MAOMBI YA KUOMBEA KIBALI KWENYE ENEO LA MAISHA YAKO LINALOHITAJI KIBALI.

Na Mwl Peter Mabula, Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

 



  Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu wote.
Leo tunaombea "KIBALI kwenye kila eneo la Maisha yako ambako unahitaji KIBALI"

Kibali ni nini?

✓✓Kibali ni idhini anayopata mtu ili kupata vitu fulani avitakavyo.

✓✓Kibali ni kukubaliwa kufanya jambo jema unalolitaka kulifanya.

✓✓Kibali ni ruhusa inayovisukuma nje vizuizi vyote.

✓✓Kibali ni ridhaa ya kutenda unachotaka kutenda.

Zingatia somi hili   itakusaidia.

Zingatia somi hili   itakusaidia.

1 Samweli 2:26 ''Na yule mtoto, Samweli, akazidi kukua akapata kibali kwa BWANA, na kwa watu pia.''

 Samweli alikuwa mteule wa MUNGU kama ulivyo wewe ulieokolewa na Bwana YESU.

Samweli alikuwa na  kibali kwa MUNGU na kwa wanadamu.

Kibali kilikuwa kimemtangulia Samweli katika maisha yake, alipata kibali mbele za MUNGU pia ndio maana MUNGU alisema naye mara kwa mara.
1 Samweli 3:10-11 " BWANA akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, BWANA; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. BWANA akamwambia Samweli, Angalia, nitatenda tendo katika Israeli, ambalo kila atakayelisikia masikio yake yatamwasha."

Kibali kilifanya Samweli awe mtawala wa waisraeli wote bila kuchaguliwa na watu wala kuteuliwa, alikuwa mwamuzi wa mwisho kabla ya mfumo wa ufalme haujaanza katika Israeli.
1 Samweli 7:15 "Naye huyo Samweli akawaamua Israeli siku zote za maisha yake."

Biblia inasema watu  walikuwa wanamfuata ili awaamue na kuwafundisha na kuwaelekeza, Kwa sababu ya nini?

 Ni kwa sababu ya kibali.

Baadae Waisraeli walitaka mfalme ndipo MUNGU akasema na Samweli na kwa kupitia Samweli,  Sauli akawa mfalme. Lakini jambo la ajabu ni kwamba Samweli alikuwa na nguvu wakati mwingine kuliko Mfalme maana hata Mfalme alihitaji Msaada kwa Samweli mwenye kibali kwa MUNGU na wanadamu.

Kibali kina nguvu sana sana.

Ukishindana na mtu mwenye kibali itakusumbua sana kumshinda.

Nilichojifunza ni kwamba kila eneo la maisha yako unahitaji kibali cha MUNGU ndipo utafanikiwa na kustawi.

Sio waliosoma wote na kazi nzuri, wenye vibali haijalishi wana elimu ndogo   wana kazi.

Sio mabinti wazuri na warembo wote wamefunga ndoa takatifu, wenye vibali ndio walifanikiwa kufunga ndoa takatifu.

Sio wahubiri wazuri wote wana makanisa makubwa sana, wenye vibali ndio wamefanikiwa.

Nimewahi kukutana na wanaume wenye kazi nzuri na maisha mazuri lakini kila akimchumbia binti anakataliwa, ndugu mmoja mwanaume  alinipigia simu akisema afanye nini ili naye apate mchumba? 

Ndugu yule aliongea kwa uchungu sana huku analia sana.

Nikamuuliza ana miaka mingapi, akasema miaka 42 na amejaribu sana kutafuta mchumba lakini hajafanikiwa kumpata, hana tatizo lolote la maumbilie au uchumi lakini hakuna binti amewahi kumkubali ili wachumbiane kisha wafunge ndoa.

Kibali ni kitu muhimu sana.

 ''Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa BWANA.-Mithali 18:22 ''

 Tafasiri ya BHN inasema '' Anayempata Mke amepata bahati njema; Hiyo ni fadhili kutoka kwa MUNGU''

Mke au Mume anayezungumzwa hapa kwamba ukimpata umepata bahati njema inayotokana na fadhili za MUNGU sio kila Mke au Kila Mume bali ni Mke Mwema au Mume Mwema.

Huyo mke mwema au mume mwema ili umpate unahitaji fadhili za MUNGU na fadhili za MUNGU zimebeba kibali cha MUNGU cha kukufanikisha ili umpate huyo Mke Mwema wako au Mume mwema wako.

 Kuna watu wako katika ndoa kabisa lakini hawana vibali kwa wenzi wao. Unakuta mama wa familia hata aongee nini mumewe hawezi kukubaliana naye japokuwa mama huyo anaongea jambo sahihi na muhimu kabisa.
Mama unahitaji kibali cha MUNGU cha kukubaliwa.

 Dada unahitaji kibali cha MUNGU na kutendewa mema.

