KANUNI TANO(5) ZA KUPOKEA KUTOKA KWA MUNGU.

Mwl Peter Mabula.



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni sana tujifunze Neno la MUNGU alie hai milele.
Naamini kila mtu anatamani kupokea baraka kutoka kwa MUNGU, ni sawa kabisa kutamani hivyo lakini pia ni muhimu kuzijua njia za MUNGU zinazoweza kukufanya upokee kutoka kwa MUNGU.
Hapa chini niimekuandalia kanuni za Kibiblia za kukufanya upokee kutoka kwa MUNGU na kanuni hizo zote lazima ziambatane na mtu anayehitaji kupokea kutoka kwa MUNGU.
Sio mtu ashike kanuni moja bali ashike zote ndipo atakuwa mtu wa kupokea kutoka kwa MUNGU.

Kanuni za kupokea kutoka kwa MUNGU.

1. Kanuni za kwanza ya kupokea ni kutoa.

Luka 6:38 "Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa."

Kwanini utoe?

Ni kwa sababu kutoa ni kupanda katika ufalme wa MUNGU hivyo utapokea kama ulipanda kwa kutoa kwa MUNGU.

2 Wakorintho 9:6 "Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu."

Kutoa ni ufunguo wa kupokea.

Mithali 11:24-25 "Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi; Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji. Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa; Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe."

Unatoa kwa njia gani?

a. Unatoa fungu la kumi na dhabihu.

Malaki 3:10 "Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la."

b. Kutoa sadaka.

Walawi 1:1-2 " BWANA akamwita Musa, na kusema naye kutoka katika hema ya kukutania, akamwambia,
Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtu wa kwenu atakapomtolea BWANA matoleo, mtatoa matoleo yenu katika wanyama wa mifugo, katika ng'ombe na katika kondoo."

c. Kusaidia wahitaji.

Kumbu 15:11 "Kwa maana maskini hawatakoma katika nchi milele; ndipo ninakuamuru na kukuambia, Mfumbulie kwa kweli mkono wako nduguyo, mhitaji wako, maskini wako, katika nchi yako."

d. Kuitegemeza kazi ya MUNGU.

Hagai 1:8,10 " Pandeni milimani, mkalete miti, mkaijenge nyumba; nami nitaifurahia, nami nitatukuzwa, asema BWANA. Basi, kwa ajili yenu mbingu zimezuiliwa zisitoe umande, nayo nchi imezuiliwa isitoe matunda yake."

Kuisahau kazi ya MUNGU kunaweza kusababisha baadhi ya vitu vyema kwako kuzuiliwa, hivyo ukiwa mtu wa kuitegemeza kazi ya MUNGU huo ni Mlango wa kupokea maana hakuna kizuizi.

e Nadhiri

Hesabu 30:2 "Mtu atakapomwekea BWANA nadhiri, au, atakapoapa kiapo ili kufunga nafsi yake kwa kifungo, asilitangue neno lake; atafanya sawasawa na hayo yote yamtokayo kinywani mwake."

Hivyo kazi ya kwanza ya kupokea ni kutoa, kama wewe sio mtoaji kuna baraka za kiroho na kimwili hutahusika nazo kamwe.

Kumbuka pia kuna mafanikio na baraka, wapo watu wamefanikiwa lakini hawajabarikiwa ndio maana unaweza kumkuta tajiri lakini kila siku mawazo , anatamani kufa na hana furaha na mali zake kabisa.
Hivyo ni muhimu sana kutafuta baraka za MUNGU na kanuni ya kubarikiwa ya kwanza ni kutoa.
Hakikisha unakuwa mtoaji katika MUNGU.
Maana baraka ya MUNGU huwa haichanganywi na huzuni.

Mithali 10:22 "Baraka ya BWANA hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni nayo."

Hivyo ihitaji baraka ya MUNGU huku ukitimiza sana kanuni hii ya Kibiblia ya kutoa.

