazi wako wanaweza kuifunga milango ya baraka zako.


Lakini Wazazi wako wanaweza kukufungulia mlango wako wa baraka kwa malezi yao, kukusomesha na kukufundisha jinsi ya kumtegemea MUNGU.


✓✓Watumishi wa MUNGU wanaweza kuifunga milango ya baraka zako.


Kama watumishi watakufundisha kinyume na kweli ya MUNGU katika KRISTO YESU watakuwa wanakupotosha na kukukosanisha na MUNGU hivyo milango ya baraka zako kufungwa.


Lakini Watumishi wa MUNGU wanaweza kukufungulia mlango wako wa baraka kwa kukufundisha Neno la MUNGU la kweli na kukufunulia kanuni za MUNGU za kukufanya mlango wako wa baraka ufunguke na Kukuombea.


Kumbuka pia Mabaya yakija kwako ni kwa sababu kuna mlango umefunguliwa kwako hata hayo mabaya yakaja kwako.


Wafunguaji wa mlango wa mabaya kwako ni;


✓✓ MUNGU.


Kwa sababu ya uovu wako MUNGU anaweza akaruhusu mlango wa mabaya kufunguka kwako ili kukufanya utubu na kuacha mabaya hayo.


Ukisoma Kitabu cha waamuzi utaona jinsi ambavyo waisraeli walivyokuwa wanamwasi MUNGU na MUNGU anafungua mlango wa waisraeli kuwa watumwa kwa miaka kadhaa, wakitubu MUNGU anawaondoa maadui zao.


✓✓ Shetani.


Shetani anaweza kukufungulia mlango wa mabaya kwa sababu ya wewe kukosa ulinzi wa MUNGU.


 Anaweza kukufungulia mlango huo kwa sababu huombi na anaweza kukufungulia mlango huo kwa sababu huzijui ahadi za MUNGU kwako na hulitendei kazi vyema Neno la MUNGU. Kazi ya shetani ni kuhakikisha wewe hufanikiwi na wewe unakuwa mtu wa kulia kila siku. 


✓✓Kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi, Maombi katika jina la YESU,utoaji sahihi, utakatifu na wewe kumskiliza ROHO MTAKATIFU hakika shetani atafungua milango ya mabaya lakini haitafunguka na wala hayo aliyokusudia hayatakupata maana utakuwa sasa unalindwa na damu ya YESU KRISTO.


✓✓ Wewe mwenyewe.


Wewe mwenyewe unaweza ukafungua mlango wa mabaya kwako kwa sababu dhambi zako hata ulinzi wa MUNGU juu ya baraka zako unaondoka. 


Wewe unaweza ukaufungua mlango wa mabaya kwa sababu humtii ROHO MTAKATIFU. 


Mlango wako wa mabaya unaweza ukafunguka kwa sababu hukai kwenye kusudi la MUNGU na wala huombi.


 ✓✓Watu wanaweza kuufungua Mlango wa mabaya kwako kwa sababu ya kukunenea mabaya


 Watu wanaweza kuufungua Mlango wa mabaya kwako kwa sababu ya kukunenea mabaya huku wewe hukimbilii kwa YESU hata mabaya hayo yasikupate.


Kinywa kinaumba hivyo kama watu wanakunenea mabaya na wewe huna uhusiano mzuri na MUNGU hakika yanaweza kukupata hayo mabaya maana wamekufungulia mlango wa hayo.


Mithali 18:20-21 ''Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake. Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.'' 


Kumbe kwenye kinywa kunaweza kutoka uzima na kwenye kinywa pia kunaweza kutoka mauti. Mauti ni vitu vibaya vyote, Mtu anaweza kujinenea mabaya na hayo maneno yake yakafungua mlango wa mabaya lakini pia watu wanaweza kumnenea mabaya na mlango wa mabaya ukafunguliwa kwake.


✓✓ Jina lako.


Jina lako kama litaambatana na maagano ya kipepo hakika huo ni mlango wa mabaya yako.


Jina lako ndio utambulisho wako popote, jina lako kama limembeba shetani huo ni mlango wa mabaya kwako, ni muhimu sana kuombewa maombi ya kulitakasa jina lako.


Kumbuka Mithali 16:25 '' Mtu asiyefaa kitu huchimba shimo la madhara; Katika midomo yake mna moto uteketezao.''


 Walipokuwa wanakupa jina walitamka nini?


 walikuchimbia shimo gani kupitia jina lako walilokupa?


Walibebesha jina lako nini cha madhara?


