MAOMBI YA KUOMBEA NDOTO YAKO.

 

Mwl Peter Mabula, Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze somo fupi la maombi ili litupe maarifa ya maombi ya leo.

Kuna aina mbili za neno "NDOTO"

■Maana ya kwanza ni ndoto ambazo mtu anaota akiwa amelala.

●Ndoto hizi maana yake ni matukio ambayo mtu anayaona kwa kutumia utu wake wa ndani akiwa amelala usingizi.

Ndoto hizi jina lingine zinaitwa njozi.

Mfano ,
Danieli 2:3 "Mfalme akawaambia, Nimeota ndoto, na roho yangu imefadhaika hata niijue tafsiri yake."

■Maana ya pili ya ndoto ni mipango au malengo mema anayoyapanga mtu hatua kwa hatua hadi namna ambavyo mambo hayo mema yatakuja kutokea katika maisha yake.

Mfano hai ni kwamba ndoto ya Daudi ni siku moja ajenge nyumba ya kumwabudia MUNGU.

1 Wafalme 8:17-18 " Basi ilikuwa moyoni mwake Daudi, baba yangu, kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli. Lakini BWANA akamwambia Daudi baba yangu, Kwa kuwa ilikuwa moyoni mwako kujenga nyumba kwa jina langu, ulifanya vema kuwaza hivi moyoni mwako."

Ni sawa kabisa mtu wa MUNGU yeyote kuwa na ndoto yake njema maana Biblia inasema

Ayubu 22:28 "Nawe utakusudia neno, nalo litathibitika kwako; Na mwanga utaziangazia njia zako."

●Sasa mimi leo sizungumzii ndoto za kuota ukiwa umelala bali nazungumzia ndoto yaani malengo au mipango yako mizuri unayotaka itimie baadae.

●Narudia tena mimi leo nazungumzia ndoto yaani malengo yako.

Inawezekana una ndoto ya kuja kuwa mfanya biashara mkubwa baadae.

Inawezekana una ndoto ya kuwa na watoto 12 kwenye ndoa yako.

Inawezekana una ndoto ya kuwa na elimu ya PHD.

Mwingine ndoto yake ni kusoma hadi diploma au hadi chuo.

Inawezekana una ndoto ya kujenga jengo la Kanisa.

Mwingine ndoto yake ni kufunga ndoa takatifu mwaka fulani.

Mwingine ndoto yake ni kwenda taifa fulani.

Inawezekana una ndoto ya kununua kiwanja kikubwa.

Hii ni mifano michache ya ndoto ya mtu.

■Na wewe najua una ndoto zako nyingi, hakikisha tu ni katika MUNGU na kwa utakatifu huku ukifanyia kazi Neno la MUNGU na ongozwa na ROHO MTAKATIFU.

Wakolosai 3:17 "Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye."

Ndugu yangu mmoja aliniambia kwamba ndoto yake ni kuja kujenga nyumba ya ghorofa.

Mtu mmoja namfahamu aliwahi kusema zamani sana kwamba lazima aje awe Mwanajeshi na ikaja ikawa hivyo baadae.

Mtu mmoja ndoto yake ilikuwa ni kuja kuwa mwanasheria na ikaja ikawa baadae.

■Sasa kuwa na ndoto sio tatizo kwa watu wengi lakini tatizo ni nini afanye hadi atimize ndoto yake njema.

●Huwezi kuwa na ndoto ya kuja kuwa daktari wakati kwa sasa hata shule huitaki, ndoto yako haiwezi kutimia.

●Najua kila mmoja ana ndoto zake nyingi, hata mimi nina ndoto zangu nyingi, zingine zimeshatimia na zingine zinangoja wakati wa MUNGU ili zitimie.

■Lakini ukiwa na ndoto yeyote bila maombi ni vigumu kufanikiwa maana nguvu za giza na mawakala wa shetani nao wako kazini kuhakikisha ndoto yako haitimii.

Ndio maana Biblia inatushauri hivi sisi wateule wa KRISTO "Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na MUNGU. Na amani ya MUNGU, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika KRISTO YESU.-Wafilipi 4:6-7"

■Ndio maana ni muhimu sana kuombea ndoto yako.

