USIPOTEZE NAFASI YAKO KWA MAMBO MADOGO MADOGO.

Na Mwl Peter Mabula, Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

 


Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe sana Ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Kwanini unapoteza nafasi yako kwa mambo madogo madogo?

Mwanzo 39:2-9 '' BWANA akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri.Bwana wake akaona ya kwamba BWANA yu pamoja naye, na ya kuwa BWANA anafanikisha mambo yote mkononi mwake.Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake.Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo, BWANA akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa BWANA ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba. Akayaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu cho chote chake, ila hicho chakula alichokula tu. Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami. Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu. Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu cho chote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. NIFANYEJE UBAYA HUU MKUBWA NIMKOSE MUNGU? ''

Yusufu angekubali kutembea na mke wa bosi wake hakika angepoteza nafasi yake ya kuwa waziri mkuu katika taifa la ugenini Misri.

Inawezekana kabisa Yule mama ambaye ni mke wa Potifa baada ya kutembea na Yusufu angeweza kumjengea Nyumba Yusufu na kumpa mali nyingi, Lakini Yusufu hakutaka kuipoteza nafasi yake aliyopangiwa na MUNGU baadae.

●Vitu vidogo vidogo vinawapotezea nafasi zao za baadae watu wengi sana.

●Ndugu nakuomba usikubali kitu chochote kikuondolee nafasi yako uliyopangiwa na MUNGU kwako baadae.

■Mwanafunzi unaweza ukaiba sasa na kukamatwa na kufungwa, na ndoto yako ya kusoma ili uje uwe kiongozi inafia hapo hapo.

■Binti unaweza kufanya dhambi ya uzinzi na kupewa mimba au magonjwa na hatima yako inakuwa umepinda kwa sababu ya mambo madogo madogo.

■Mfanya kazi wa serikali unaweza ukala rushwa mara moja tu na kukamatwa na kazi unafukuzwa, na kwa njia hiyo unakuwa umepishana na nafasi yako ya baadae uliyopangiwa.

■Unaweza ukaaminiwa na kukabidhiwa biashara nzuri lakini wizi kidogo unaweza ukakusababishia ukarudi kijijini ukilia na hujui pa kuanzia.

■Unaweza ukawa Mtumishi wa MUNGU na huduma kubwa na ukawa na watu wengi chini yako lakini dhambi kidogo inaweza ikakufanya ukapoteza nafasi yako.

Yusufu hakukubali kabisa nafasi yake ya kuwa mkubwa baadae iondolewe na uzinzi wa mwanamke kahaba.

Hata wewe unaweza kuyaepuka mambo madogo madogo na kwa njia hiyo unakuwa umeiponya nafsi yako.

●Unaweza ukapoteza hata maisha kwa sababu ya mambo madogo madogo tu unayoyaendekeza.

●Ndugu yangu, nakushauri fanya mema siku zote na sio dhambi.

Kwa Neno au kwa tendo fanya mambo yanayompendeza MUNGU.

Wakolosai 3:17 '' Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye. ''

MUNGU akubariki sana na usikubali mambo madogo madogo yakakuondoa kwenye wokovu wa Bwana YESU.
Amen Amen
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292
Ubarikiwe

Comments