MAOMBI YA KUOMBA MUNGU ASEME NA TATIZO LINALOKUTESA ILI HILO TATIZO LIKUACHIE.

 

Mwl Peter Mabula na Jemimah Mabula
Watenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.

Karibuni sana tujifunze Neno la MUNGU kisha tuombe maombi ya ushindi mkuu kupitia jina la YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.

Kama ulikuwa hujui ni kwamba yapo pia maombi na kumuambia MUNGU aseme na tatizo linalokutesa ili hilo tatizo likuachie, liondoke na wewe uwe huru.

MUNGU anaweza kusema na adui anayekutesa na huyo adui akaondoka na asirudi tena katika maisha yako.

Hakuna adui yako  yeyote kwenye ulimwengu wa roho anayeweza kuambiwa na MUNGU aondoke harafu asiondoke, labda tu wewe ukosane tena na MUNGU ili kumpa nafasi adui huyo kurudi.

 ●MUNGU anaweza kusema na tatizo lako na hilo tatizo  likakuachia kabisa.

●MUNGU anaweza akasema na adui aliyekushikilia ili akuachie na adui huyo akakuachia kabisa.

Ukisoma katika Yona sura ya pili unaona Yona akiwa amemezwa na samaki na chanzo kilikuwa ni makosa ya Yona mwenyewe, lakini Yona alipotambua kwamba MUNGU anaweza kusema hata na huyo Nyangumi basi alianza kuomba akiwa huko huko katika tumbo la Samaki na MUNGU akasema na Yule samaki aliyemmeza Yona na Yona akatoka akiwa huru kabisa.

Yona 2:1 Biblia inasema ‘’ Ndipo Yona akamwomba BWANA, Mungu wake, katika tumbo la yule samaki, ‘’

Baada ya Yona kuomba kwa MUNGU tunaona MUNGU anasema huyo aliyekuwa amemmeza Yona ili amtapike sehemu nzuri na ikawa hivyo hivyo.

 Yona 2:10 ‘’BWANA akasema na yule samaki, naye akamtapika Yona pwani.’’

■Nalipenda neno hili ‘’BWANA akasema na Yule samaki’’

Kumbe MUNGU anaweza akasema na yule aliyemshikilia mtu wa KRISTO ili huyo adui amwachie huyo mteule.

●MUNGU akasema na Yule samaki, MUNGU aseme na ugonjwa unaokutesa na ugonjwa huo utakuachia.

●MUNGU anaweza akasema na hizo kamba ambazo zimekufunga kiroho na zikakuachia mara moja.

●MUNGU anaweza kusema na huo utasa au ugumba ndani yako na huo utasa ukakuachia ukazaa.

●MUNGU anaweza akasema na adui yako aliyekumeza au aliyemeza ndoa yako na huyo adui akakuachia wewe au akaiachia ndoa yako iliyokuwa imemezwa.

●MUNGU anaweza akasema na adui anayetaka kuiua ndoa yako na huyo adui akaiachia ndoa yako.

Leo omba MUNGU aseme na adui anayekutesa, omba MUNGU apigane na adui anayekutesa.

Zaburi 35:1 "Ee BWANA, utete nao wanaoteta nami, Upigane nao wanaopigana nami."

●MUNGU anaweza akasema na nguvu za giza zinazokutesa na hizo nguvu za giza zikakuachia kabisa.

●MUNGU anaweza akasema na jini au mchawi au mzimu anayekutesa na huyo wakala wa shetani akaondoka katika maisha yako.

Omba tu leo kwa MUNGU Baba ili aseme na adui anayekutesa na huyo adui ataondoka mara moja, omba tu kwa imani ukimsihi MUNGU na itakuwa.

Katika maandiko kuna mtu ambaye tatizo lake lilikuwa ni mapepo yaliyotesa sana hadi akaonekana kituko kwa wanadamu lakini alipokutana na Mfalme wa wafame alipona kwa jinsi ya ajabu sana.

Unajua ilikuaje?

YESU KRISTO ambaye ni Mfalme wa wafalme alisema na hayo mapepo nayo yakatii na kutoka.

Mathayo 8:32 ‘’ Akawaambia, Nendeni. Wakatoka, wakaingia katika nguruwe; na kumbe! Kundi lote wakatelemka kwa kasi gengeni hata baharini, wakafa majini.’’

