BINTI YANGU UNAPOIKARIBIA NDOA. (Day 1)

 


Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu atukuzwe.

Huu ni mfululizo wa masomo kuhusu Binti ambaye anaratajia kufunga Ndoa takatifu katika Maisha yake.


Inawezekana Binti huyu ana mchumba au hana mchumba ila atapata mchumba kwa Jina la YESU KRISTO na masomo haya yanamhusu.

Wazazi pia mnaweza kujifunza kwa ajili ya Watoto wenu.


◾Ndoa ni nini?


Ndoa ni taasisi ambayo ni MUNGU aliianzisha ili Mwanaume mmoja na Mwanamke mmoja wawe Mume na Mke.


Marko 10:6 "Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke."


✔️Ndoa ni taasisi ambayo MUNGU aliianzisha ili Mwanaume asiye na Mke aoane na Mwanamke asiye na Mume ili Sasa hawa Wanadamu wawili wawe Mwili mmoja ambao ni Ndoa takatifu.


Ndoa ni taasisi Muhimu sana ambayo Ina matokeo ya miaka mingi, hivyo ndoa inatakiwa iheshimiwe sana 


Waebrania 13:4 "Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi MUNGU atawahukumia adhabu."


Ndoa inatakiwa iheshimiwe sana na akina nani?


✔️✔️Ndoa inatakiwa iheshimiwe na Watu wote.


Watu hawa ni watu Gani ambao MUNGU Baba anataka Waiheshimu Ndoa?


1. Wanandoa wenyewe wanatakiwa Waiheshimu Ndoa Yao.


2. Wazazi pande zote mbili wanatakiwa Waiheshimu Ndoa ya Watoto wao, Wasiiingilie wala kuivuruga kwa lolote.


3. Ndugu pande zote mbili wanatakiwa Waiheshimu Ndoa hiyo.


4. Watu wa Kanisa wanatakiwa Waiheshimu Ndoa hiyo.


Ndoa inatakiwa iheshimiwe sana maana ndio msingi wa kizazi.

Mfano hai Ibrahimu na Sarah ndio mwanzo au msingi wa taifa la Israeli.

Ndoa hii ya Ibrahimu MUNGU hakuruhusu Mtu yeyote aingilie maana kama Mtu angeiingilia lisingetokea taifa la Israeli.


Ona mfano wa huyu Abimeleki alipotaka kuiingilia Ndoa hii ya Ibrahimu.


Mwanzo 20:2-4 " Ibrahimu akamnena Sara mkewe, Huyu ni ndugu yangu. Basi Abimeleki mfalme wa Gerari akapeleka watu akamtwaa Sara. Lakini MUNGU akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu. Basi Abimeleki alikuwa hakumkaribia, akasema, Ee BWANA, Je! Utaua hata taifa lenye haki?"


MUNGU aliadhibu familia hii kwa sababu Baba wa familia alitaka kuingilia ndoa ya Ibrahimu aliyetakiwa kuleta Taifa la Israeli.


Mwanzo 20:17-18 " Ibrahimu akamwomba MUNGU, MUNGU akamponya Abimeleki, na mkewe, na wajakazi wake, nao wakazaa wana. Maana BWANA alikuwa ameyafunga matumbo ya watu wa nyumbani mwa Abimeleki, wasizae, kwa ajili ya Sara mkewe Ibrahimu."


✔️✔️Ndoa yako Binti yangu unayoiendea unaweza kuwa chanzo Cha jamii ya Wacha MUNGU wanaomwamini YESU KRISTO siku zote. Maana ukienda kuzaa katika Ndoa yako, ukawafundisha Watoto wako kumcha MUNGU na wao baadae wakafundisha Watoto wao baada ya miaka 70 Wewe utakuwa umetengeneza ukoo mkubwa au jamii kubwa ya Wacha MUNGU wanaookolewa na Bwana YESU KRISTO Mwokozi.


Kumbu 4:10 "siku ile uliyosimama mbele za BWANA wako huko Horebu, BWANA aliponiambia, Nikusanyieni watu hawa, nami nitawasikizisha maneno yangu, ILI WAJIFUNZE KUNICHA MIMI SIKU ZOTE WATAKAZOISHI DUNIANI, WAKAPATE NA KUWAFUNDISHA WATOTO WAO."


◾Binti yangu umebeba uzao, inawezekana umebeba jamii kubwa, inawezekana umebeba Taifa.


✔️Je hiyo jamii uliyoibeba itakuwaje?


✔️Je hilo taifa ulilolibeba litakuwaje?


Jitunze, ishi katika Wokovu wa YESU KRISTO na yajue ya Kibiblia utakayotakiwa kuyafanya katika Ndoa yako na kwa uzao wako.


Baadhi ni haya

1. Uwe kielelezo chema kwa mema.


2 Timotheo 1:13 "Shika kielelezo cha maneno yenye uzima uliyoyasikia kwangu, katika imani na upendo ulio katika KRISTO YESU."


2. Ingia kwenye Ndoa ukiwa mtakatifu Yaani hujajichafua kwa uasherati na huyo Mchumba wako.


1 Wathesalonike 4:3-5 " Maana haya ndiyo mapenzi ya MUNGU, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati;  kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima; si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua MUNGU."


3. Jiandae kufundisha Watoto wako Wokovu wa Bwana YESU KRISTO.


Kumbu 6:7 "nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo."


4. Jiandae kuwafundisha Watoto wako kumtegemea MUNGU kwa Maombi.

Wazazi wengi huwafundisha Watoto wao kwenda kwa waganga maana wanawaona wazazi wakienda hiyo hupelekea Mtoto hata akiwa Mtu mzima badala ya kumtegemea Bwana YESU KRISTO yeye atategemea waganga na kuongeza unajisi kwenye kizazi Cha Mama yake.


Biblia inamkataza Mzazi kutoa wazao wake kwa moleki, moleki ni miungu.


 Walawi 18:21 "Nawe usitoe kizazi chako cho chote na kuwapisha kwa Moleki, wala usilinajisi jina la MUNGU wako; mimi ndimi BWANA."


Kwanini ulete kizazi kitakachokataliwa na MUNGU? Mfano ni kizazi Cha Israeli kipindi fulani walikataliwa na MUNGU.


2 Wafalme 17:20 "Basi BWANA akakikataa kizazi chote cha Israeli, akawatesa, na kuwatia katika mikono ya watu wenye kuwateka nyara, hata alipokwisha kuwatupa, watoke machoni pake."


Je ulete kizazi kitakachokataliwa na MUNGU?

Naomba usiwe Wewe, yajue haya kabla hujaingia kwenye Ndoa Binti yangu.


✔️✔️Wewe hakikisha unaleta kizazi kinachomtafuta MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.


Zaburi 24:6 "Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao, Wakutafutao uso wako, Ee MUNGU wa Yakobo."


✔️✔️Itakupasa kuwafundisha Watoto wako kumcha MUNGU.


✔️✔️Itakupasa kuwatolea sadaka Watoto wako na utawafundisha na wao kumtolea Sadaka MUNGU kwa ajili Yao na kwa ajili ya Watoto wao.

Naamini Binti yangu unaelewa.

Hii ni sehemu ya kwanza tu.

Sehemu ya pili itafuata ikiwa imebeba vitu vingine kabisa.

Na siku Moja mfululizo huu wa mafundisho kuhusu Binti anayetarajia ndoa takatifu nitayaweka kwenye Kitabu.

MUNGU akubariki sana 

By Mwl Peter Mabula

Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele.

+255714252292

Ubarikiwe

Comments