MAOMBI YA KUOMBA KUKUMBUKWA MBELE ZA MUNGU KWA AJILI YA HITAJI LAKO.

Na Mwl Peter Mabula



Bwana YESU KRISTO asifiwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU Kisha tuombe Maombi ya ushindi.

Ukisoma Isaya 43:26 MUNGU anasema tumkumbushe kwa kueleza mambo yetu ili tupate kupewa haki yetu.

Biblia inasema "Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako."

MUNGU anaposema tumkumbushe haina maana amesahau maana ukisoma Zaburi 112:6 Biblia inasema kwamba mbele za MUNGU mtu mwenye haki atakumbukwa milele, ukiwa mwenye haki katika KRISTO YESU hutasahaulika kamwe.

Lakini kwa habari ya Maombi MUNGU anataka tumkumbushe.

Unajua Kwanini MUNGU anataka tumkumbushe?
Baadhi ya sababu ni hizi

1. Inawezekana tulipoomba Mwanzo  tuliomba vibaya.

Yakobo 4:3 "Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu."
[8/15, 5:10 AM] Mwl Peter Mabula: 2. MUNGU anataka tujieleze kwa uhakika na usahihi maana inawezekana Mwanzo hatukujieleza kwa usahihi mbele zake.

Mfano inawezekana Wewe ni Mwanamke na uliomba hivi "MUNGU naomba uniinue katika ndoa yangu" 
Swali je akuinue ili umtawale Mumeo. Je akuinue ili mmeo afukuzwe kazi ili wewe umzidi mshahara? Maana ili uinuliwe Kuna njia nyingi.
Huo ni mfano mmoja tu ndio maana MUNGU wakati huu anataka umkumbushe kwa kujieleza vizuri ili ueleweke.

Huwezi kuomba Samaki harafu MUNGU akupe nyoka, jieleze tu kwa usahihi ili ijulikane kwamba unataka samaki na sio vinginevyo.

Mathayo 7:10-11 "Au akiomba samaki, atampa nyoka? Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana BABA yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?"

 3. Wanadamu hubadilika badilika nia, mitazamo, Imani n.k hivyo MUNGU anataka ajue hali yako ya Sasa juu ya hitaji lako kabla hajakupa.

4. Inawezekana hali yako ya kiroho wakati unaomba Mwanzo haikuwa nzuri kama Sasa Hali yako Iko vizuri hivyo mkumbushe MUNGU wakati huu anaenda kukutendea.

5. MUNGU anataka kuiona Imani yako maana wako watu baada ya kuomba akakaa muda kidogo akaona hajajibiwa kwa wakati aliotaka hudhani MUNGU hawakumbuki kumbe sio kweli.

Zaburi 31:12 "Nimesahauliwa kama mfu asiyekumbukwa; Nimekuwa kama chombo kilichovunjika."

Ndugu yangu, Mimi Peter Mabula nakushauri Wewe rafiki yangu kwamba unapokuwa katika Maombi ya kuomba kukumbukwa mbele za MUNGU kwa ajili ya mahitaji yako kumbuka pia kwamba MUNGU huwa anakumbuka nini hata akutendee mahitaji yako.

✔️Je MUNGU hukumbuka nini hata akutendee mahitaji yako?

Baadhi ya ambavyo MUNGU hukumbuka ni hivi

1. MUNGU hukumbuka rehema zake au huruma zake kama aliwahi kuzitamka kabla juu ya Mtu husika.

Mfano MUNGU alikumbuka huruma zake kwa Waisraeli kama alivyowaambia  Ibrahimu, Isaka na Yakobo juu ya wana wao  hivyo MUNGU akaamua kuwasaidia wana wao.

Luka 1:54-55 " Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; Ili kukumbuka rehema zake; Kama alivyowaambia baba zetu, Ibrahimu na uzao wake hata milele."

2. MUNGU hukumbuka Sadaka njema ambazo Mtu amewahi kutoa kwake.

Mfano hai ni huu Matendo  10:31 " akasema, Kornelio, kuomba kwako kumesikiwa, na sadaka zako zinakumbukwa mbele za MUNGU."

 3. MUNGU hukumbuka ahadi aliyowahi kuisema.

Mfano hai alimkumbuka Nuhu maana aliwahi kumwambia kabla kwamba Nuhu na wengine wenye uhai ndani ya Safina wataishi na kuwa Mwanzo mpya wa jamii ya viumbe hai Duniani.

