ACHA KUWAPA UTUKUFU WANADAMU.

 

Peter na Jemimah Mabula baada ya ibada, wakiwa na Watumishi wengine wa Bwana YESU KRISTO



Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe sana Ndugu zangu wote.
Jifunze kitu kupitia ujumbe wangu huu mfupi.

✓✓Kwanini MUNGU akubariki kisha shukrani umpe mwingine na sio MUNGU?

Ulilia sana kwenye maombi kwamba upate mchumba, MUNGU amekupa na shukrani zote unampa mchumba na sio MUNGU.

YESU amekuponya baada ya watumishi kukuombea, wewe shukrani zote unawapa watumishi hadi unawasujudia.

Kuanzia Leo jifunze kumpa MUNGU utukufu.

Kumbu 32:3 "Maana nitalitangaza Jina la BWANA; Mpeni ukuu MUNGU wetu."

Ulikuwa unateswa sana na vifungo vya Giza, kwa Neema Bwana YESU amekuondolea vifungo, wewe sifa zote na heshima na shukrani umewapa watumishi ambao hata wao hawajui uliponaje hata kama ni wao walikuombea.

Mlikuwa hamna mtoto kwa miaka 10 katika ndoa yenu, kwa Neema ya MUNGU kwa njia ya maombi YESU KRISTO anawabariki uzao. Sasa wewe kila siku asubuhi mchana na jioni unamshukuru Mumeo au mkeo kwa kukupa uzao, unasahau ni MUNGU tu ndio kawabariki uzao.
Mbona mkeo au mumeo kwa miaka 10 hakukupa uzao?
Umesahau au?

Ndugu mtukuze MUNGU

Zaburi 50:15 "Ukaniite siku ya mateso; Nitakuokoa, na wewe utanitukuza."

Umefanikiwa kiuchumi au kikazi baada ya kuombewa, wewe sasa kila siku asubuhi hadi jioni unamtaja mtumishi aliyekuombea wakati aliyekutendea muujiza ni MUNGU wa huyo mtumishi na sio huyo mtumishi.

Biblia inasema Mshukuruni JEHOVAH MUNGU wa uzima kwa maana yeye fadhili zake ni za milele.

Jifunze kumpa Bwana YESU KRISTO utukufu wote.
1 Nyakati 16:28 "Mpeni BWANA, enyi jamaa za watu, Mpeni BWANA utukufu na nguvu."

Hakuna mwanadamu mwenye fadhili za milele hivyo mshukuru MUNGU na mpe heshima stahiki.
Sina maana mtumishi aliyekuombea usimshukuru Bali mshukuru Mara moja ila shukrani hiyo kwa mwanadamu isiwe ya kumpa heshima na sifa mwanadamu huyo.
Heshima, sifa, utukufu na adhama ni vya MUNGU tu.

Zaburi 136:3-4 " Mshukuruni BWANA wa mabwana; Kwa maana fadhili zake ni za milele.Yeye peke yake afanya maajabu makuu; Kwa maana fadhili zake ni za milele."

MUNGU akubariki
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.
+255714252292
Ubarikiwe.

Comments