BINTI YANGU UNAPOIKARIBIA NDOA(Sehemu ya 2)

 

Na Mwl Peter Mabula 


Bwana YESU KRISTO asifiwe.
Tunaendelea na ujumbe wetu uitwao BINTI YANGU UNAPOIKARIBIA NDOA.
Ujumbe huu ni maalumu kwa ajili ya Wanawake wanaotarajia kuingia kwenye Ndoa.

Baada ya kupitia hatua 4 za kwanza Sasa tunaingia hatua ya 5

5. Ndoa takatifu wakati wa kuifunga.

Ndoa takatifu ni tukio ambalo hadi Mbinguni linajukikana.
Mfano hai ni huu ambapo Mwanaume mmoja alimuoa Binti mmoja.

Kutoka 2:1 "Mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaondoka akaoa binti mmoja wa Lawi."

MUNGU alikuwa anashughulika na Ndoa hiyo ndio maana mmoja wa Watoto kutoka katika ndoa hiyo alilindwa na MUNGU hata katika mazingira magumu sana yaa baada tu ya kuzailiwa, MUNGU alikuwa na kusudi na Mtoto aliyetoka katika Ndoa hiyo, miaka kadhaa baadae MUNGU kupitia Malaika  akamtokea Mtoto huyu na kumtumia kuwatoa Waisraeli kutoka Utumwani Misri.

Kutoka 3:2 "Malaika wa BWANA akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea."

Nini nataka kusema kwako Binti yangu?
Inawezekana kabisa umebeba uzao watakaokuwa Watumishi au watu ambao MUNGU atataka awatumie kwa kusudi lake, uwe na uhakika MUNGU anaitazama Ndoa yake unayoenda kuingia, hakikisha unaiingia Ndoa yako kwa utakatifu ili iwe Ndoa takatifu kabisa na iambatane na baraka za MUNGU zinazoiendea Ndoa takatifu.

Binti yangu, vumilia  bila uasherati hadi baada ya kufunga ndoa.

Msaide mchumba wako ili awe na uvumilivu ili msikutane kimwili hadi baada ya kufunga ndoa takatifu.

✓✓Ili muingie kwenye ndoa yeye kibali cha MUNGU na Baraka za MUNGU ni muhimu sana tendo la ndoa liwe ndani ya ndoa tu.

Kwenye kufunga ndoa akili yako isiwaze tu shera na namna utakavyopendeza bali akili yako iwaze utakatifu na namna unatamani ndoa yako iwe

Ni siku yako ya kipekee kwa hiyo furahi na kama kuna mambo mema mengi  siku hiyo ya kuyafanya yafanye kwa utukufu wa MUNGU.
Mimi nilipofunga ndoa na mke wangu Jemmimah baada ya kufunga ndoa jumamosi, jumapili tulienda kwa Mchungaji nyumbani kwake kupeleka sadaka nzuri ya shukrani kwa MUNGU ametupa neema ya kufunga Ndoa takatifu, hapo ilikuwa ni Mwanza sehemu ambayo tulifungia ndoa. Tuliporudi Dar es salaamu Kanisani tunakoabudu tulitoa tena Sadaka nzuri ya shukrani kwa MUNGU kwa kutuwezesha kufunga Ndoa takatifu

MAMBO YA BINTI KUMSAIDIA KIJANA ILI WASIKUTANE KIMWILI KABLA YA NDOA.

1. Uwe na akili .

1 Petro 4:7 "Lakini mwisho wa mambo yote umekaribia; basi, iweni na akili, mkeshe katika sala."

Unapogundua tu mnakoelekea ni kwenye dhambi unatumia mbinu zote kukwepa kukutana kimwili.
Amua kuikimbia zinaa wakati huo ili kusababisha mwingie kwenye ndoa na mavazi machafu kiroho.
1 Wakorintho 6:18 "Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe."

2. Uwe mtu wa maombi na mshauri mchumba wako pia.

Wafilipi 4:6 "Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na MUNGU."

Maombi yana kazi nyingi, kazi mojawapo ni kuiitisha mwili ,hivyo hamtafanya  uasherati mkiwa watu wa maombi na mnaotumia akili.

3. Umtembelee mchumba wako kamwe kwenye chumba chake.

Hiyo itamsaidia kuondoa fikra za uasherati

4. Usikubali mkae gizani wawili tu wewe na mchumba wako.


Hiyo itawasaidia kuepuka uasherati

5 .  Chagueni sehemu ya wazi wakati mnapopanga kuwa na mazungumzo 
Mfano kanisani, yaani kwenye viwanja vya kanisa

SIKU YA KUFUNGA NDOA UWE MAKINI NA HAYA.

Nina shuhuda za baadhi ya watu katika utumishi wangu kwa kristo kwa miaka zaidi ya14, ni baadhi ya shuhuda kwa baadhi ya watu , sio kwamba na kwako itakuwa hivi ila kuna maadui kwenye ulimwengu wa roho kazi yao ni kukufanyia mabaya kwenye hatima yako njema.

Mfano hai ni farao na jeshi lake walipotaka kuwazuia Waisraeli kuifikia  hatima yao ya kuvuka bahari ya shamu ili wawe wametoka nje ya mipaka ya Misri tayari kuingia nchi ya ahadi.

Kutoka 14:5-7 " Mfalme wa Misri aliambiwa ya kuwa wale watu wamekwisha kimbia; na moyo wa Farao, na mioyo ya watumishi wake, iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni nini jambo hili tulilotenda, kwa kuwaacha Waisraeli waende zao wasitutumikie tena? Akaandalia gari lake, akawachukua watu wake pamoja naye; tena akatwaa magari mia sita yaliyochaguliwa, na magari yote ya Wamisri, na maakida juu ya magari hayo yote."

Farao alitaka kuwazuia katika baraka Yao hata katika siku ya Mwisho ya kuvuka bahari ya shamu.

Jifunze shuhuda hizi ili ikufanye uombee sana matukio ya siku yako ya kufunga ndoa ili mawakala wa shetani wasikuzuilie.
 
Binti mmoja alipopata mchumba na ikatangazwa kwamba miezi michache ijayo atafunga ndoa, kuna wamama wawili viongozi Kanisani waliumia sana tukio hilo kwa sababu wao wana mabinti wakubwa wa kuwazaa hawajapata wachumba lakini Binti wa umri mdogo tu miezi michache ijayo anaenda kufunga ndoa , walifanya kila mbinu mbaya na hata kwenda  kwa waganga ili tu ndoa hiyo isifanyike na hata ikifanyika basi siku ya ndoa binti aanguke Kanisani au ukumbini au afe ghafla.

Unajifunza nini? 
✓✓Sio wote wanafurahia wewe unaenda kufunga ndoa.
Ombea sana siku hiyo Malaika wa MUNGU watande kila eneo la Kanisani kuhakikisha mambo yote yanaenda vizuri, shida kama nyie wachumba ni waasherati, malaika wa MUNGU watakujaje?
Somo litaendelea.
Na siku Moja mfululizo huu wa mafundisho kuhusu Binti anayetarajia ndoa takatifu nitayaweka kwenye Kitabu.
MUNGU akubariki sana 
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele.
+255714252292

Comments