Bwana YESU aliwaambia mapepo waliomtesa mtu huyo kwamba ‘’Tokeni mwende’’

 Wale mapepo wakatoka kwa mtu Yule na kwenda kwenye kundi la nguruwe.

●Kumbe Bwana YESU anaweza kuziamurisha nguvu za giza zitoke ndani ya Mtu na zinatoka.

●Bwana YESU KRISTO anaweza kusema na mapepo wanaokutesa au wanaotesa eneo lako na hao wakatoka.

Omba tu leo ukimweleza Bwana YESU KRISTO aseme na hao waliokushikilia katika ulimwengu wa roho na atasema nao nao watakuachia.

Kama Bwana YESU KRISTO aliweza kusema na majini yale anaweza kusema na mchawi anayekusumbua na hutaona tena mchawi huyo akikusumbua tena.

Mimi sijui tatizo lako wewe ni nini lakini ninachojua ni kwamba ukimweleza MUNGU aseme na tatizo hilo anaweza na tatizo hilo likakuachia mara moja.
Mimi Peter Mabula sijui shida gani inakutesa ila ninachojua ni kwamba MUNGU wa Mbinguni anaweza akasema na shida hiyo na ikaondoka kwako.

 Huyu YESU KRISTO hakika anaweza yote, anaweza kusema na viumbe hai na anaweza kusema hata na vile ambavyo sio viumbe hai navyo vikasikia.

Kama Bwana YESU KRISTO anaweza akasema hata na upepo tu nao ukatulia atashindwa nini kusema na miungu ya ukoo inayokutesa?

Atashindwa nini kusema na madhabahu za giza zinazokutesa?

Atashindwa nini kusema na madawa ya kichawi uliyopakwa kichawi ili uteseke, hakika ataweza kusema na tatizo lako nalo litatii na kuondoka.

Atashindwa nini kusema na huo ugonjwa ndani yako ili uondoke.

Hakikisha tu umeokoka na unaishi maisha matakatifu katika yeye.

Hakikisha tu unaomba kwa imani katika jina lake takatifu.

Ufunuo huu ni wa ajabu sana na namshukuru ROHO MTAKATIFU ambaye ndiye aliyenipa ufunuo huu.

Ndugu kama hujui kwamba MUNGU anaweza akasema na adui yako soma 

1 Nyakati 16:22 ambapo Biblia inasema  "Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu."

MUNGU anawaambia mawakala wa shetani kwamba "Msiwaguse wapakwa mafuta wangu"

Kama anaweza kusema na shetani ili asiguse wateule wa KRISTO atashindwa nini kusema na mchawi ili asikuloge, hakika inawezekana. 

Mwambie MUNGU asema na kila adui yako anayewinda uhai wako, afya yako, ndoa yako na baraka yako hakika MUNGU atasema na adui huyo na huyo adui hutamuona tena katika maisha yako yote. 

 Ukiomba MUNGU akulinde hakika atakulinda na njia moja wapo ya ulinzi wa MUNGU kwako ni MUNGU kumwambia adui yako asikuguse.

Omba MUNGU akulinde  na atakulinda. 

2 Wathesalonike 3:3 "Lakini BWANA ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu."

 Kuna Mwanaume mmoja alitaka kumchukua mke wa Mtu ili awe mkewe. MUNGU akasema naye kwa ukali ndotoni na Mwanaume huyo akaacha mpango huo wa kuchukua mke wa mtu, hiyo iko 

Mwanzo 20:3 ambapo Biblia inasema "Lakini MUNGU akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu."

Kama MUNGU alisema na mtu huyo kwa ndoto atashindwa nini kusema na huyo Mwanaume au Mwanamke anayetaka kuivunja ndoa yako.

Atashindwa nini kusema na huyo anayewagombanisha katika ndoa au uchumba ili ndoa ife au uchumba uvunjike. Ndugu unayo nafasi ya kuomba katika jina la YESU KRISTO na MUNGU atasema na huyo mtesi wako anayekufanya ukose amani kila siku.

MUNGU anaweza kumlazimisha adui akusihi kipindi yuko taabuni na matesoni.