Kuna watu katika ukoo huonekana kama takataka tu maana hawana kibali, ndugu uhahitaji kibali cha MUNGU kwa ndugu zako.

Mtumishi unahitaji kibali cha MUNGU kwa wote unaowaendea ili kuwahubiria injili ya KRISTO.

Jambo muhimu sana kujua ni kwamba kila mwanadamu huumbwa na kibali fulani katika maisha yake, kibali hicho hutolewa na MUNGU hata kabl

a mwanadamu huyo hajazaliwa.

Ona Mfano huu, Yeremia 1:5 '' Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.''

Yeremia aliumbwa na MUNGU huku akiwa na kibali cha kuwa nabii wa mataifa.

Hata wewe ulipoumbwa na MUNGU katika tumbo la mama yako ulipewa na MUNGU kibali katika vitu fulani katika maisha yako.

Tatizo tu wengi hawajui wamepewa vibali katika jambo gani  kwa utukufu wa MUNGU.

 Wengi shetani huwateka mapema sana na kuvigeuza vibali vyao ili badala ya kuvitumia vibali hivyo kwa utukufu wa MUNGU, wao wanavitumia kwa utukufu wa shetani na kujipoteza kabisa wao wenyewe.

Kuna waimbaji MUNGU amewapa kibali cha uimbaji cha kimataifa kabisa lakini wao wanatumia vibali hivyo kumwimbia shetani na sio MUNGU aliyewapa sauti na karama hiyo.

Unakuta kuna mwimbaji wa kidunia alipewa kibali na MUNGU ili amwimbie MUNGU katika kanisa lakini yeye alichagua kumwimbia shetani duniani na kujipoteza kabisa.

Wapo watu wana vibali katika nguvu lakini badala ya nguvu hizo kuzitumia kupeleka injili wao hutumia nguvu zao katika wizi na ujambazi.

Katika Mwili wa KRISTO Kila Mteule wa MUNGU na kibali cha MUNGU lakini wengine vibali vyao vimezibwa kipepo ndio maana hawawezi kusimama katika nafasi zao kiutumishi.

Wengine kwa sababu ya maisha ya dhambi ndio maana vibali vyao havifanyikazi yake.

Vibali vya MUNGU viko vingi sana sana.

Hujawahi kukutana na binti ambaye watu walikuwa wanamwita mbaya wa sura lakini kwa kibali anafunga ndoa takatifu na kuishi maisha ya ndoa ya furaha kuliko hata waliokuwa wanambeza?

Hujawahi kuona mtu anapata madaraka fulani lakini wenye nguvu kuliko yeye na wenye elimu nzuri kuliko yeye wapo tu wanaangalia?

Kuna wenye vibali vya kimataifa kama Yeremia na kuna kuna wenye vibali katika taifa, kuna wenye vibali katika mji na kuna wenye vibali katika maeneo fulani.

 Jambo muhimu tu kujua ni kwamba una kibali katika nini?

Ndugu ombea kibali chako ulichoumbwa nacho na MUNGU na kitumie kibali hicho kwa utukufu wa MUNGU.

Shetani anaweza kuharibu kibali  ndio maana kuna watu hufanya baadhi ya vitu bila kibali na watu hao hujikuta wameanguka sana na bila mafanikio

MUNGU ametuumbia kibali na MUNGU pia ametuumbia matendo mema ili tuyaishi tukitumia vibali vyetu kwa kusudi lake.

 Waefeso 2:10 ''Maana tu kazi yake(MUNGU), tuliumbwa katika KRISTO YESU, tutende matendo mema, ambayo tokea awali MUNGU aliyatengeneza ili tuenende nayo.''

Ndugu una kibali katika nini?
Nakuomba fanyia kazi kibali chako.
Kuna vibali vya aina nyingi sana.
Kuna watu wana vibali katika vinywa yaani matamshi yao yana nguvu kubwa sana inayowafanya watu wengine kuwasikiliza na hata kuwafuata.

Kuna watu wana vibali kuandika, ndugu andika Neno la MUNGU.
Kuna watu wana vibali vya ushawishi.

Kuna watu wana vibali vya kupendwa na kukubaliwa sana katika jamii.

Kuna watu wana vibali vya kuongoza.
Kuna watu wana vibali vya kusikilizwa.
Vipo vibali vingi sana.

Kwanini uombee kibali?

Hebu ngoja nikufundishe kazi za kibali ili upate msukumo wa kuombea kibali chako.
 
1. Kibali kinafungua macho ya watu kukuona na kukutendea mema.

2. Kibali kinaamrisha watu kukukubali na kukutendea mema, hata kama huna sifa za kukubaliwa

3. Kibali kinawafanya watu kukuheshimu na kukuthamini.

4. Kibali kinawafanya watu kukupenda na kukufanyia mema, hata kama huna sifa za kupendwa.

5. Kila kinawafanya watu wakufuate katika unayoyasema na kuyafanya.

6. Kibali kinakutengeneza ili ufae, hata kama hufai.

7. Kibali kinaleta upendeleo kwako, hata kama hustahili kupendelewa.

Zaburi 106:4- '' Ee BWANA, unikumbuke mimi, Kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako. Unijilie kwa wokovu wako, Ili niuone wema wa wateule wako. Nipate kuifurahia furaha ya taifa lako, Na kujisifu pamoja na watu wako.''

