![]() |
Na Mwl Peter Mabula, Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe rafiki yangu mahali kokote ulipo.
Leo katika awamu hii ya pili tunayo Maombi ya kuomba kuondoka katika Mlima uliokaa Muda mrefu.
Ukisoma Kumb 1:6-7 unaona MUNGU akiwaambia Waisraeli waondoke katika mlima waliokaa muda mrefu.
Biblia
inasema "BWANA, Mungu wetu, alituambia huko Horebu, akasema, MLIVYOKAA
KATIKA MLIMA HUU VYATOSHA; geukeni mshike safari yenu mwende nchi ya
milima ya Waamori, na mahali pote palipo karibu ya hapo, katika hiyo
Araba, na nchi ya vilima-vilima, na huko Shefela, na Negebu, na
pwani-pwani, nchi ya Wakanaani, na Lebanoni, mpaka mto huo mkubwa, mto
wa Frati."
Waisraeli walikuwa kwenye safari 2 kwa wakati mmoja.
●
Safari ya kwanza ilikuwa safari ya maisha, yaani kuishi ni safari
inayoendelea hadi pale Mtu anapomaliza Muda wake wa kuishi Duniani.
●Safari ya pili ilikuwa ni Safari ya kusafiri kwenda nchi ambayo MUNGU aliwaambia waende yaani Kaanani.
Mimi Peter Mabula na Wewe rafiki yangu wote pia tuko katika safari 2 kwa wakati mmoja.
■
Safari ya kwanza ni Safari ya Maisha ya Wokovu wa KRISTO ili tuipate
Uzima Wa Milele aliouahidi MUNGU kwa wampendao ndio maana tunaishi
Maisha Matakatifu.
■Safari
ya pili ni Safari ya kuzielekea Baraka zetu, kila baraka kwa wakati
wake au zile baraka zaidi ya moja ambazo huja kwa wakati mmoja.
Kuna Mtu baraka yake anaelekea Ndoa, mwingine kuzaa, mwingine kupata kazi, mwingine kupona ugonjwa, mwingine kushinda vita n.k
Sasa
katika ujumbe huu wa Maombi nimetumia Neno "Mlima" kama Biblia
inavyosema nikiwa na maana ya kukaa muda mrefu sehemu usiyoitaka,
naamini hata Waisraeli walikuwa wanataka kufika Kaanani na sio Kubaki
hapo Mlimani.
Kuna milima
ya kiroho inayoweza kumchelewesha mtu, anatamani kitu fulani kizuri
kitokee lakini imeshindikana kwa sababu yuko katika Mlima.
Kuna watu wanatumia muda mrefu kuzunguka kwenye mlima na sio kuondoka kwenye huo mlima ili wapokee baraka zao.
Waisraeli waliambiwa na MUNGU imetosha kuzunguka Mlima waondoke hapo.
Kumbu 2:3 "MLIVYOUZUNGUKA MLIMA HUU VYATOSHA; geukeni upande wa kaskazini."
●Je una changamoto ambayo ni kama unaizunguka tu yaani haikuachii?
◇ Je kiroho ni eneo gani umebaki muda mrefu unatamani kuondoka eneo hilo?
●Je
uko kwenye Ndoa lakini mlima wako ni kukosa mtoto muda mrefu? Leo
Mwambie Bwana YESU KRISTO kwamba unapoingia Mwaka mpya usibaki katika
eneo hilo la utasa bali ukapate Mtoto.
●Je unaumwa muda mrefu? Ni wakati wa kutoka katika mlima huo wa ugonjwa.
●
Je mlima wako uliokaa muda mrefu ni madeni au vifungo au manyanyaso au
nini? Katika jina la YESU KRISTO kupitia maombi haya unaenda kutoka
katika huo mlima uliokaa muda mrefu.
Ukiomba kuna Neema ya MUNGU ya kukuondoa katika tatizo la Muda mrefu.
Ukiomba kuna neema ya MUNGU ya kukupa kujua nini cha kufanya ili utoke salama katika mlima huo uliokaa muda mrefu.
Ngoja nikupe mfano huu, ukisoma
Mwanzo
28:2 Biblia inasema "Ondoka, uende Padan-aramu, mpaka nyumba ya
Bethueli baba ya mama yako, ukajitwalie huko mke katika binti za Labani,
ndugu wa mama yako."
