MAOMBI YA KUWAPIGA NA KUWAFUKUZA WAKUU WA GIZA MAISHANI MWAKO.

Na Mtumishi Peter Mabula



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Katika siku Moja Mimi Peter Mabula nikiwa katika maombi ya mkesha Kanisani nilipata ufunuo ambao uliniamsha katika maombi. Ufunuo huo ulisema ''OMBA UKIHARIBU WAKUU WA GIZA''
Ghafla nilichangamka katika maombi hayo na kuanza kuomba nikiwatoboa macho yao yote wakuu wote wa giza wanaofuatilia huduma yangu, wakuu wa giza wote wanaofuatilia afya yangu, Ndoa yangu, uzao wangu, wakuu wa giza wote wanaofuatilia familia na ukoo wangu, wakuu wa giza wote wanaofuatilia uchumi wangu, na hakika nilichangamka katika kuwashambulia wakuu wote wa giza.

 ✔️Ukisoma maandiko Biblia inaonyesha kuna Wakuu wa giza.

Waefeso 6:12 ''Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.''

Ni muhimu sana kujua siri hii ya maombi inayotokana na neno la MUNGU.

Wakuu wa giza ni wale ambao hutuma nguvu za giza.

✔️Lakini pia Wakuu wa giza wengine wanashikilia anga ndio maana wanaitwa Wakuu wa anga sababu  wanashikilia anga.

Waefeso 2:2 "ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi;"

 ✔️Wakuu wengine wa giza wanashikilia eneo, ukoo, nchi n.k mfano ni huu mkuu wa giza anayeshilikia nchi nzima ya uajemi aliyekuwa anapambana na Malaika.

Danieli 10:20 "Ndipo akasema, Je! Unajua sababu hata nikakujia? Na sasa nitarudi ili nipigane na mkuu wa Uajemi; nami nitakapotoka huku, tazama, mkuu wa Uyunani atakuja."

◾Vipi kama vita yako wewe ya mafanikio kwenye eneo lolote unalohitaji kufanikiwa, vipi kama anayekuzuia ni mkuu wa giza wa eneo na Wewe unapambana tu na watu na ndio maana vita hujafanikiwa?

Nimekueleza hayo kwa upana kidogo ili ujue vita nyingine kushinda ni Hadi umshinde mkuu wa giza aliyeshikilia eneo husika.

Ndugu, Jina la mkuu wa giza wala lisikutishe kama wewe ni mtakatifu wa KRISTO unayejua kuzitumia silaha za MUNGU za Kiroho katika Maombi.

 Mara nyingi tumekuwa tukipambana na nguvu za giza zilizotumwa na wakuu wa giza na kuwaacha salama wakuu wa giza.

Unaweza ukapambana na jini aliyetumwa kwako lakini ukasahau kumwangamiza aliyemtuma jini huyo, aliyemtuma jini huyo anaitwa mkuu wa giza.

 Anaweza kuwa mwanadamu wakala wa shetani  au anaweza kuwa roho ya kuzimu iliyo na maroho mengine mengi ya kukusumbua. Mfano kama utapambana na jini aliyetumwa kwako ili kukuharibia ndoa na kwa maombi yako hakika ukamwangamiza huyo jini lakini baada ya muda anatumwa jini mwingine. unaweza kwa mwaka mzima ukawa unapambana na majini na hayaishi hata kama unayashinda kila siku, lakini ukimponda anayetuma majini hayo ndio mwisho wa vita yako. Pambana leo ili ushinde.