Hujawahi kumuona mtu ambaye watu wengi sana wanamkubali sana sana hata kama hana sifa yeyote njema, huyo mtu ana kibali.

 Omba MUNGU akuletee watu wanaokiona kibali chako kutoka kwa MUNGU na kukithamini.

Jambo kubwa tu kumbuka tuliumbiwa matendo mema ili tuyaishi hivyo kibali alichokupa MUNGU ni kwa mema na sio mabaya.

E

ndelea kujifunza somo hili itakusaidia.

Dalili za mtu ambaye kibali chake shetani amekiharibu.

1. Hafanikiwa hata kama ana sifa zote za kufanikiwa.

2. Kutumia nguvu nyingi sana hata pale ambapo asingetumia nguvu nyingi  akiwa na kibali.

3. Kukataliwa bila sababu, kuonewa bila sababu wala kosa na kupuuzwa bila sababu za msingi zozote.

4. Kutokufikia lengo la mafanikio yaliyokusudiwa.

Ndugu unahitaji sana kuombea kibali chako.

Kuna watu wana vibali vya kupendwa kwa mfano.

Mtu kama huyo akifungua biashara atafanikiwa sana maana watu wanampenda na hata hawajui kwanini wanampenda.

Kila mtu ana kibali katika jambo fulani.

Ukitaka ujue hivyo chunguza tu katika Kanisa la MUNGU.

Sio wote wana kibali katika uimbaji wao, kuna wenye sauti nzuri za kuimba lakini hawana kibali.

Sio watu wote wana uwezo wa kushawishi, wenye kibali hicho hata akiwa kiongozi mfano wa vijana, anaweza kuwashawishi vijana kushuhudia na ukashangaa sana matokeo yake kuwa makubwa sana.

Ndugu ombea kibali chako.

Unaweza ukawa na elimu nzuri lakini watu wanakuweka katika kundi moja na ambao hawakusoma  kwa sababu tu shetani ameharibu kibali chako na kazini wewe ndio umegeuka mtumwa tu na sio bosi.

Kibali kina nguvu sana.

Kila jambo katika maisha yako omba kibali cha MUNGU cha kukuwezesha.

Watu wengi hawajui kabisa kwamba hata ukiomba jambo fulani kwa MUNGU tambua kwamba unahitaji kibali cha MUNGU ili kupokea baraka hiyo.

Kuna kibali cha kupata Mchumba lakini pia kuna kibali cha kufunga ndoa, tena kuna kibali cha kuishi maisha ya ndoa na hata kuna kibali cha kuishi maisha ya ndoa ya furaha.

Ukiomba tu upate kibali cha kupata mchumba basi unaweza ukampata mchumba na kabla ya ndoa uchumba unavunjika kwa sababu shetani ameshaharibu kibali chako cha kufunga ndoa.

Katika eneo la maisha yako muombe MUNGU akupe kibali.

 Katika maombi yako juu ya kibali omba maombi yafuayato.

1. Omba kibali ulichoumbwa nacho na MUNGU kifanye kazi  sahihi kwa utukufu wa MUNGU.

2. Komboa kibali chako kwa maombi kama mawakala wa shetani wamekiharibu.

3. Omba kibali cha MUNGU katika yote unayoamua kufanya kwa utukufu wa MUNGU.

Mithali 3:3-4 ''3 Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako. Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za MUNGU na mbele ya

Ndugu endelea kuomba  na utakuwa na kibali.

Inawezekana unatafuta kazi, wewe kibali tu ndio hupata kazi.

Inawezekana hakuna anayetaka kufunga ndoa na wewe kwa sababu tu huna kibali.

Inawezekana katika ukoo wenu au familia yenu wewe unadharaulika kwa sababu tu hauna kibali.

Kibali ni muhimu Sana.

Kibali huleta kustahili hata Kama hustahili.

 Wakati mwingine ndoa yako inaweza kuwa na migogoro kila mara kwa sababu tu huna kibali kwa mwenzi wako, ndugu ombea kibali chako.

Omba ukitaja maeneo yako unayohitaji kibali na utapata kibali hicho kibali.

Inawezekana biashara yako haina kibali, omba MUNGU akupe kibali na biashara yako aipe kibali.

 Najua kabisa unahitaji Sana kibali, omba leo Katika jina la YESU KRISTO utapata kibali.
MUNGU akukumbuke, akulinde na  akubariki sana.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi Katika shamba la MUNGU.
+ 2 5 5 7 1 4 2 5 2 2 9 2

Comments