2. Kanuni ya pili ya kupokea ni kuisikiliza sauti ya MUNGU na kuifanyia kazi.

Kumbu 28:1-2 " Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako."

Sauti ya MUNGU inaweza kukuijia kwa njia nyingi kama ndoto, maono, mahubiri na ufunuo wa ROHO MTAKATIFU, izingatie sana sauti ya MUNGU kama unataka kupokea kutoka kwa MUNGU.

Hata kanuni ya kutoa iliyo bora huambatana na kuisikiliza sauti ya ROHO MTAKATIFU kupitia ufunuo au Neno la MUNGU.

Unaweza ukajifunza Neno la MUNGU na ukapata msukumo wa kutoa basi ujue MUNGU anasema na wewe juu ya kutoa.
Lakini pia sauti ya MUNGU huwa ina maelekezo ya MUNGU hivyo yako maelekezo ya MUNGU ya namna nyingi, muhimu yafanyie kazi maelekezo ya MUNGU aliyosema na wewe kwa njia yeyote.

Ukitaka kupokea kutoka kwa MUNGU basi izingatie sauti ya MUNGU inayokuwa inasema na wewe, hata kupitia somo hili inawezekana kabisa MUNGU akawa anasema na wewe, muhimu tu ukithibitisha ni MUNGU anasema na wewe kupitia somo hili basi zingatia.

Kumbuka pia kuna kulisikia Neno la MUNGU na kuna kuisikia sauti ya Neno la MUNGU.
Watu wote wanaweza kulisikia Neno la MUNGU lakini watakaofanyia kazi hilo Neno la MUNGU hao ndio wameisikia sauti ya Neno la MUNGU.

3. Kanuni ya tatu ya kupokea ni kuwa mtu wa maombi.

Mathayo 7:7-8 "Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa."

Huwezi ukapewa kama hujaomba upewe hivyo maombi ni muhimu sana.
Kumbuka sadaka hufungua mlango lakini maombi huleta hicho kilichofunguliwa mlango, hivyo utoaji ni vyema sana ukaambatana na maombi sahihi katika jina la YESU KRISTO.
Maombi yanahitajika sana kama mtu unataka kupokea kutoka kwa MUNGU.

4. Kanuni ya nne ya kupokea ni kuwa ni wa shukrani mbele za MUNGU.

Zaburi 50:23 "Atoaye dhabihu za kushukuru, Ndiye anayenitukuza. Naye autengenezaye mwenendo wake, Nitamwonyesha wokovu wa MUNGU."

Kuna watu hutendewa na MUNGU ila hawana shukrani kwa MUNGU, ni hatari sana.
Ukitaka uwe mtu wa kupokea kwa MUNGU hakikisha pia unakuwa mtu wa shukrani kwa MUNGU.
Shukrani hufungulia kupokea zaidi.

Walawi 22:29 "Tena mtakapomchinjia BWANA dhabihu ya shukrani, mtamchinja ili mpate kukubaliwa."

Hivyo ukizingatia kuwa mtu wa shukrani kwa MUNGU ujue umefungulia kupokea zaidi kutoka kwa MUNGU.
Mshukuru MUNGU kwa maombi na kwa sadaka njema ya shukrani.

5. Kanuni ya tano ya kupokea ni wewe kuacha dhambi na maovu.

Kuna vitu huzuiliwa kwa sababu ya dhambi na maovu ya mtu.

Isaya 59:1-2 "Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia."

Hivyo unaweza usipokee kutoka kwa MUNGU kwa sababu tu ya dhambi zako.
Dhambi humzuia MUNGU kukupa hivyo ili upokee kwa MUNGU zingatia sana kujitenga mbali na dhambi na maovu.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU na zingatia sana hizo Kanuni zote tano utamuona MUNGU.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, kuandika meseji, Sadaka ya kuipeleka injili Mbele na whatsapp).
Ubarikiwe

 

Comments