Nimewahi kuandaa masomo kuhusu jina na huko nilifafanua sana lakini ni muhimu sana kujua kwamba jina lako linaweza kuwa mlango wa mabaya kuja kwako.


 ✓✓Madaraka yako au nafasi yako kwa jamii.


Mlango wa mabaya kufunguliwa kwa mtu kunaweza kuja kwa sababu na madaraka yake au nafasi yake.


Mabaya kumpata mtu sio umasikini tu bali hata jehanamu ni mabaya makubwa zaidi.


  Mithali 16:20 ''Atakayelitafakari neno atapata mema; Na kila amwaminiye BWANA ana heri.''


Mtu mwenye madaraka, madaraka yake humtenga na baadhi ya watu ambao wangemsaidia kiroho,  kumjulisha Neno la MUNGU na mpango wa MUNGU ili atengeneze njia zake. 


Mwenye mali huamini mali zake na sio MUNGU na huo kuwa mlango wa mabaya kwake.


Mwenye madaraka makubwa huyaamini madaraka yake makubwa na sio kumwamini MUNGU.


Mfano kumuona tajiri mkubwa ili umwambie kwamba ampokee YESU ni kazi ngumu maana kila muda yuko busy, hukutana na watu wa hadhi yake tu, hata ukienda kwake kuna ulinzi kuanzia geti la kwanza hadi geti la kuingia ndani na hairuhusiwi kumuona.


Kiongozi ili umuone labda utume maombi na hayo yanaweza kukubaliwa na kukataliwa, nafasi yake ile kwa sababu mlango wa jehanamu ulikuwa umefunguliwa kwake tangu zamani basi ni neema ya MUNGU watumishi kumsaidia kiroho ili mlango ule wa ziwa la moto ufungwe na sasa ufunguliwe mlango wa uzima wa milele kupitia YESU KRISTO na utakatifu.


 ✓✓Kutegemea akili zako.


 Akili za mwanadamu zina mwisho.


Akili za mwanadamu bila kumtegemea MUNGU huwa hazifiki popote.


Yeremia 17:5-8 ''BWANA asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha BWANA. Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda.''


Akili zako zinaweza kukufanya ujitegemee wewe bila MUNGU na huo ukawa mlango wa mabaya kuja kwako.


 Kila kitu ili kije kutoka kwenye ulimwengu wa roho kuja ulimwengu wa mwili lazima kifunguliwe mlango.


✓✓Maombi ya kuifunga milango ya kishetani iliyofunguliwa kwetu ni ya muhimu sana kuyaomba.


✓✓Maombi ya kumsihi MUNGU ili afungue milango ya baraka zetu ni ya muhimu sana kuyaomba. Baraka huwakilisha vitu vingi sana.


Kuna baraka za kiafya, kuna baraka za kiuchumi, kuna baraka za familia na uzao.


Ngoja nikupe maandiko haya kuhusu milango naamini utaelewa umuhimu wa kuombea milango ya kiroho.


✓✓Mlango wa tumbo la uzao kwa mtu  ukifungwa haiwezekani kuzaa.


Ayubu 3:10 '' Kwa sababu haukuifunga milango ya tumbo la mamangu. Wala kunifichia taabu machoni.''


Kuna milango ya tumbo la uzao, hiyo inaweza kufungwa kipepo na pia kwa maombi inaweza kufunguliwa hata mtu asiyeweza kuzaa akazaa.


✓✓Milango ilifunguliwa kwa mfalme Koreshi ili atimize kusudi la MUNGU na kubarikiwa.


Isaya 45:1-3 ''Haya ndiyo BWANA amwambiayo Koreshi, masihi wake,ambaye nimemshika mkono wake wa kuume,ili kutiisha mataifa mbele yake,name nitalegeza viuno vya wafalme;ili kufungua milango mbele yake,hata malango hayatafungwa. Nitakwenda mbele yako, na kupasawazisha mahali palipoparuza; nitavunja vipande vipande milango ya shaba, na kukata-kata mapingo ya chuma; nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni BWANA, nikuitaye kwa jina lako, naam, MUNGU wa Israeli.''


Koreshi alipata neema ya MUNGU kwa kufunguliwa milango ya kuwashinda wafalme wengine katika vita, mlango ulipofunguliwa alitiisha mataifa.


Alipata hazina za gizani yaani ni baraka ambazo zilikuwa zimefichwa, lakini milango ya kiroho ilipofunguka alipewa hazina za gizani.


Baraka zilizokuwa zimefichwa mahali pa siri ziliibuliwa baada ya mlango kufunguliwa.


MUNGU alitukuzwa.