Yakobo inawezekana alikuwa na
maswali mengi juu ya nani atafaa kuwa mke wake hadi alipopata ufahamu
wa ataoa wapi na ataoa familia ya nani?
■
Inawezekana hujui utatokaje katika changamoto uliyopo ila sasa katika
mwaka mpya unaouendea kupitia maombi haya ukafanikiwe kwa jina la YESU
KRISTO.
●Nini nataka kusema?
■■Omba
kwa MUNGU utoke katika tatizo au jaribu ambalo umekaa nalo muda mrefu
hadi umechoka, kwa YESU KRISTO inawezekana kutoka kwenye tatizo hilo.
●●Inawezekana
unaumwa na umeambiwa huponi, huo ni mlima mkubwa lakini YESU KRISTO
kukutoa hapo kwa kukuponya ni sekunde tu, mwamini na omba kupitia ufunuo
huu wa Maombi.
●●
Inawezekana umeambiwa huwezi kuzaa, Dada mmoja aliambiwa hana yai hata
moja la uzao, mwamini YESU KRISTO anayeweza kubadilisha historia yako
ndugu. Katika mwaka mpya unaouendea mweleze MUNGU yatosha kukaa katika
hali ya kukosa mtoto, omba mwakani uwe ni mwaka unaoambatana na uzao
kwako, katika jina la YESU KRISTO itawezekana.
Ni
kweli umechoka na masimango ya watu kama huyu anayesema katika Zaburi
6:6-7 "kwamba Nimechoka kwa kuugua kwangu; Kila usiku nakieleza kitanda
changu; Nalilowesha godoro langu kwa machozi yangu. Jicho langu
limeharibika kwa masumbufu, Na kuchakaa kwa sababu yao wanaoniudhi."
Lakini ukiomba katika jina la YESU KRISTO huku ukiishi maisha matakatifu
hakika MUNGU atakutendea miujiza ghafla na utakuwa Kawa hawa ambao
walipokutana na miujiza ya MUNGU walidhani wanaota ndoto kumbe sio ndoto
bali ni kweli.
Zaburi
126:1-2 " BWANA alipowarejeza mateka wa Sayuni, Tulikuwa kama waotao
ndoto. Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko, Na ulimi wetu kelele za
furaha. Ndipo waliposema katika mataifa, Bwana amewatendea mambo makuu."
●Watu
wengine milima yao ni kukosa kazi, Kukosa Mtu wa kufunga nae Ndoa,
wengine milima yao ni madeni, wengine kunyanyaswa, wengine magonjwa,
kuonewa,kuibiwa kila mara , ajali, mikosi, balaa na wengine milima yao
ni vifungo vya giza. Leo omba ukisema "Yatosha kukaa katika mlima huu wa
................(utaje), sasa kwa jina la YESU KRISTO natangaza kutoka
katika mlima huu kuanzia leo, ninaomba mwaka mpya ninaouendea tatizo
hili halitanitesa tena"
Nini Ufanye katika Maombi?
1. Omba neema ya MUNGU ya kukutoa katika hiyo changamoto.
1 Wakorintho 15:10 "Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; ......"
Neema ya MUNGU itakufanya utoke kwenye changamoto, utakuwa vile atakavyo MUNGU.
2. Omba maombi ya Imani ya kuondoka katika Mlima huo
Yohana 16:24 "Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu."
3. Pambana kimaombi na aliyeshikilia baraka yako ambayo MUNGU ameshakupa.
Kumbu
"2:24 Ondokeni, mshike safari yenu, mvuke bonde la Arnoni; tazama,
nimemtia Sihoni Mwamori mfalme wa Heshboni mkononi mwako, na nchi yake;
anzeni kuimiliki, mshindane naye katika mapigano."
Hapa chini ni ya MAOMBI YA KUONDOKA KWENYE MLIMA ULIOKAA MUDA MREFU.
Maombi
haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba
kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi
yake.
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini.
MAOMBI YA KUONDOKA KWENYE MLIMA ULIOKAA MUDA MREFU.
MUNGU
Baba ninakuabudu kwa kuwa Wewe ni Mwema BWANA. Ninakushukuru kwa neema
yako, Asante BWANA Mungu maana umenilinda Mwaka huu wote hadi kufika
leo.