Yeremia 15:11 "BWANA akasema, Hakika nitakutia nguvu upate mema; hakika nitamlazimisha adui akusihi wakati wa uovu, na wakati wa taabu."

Ndugu omba kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi MUNGU anaweza kusema na anayekutesa ili asikutese tena.

 Katika maombi ufanyeje?

1. Tubia dhambi zako zote na kujitakasa ili uwe safi mbele za MUNGU.

Dhambi ndio zinaweza kumzuia MUNGU asiseme na adui zako wala asiwazuie kukudhuru, ndugu tubu na acha dhambi kuanzia leo.

Isaya 59:1-3 " Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia. Kwa maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu, na vidole vyenu vimetiwa unajisi kwa uovu; midomo yenu imenena uongo, ndimi zenu zimenong'ona ubaya."

2. Omba Bwana YESU KRISTO aseme na tatizo ndani ya mwili wako  ili hilo tatizo liondoke.

Mfano hai  ni Bwana YESU KRISTO  alisema na mapepo yaliyokuwa ndani ya mtu na mapepo hayo yakatoka yakaingia kwa nguruwe na huyo mtu akawa huru tangu muda ule.

Mathayo 8:32 ‘’ Akawaambia, Nendeni. Wakatoka, wakaingia katika nguruwe; na kumbe! Kundi lote wakatelemka kwa kasi gengeni hata baharini, wakafa majini.’’

 3. Omba MUNGU aseme na adui aliyekushikilia ili huyo adui akuachie.

Mfano hai ni pale MUNGU aliposema na Nyangumi aliyekuwa amemshikilia Yona na huyo Nyangumi akamtapika Yona, Yona akawa huru.

Yona 2:10 ‘’BWANA akasema na yule samaki, naye akamtapika Yona pwani.’’

4. Omba MUNGU aseme na adui aliyeshikilia ndoa au ardhi au eneo lako la biashara na huyo adui ataachia hapo.


Mathayo 7:8 "kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa."

Ndugu omba na utamuona MUNGU.

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kueleea naamini  ameelewa .

 Hapa chini ni MAOMBI YA KUOMBA MUNGU ASEME NA TATIZO LINALOKUTESA ILI HILO TATIZO LIKUACHIE.

Maombi haya ni kwa ajili ya mtu ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba.

Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea.

MAOMBI YA KUOMBA MUNGU ASEME NA TATIZO LINALOKUTESA ILI HILO TATIZO LIKUACHIE.

Baba katika jina la YESU KRISTO ninakushuru kwa neema hii na nafasi uliyonipa ya kuombe mbele zako kwa ajili ya kufanikiwa kwangu na kuwa huru kwangu dhidi ya maadui zangu.

Ninatubu BWANA nikiomba unisamehe kwa jambo lolote nililokosea mbele zako MUNGU wangu. 

Nisamehe kwa makosa ambayo nimekosea mbele zako kwa kuongea au kutenda au kuwaza, naomba unisamehe MUNGU Baba wa Mbinguni. 

Ninaomba kwako nikikusihi damu ya YESU KRISTO initakase na kunisafisha ili niwe safi mbele zako MUNGU wangu.

Niko sasa mbele zako nikikusihi BWANA usema na maadui zangu wote ili wakae mbali nami na wasinitese tena.

Neno lako katika  Mathayo 7:8 linasema kwamba "kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa." Nami naomba YAHWEH MUNGU wangu nipokee ushindi kutoka kwako nikikusihi useme na kila adui kwenye ulimwengu wa roho ili huyo adui aachie maisha yangu.

Bwana YESU KRISTO nakusihi Bwana usema na kila mchawi  au mganga  su jini yeyote anayewinda maisha yangu, sema na huyo ili asiguse maisha yangu, huyo adui akishupaza shingo nakusihi Bwana YESU umwadhibu kwa adhabu kubwa kama Isaya 24:21  inavyosema kwamba "Tena itakuwa katika siku hiyo, BWANA ataliadhibu jeshi la mahali palipo juu katika mahali palipo juu, na wafalme wa dunia katika dunia;"

Bwana MUNGU sema na wafalme wa giza wote katika mji ninaoishi ili waachie ndoa yangu, uzao wangu,  uchumi wangu,  afya yangu na mwili wangu na wakishupaza shingo nakusihi Eee MUNGU wangu uwaadhibu maana Neno lako linasema utawaadhibu wafalme wa dunia.

