MAOMBI YA KUTUBIA KILICHOSABABISHA USITENDEWE NA MUNGU KWA WAKATI JUU YA HITAJI LAKO

 

Na Mwl Peter Mabula 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe.
Karibu tujifunze Kisha tuombe Maombi ya ushindi.

Ukisoma Isaya 59:1-3 Biblia inaonyesha kwamba MUNGU huwa hawi mbali watu wamwitapo kwa Maombi lakini dhambi na makosa ndio humfanya MUNGU awe mbali.
Biblia inasema " Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia. Kwa maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu, na vidole vyenu vimetiwa unajisi kwa uovu; midomo yenu imenena uongo, ndimi zenu zimenong'ona ubaya."

 ✔️Sasa inawezekana Wewe umewahi kumwita MUNGU kwa Maombi lakini hujatendewa na imefika hatua unadhani MUNGU amekusahau.

Ndugu inawezekana ni kweli umesahaulika kwa sababu hauna uhusiano Mzuri na MUNGU kwa wakati huu.

✔️Au ulipoomba ulikuwa Mtakatifu lakini baada ya hapo ukajitenga na MUNGU ndio maana MUNGU hakukutendea ulichoomba.

Biblia inakutaka ukumbuke ni wapi na wakati Gani ulivunja uhusiano wako na MUNGU katika KRISTO YESU, ukishakumbuka tubu na tenda mema aliyokueleza MUNGU.

Ufunuo  2:5 "Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu."

 ◾Inawezekana kabisa uliomba na MUNGU  baada ya miezi kadhaa au baada ya muda akamtuma Malaika akuletee baraka yako, Wakati Malaika siku anakuletea majibu yako akakukuta umejichafua Kiroho. Malaika anarudi Mbinguni na baraka yako maana alipoleta baraka hiyo hukuwa tayari kupokea. Baada ya muda wewe ukadhani MUNGU amekusahau wala hakukumbuki kumbe siku ulipomwacha na yeye alikuacha.

2 Mambo ya Nyakati 15:2 "........... BWANA yu pamoja nanyi, mkiwa pamoja naye; nanyi mkimtafuta ataonekana kwenu; lakini mkimwacha atawaacha ninyi."

 ✔️Unapomwacha YESU KRISTO kwa dhambi na kufuata manabii wa uongo ujue na yeye anakuacha, Wakati mwingine unapomwacha MUNGU yeye naye anaweza kukutendea mabaya badala ya kukutendea mema.

Yoshua 24:20 "Kama mkimwacha BWANA na kuitumikia miungu migeni, ndipo atageuka na kuwatenda mabaya na kuwaangamiza, baada ya kuwatendea mema."

✔️✔️Ndugu tubia kilichochelewesha baraka yako.
Mwambie Bwana YESU KRISTO akusamehe makosa yako yote, maovu yako yote na dhambi zako zote.

✔️Inawezekana unaomba MUNGU akupe mtoto katika ndoa yako, unafanya Maombi lakini baada ya hapo ROHO MTAKATIFU anakuambia Cha kufanya lakini hufuati hivyo baraka yako ya uzao inachelewa.
Ndugu, Leo omba ukitubia makosa yako yaliyopelekea baraka yako kuchelewa.

Mimi sijui unahitaji baraka Gani lakini tubia makosa yako yaliyochelewesha baraka hiyo

 ✔️Inawezekana unaombea Ndoa kwamba ufunge Ndoa lakini kabla MUNGU hajakujibu unazini hivyo kwa dhambi hiyo unaikimbiza baraka yako ya Ndoa.

✔️✔️Leo kwa Jina la YESU KRISTO tubia dhambi zako zote na maovu yako yote yaliyosababisha MUNGU akachelewa kukujibu.

Nini ufanye?

1. Kumbuka uliposikia Neno la kweli la MUNGU katika KRISTO YESU, tubu kwa kwenda kinyume na Neno la MUNGU.

Ufunuo 3:3 "Basi kumbuka jinsi ulivyopokea, na jinsi ulivyosikia; yashike hayo na kutubu. Walakini usipokesha, nitakuja kama mwivi, wala hutaijua saa nitakayokuja kwako."

2. Kumbuka kuyafanya maagizo ya MUNGU aliyokuagiza kabla.

Hesabu 15:40 " ili mpate kukumbuka na kuyafanya maagizo yangu yote, na kuwa watakatifu kwa MUNGU wenu."

3. Mkumbuke MUNGU siku zote ili akubariki na ili usimkosee.

Zekaria 10:9 "Nami nitawapanda kama mbegu kati ya mataifa; nao watanikumbuka katika nchi zilizo mbali; nao watakaa pamoja na watoto wao; tena watarudi."

MUNGU akubariki.
Omba Maombi ya toba juu ya kuchelewa kwa baraka yako ambaye umewahi kuiombea kwa MUNGU.
Omba katika jina la YESU KRISTO na MUNGU hatakutazama kwa hasira Tena  Bali atakutazama kwa huruma na kukutendea mahitaji yako.
MUNGU akubariki.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.
+255714242292
Ubarikiwe

Comments