Hata wewe inawezekana kabisa unataka kulitimiza kusudi la MUNGU la kuokolewa kwako na Bwana YESU ila milango bado imefungwa.


Inawezekana kabisa kuna baraka zako zimefichwa na hata hujui ziliko.


Inawezekana kabisa mlango wako wa baraka za kiroho umefungwa na wachawi au waganga ndio maana kila ukijaribu kwa akili zako hufanikiwi.


Ndugu yangu naomba utambue kwamba Bwana YESU anaweza kukushindia sasa.


Ni muda wako wa kuishi maisha matakatifu katika KRISTO na kisha omba sasa ukiifungua milango ya baraka zako iliyokuwa imefungwa.


✓✓ Dhambi hufungua mlango wa jehanamu lakini utakatifu katika KRISTO hufungua mlango wa uzima wa milele.


Mathayo 7:13-14 '' Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.'' 


Inawezekana mlango wa uzima wa milele umefunguliwa kwako lakini hata huuoni kwa sababu hutaki kuokoka.


Inawezekana kabisa wewe unaona mlango mpana tu ambao ndio wa jehanamu.


Kama vitu vyote hupita mlangoni basi hata wewe utapita Mlangoni kwenda ama mbinguni ama jehanamu.


Ndugu ufunge mlango wa jehanamu kwa kumpokea YESU na kuanza kuishi maisha matakataifu katika yeye. Anza kumtii MUNGU na Neno lake, Mtii ROHO MTAKATIFU na anza kuliishi Neno la MUNGU.


✓✓Kanisa la MUNGU duniani limefunguliwa milango ambayo shetani hawezi kulishinda, labda tu kanisa lilale.


Mathayo 16:18 Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.'' 


Kumbe huwa kuna milango ya kuzimu.


Ndugu ifunge milango yote ya kuzimu iliyofunguliwa katika maisha yako.


Wewe ni Kanisa na milango ya kuzimu haitakiwi kukushinda.


Magonjwa hutokea milango ya kuzimu, ajali na balaa zote hutokea milango ya kuzimu, Ifunge leo milango yote ya kuzimu, ifunge kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO Mfalme wako wa uzima wako.


✓✓YESU KRISTO ndio mlango uliofunguliwa kupita watakatifu, ukimtii yeye na Neno lake hakika wewe kwenu ni mbinguni na sio kuzimu. Ukimtii YESU na kuomba hakika milango yote ya kipepo itajifunga na sasa wewe utapata malisho mema kwa YESU.


Yeye Bwana YESU anasema  ''Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho.-Yohana 10:9 ''


✓✓Watu wasio wayahudi walifunguliwa mlango wa imani ya wokovu.


Matendo 14:27 '' Hata walipofika wakalikutanisha kanisa, wakawaeleza mambo yote aliyoyafanya Mungu pamoja nao, na ya kwamba amewafungulia Mataifa mlango wa imani.''


 Hata ndugu  zako mlango wa imani ya Wokovu wa KRISTO umeshafunguliwa kwao, kazi yako ni kuwapelekea injili tu, usiwaogope ila nenda kawahubirie.


✓✓MUNGU anaweza akakufungulia Mlango wa kuhubiri injili na huduma hata wanaokupinga wasifanikiwe.


1 Kor 16:9 '' kwa maana nimefunguliwa mlango mkubwa wa kufaa sana, na wako wengi wanipingao. ''


✓✓Wakati mwingine unaweza kupitia katika majaribu mbalimbali lakini MUNGU anaweza pia kukufungulia mlango wa wewe kutoka katika majaribu hayo.


1 Kor 10:13 ''Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila MUNGU ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.''


Muombe MUNGU akufungulie mlango wa kutoka katika majaribu hayo uliyonayo.


✓✓YESU KRISTO anaweza kukufungulia  mlango wa baraka au wa mafanikio katika huduma yako au kazi  na asiwze yeyote mwingine kuufunga mlango huo.


Ufunuo 3:8 '' Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu.''


Labda tu mlango huo uufunge wewe mwenyewe kwa kujitenga na imani.


✓✓Hata kulielewa nyema neno  la MUNGU  kunahitajika kufunguliwa mlango.


Wakolosai 4:3 '' mkituombea na sisi pia, kwamba Mungu atufungulie mlango kwa lile neno lake, tuinene siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake nimefungwa,''


Baada ya maelekezo hayo sasa najua umeelewa umuhimu wa milango katika ulimwengu wa roho.


✓✓✓Utajuaje kama MUNGU amekufungulia Mlango wa mafanikio?