Mwanzo 8:1 "Na MUNGU akamkumbuka Nuhu, na kila kilicho hai, na wanyama wote waliokuwamo pamoja naye katika safina; MUNGU akavumisha upepo juu ya nchi, maji yakapungua;"

4. MUNGU humkumbuka Mtumishi wake na kuwatendea mema wanaomhusu Mtumishi huyo.

Mfano hai MUNGU alimkumbuka Ibrahimu akamponya Lutu nduguye.

Mwanzo 19:29 "Ikawa MUNGU alipoiharibu miji ya Bondeni, MUNGU akamkumbuka Ibrahimu, akamtoa Lutu katika maangamizi alipoiangamiza miji hiyo aliyokaa Lutu."

5. MUNGU hukumbuka Maombi ambayo Mteule wake amewahi kuomba.

Mfano MUNGU alikumbuka Maombi ya Raheli na hitaji lake la uzao.

Mwanzo 30:22-23" MUNGU akamkumbuka Raheli; MUNGU akamsikia, akamfungua tumbo. Akapata mimba, akazaa mwana, akasema, MUNGU ameondoa aibu yangu."

6. MUNGU hukumbuka Agano au nadhiri 

Kutoka 2:24 "MUNGU akasikia kuugua kwao, MUNGU akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu na Isaka na Yakobo."

✔️Kama umewahi kufanya Agano na MUNGU hakika  MUNGU hukumbuka Agano na anaweza kukutendea.
Pia Kama umewahi kuweka nadhiri MUNGU hukumbuka nadhiri pia

 7. MUNGU hukumbuka uonevu ambao mtu amewahi kufanyiwa.

Zaburi 9:12 "Maana mlipiza kisasi cha damu awakumbuka, Hakukisahau kilio cha wanyonge."

Kama umewahi kuonewa uonevu mbaya, ipo siku MUNGU atatokea kukulipizia kisasi kwa adui zako.
Ila kama tu hukulipiza kisasi Wewe na uliachilia na kumkabidhi MUNGU teso lako.

Katika Maombi ufanyeje?

1. Tubia kilichosababishwa usikumbukwe na MUNGU kwa wakati.

Isaya 59:1-2 " Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia."

 2. Omba MUNGU akukumbuke ili ushinde vita dhidi ya nguvu za giza.

Hesabu 10:9 "Tena hapo mtakapokwenda kupiga vita katika nchi yenu, kupigana na adui awaoneaye ninyi, ndipo mtakapopiga sauti ya kugutusha kwa tarumbeta; nanyi mtakumbukwa mbele za BWANA, MUNGU wenu, nanyi mtaokolewa na adui zenu."

3. Msihi MUNGU akumbuke Agano kama ulifanya Agano naye.

Kutoka 6:5 "Na zaidi ya hayo, nimesikia kuugua kwao wana wa Israeli, ambao Wamisri wanawatumikisha, nami nimelikumbuka agano langu."

4. Kuna saa ya kukumbukwa mbele za MUNGU, mweleze akutendee Sasa na atakutendea.

Zaburi 115:12 "BWANA ametukumbuka, Naye atatubariki sisi. Ataubariki mlango wa Israeli, Ataubariki mlango wa Haruni,"

5. Msihi MUNGU akumbuke mema uliyotenda na umeendelea kutenda mema bila kuacha.
Mfano hai ni Hezekia katika Isaya alimkumbusha MUNGU.

Isaya 38:3 "akasema, Ee BWANA, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana."

Hapa chini ni  ya MAOMBI YA KUOMBA KUKUMBUKWA MBELE ZA MUNGU KWA AJILI YA HITAJI LAKO.

Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake.
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini.

MAOMBI YA KUOMBA KUKUMBUKWA MBELE ZA MUNGU KWA AJILI YA HITAJI LAKO.

Baba MUNGU ninakushukuru kwa neema yako na kwa kunilinda hata Sasa.

Nakushukuru kwa neema ya Wokovu wako kwa KRISTO YESU Bwana wangu.