Ni ufunuo mpana sana na hakika siku hiyo napata ufunuo huu  nilishangaa sana.
Kama mchawi ndiye anayekusumbua  kwa kukutumia mapepo na wewe kila siku unapambana na mapepo  lakini anayeyatuma mapepo hayo kwako yuko salama maana hujamgusa. Anayetuma nguvu za giza kwako huyo ndio mkuu wa giza, pambana na huyo ndipo utashinda katika hiyo vita yako, kama utakuwa unapambana na waliotumwa tu basi wewe utaendelea na vita siku zote maana anayetuma nguvu hizo za giza anazo nyingi hivyo wewe utazipunguza tu na sio kuzimaliza, lakini ukipambana na anayetuma nguvu za giza hakika umeshinda na vita itakoma. Ndio maana Biblia inatushauri kupambana na wakuu wa pepo wabaya na kupambana na wakuu wa giza. ukimwangamiza mkuu wa giza hakika umeshinda maana anaowatuma hata hawatakuja maana kama mkuu wao umemuweza basi wao wataogopa na utaendelea kuwa mshindi daima.
Bwana YESU anasema ''Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili BABA atukuzwe ndani ya MWANA. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya. Yohana 14:13-14 ''

Kwa sababu jina la YESU KRISTO lipo leo na sisi waombaji tupo leo basi twende tukaombe. 

Lakini pia Wako watu wako katika mikataba ya kishetani inayowatesa sana.
Wako watu wako katika vifungo vya kishetani walivyoviingia wenyewe, hawavipendi ila wanaogopa kutoka katika vifungo hivyo kwa kuwaogopa wakuu wa giza.

Wako watu kwa kuogopa mashariti ya waganga wa kienyeji wameendelea kuwa watumwa wa nguvu za giza.

Wako watu kwa kuwaogopa majini waliowafunga vifungo, wameshindwa kujinasua katika kamba hizo za kuzimu.

Ndugu unatakiwa utoke katika mikataba hiyo ya kishetani, unatakiwa ufunguliwe kutoka vifungo vya giza. Anayeweza kukufungua na kukuweka huru kisha asiwepo mkuu wa giza wa kukudhuru, ni YESU KRISTO Mwokozi.
Bwana YESU ni Mwokozi maana yake anakuokoa, anakufungua na kukulinda dhidi ya waliokuwa wamekufunga.

 Labda ngoja nikupe siri hii ambayo labda ulikuwa huijui.

Siri yenyewe ni hii kwanini utoke katika mikataba ya kishetani?

1. Ili MUNGU katika KRISTO YESU sasa awe kiongozi wako.

2. Ili uwe huru.

3. Ili ujitenge na nguvu za Giza.

4. Ili uwe huna kifungo tena cha kipepo kilichokufunga .

Ndugu yangu, kanuni ni moja tu ukitaka kutoka katika mikataba ya kishetani kisha ubaki salama bila kufuatiliwa na mawakala wa shetani. Kanuni ni wewe kumkimbilia Bwana YESU Mwokozi ili akuokoe, acha dhambi na anza sasa kuishi maisha matakatifu ya Wokovu Kisha Maombi yako yatakuwa yenye ushindi mkuu.

Ni YESU tu anayeweza kukufungua mikataba ya kishetani yote iliyokufunga na kisha anakulinda kuanzia hapo.
Bwana YESU anasema na wewe sasa kupitia Neno lake akisema "Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.-Mathayo 11:28"

 Mambo yanayowafanya watu wengi wasitoke katika mikataba ya kishetani waliyoingia.
1. Kuchanganyikiwa.
2. Kuwa waoga.

3. Kufikiria kwamba milango ya giza iliyowafunga kwamba haiwezi kufunguliwa.

 Ndugu, Ukitaka kufunguliwa vifungo vya giza na mikataba ya kishetani kisha ubaki salama siku zote za maisha yako inakupasa sana uokolewa na YESU KRISTO na kuwa mtu wa Maombi ukiwa ndani ya Wokovu.

Ni kwa YESU tu ndio kwenye mikono salama baada ya kufunguliwa vifungo na mikataba ya giza.
Bwana YESU anasema "Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu. Mimi na Baba tu umoja.-Yohana 10:28-30
 
YESU akikufungua ndugu na atakulinda hivyo usiogope kukimbilia kanisani au kwenye mikutano ya injili kule anakohubiriwa YESU maana waliokutisha kwamba ukivunja mkataba watakuua, wakati huu ukiwa kwa YESU hakika MUNGU hatawaruhusu hata kukugusa.

