HAKIKISHA UNATAWALA KINYWA CHAKO.

 

Na Mwl Peter Mabula, Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.

Karibu tujifunze Neno la MUNGU.


Mithali 10:19-20 '' Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili. Ulimi wa mwenye haki ni kama fedha teule; Moyo wa mtu mbaya haufai kitu. ''


Maandiko haya hapo juu yanaonyesha, Kadri Mtu Anavyosema Maneno Mengi, Ndivyo Alivyo Katika Hatari Ya Kufanya Dhambi.


Kwanini?


Ni Kwa Sababu Ataongea Mambo Mazuri Yataisha Na Yeye Anaendelea Kuongea Na Kujikuta Akiongea Yasiyotakiwa.


Vinywa vina madhara makubwa kama hatutavilinda na kuvitiisha kwa damu ya YESU KRISTO. 


MUNGU anaonya kuhusu matumizi mabaya ya kinywa,BWANA anasema '' Amsingiziaye jirani yake kwa siri, Huyo nitamharibu. Mwenye macho ya kiburi na moyo wa majivuno, Huyo sitavumilia naye.Macho yangu yatawaelekea waaminifu katika nchi, Hao wakae nami. Yeye aendaye katika njia kamilifu, Ndiye atakayenitumikia.-Zaburi 101:5-6 ''


●Ni vizuri watu wa MUNGU kuwa na kiasi katika mazungumzo.


●Ni vizuri watu wa MUNGU kujitenga na mazungumzo mabaya.


●Ni heri ndugu usijinajisi kwa kushabikia mambo mabaya katika maongezi.


Ndugu, Muombe MUNGU ili akupe kiasi katika maongezi, akuwekee mlinzi katika kinywa chako ili usiseme uongo na mabaya.


 Zaburi 141:3 '' Ee BWANA, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu. ''


Mfano Mnaweza Kuwa Mnaongea Kuhusu Uzuri Wa Tanzania Lakini Points Kuhusu Tanzania Zikiisha Mtajikuta Mnaanza Kumsengenya Mtu Atakayepita Mbele Yenu Hapo Mlipokaa, Hiyo Ni Dhambi.


MUNGU anataka tuwe wenye hekima katika mazungumzo na katika mambo yote. 


Mithali 16:23 ''Moyo wake mwenye hekima hufundisha kinywa chake; Huzidisha elimu ya midomo yake. ''


Biblia Inakushauri Kuutawala Mdomo Wako.


Kuna watu akianza tu kuongea mbele za watu utaona baadhi ya watu wanaondoka. Ni kwasabbu akianza kuongea mtu huyo huwa hamalizi na huwa hawapi nafasi wenzake kuongea na zaidi sana akianza kuongea yeye huongea pumba tu.


Ndugu , Kama wewe ni mcha MUNGU harafu una tabia hizo maana yake hujazuia kinywa chako, kinywa kimekuwa chanzo cha kujinajisi kwako.


Mithali 17:27-28 '' Azuiaye maneno yake ni mwenye maarifa; Na mwenye roho ya utulivu ana busara. Hata mpumbavu akinyamaza, huhesabiwa hekima; Akifumba midomo yake, huhesabiwa ufahamu.''.


Heri kuzuia kinywa chako kwa baadhi ya mambo maana utaonekana una akili.


Ni muhimu kukitiisha kinywa chako.


Kataa ushabiki na kukuza mambo ambayo ni hatari na hutakiwi kabisa kuyanena, mambo ambayo wala sio ya MUNGU bali uzushi wa kidunia.


 Mithali 26:20 ''Moto hufa kwa kukosa kuni; Na bila mchongezi fitina hukoma. ''


Kuna watu huwa hawawezi kujizuia katika baadhi ya vitu, ataongea tu hata kama hatakiwi kuongea kwa wakati jambo hilo.


Yakobo 1:19 '' Hayo mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika; ''.


Biblia inatutaka tusiwe wepesi wa kuongea.


Uongeaji sana katika mambo ambayo hata huna ufahamu nayo na wala hayahusu Wokovu sana unaweza kujinajisi. 


Mfano unakuta watu wakimjadili mwanasiasa fulani kwamba ni mwizi na katika maongezi hayo mnaweza kujikuza mkiongea ambayo hata sio ya kweli na wala hamjathibitisha kama ni kweli au sio kweli. 