1. Kwa kujulishwa na MUNGU kwa njia ya ndoto, kwa njia ya maono, kwa njia ya Neno la MUNGU,  kwa njia ya Mtumishi wa MUNGU kukujulisha na  kwa njia ya mazingira.


Mfano Yusufu aliota ndugu zake wakimwinamia na ndivyo ilikuja kuwa hivyo baadae baada ya MUNGU kumfungulia mlango wa kuiongoza Misri akiwa mtu wa pili kwa madaraka makubwa katika taifa.


 2. ROHO MTAKATIFU kukujulisha kwa njia ya kukupa msukumo na shauku juu ya jambo hilo ambalo umefunguliwa mlango wa baraka na MUNGU.


3. Wewe kuona kibali cha MUNGU  juu ya baraka hiyo.


4.  Mengine yote kuzuiliwa kwako ili  ulitendee kazi hilo.


Mfano MUNGU anaweza akakufungulia mlango wa kuipeleka injili na ili ufanye vyema mengine yote yanaweza yakazuiliwa ili utimize jambo hilo ambalo MUNGU amekufungulia mlango.


Mtu mmoja Zanzibar aliambiwa awe Mchungaji akawa Mchungaji lakini huku akiendelea na kazi za kuajiriwa, MUNGU alizuia kazi akaondolewa kwenye kazi yule Mchungaji. Baada ya hapo akawa kila akipata kazi anaachishwa hadi alipogundua kwamba MUNGU amemfungulia mlango kwenye kuipeleka injili, alipotii alifanikiwa sana.


MUNGU anaweza akakufungulia mlango wa wewe kumuoa dada fulani au wewe dada, MUNGU anaweza kukufungulia Mlango wa kuolewa na kaka fulani. MUNGU anachokifanya anaweza kuwaondoa kwake wale ambao sio sahihi ili wewe upate nafasi ya kufunga ndoa takatifu na mtu huyo sahihi kwako.


Yako mambo mengi sana ambayo MUNGU anaweza kuyazuia kwa mtu ili kwamba huyo mtu atendee kazi pale alipofunguliwa mlango na MUNGU. Changamoto ya watu wengi hutendea kazi kule ambako hawajafunguliwa mlango na ndio maana mipango yao ya kila mwaka wanayoipanga huwa haifanikiwi kwa sababu wanatendea kazi sehemu ambayo mlango wake wa kufanikiwa umefungwa.


5. Kupewa vitendea kazi vinavyohitajika kwenye baraka husika.


Mfano MUNGU amekufungulia mlango wa kuhubiri injili atakupa ujumbe unaohitajika , atakuinulia waombaji, atakupa muda. Hivyo ndivyo vitendea kazi ambavyo vinakujulisha kwamba umefunguliwa mlango wa kuipeleka injili.


Mfano mwingine MUNGU amekufungulia malngo ili wewe ufunge ndoa. MUNGU atakupa mtu husika kutoka kwake, atakuinulia watumishi wa kukusaidia na kukushauri ili ufanikiwe kufunga ndoa katika hali ya utakatifu.


Mfano MUNGU akikufungulia mlango katika uimbaji wa nyimbo za injili.


ROHO MTAKATIFU atakupa nyimbo na shauku ndani ya kutimiza huduma yako hiyo njema.


✓✓✓Utajuaje Mlango wa dhambi fulani umefunguliwa kwako?.


1. Utawaza dhambi hiyo hata kipindi ambacho hutaki kuiwaza.


2. Utatamani dhambi husika.


3. Kwa kufunuliwa na MUNGU kwa ndoto au maono au mazingira au ufunuo au Neno au kwa kujulishwa na watumishi wa MUNGU.


4.Kuota roho ya kiburi ndani yako inayokusukuma kutokutii Neno la MUNGU wala watumishi wa MUNGU.


 ✓✓✓Utajuaje kama mlango wa baraka fulani umefungwa kwako?


1. Kwa kujulishwa na MUNGU kwa njia ya ndoto, maono, Neno la MUNGU, watumishi wa MUNGU au mazingira.


2. Kila ukijaribu kuipata baraka hiyo unashindwa kuifikia.


Unaweza ukaiona baraka hiyo  kwenye ulimwengu wa roho lakini kuimiliki wewe kwenye ulimwengu wa mwili inashindikana.


3. Kukutana na vita kubwa sana ya shetani ikikuzuia juu ya baraka hiyo.


✓✓Utafanyaje ili Mlango wa baraka zako uliofungwa ufunguliwe?


1.  Tubu kwa MUNGU juu ya kilichosababisha mlango huo kufungwa.


2.  Muombe ROHO MTAKATIFU akujulishe namna ya kuombea


 jambo hilo ili mlango huo ufunguliwe kwako.


