MUNGU HAJAKUSAHAU BADO

 

Na Mwl Peter Mabula 



Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu atukuzwe sana rafiki yangu.
Karibu tujifunze Neno la KRISTO YESU Mwokozi wetu.

Katika safari ya watu wa MUNGU duniani wakati mwingine kuna kupitia vipindi mbalimbali.

✓Kuna wakati wa kupitia vipindi vizuri na kuna wakati wa kupitia vipindi vigumu.

✓Watu wengi wakati wa kupitia vipindi vizuri huwa hawaoni shida ila wakati wa kupitia vipindi vigumu ndipo inafika kipindi hadi baadhi ya watu hao kudhani kwamba  MUNGU amewaacha ndio maana wanapitia magumu hayo, lakini leo tunao ujumbe usemao  kwamba MUNGU hajakusahau bado.

  Isaya 49:14-16 " Bali Sayuni alisema, YEHOVA ameniacha, BWANA amenisahau. Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, LAKINI MIMI SITAKUSAHAU WEWE. Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima."

Katika Maisha ya Waisraeli kipindi fulani walidhani MUNGU amewasahau, lakini MUNGU Baba wa Mbinguni alikuwa hajawasahau.
Kupitia Nabii Isaya MUNGU akasema kwamba ingawa ni vigumu sana Mama aliyezaa siku za karibuni akamsahau mtoto wake mchanga anyonyaye, lakini MUNGU anasema ni rahisi zaidi Mwanamke huyo kumsahau mtoto wake mchanga kuliko MUNGU kuwasahau wateule wake wanaomcha yeye katika KRISTO YESU na waombaji.
Mimi Peter Mabula sijui mazingira unayopitia wewe rafiki yangu unayesoma ujumbe huu lakini ni  ukweli  mmoja kwamba MUNGU hajakusahau .

✓✓Mimi sijui hitaji lako la muda mrefu ni nini lakini ukweli mmoja  ni kwamba Bwana YESU KRISTO hajakusahau na anakumbuka Maombi uliyoomba katika jina lake hivyo atakutendea.

✓✓Inawezekana Yuko Mtu anayesoma ujumbe huu amechoka kwa habari ya kusubiri Ndoa yake au Uzao au Kazi au Kupona ugonjwa lakini ndugu yangu Ninao ujumbe leo kwamba "MUNGU hajakusahau " atakutendea sawasawa na mahitaji yako. 
Endelea kumwamini Bwana YESU KRISTO, endelea kuomba, endelea kumsikiliza ROHO MTAKATIFU na endelea kutimiza wajibu wako kwa KRISTO YESU.

√ Kuna watu hufanya maombi lakini inafika muda wanakata tamaa na kuacha maombi wakidhani MUNGU amewasahau.

√ Kuna mtu anasubiri muujiza wake lakini akiona muujiza huo umechelewa , anadhani MUNGU amemsahau, Ndugu MUNGU wa Mbinguni hajakusahau.

✓ inawezekana Raheli alidhani MUNGU amemsahau lakini MUNGU alikuwa hajamsahau  ndio maana  Biblia inasema  akasikia Maombi yake kulingana na majira aliyokusudia MUNGU akamzaa Mtu sahihi kwa majira sahihi ili akaliishi kusudi la MUNGU sahihi.
Mwanzo 30:22-24 "MUNGU akamkumbuka Raheli; MUNGU akamsikia, akamfungua tumbo.  Akapata mimba, akazaa mwana, akasema, MUNGU ameondoa aibu yangu. Akamwita jina lake Yusufu, akisema, BWANA aniongeze mwana mwingine."

Ndugu, Raheli alikuwa tasa kabisa lakini akazaa, Wewe utazaa kwa jina la YESU KRISTO wewe ambaye hitaji lako ni uzao katika Ndoa yako.

Wewe utapata mwenzi wa Ndoa na utafunga ndoa takatifu wewe ambaye hitaji lako ni Ndoa.

✓ Inawezekana Bartmayo alijua maisha yake yote atakuwa kipofu lakini MUNGU alikuwa hajamsahau kwa uponyaji, siku ikafika  Bwana wetu YESU KRISTO akamponya.

  Marko 10:46-52 " Wakafika Yeriko; hata alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake, na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando ya njia. Naye aliposikia ya kwamba ni YESU Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi, YESU, unirehemu. Na wengi wakamkemea ili anyamaze, lakini alizidi kupaza sauti, Mwana wa Daudi, unirehemu. YESU akasimama akasema, Mwiteni. Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, Jipe moyo; inuka, anakuita.  Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea YESU. YESU akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona. YESU akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani."