Mithali 10:18 '' Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo, Na yeye asingiziaye ni mpumbavu. ''


Ndugu zangu, ni vizuri kuongelea jambo ambalo unalifahamu kwa kina, hata ukiulizwa swali unaweza ukajibu, sio kujadili jambo ambalo hulijui hata kidogo, Kwa wanaojua jambo hilo utaonekana muongo na usiyejua lolote. na Kama umeokoka watu wataanza hata kutukana Wokovu wako , kumbe ulitakiwa kujizuia. 


Biblia inawaonya wateule wa KRISTO katika hilo ikisema '' Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti. Kwa huo twamhimidi MUNGU BABA yetu, na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa MUNGU. Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo. - Yakobo 3:8-10 ''.


Unakuta mtu ameokoka lakini kinywa chake hakijaokoka maana hakawii kuwaita watoto wake mbwa.


Ameokoka lakini ni mwanasiasa muongo anayedanganya kila kukicha.


 Biblia inasema haifai kuwa hivyo.


Umeokoka lakini kwa sababu wewe ni Mchungaji hukawii kuwalaani washirika kwa sababu tu ya wanajadili jinsi unavyolazimisha mambo ambayo hata Biblia inakupinga. 


Biblia inasema haifai kuwa hivyo. 2 Kor 12:20 '' Maana nachelea, nisije nikawakuta si kama vile nitakavyo kuwakuta, nikaonekana kwenu si kama vile mtakavyo; nisije nikakuta labda fitina na wivu, na ghadhabu, na ugomvi, na masingizio, na manong'onezo, na majivuno, na ghasia; ''


Ni Rahisi Kusema Upuuzi Kama Ukiongea Masaa Mengi, Utazidisha Chumvi, Mara Nusu Ukweli Nusu Uongo.


Yakobo 3:5-6 "Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana. Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum."


Sio Vizuri Kuyafurahia Mazungumzo Mabaya


 Mithali 18,8 '' Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo; Nayo hushukia pande za ndani za tumbo."


Kueneza Uvumi, Au Kuwasingizia Wengine Ni Vibaya.


Zaburi 31:13 ''Maana nimesikia masingizio ya wengi; Hofu ziko pande zote. Waliposhauriana juu yangu, Walifanya hila wauondoe uhai wangu. ''.


Tena Biblia inaendelea kutuonya '' Umekaa na kumsengenya ndugu yako, Na mwana wa mama yako umemsingizia. Zaburi 50:20''


●Kutokujidhibiti kinywa na moyo hupelekea kusengenya watu, masengenyo ni dhambi.


Katika kizazi hili Biblia inasema kuna mambo mengi mabaya yanayofanywa na wanadamu, katika hayo mabaya kinywa ni injini ya mabaya hayo ''Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao-Warumi. 1:29-30''


●Usipoweka moyoni mwako neno la MUNGU hakika utaliweka  neno la shetani. 


neno la shetani halitakiwi katika maisha yao. bali wena neno la MUNGU lenye uzima.


Maneno Ya Upuuzi Huleta Utata.


Mithali 26:28 '' Ulimi unenao uongo huwachukia wale uliowajeruhi; Na kinywa cha kujipendekeza hutenda uharibifu."


Hayo Ni Machukizo.


Ndugu usikubali kumhukumu ndugu yangu, usimsingizie maana neno la MUNGU linakataza, litii Neno la MUNGU ndugu.


Yakobo 4:11-12 '' Ndugu, msisingiziane; amsingiziaye ndugu yake, au kumhukumu ndugu yake, huisingizia sheria na kuihukumu sheria. Lakini ukiihukumu sheria, huwi mtenda sheria, bali umekuwa hakimu. Mtoa sheria na mwenye kuhukumu ni mmoja tu, ndiye awezaye kuokoa na kuangamiza. U nani wewe umhukumuye mtu mwingine? ''


-Ndugu, Hukumu mwachie Bwana YESU KRISTO pekee, usimhukumu mtu bali muonye kama anakosea pasipo mashindano.


MUNGU Anaonya.


1 Petro 2:1-3 '' Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote. Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu; ikiwa mmeonja ya kwamba BWANA ni mwenye fadhili. ''


Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine na kama hujampokea Bwana YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO Bwana. 

MUNGU akubariki sana .

By Peter Mabula. 

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi. 

+255714252292(Whatsapp, Ushauri, Maombezi, Sadaka n k)

Ubarikiwe

Comments