3. Omba maombi katika ROHO MTAKATIFU ya kuufungua mlango huo; Ukitumia jina la YESU KRISTO, Damu ya YESU KRISTO, Neno la KRISTO na nguvu za ROHO MTAKATIFU.


5.  Soma Neno la MUNGU na tafakari katika maeneo yanayowahusu watumishi wa MUNGU waliopitia hayo yaliyo kama yako ndani ya Biblia na wakashinda.


6.  Uliza watumishi wa MUNGU waaminifu ili katika ROHO MTAKATIFU wakipata neema wakujulishe.


7. Funga na kuomba.


Maana kuna mengine huwezekana tu baada ya kufunga na kuomba.


Mathayo 17:21 ''[Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.] ''


 Ningeweza kusema mengi sana ila nafasi yangu kwa leo inaishia hapa.


Somo hili pia litakuwa kwenye kitabu kwa


ufafanuzi zaidi wa kimaandiko,  ukiguswa kunisaidia katika kufanikisha kuchapisha vitabu unaweza kunitumia Pesa yako kwa namba yangu ya simu ambayo hiyo iko chini ya kila somo langu na kwenye Blog yangu na kwenye page yangu ya facebook ambayo ni +255714252292, pia unaweza kiwasiliana nami hasa WhatsApp inbox.


Maombi haya chini naomba yamsaidie muombaji mchanga katika kuliendea hitaji lake. Kwa waombaji wazoezi naamini baada tu ya kujifunza somo wanajua wataombea mambo gani katika habari za milango ya kiroho. Pia somo hili unaweza ukawa unalipitia mara kwa mara ili nikusaidie kugundua kitu kingine cha kuombea kwa habari ya milango. Maombi yangu kwa Bwana YESU naamini kila mmoja ataenda kuvuka baada ya kuuzingatia ujumbe huu wote wa leo.


  MAOMBI YA KUFUNGA MILANGO YA KIPEPO NA KUFUNGUA MILANGO YA KIMUNGU KWENYE MAISHA YAKO.   


YAHWEH MUNGU wangu uliye hai milele, nakutukuza na nakuhimidi MUNGU wangu.


Asante kwa siku ya leo ambayo umenipa kuiishi na kuomba kwako maombi ya  ushindi.


Katika jina la YESU KRISTO ninafunga milango yote aliyoifungua shetani na mawakala zake kwenye maisha yangu, Ninaifunga milango hiyo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.


Ninaifunga milango ya magonjwa iliyofunguliwa kwangu, naufunga kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.


Ninaifunga milango ya mikosi iliyofunguliwa kwangu, Naifunga kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.


Naifunga milango ya kuonewa, naifunga kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.


Naifunga milango yote ya kuonewa na majini na wachawi, Naifunga kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.


Kila mlango wa mapepo uliofunguliwa kwenye maisha yangu, ninaufunga kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.


Hakuna jini atakayefungua mlango kwenye maisha yangu, hakuna mchawi wala mganga atakayefungua mlango katika maisha yangu.


Milango yote mibaya ambayo wanadamu wameifungua katika maisha yangu kwa vinywa vyao, Ninaifunga milango hiyo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.


Milango niliyoifunga kwa jina la YESU KRISTO hakuna wakala wa shetani ataifungua tena.


Aliyekuwa amefunga milango yangu ya mafanikio na baraka,  naifungua  Milango hiyo sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.


Milango ya baraka yangu ya kuoa/Kuolewa,


naifungua  Milango hiyo sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.


Milango ya kufanikiwa kwangu kazi,  naifungua  Milango hiyo sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.


Milango yangu ya kufanikiwa katika biashara yangu,  naifungua  Milango hiyo sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.


Milango yangu ya uzao wangu, naifungua  Milango hiyo sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.


Milango ya kufanikiwa katika masomo, naifungua  Milango hiyo sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.


Milango ya tumbo la uzao wangu, naifungua  Milango hiyo sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.


Milango ya ufahamu mzuri, naifungua  Milango hiyo sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.


Milango ya huduma yangu, naifungua  Milango hiyo sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.


Milango yamgu ya kumiliki na kutawala katika ulimwengu wa roho,naifungua  Milango hiyo sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.


 Asante MUNGU BABA maana umenishindia.


Katika jina la YESU KRISTO hakuna atakayeifunga milango yangu ya baraka.


Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea ushindi.


Amen Amen Amen.

 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.

Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.

Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.

Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.

By Peter Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

+255714252292.

Ubarikiwe

Comments