OMBEA FAHAMU ZAKO ILI ZIKUBALIANE NA WEMA WA MUNGU.

 

 
Na Mwl Peter Mabula


Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu atukuzwe ndugu zangu wote.
Katika safari yangu ya utumishi nimewahi kukutana na marafiki ambao walikuwa vizuri sana na MUNGU na nguvu za MUNGU zilikuwa ndani Yao lakini  baadae nikaambiwa wameacha Wokovu nilisikitika sana na kuumia sana moyoni.

Nilichogundua kwao shetani ndani ya mioyo yao alikuwa amefuta  kumbukumbu za Kukumbuka wema wa MUNGU.

 ✔️Biblia inamuonya Kila Mteule wa KRISTO kwamba asije akasahau mambo ambayo MUNGU amewahi kuyafanya.

Kumbu  4:9 "Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako;"

Inawezekana bado hujanielewa, ngoja niseme kwa mifano hali iliyowahi kutokea.

Dada mmoja ambaye tulikuwa tunaimba naye Kwaya Zanzibar na ambaye tulikuwa tunafanya nae huduma ya kuombea watu Kanisani. Dada huyu baada ya kuona amekaa muda mrefu  kama miaka 2 bila kupata Mchumba  akaamua kuacha Wokovu.
 Dada huyu alipokuwa ndani ya Wokovu alikuwa na nguvu za MUNGU lakini alipoacha Wokovu nguvu za MUNGU zikaondoka ndani yake akaanza kufuata wapinga KRISTO na  waganga wa kienyeji na kujikita  amedanganyika.  Baadae akajikuta amekuwa mwasherati na amebebeshwa mimba maana hakuwa na hofu ya MUNGU tena. Siku Moja akavamiwa na mapepo akaenda kwa mganga wa kienyeji na kufia huko, inasikitisha sana

 Ndugu zangu, wako watu wanalalamika kwamba MUNGU amewasahau na wanaacha Wokovu, ndugu nakuomba sana usiwe Wewe.

Watu wengi MUNGU amewahi kuwasaidia na kuwaokoa kwa mengi sana lakini baadae katika safari zao za maisha wanamwacha MUNGU. Hii ilitokea pia kwa Waisraeli kipindi fulani.

Waamuzi 8:34 "Kwani wana wa Israeli hawakumkumbuka BWANA, Mungu wao, ambaye ndiye aliyewaokoa na mikono ya adui zao wote pande zote;"

✔️✔️Ndugu, Leo ombea fahamu zako zikumbuke wema wa MUNGU ili ubaki kwenye kumtegemea MUNGU maana ndiye pekee anayeweza kukushindia.

Kumbu 7:18 "Usiwaogope; kumbuka sana BWANA, Mungu wako, alivyomfanya Farao na Misri yote;"

 Kwanini Leo unalalamika MUNGU amekusahau wakati wakati yapo mambo mengi ambaye MUNGU amekutendea?

 Ndugu kumbuka hata hayo ili umtukuze MUNGU na haya mahitaji ya Sasa atakutendea pia


✔️✔️MUNGU anawaambia watu wake wakumbuke wema wake.

Isaya 44:21 "Kumbuka haya, Ee Yakobo; nawe Israeli, maana wewe u mtumishi wangu; nimekuumba; u mtumishi wangu; Ee Israeli, hutasahauliwa na mimi."

Wako watu Bwana YESU KRISTO aliwashindia dhidi ya wachawi, roho za mauti, mapepo, mizimu na miungu. 
✔️MUNGU kama aliweza kutenda hayo makubwa atashindwa nini  kukuponya Sasa Wewe unayeumwa?

✔️Atashindwa nini kukupa mwenzi wa ndoa wewe unayehitaji Ndoa?

 ✔️YESU atashindwa nini kukubariki uzao wewe unayehitaji Mtoto katika ndoa yako? Kama aliweza kumpa uzao Sarah Mzee sana wa miaka 90 atashindwa nini kukupa Mtoto Wewe ambaye hata miaka 50 hujafikisha?
Napenda kukuambia kwamba akina Hannah na Elizabeth walizaa wakiwa na umri mkubwa kuliko Wewe na inawezekana walizaa wakiwa na umri mkubwa kuliko hata umri wa Mama yako Mzazi.

Hebu ndugu mkumbuke MUNGU na Miujiza yake.
Ombea fahamu zako kama umefika hatua huoni wema wa MUNGU ingawa wema wa MUNGU upo.

Ndugu, unakumbuka YESU alikokutoa?

Kumbu 24:22 "Nawe kumbuka ya kuwa ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri; kwa hiyo nakuamuru kutenda neno hili."

 ◾Ulikuwa mtumwa YESU akakuandika huru.
Ulikuwa husameheki lakini kwa damu yake ya Agano jipya na kwa upendo wake akakusamehe, mbona unaanza kusahau wema wake.

Kuna watu Hadi Bwana YESU KRISTO awatazame  kama alivyomtazama Petro ndipo watakumbuka.

Luka 22:61 "Bwana(YESU) akageuka akamtazama Petro. Petro akalikumbuka lile neno la Bwana jinsi alivyomwambia, Leo kabla hajawika jogoo utanikana mara tatu."

Nini ukumbuke?

1. Kumbuka njia aliyokuongoza MUNGU kwenye ushindi kabla

Kumbu 8:2 "Nawe utaikumbuka njia ile yote BWANA, Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo."

 2. Kumbuka kabla ulikuwa kwa shetani kabla YESU KRISTO hajakuokoa na kukuandika jina lako kwenye Kitabu Cha Uzima Mbinguni 

Kumbu 15:15 "Nawe kumbuka kwamba ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, akakukomboa BWANA, Mungu wako; kwa hiyo mimi nakuamuru neno hili hivi leo."

Nini ufanye katika Maombi 

1. Katika Maombi ombea fahamu zako ili zikumbuke Matendo ya MUNGU.

Zaburi 77:11 "Nitayakumbuka matendo ya BWANA; Naam, nitayakumbuka maajabu yako ya kale."

2. Katika Maombi yako kataa hofu na ruhusu ufahamu wako kuona Yale Matendo makuu ambayo MUNGU amewahi kuwatenda mawakala wa shetani hata hawakukuonea.

Kumbu 7:18 "Usiwaogope; kumbuka sana BWANA, Mungu wako, alivyomfanya Farao na Misri yote;"

3. Ombea fahamu zako zimkumbuke YESU KRISTO siku zote ili ubaki upande wake siku zote za maisha yako.

Zekaria 10:9 "Nami nitawapanda kama mbegu kati ya mataifa; nao watanikumbuka katika nchi zilizo mbali; nao watakaa pamoja na watoto wao; tena watarudi."

Omba ndugu yangu.
Omba katika jina la YESU KRISTO.
Ombea fahamu zako ili ziwe daima zinaona wema wa MUNGU.
MUNGU akubariki.
By Mwl Peter Mabula
+255714252292
Ubarikiwe

Comments