Bwana MUNGU  nakusihi useme na kila adui ambaye huwa namuona ndotoni au kwenye maono akiwa amevaa sura za nyoka au wanyama wengine au wadudu, sema na huyo BWANA ili asiyaguse maisha yangu popote na akishupaza shingo huyo roho wa kuzimu naomba akutane na upanga wako usiosamehe  kama Isaya 27:1 inavyosema kwamba " Katika siku hiyo BWANA, kwa upanga wake ulio mkali, ulio mkubwa, ulio na nguvu, atamwadhibu lewiathani, nyoka yule mwepesi, na lewiathani, nyoka yule mwenye kuzonga-zonga; naye atamwua yule joka aliye baharini."

MUNGU muumbaji wangu nakusihi useme na kila nguvu za giza zilizonimeza au kumeza ndoa yangu au uzao wangu au uchumi wangu  ili ziachie baraka zangu hizo.

MUNGU Baba nakusihi sema nao kwa ukali na  kila Wanadamu wanaowinda maisha yangu, ndoa yangu, uzao wangu,  kazi yangu na biashara yangu  na wasifanikiwe kamwe kuniletea madhara waliyoyakusudia.

Nakusihi tena MUNGU Baba sema na kila pando la shetani lililopandwa katika mwili wangu ili hilo litoke na liniachie ili niwe huru na ili nipate Baraka zangu.

MUNGU Baba sema na kinachotembea ndani yangu ili kitoke niwe huru, sema na roho ya kuharibu mimba ndani yangu ili iniachie nizae katika ndoa yangu, sema ugonjwa(taja) ili utoke ndani yangu niwe huru.

Nakusihi BWANA sema na kila tatizo ndani ya mwili wangu ili hilo tatizo litoke niwe huru, sema na adui aliyeshikilia ardhi yangu au nyumba yangu au ndoa yangu na sasa kwa jina la YESU KRISTO adui huyo atoke na asirudi tena.


JEHOVAH MUNGU wangu nakuomba sema na kila anayetaka kunionea awe ni mwanadamu au nguvu za giza ili asifanikiwe kunionea tena.

Nakushukuru MUNGU Baba wa Mbinguni maana nimesema na wewe na naamini umetenda kwa utukufu wako.


Kwa maadui ambao inatakiwa usema nao BWANA nakuona utete nao ili waachie kila baraka yangu na maisha yangu.

Kwa maadui ambao inatakiwa uwapige, BWANA nakusihi uwapige na wakae mbali na maisha yangu milele.

Imeandikwa Zaburi 35:1  kwamba "Ee BWANA, utete nao wanaoteta nami, Upigane nao wanaopigana nami."

Nakushukuru MUNGU Baba maana umeniletea ushindi leo kwa sababu umewadhibiti adui zangu.

Mimi ni mshindi kuanzia leo katika jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu. 

Nakushukuru MUNGU Baba maana umetenda.

Ni katika jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu nimeombanakushukuru. 

Amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen. 

Ndugu omba zaidi ya maombi haya ya kuanzia, omba ukitaja eneo la maisha yako ulilokuwa unateseka.

Uwe huru mbele za MUNGU kutaja tatizo lako ili MUNGU aliamuru hilo tatizo kuondoka.

Omba ndugu na utamuona MUNGU. 

Omba kwa imani ukizungumza na MUNGU Baba wa Mbinguni. 

Maombi haya ni ya kuzungumza na MUNGU hivyo usikemee bali zungumza na MUNGU naye atatenda.
MUNGU akubariki sana. 
By Peter Mabula. 
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi. 
+255714252292.
Omba ndugu na utamuona MUNGU wa matendo makuu ya Miujiza. 
Ndugu omba kwa imani katika jina la YESU KRISTO. 
Wakati naandaa somo hili nimeona kuna mtu kisukari kinahama ndani ya Mwili wake.
Yaani alikuwa mgonjwa wa kisukari na hali haikuwa nzuri lakini nikamuona wakati anamsihi MUNGU ili amuondolee ugonjwa wa kisukari unaomtesa, nikaona  ugonjwa huo ukijikusanya ndani ya mwili wake na kuondoka.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

Comments