DHAMBI YA KUTOKUMWAMINI YESU KRISTO KAMA MWOKOZI INAWEZA KUMPELEKA MTU JEHANAMU.

 

Na Mwl Peter Mabula, Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai 


Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.

Karibu nikujuze maneno ya uzima.


Dhambi ni mbaya sana.

✓✓Ni dhambi pekee inayoweza kusababisha mwanadamu asiende uzima wa milele.


✓✓Dhambi haina haya, ukiiruhusu inakuangamiza


✓✓MUNGU anawapenda watu wanaoshinda dhambi kila iitwapo leo.


✓✓Dhambi zote ni mbaya na hazifai, na dhambi ya kwanza ni kumkataa YESU kama Mwokozi.


 Hivyo kuna mtu anaweza akajiona hana dhambi lakini kumkataa YESU KRISTO kama Mwokozi ni dhambi tosha inayoweza kumkosesha mtu uzima wa milele.


Biblia inasema juu ya hilo kwamba;

''Amwaminiye yeye(YESU) hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU .-Yohana 3:18''


Kwanini Biblia inasema kwamba amwaminiye YESU KRISTO kama mkombozi wake hahukumiwi?


Je wote wanaosema wanamwamini YESU, ni kweli wanamwamini?


Nini maana ya Kumawmini YESU?


Je kila anayesema anamwamini YESU ni kweli anamwamini kama Biblia inavyoagiza?


Kumwamini YESU sio jambo dogo kama baadhi ya watu wanavyodhani.


✓✓Kumwamini Bwana YESU kuna maana Saba(7) ambazo huyo anayemwamini lazima azitii zote na kuziishi zote, sio moja wala mbili wala tatu bali zote, ndipo utakuwa umetimiza kumwamini YESU KRISTO aliye hai milele..


MAANA SABA ZA KUMWAMINI YESU KRISTO.


1. Kumpokea YESU KRISTO  kama Bwana na Mwokozi wako, na Kumkiri Kama Mwokozi wako wa milele.


Warumi 10:9-11,13 ''Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika.  kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la BWANA ataokoka.''


2. Kumtegemea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na atakayekupeleka uzima wa milele.


1 Yohana 5:11-12 '' Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba MUNGU alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa MUNGU hana huo uzima.''


3. Kumtii YESU KRISTO. 


Yohana 1:12-13 ''  Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU. ''


4. Kutii Neno lake ambalo ni Biblia.


Matendo 4:12 ''Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. ''


✓✓Kutii Neno la KRISTO ni pamoja na kuacha dhambi zote.


5. Kumfuata YESU KRISTO.


Marko  8:34 "Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu yeyote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate" 


6. Kutenda mema yanayoagizwa na Neno la MUNGU.


Waefeso 2:10 '' Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika KRISTO YESU , tutende matendo mema, ambayo tokea awali MUNGU aliyatengeneza ili tuenende nayo. ''


✓✓Mema ni pamoja na kumwabudu MUNGU katika Roho na kweli.


✓✓Mema ni pamoja na Kumpokea ROHO MTAKATIFU na kukubali kuongozwa na yeye daima.


✓✓Mema ni pamoja na kumtumikia MUNGU.


✓✓Mema ni pamoja na kuwa mwaminifu kumtolea MUNGU fungu la kumi na sadaka njema.


✓✓Mema ni pamoja na kujifunza Neno la MUNGU na kulitafakari.


7. Kumwamini maana yeye ni njia ya uzima anayeweza Yote.


Yohana 14:6-7,23 ''YESU akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa BABA, ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na BABA; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. YESU akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na BABA yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. ''


✓✓Kumpokea YESU KRISTO ndio mwanzo wa kuabudu katika kweli ya MUNGU.


✓✓Kumwamini YESU KRISTO ni kuishinda dhambi mbaya mno ambayo imewapeleka wengi jehanamu.


Kama humwamini YESU hakika hawezi kukuokoa na asipokuokoa huwezi kuingia uzima wa milele, maana pasipo YESU hakuna uzima wa milele.


Yohana 14:6-7 '' YESU  akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa BABA , ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na BABA ; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona.''


Ni dhambi kutokumwamini YESU kama mwokozi wako, na dhambi hiyo hata ukitenda mema yote duniani  lakini kwa kosa la hiyo dhambi moja huwezi kuingia uzima wa milele.


''Yeye amwaminiye Mwana wa MUNGU(YESU) anao huo ushuhuda ndani yake. Asiyemwamini MUNGU amemfanya kuwa mwongo, kwa kuwa hakuuamini huo ushuhuda ambao MUNGU amemshuhudia Mwanawe(YESU).Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba MUNGU alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana(YESU), anao huo uzima; asiye naye Mwana wa MUNGU(YESU) hana huo uzima.Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa MUNGU.-1 Yohana 5:10-13 ''


Amwaminiye YESU kwa kufuata mambo  saba hapo juu, huyo anao uzima wa milele.

Usipomwamini YESU kama Mwokozi wako hakika unamfanya MUNGU kuwa muongo na kwa kosa hilo huwezi kuingia uzima wa milele Ndio maana MUNGU kwa neema yake anawatuma watumishi wake kila iitwapo leo ili wahubiri injili ya KRISTO iiokoayo.


Injili ni habari njema za ufalme wa MUNGU zilizo katika KRISTO YESU tu.


Marko 16:15-16 ''Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.''


✓✓Kumbe ni jambo la lazima kwa kila mwanadamu kumwamini YESU KRISTO ili mwanadamu huyo apate uzima wa milele.


YESU anasema kama unamwamini kwa kufuata hizo maana saba za kumwamini hakika hata ukifa leo utaenda mbinguni hivyo utakuwa unaishi kabisa ukiwa na mwili mpya ukiwa mbinguni na watakatifu wengine.


Yohana 11:25 '' YESU  akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi;naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo? ''


Tunaitwa waaminio kwa sababu tunamwamini YESU KRISTO.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.

Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.

Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.

Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.

By Mwl Peter  Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO.

+255714252292.

Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Share kwa marafiki zako somo hili.

Comments