SIFA NZURI ZA MTU MZEE KIBIBLIA

 

Na Mwl Peter Mabula, Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe.
Karibu kujifunza Neno la MUNGU.

Tito 2:1-2 " Lakini wewe nena mambo yapasayo mafundisho yenye uzima; ya kwamba wazee wawe wenye kiasi, wastahivu, wenye busara, wazima katika imani na katika upendo na katika saburi."

Ukisoma maandiko haya unaona sifa 6 Biblia inazungumza Mtu Mzee kiumri  anatakiwa kuwa nazo.

✓✓Hivyo Wewe uliyemzee kwa umri hakikisha una sifa hizo ambazo Biblia inasema zinatokana na  mafundisho ya uzima.

✓✓Hivyo Wewe ambaye unatarajia kuwa Mzee zizingatie sifa hizi.

✓✓Wewe ambaye sio mtoto Sasa ni Mtu mzima zingatia sifa hizi ambazo wazee walio na YESU KRISTO wanatakiwa wawe nazo.

Sifa ziwapasao wazee watakatifu ni hizi


1. Awe na Kiasi.

Kiasi ni nini?
Kiasi  ni   uwezo wa kudhibiti jambo au tendo ili lisipitilize mipaka yake.

Mtu Mzee ni muhimu sana kuwa mtu wa kiasi na  kuhakikisha Mambo yote yanafanywa kwa mipaka.

Warumi 12:3 "Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na NIA YA KIASI, kama MUNGU alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani."

Mfano Kama huna kiasi unaweza kujikuta unamuonya mtoto wako aliyekosea lakini kwa Sababu huna kiasi huishi tu kumuonya bali na kumlaani unamlaani.
 
2. Awe Mstahivu 


Mtu Mstahivu ni Mtu mwenye heshima anayeweza kuvumilia hata vitu vigumu.

Mstahivu ni Mtu mwenye ushupavu wa moyo na mtu mwenye subiri.

1 Timotheo 3:4 "mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika USTAHIVU;"

3. Awe mwenye busara.

Busara ni nini?
Busara ni Maarifa ya kumwezesha Mtu kuamua na kutenda mambo yanayofaa.

Mithali 2:11 "Busara itakulinda; Ufahamu utakuhifadhi."

Ni vizuri sana Mzee kuwa na Busara.

4. Awe Mtu mzima katika Imani.

Tunayo Imani Moja ya waenda Mbinguni, ni Imani katika Wokovu wa Bwana wetu YESU KRISTO.
 
Yuda 1:3 "Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu."

Mzee inampasa kuwa mzima kiimani.
1 Wakorintho 13:11 "Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto."

Mzee ana watu wengi chini yake, akiwa mzima kiimani atawasaidia na Watoto wake na Wajukuu zake wasichukuliwe na Imani za mashetani Bali wabaki katika Moja pekee ya kuwapeleka watu Uzima wa milele ambayo ni Imani ya kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi na kuokoka.

5. Mwenye upendo.

Upendo ni pamoja na kuwapenda wengine, usiwe na uchungu nao.
Upendo ni pamoja na kuwaombea wengine, kuwaonya na kuwashauri ili waishi kwenye kusudi la MUNGU la Wokovu.

1 Wakorintho 16:14 "Mambo yenu yote na yatendeke katika upendo."

6. Akikaa kwenye Saburi

Neno Saburi lina maana ya uvumilivu.

2 Wakorintho 6:6 "katika kuwa safi, katika elimu, katika uvumilivu, katika utu wema, katika ROHO MTAKATIFU, katika upendo usio unafiki;"

Mzee inampasa kuwa mvumilivu.
MUNGU akubariki Wewe Mzee kiumri.
MUNGU akubariki Wewe Mzee ajaye, zingatia Neno la KRISTO na utaitwa heri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU KRISTO Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU KRISTO Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.
+255714252292(Whatsapp, Sadaka ya kuipeleka Injili, Ushauri na Maombezi)
Ubarikiwe


Comments