KIBALI.

Na Mwl Peter Mabula 

 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.

Karibu kujifunza Neno la MUNGU.

Kwa ufupi leo nazungumzia kibali.

Kibali ni nini?

●Kibali ni kitu cha kiroho unachokipata ili kukufanya ukubalike.

●Kibali ni idhini anayopata mtu ili kupata vitu fulani avitakavyo.

●Kibali ni kukubaliwa kufanya jambo jema unalolitaka kulifanya.

●Kibali ni ruhusa inayovisukuma nje vizuizi vyote.

●Kibali ni ridhaa ya kutenda unachotaka kutenda.

Mwanzo 39:21-22 " Lakini BWANA akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza. Mkuu wa gereza akawatia mkononi mwa Yusufu watu wote waliofungwa, waliomo gerezani; na yote yaliyofanyika humo ndiye aliyeyafanya."

Kibali ni kitu cha thamani sana kuwa nacho.

■Kibali cha Yusufu kilimfanya awe bosi wa wafungwa wote na kila kitu walifanya kwa maelekezo yake, yaani alikuwa kama sio mfungwa.

Kwani Yusufu awe kiongozi na sio wale wengine?

Jibu ni kwamba Yusufu alikuwa na kibali, ukiwa na kibali katika jambo fulani hakika hutatumia nguvu nyingi katika mambo yakipasacho kibali chako kufanya kazi.

■Musa alikuwa na kibali Misri kiasi ambacho alikuwa mweshimiwa hadi mbele ya watawala ambao ni Wamisri.

Kutoka 11:3 "BWANA akawapa watu hao kibali machoni pa Wamisri. Zaidi ya hayo, huyo Musa alikuwa ni mkuu sana katika nchi ya Misri, machoni pa watumishi wa Farao, na machoni pa watu wake."

Sasa nisikilize kwa maandishi haya itakusaidia.

▪︎Kibali huwa kina uwezo wa kukuelekeza ufanye nini.

Kibali cha Musa Misri kilimfanya awe mkuu sana Misri.

Je kibali chako kinakuelekeza kufanya nini?

▪︎Watu wengi wana vibali fulani ila hawajui vibali vyao vinawaelekeza kufanya nini.

○Kuna mtu ana kibali katika kufundisha lakini yeye anahubiri ndio maana kwenye kuhubiri kibali chake hakifanyi kazi.

○Kuna mtu ana kibali katika biashara fulani njema lakini hana kibali katika biashara nyingine njema.

Ni muhimu sana kujua una kibali katika nini na una kibali kwa akina nani?

■Ukitaka kukitumia kibali chako katika eneo lisilo sahihi ujue kibali hicho hakitafanya kazi maana sio katika eneo lake.

Hiyo ni katika mambo ya kiroho yote na hata ya kimwili.

Ngoja nikupe mfano wa kimwili ulio rahisi.

Kama umepewa Visa ya kusafiria kwenda Marekani maana yake umepewa kibali cha kwenda Marekani. Sasa kama wewe kwa sababu una Visa ya Marekani lakini ukataka kwenda Ujerumani ujue kibali chako cha Marekani hakitakupa ruhusa kukaa Ujerumani, ndivyo ilivyo pia katika mambo ya vibali kiroho.

○Inawezekana wewe una kibali katika kuimba lakini huna kibali katika kuhubiri, unaweza ukaacha kuimba ili uhubiri na ukashangaa hupati kibali katika kuhubiri.

Wako watu pia wana vibali katika maeneo zaidi ya moja, muhimu tu fanyia kazi kibali chako kama kilivyo.

Je kibali ulichonacho mbele za watu kinakuelekeza nini?

■Ni vigumu sana kushindana na mtu mwenye kibali kama mtu huyo anajua kibali chake na anajua kibali chake kinafanyaje kazi.

1 Samweli 2:26 "Na yule mtoto, Samweli, akazidi kukua akapata kibali kwa BWANA, na kwa watu pia."

Ni muhimu kujua kibali chako kinafanyaje kazi.

Mfano kama una tiketi ya basi maana yake una kibali cha kusafiri katika basi hiyo tu na kwa muda maalum tu.

Ukipewa mfano tiketi ya basi kutoka Dar kwenda Mwanza kisha wewe ukaenda Dar airpot ili uende Mwanza ujue hutaweza kusafiri kwa tiketi/kibali cha basi.

●Hakikisha una kibali kwa mwenzi wako wa ndoa.

●Hakikisha una kibali kazini kwako.

●Hakikisha una kibali katika familia yako na ukoo wako.

●Hakikisha una kibali cha kihuduma n.k

Kibali kinapatikanaje?

■■Kibali kinapatikana kwa maombi na kuishi maisha matakatifu ya haki.

Kibali kina nguvu sana na ni vigumu kushindana na mtu mwenye kibali anayejitambua.

Mfano kulikuwa na wasichana wengi sana sana waliotamani kuolewa na Mfalme Ahusuero, inawezekana wapo waliojaribu kujipamba, kuvaa kikahaba, kubadilisha sauti, kutumia madawa, kujipendekeza n.k lakini Msichana Esta alikuwa na kitu kimoja tu muhimu sana kuliko wao ambacho ni kibali, ndio maana akaolewa yeye huku wengine waliojiona wazuri ku

liko yeye wakibaki wanashangaa.

Esta 2:15-17 " Hata ilipowadia zamu yake Esta, binti Abihaili, mjomba wake Mordekai, ambaye alimtwaa kuwa binti yake, ili aingie kwa mfalme, yeye hakutaka kitu, ila vile vilivyoagizwa na Hegai, msimamizi wake mfalme, mwenye kuwalinda wanawake. Naye huyu Esta alikuwa amepata KIBALI machoni pa wote waliomwona. Basi Esta alipelekwa kwa mfalme Ahasuero, katika nyumba ya kifalme, mwezi wa kumi, ndio mwezi wa Tebethi, mwaka wa saba wa kumiliki kwake. Mfalme akampenda Esta kuliko wanawake wote, naye akapata neema na KIBALI machoni pake kuliko mabikira wote; basi akamtia taji ya kifalme kichwani pake, akamfanya awe malkia badala ya Vashti."

Inawezekana wapo walioota ndoto kwamba wataolewa na mfalme Ahusuero, inawezekana wapo waliotabiriwa na manabii wa uongo kwamba wataolewa na mfalme, wanawake hawa walikuwa na sifa zote lakini walikosa kitu kimoja tu muhimu sana kiitwacho "kibali"

Kwa sababu ni Esta ndiye alikuwa na kibali ndio maana mfalme alimuoa yeye na kumfanya malikia anayelindwa kama mmoja wa wakubwa wa nchi.

■■Ndugu, katika mambo yote unahitaji kibali cha ki MUNGU.

Sasa inawezekana wewe una kibali kikubwa sana sasa lakini hujui kukifanyia kazi kibali chako.

Hebu kijue kibali chako na fanyia kazi Kibiblia yakupasayo ili kibali chako kionekane siku zote.

■Jitenge mbali na dhambi na uovu wa kila namna.

■Mche MUNGU katika KRISTO YESGU na utakuwa na kibali sana.

Gundua mwenyewe nini kibali chako kinakuelekeza kufanya.
MUNGU akubariki sana.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Whatsapp, sadaka ya kuipeleka Injili mbele, Maombezi na Ushauri)
Ubarikiwe sana na ombea kibali chako katika maeneo unayohitaji kibali.

Comments