Niko mbele zako
katika jina la YESU KRISTO nikiomba unisamehe dhambi zangu zote,
nisamehe makosa yangu yote na nisamehe na maovu yangu yote.
Ninatubia
dhambi nilizowahi kutenda zote, dhambi ninazozikumbuka na dhambi zote
pia ambazo sizikumbuki ila kwako BABA wa Mbinguni zinafahamika.
Kwa damu ya YESU KRISTO ya agano jipya naomba unitakase roho yangu yote, nafsi yangu yote na mwili wangu wote.
Niko
sasa mbele zako Bwana YESU KRISTO nikiomba neema yako ya kunitoa katika
kila milima niliyokaa muda mrefu, naomba neema ya kutoka hapo ili sasa
nami nikafanikiwe kwa jina lako takatifu.
Bwana wangu YESU KRISTO ninaomba neema yako ya kuniondoa katika mlima wa utasa na ugumba na nikazae katika ndoa yangu sasa.
Bwana
wangu YESU KRISTO ninaomba neema yako ya kuniondoa katika mlima wa
madeni na masumbufu na sasa nipate mpenyo wa kulipa madeni yote na
masumbufu yaachie maisha yangu.
Bwana
wangu YESU KRISTO ninaomba neema yako ya kuniondoa katika mlima wa
kukosa kazi na sasa nikapate kazi katika jina la YESU KRISTO.
Bwana
wangu YESU KRISTO ninaomba neema yako ya kuniondoa katika mlima wa
vifungo vya giza na sasa nikawe huru kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi
wangu aliye hai.
Bwana
wangu YESU KRISTO ninaomba neema yako ya kuniondoa katika mlima wa
magonjwa na sasa nikapone kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye
hai.
Bwana wangu
YESU KRISTO ninaomba neema yako ya kuniondoa katika mlima wa mateso na
sasa nikaipate furaha ya kudumu kwenye maisha yangu.
Bwana wangu YESU KRISTO ninaomba neema yako ya kuniondoa katika mlima wa kiroho niliokaa muda mrefu nikiteseka.
Naiombea familia yangu na Uzao wangu watoke kwenye milima ya matatizo katika jina la YESU KRISTO.
Imeandikwa katika Kumb 1:6 kwamba "MLIVYOKAA
KATIKA MLIMA HUU VYATOSHA" sasa natangaza kwa jina la YESU KRISTO
kutoka kwenye kila mlima mbaya ambao nilikaa muda mrefu.
Natangaza kutoka kwenye magumu niliyokaa muda mrefu.
Natangaza kutoka kwenye tatizo niliyokaa muda mrefu, kwa jina la YESU KRISTO ninatoka sasa katika tatizo hilo.
Imeandikwa katika Kumbu
2:3 "MLIVYOUZUNGUKA MLIMA HUU VYATOSHA" Kwa jina la YESU KRISTO
ninatangaza kutoka katika mlima wa kiroho niiozunguka muda mrefu bila
kutoka hapo. Haiwezekani kila nikipata Mchumba naishia uchumba tu na sio
Ndoa, nimechoka kuzunguka Mlima wa uchumba tu sasa kwa jina la YESU
KRISTO ninatoka katika mlima huo na Sasa naenda kuingia katika Ndoa
takatifu yenye ushuhuda mkubwa.
Kila
adui wa kiroho na kimwili anayenizuilia na kunilazimisha nibaki katika
hali mbaya tu, huyo adui namtowesha kwa jina la YESU KRISTO na sehemu
yake haitakuwepo tenamaishani mwangu.
Ninakushukuru
MUNGU Baba kwa kuniondoa katika milima ya matatizo niliyokuwepo na Sasa
ni huru kabisa kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai Milele.
Nakushukuru MUNGU Baba kwa Neema hii.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea ushindi.
Asante MUNGU BABA mwenyezi kwa kunipa ushindi leo.
Asante Bwana YESU maana damu yako na jina lako vimenishindia.
Asante ROHO MTAKATIFU maana katika wewe nimeshinda.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea ushindi.
Amen Amen.
MUNGU akubariki sana.
Omba sana katika jina la YESU KRISTO na utamuona MUNGU wa Miujiza.
MUNGU akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.
+255714252292
Ubarikiwe
Comments