Hapa chini ni  ya MAOMBI YA KUWAPIGA NA KUWAFUKUZA WAKUU WA GIZA.
Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake.
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini.


Anza na kutubu na kuokoka kama bado hujaokoka, kisha omba kwa imani katika jina la YESU KRISTO.

Maombi haya ni muhimu sana lakini pia maombi haya ni dira kwako ambaye ni mwombaji mchanga ili kukufundisha ili wewe ukaombe zaidi ya haya katika hitaji lako mwenyewe.

Maombi.

 BABA wa mbinguni pokea sifa milele.

 Asante BWANA maana fadhili zako ni za milele.

 Asante kwa kunilinda katika maisha yangu yote. Ninaishi kwa sababu JEHOVAH BWANA umeamuru niishi.

 nakutukuza mfalme wa Mbinguni kwa neema yako kwangu.

Asante Bwana YESU kwa ufunuo huu wa kunitaka mimi niwapige na  niwaharibu na KUWAFUKUZA maisha mwangu wakuu wote wa giza wanaonifuatilia.

Kwa jina la YESU KRISTO ninawafuata wakuu wote wa giza na kuwapofusha macho yao yote na kuanzia sasa hawataniona kamwe maana damu ya YESU inawaharibu sana.

Kila mkuu wa giza anayefuatilia ndoa yangu, ninamfukuza na  ninampofusha  macho yake yote  kwa jina la YESU KRISTO.

Kila mkuu wa giza anayemfuatilia mchumba wangu, ninampiga na kumfukuza na ninampofusha macho yake yote kwa  jina la YESU KRISTO.

Kila mkuu wa giza anayefuatilia afya yangu,ninampiga na kumfukuza na ninampofusha macho yake yote kwa  jina la YESU KRISTO.

Kila mkuu wa giza anayefuatilia biashara yangu,ninampiga na kumfukuza na ninampofusha macho yake yote kwa  jina la YESU KRISTO.

Kila mkuu wa giza anayefuatilia wazazi wangu, ninampiga na kumfukuza na ninampofusha macho yake yote kwa  jina la YESU KRISTO.

Kila mkuu wa giza anayefuatilia masomo yangu na ufahamu wangu, ninampiga na kumfukuza na ninampofusha macho yake yote kwa  jina la YESU KRISTO.

Kila mkuu wa giza anayefuatilia familia yangu na ukoo wangu,ninamtoboa macho yake yote  kwa jina la YESU KRISTO.

Kila mkuu wa giza anayefuatilia uchumi wangu,ninamtoboa macho yake yote kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.

Kila mkuu wa giza anayefuatilia kanisa letu,ninampiga na kumfukuza na ninampofusha macho yake yote kwa  jina la YESU KRISTO.

Kila mkuu wa giza anayeleta magonjwa na mikosi,ninamtoboa macho yake yote  kwa jina la YESU KRISTO.

Kila mkuu wa giza anayeleta roho ya kukataliwa,ninampiga na kumfukuza na ninampofusha macho yake yote kwa  jina la YESU KRISTO.

Kila mkuu wa kiza anayeleta balaa na majanga kwangu,ninampiga na kumfukuza na ninampofusha macho yake yote kwa  jina la YESU KRISTO.

Kila mkuu wa giza na kazi zake zote naziharibu na kuziangamiza kwa jina la YESU KRISTO.
Asante BWANA YESU maana umenipa ushindi leo.
Ninakutukuza mfalme wa mbinguni maana ushindi wangu umedhihilika leo.
Asante MUNGU uliye hai uliyekuja kunishindia,
Asante BABA wa mbinguni maana umewatuma malaika wako kunisaidia kushinda vita hii.
Ni katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea ushindi,.
Amen Amen.
MUNGU akubariki.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.

Omba ndugu na utamuona MUNGU wa Miujiza.
''Jioni, asubuhi, na adhuhuri nitalalama na kuugua, Naye(MUNGU) ataisikia sauti yangu.-Zanuri 55:17''

Comments