Baba MUNGU niko tena mbele zako nikiomba Msamaha kwa mahali kokote nilikokosea mbele zako.
Naomba Baba wa Mbinguni unisamehe dhambi zangu zote, maovu yangu yote na makosa yangu yote.
Naomba Baba wa Mbinguni unisamehe pia kwa kosa langu lolote likilosababisha hukunijibu hitaji langu(litaje) kwa wakati.
Nakuomba Mfalme wa Mbinguni unisamehe dhambi hiyo pia.
Neno lako linasema katika Zaburi 32:1-2 kwamba  "Heri aliyesamehewa dhambi, Na kusitiriwa makosa yake. Heri BWANA asiyemhesabia upotovu, Ambaye rohoni mwake hamna hila." 
Nami MUNGU ninaomba unisamehe dhambi zangu zote maana ana heri mtu yule aliyesamehewa dhambi zake na Wewe kwa damu ya YESU KRISTO mwanao aliye hai.
Kile kilichonitenga Mimi na Wewe hata nisipokee baraka yangu kwa wakati naomba unisamehe na unipe Mwanzo mpya katika Wokovu wako.

Ee MUNGU Baba, wewe ulikumbuka Rehema zako ukawasaidia Waisraeli Watumishi wako kama ambavyo 
Luka 1:54  inasema kwamba " Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; Ili kukumbuka rehema zake; " nami nakusihi Baba yangu wa Mbinguni ukumbuke rehema zako unisaidie katika hitaji langu.
Nisaidie BWANA  ili nipate hitaji langu la uponyaji, Ndoa, uzao, Kazi na kibali.
Kumbuka rehema zao BWANA ili uniponye dhidi ya wachawi na waganga na dhidi ya wote wanaonionea.

Nakushukuru MUNGU maana wewe hukumbuka Sadaka, Neno lako katika  Matendo  10:31 linathibitisha pale Kornelio alipoambiwa "kuomba kwako kumesikiwa, na sadaka zako zinakumbukwa mbele za MUNGU."
Eee MUNGU ukumbukaye sadaka naomba ukumbuke sadaka zangu na unitendee sawasawa na uaminifu wangu.

Imeandikwa katika Mwanzo 30:22-23 kwamba " MUNGU akamkumbuka Raheli; MUNGU akamsikia, akamfungua tumbo. Akapata mimba, akazaa mwana, akasema, MUNGU ameondoa aibu yangu."

Eee Bwana MUNGU naomba nami Unikumbushe katika mahitaji yangu nami nipate kama Raheli alivyopata.

Nikumbuke MUNGU wangu nami nipate kazi nzuri katika jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai.

Nikumbuke MUNGU wangu nami nipate Ndoa takatifu kwa neema yako 

Nikumbuke MUNGU wangu nami nipate uponyaji katika mwili wangu.

Nikumbuke MUNGU wangu nami nipate mwenzi wa ndoa takatifu.

Nikumbuke MUNGU wangu nami nipate Watoto katika Ndoa yangu.

Nikumbuke MUNGU wangu nami nipate  kibali kazini ili nipandishwe cheo.

Nikumbuke MUNGU wangu nami nipate neema ya huduma yangu kukua na kuwafikia watu wengi zaidi kwa injili ya YESU KRISTO.

Najua hii ni saa yangu ya Kukumbukwa na MUNGU katika jina la YESU KRISTO.
Neno la MUNGU linasema katika Zaburi 115:12 kwamba  "BWANA ametukumbuka, Naye atatubariki sisi. Ataubariki mlango wa Israeli, Ataubariki mlango wa Haruni,"
Nakushukuru MUNGU wangu maana umenikumbuka na Sasa naenda kufanikiwa kwa Jina la YESU KRISTO.
Ninaamini BWANA Sasa ni saa yangu ya kujiliwa na Wewe kwa Baraka maradufu. Naamini Neno lako Bwana YESU KRISTO kama walivyoamini watu wako katika
 Kutoka 4:31 ambapo Neno lako linasema " Watu wakaamini, na waliposikia ya kuwa BWANA amewajilia wana wa Israeli, na ya kuwa ameyaona mateso yao, wakainama vichwa vyao wakasujudu."
Eee MUNGU nakushukuru sana na najua naenda kupokea kutoka kwako Muumba wangu.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea.
Amen Amen Amen.

MUNGU akubariki sana.
Omba sana na utamuona MUNGU wa Miujiza.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.
Amen

Comments