Leo nadonoa donoa katika somo hili lakini naamini kuna kitu utanajifunza na utaandika ndoto zako njema na utakuwa unaziombea, wengine hata huzitolea sadaka ndoto zao katika maombi yao ili zitimie, mimi sijui rohoni mwako unaona nini, muhimu ombea ndoto zako njema ili katika jina la YESU KRISTO zitimie.

Maombi ya leo ya kuombea ndoto.

1. Kwa maombi tubu kwa kilichosababisha ndoto yako ichelewe kutimia(kama muda wake wa kutumia umeshafika )

Matendo 3:19 "Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;"

2. Kwa maombi haribu roho ya kuchelewesha kutimia kwa ndoto yako.

Kutoka 1:8-10 " Basi akainuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu.
Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi. Haya! Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, ikitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii."

Farao huyu alihakikisha Waisraeli hawaongezeki ndio maana akasema "Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka"

Inawezekana una ndoto ya kuongezeka kiuchumi, mawakala wa shetani wanasema "Na tumtendee kwa akili, asije akaongezeka"

Hiyo ndio roho ya shetani ya kukuchelewesha.

Inawezekana ndoa yako ina umoja sana ndio maana mnapata maendeleo, sasa wakuu wa giza wanasema "Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka"

Inawezekana una ndoto ya kuolewa lakini mizimu wanasema "Na tumtendee kwa akili, asije akafunga ndoa takatifu "

Inawezekana una ndoto ya ndoa yako iwe na amani na furaha lakini wapambe wa shetani wanasema "Na tuwatendee kwa akili, wasije wakawa na ndoa yenye amani na furaha "

Una ndoto ya kufaulu masomo lakini adui zako wanasema "Na tumtendee kwa akili, asije akafaulu "

Una ndoto ya kupata kazi nzuri lakini majini wanasema "Na tumtendee kwa akili, asije akapata kazi na kuwa na maendeleo "

Una ndoto ya kuwafikia watu wengi sana kwa injili lakini wachawi wanasema "Na tumtendee kwa akili, asije akawafanya watu wengi kuokoka "

Hiyo ndio roho ya kuchelewesha yaani nguvu za giza wanafanya mipango yao ili usifanikiwe na hata ukifanikiwa ni kwa kuchelewa sana

Leo kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO haribu kila roho ya kuchelewesha kutimia kwa ndoto yako

3. Ombea ndoto yako ili itimie(itaje)

Ayubu 22:28 "Nawe utakusudia neno, nalo litathibitika kwako; Na mwanga utaziangazia njia zako."

4. Omba kwa MUNGU ili ROHO MTAKATIFU akufundishe na kukufunulia yakupasayo kufanya ili ndoto yako katika kusudi la MUNGU itimie .

1 Wakorintho 2:10 " Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU."

5. Kwa maombi pambana kiroho na maadui wanaotaka kuzuia ndoto yako.

Iga kanuni hii ambapo Waisraeli waliambiwa waanze kumiliki eneo kwa kupigana na adui anayeshikilia eneo hilo wakati huo.

Kumbu 2:24 "Ondokeni, mshike safari yenu, mvuke bonde la Arnoni; tazama, nimemtia Sihoni Mwamori mfalme wa Heshboni mkononi mwako, na nchi yake; anzeni kuimiliki, mshindane naye katika mapigano."

Hata wewe inawezekana kabisa MUNGU amekupa baraka yako au ndoto yako, hakikisha unapambana kimaombi na nguvu za giza wanaojaribu kuzuia baraka yako au ndoto yako.

■Ushauri wa mwisho ni huu, najua una ndoto nyingi sana lakini naomba ndoto yako kuu iwe ni kwenda uzima wa milele baada ya muda wako wa kuishi duniani kuishi.

●Ili ndoto yako hiyo itimie hakikisha unampokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako (Yohana 3:16) kisha ishi maisha matakatifu ya wokovu(1 Petro 1:15) na jitenge na ubaya wa kila namna (1 Thesalonike 5:22) na kumbuka kuenenda katika ROHO MTAKATIFU (Warumi 8:14)

Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTOMwokozi.
+255714252292(Kwa lolote na pia whatsapp).
Ubarikiwe.

Comments