Ndugu, Mimi Peter Mabula kwa macho yangu  nimewahi kushuhudia YESU KRISTO akiponya Kansa, Ukimwi na magonjwa mengine makubwa makubwa.
Mimi mwenyewe Mwaka 2010  YESU KRISTO aliniponya ghafla tu mwili wangu baada ya kupata ajali mbaya nikiwa Zanzibar na madaktari walisema nikisikia kwamba "huyu hawezi Kupona kwa sababu kichwani damu imechanganyikana na ubongo" lakini Malaika wa MUNGU akaniambia kwa Sauti kwamba "Daktari wa Duniani anasema huwezi Kupona lakini Daktari wa Mbinguni YESU KRISTO amekuponya" siku 5 baadae nilikuwa mzima na kuondoka Hospitali huku Daktari pale hospitali akisema "Huyo MUNGU uliyenaye mshike sana maana sijawahi kuona mgonjwa wa kiwango hiki amepona"
Ndugu yangu unayesoma masomo yangu ukiwemo na ujumbe huu nakuhakikishia ya kwamba MUNGU hajakusahau na ukikaa vizuri na Bwana YESU KRISTO hakika unapona haijalishi ni  ugonjwa gani.
Mwamini Bwana YESU KRISTO na mpokee kama Mwokozi wako, okoka na omba au kuombewa na utapona hakika katika jina la YESU KRISTO.
Acha manung'uniko na malalamiko, endelea mbele kwa utakatifu na Maombi na MUNGU wa Mbinguni anaenda kukutendea na kuwashangaza adui zako waliodhani hutafanikiwa.

✓✓ Yuko mtu alikuwa hana nguvu za kutembea ili aingie kisimani maji yakitibuka mara moja kwa mwaka lakini akakutana na mtenda miujiza YESU KRISTO akamponya bila kuingia kisimani wala bila Maji ya namna yeyote, hata Wewe unayekimbilia Maji ya upako nakuomba mkimbilie YESU KRISTO na sio Maji ya upako wala mafuta. Achana na vitu hivyo.

Yohana 5:2-9 " Na huko Yerusalemu penye mlango wa kondoo pana birika, iitwayo kwa Kiebrania Bethzatha, nayo ina matao matano. Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza, [wakingoja maji yachemke.  Kwa maana kuna wakati ambapo malaika hushuka, akaingia katika ile birika, akayatibua maji. Basi yeye aliyeingia wa kwanza baada ya maji kutibuliwa, akapona ugonjwa wote uliokuwa umempata.]
 Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane. YESU alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu. YESU akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende. Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda. Nayo ilikuwa ni sabato siku hiyo.

✓Ndugu, inawezekana imefika hatua unadhani YESU KRISTO amekusahau lakini hajakusahau Ndugu, ongeza imani kwake na omba katika jina lake.

√√ inawezekana Wewe ni Ni Binti au Kijana kwa habari ya ndoa, au Kazi  n.k MUNGU hajakusahau, endelea kuomba na kuishi maisha matakatifu.

-√√ Inawezekana wewe hitaji lako ni Kupata kazi,  au Kupona au kupata kibali, Ndugu  MUNGU hajakusahau, endelea kunyenyekea kwake na timiza wajibu wako kwa KRISTO YESU.

   Nini ufanye?

1. Endelea mbele katika KRISTO na kutimiza wajibu wako kwa MUNGU 
               
Kutoka 14:15 "BWANA akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele."


2. Endelea kufanya maombi katika jina la YESU KRISTO.

  1 Wathesalonike 5:17 "ombeni bila kukoma;"

3. Endelea kumsikiliza ROHO MTAKATIFU na kufuata maelekezo yake.

Yohana 14:17 "ndiye ROHO wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.''

Yohana 14:26 "Lakini huyo Msaidizi, huyo ROHO MTAKATIFU, ambaye BABA atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia."

4. Omba nguvu zako za Rohoni zinazofanya usirudi nyuma.

Isaya 35:3 "Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea."

Zaburi 84:5 "Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako(MUNGU), Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake."

5. Usiwasikilize watu wanaokutoa katika mpango wa MUNGU na katika Wokovu wa KRISTO.

Mithali 11:9 "Asiyemcha MUNGU humpoteza jirani yake kwa kinywa chake; Bali wenye haki watapona kwa maarifa."

6. Endelea kumngoja MUNGU 
                
Zaburi 27:14 "Umngoje BWANA, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje BWANA."

7. Tumia akili baada ya Maombi kwa mambo ambayo yanahitajika utumie akili pia 

   1 Petro 4:7 "Lakini mwisho wa mambo yote umekaribia; basi, iweni na akili, mkeshe katika sala."

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU KRISTO Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU KRISTO Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.
+255714252292(Whatsapp, Sadaka ya kuipeleka Injili mbele, Ushauri na Maombezi)
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments