MASWALI NA MAJIBU -3

 

Majibu na Mwl Peter Mabula.



Haya ni sehemu ya maswali ambayo baadhi ya marafiki zangu waliniuliza kisha mimi nikawajibu.

Jifunze kitu katika maswali haya na majibu.

1. Swali la kwanza.

Mtumishi kwanini tunabatizwa kwa jina la MUNGU Baba, MWANA na la ROHO MTAKATIFU ?

Majibu ya Mtumishi Mabula.

Tunabatizwa kwa jina la MUNGU Baba, Mwana na Roho Mtakatifu kwa sababu Mwokozi wetu YESU KRISTO ndiye aliyeagiza, agizo la YESU KRISTO ndio agizo la MUNGU mwenyewe.

Mathayo 28:19-20 " Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari."

2. Swali la pili.

Mtumishi Kwanini Biblia inaitwa maandiko matakatifu?

Majibu ya Mtumishi Mabula.

Ni kwa sababu kwanza neno "Biblia " limetokana na Neno "Biblos " la lugha ya Kigiriki ambalo kwa Kiswahili lina maana ya "Kitabu cha vitabu vitakatifu " Hii ni kwa sababu Biblia ni mkusanyo wa vitabu vilivyo maandiko matakatifu.

Biblia ni maandiko matakatifu kwa sababu kwanza ni maandiko matakatifu kama ilivyo na pia hata ndani ya Maandiko hayo pia yanajithibitisha kwamba ni maandiko matakatifu.

Warumi 1:2 "ambayo MUNGU amekwisha kuiahidi kwa kinywa cha manabii wake katika maandiko matakatifu;"

Pia Biblia ni maandiko matakatifu kwa sababu ni Neno la MUNGU aliye mtakatifu.

1 Samweli 2:2 "Hakuna aliye mtakatifu kama BWANA; Kwa maana hakuna ye yote ila wewe, Wala hakuna mwamba kama MUNGU wetu."

3.Swali la tatu.

Mtumishi Mabula Nini maana ya ushirika na ROHO MTAKATIFU?

Majibu ya Mtumishi Mabula.

Ushirika na Roho Mtakatifu ina maana hizi tatu.

A. Ushirika na ROHO MTAKATIFU ni hali ya mteule wa KRISTO kuungana pamoja na ROHO MTAKATIFU ili kufanya jambo jema limpasalo mteule huyo.

1 Yohana 4:4 "Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na MUNGU nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia."

ROHO MTAKATIFU kuwa ndani yako maana yake wewe una ushirika naye na uko tayari kumtii na kumsikiliza.

B. Ushirika na ROHO MTAKATIFU ni hali ya mteule wa KRISTO kuwa ROHO MTAKATIFU na kisha kumruhusu ROHO MTAKATIFU kumsaidia mteule huyo katika kazi fulani, muongozo fulani na kila msaada wa kiroho.

Zaburi 32:8 " Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama."

Kwa hiyo kama Kanisa hai la KRISTO duniani ni lazima sana tuwe na ushirika na ROHO MTAKATIFU.

2 Wakorintho 13:14 " Neema ya Bwana YESU KRISTO, na pendo la MUNGU, na ushirika wa ROHO MTAKATIFU ukae nanyi nyote."

C. Maana nyingine ya ushirika na ROHO MTAKATIFU ni kuwa na ushirikiano na ROHO MTAKATIFU katika mambo yote maana sisi tu watoto wa MUNGU.

Warumi 8:14" Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU."

4. Swali la nne.

Mtumishi Mabula unaweza kuniambia mstari mfupi zaidi katika bibilia ni upi? Na msitar mrefu ni upi?

Majibu ya Mtumishi Mabula.

Mstari mfupi zaidi ndani ya Biblia inategemea na lugha husika, kwa kifupi katika Biblia ya KJV Kiswahili naweza nikakujbu hivi mstari mfupi zaidi ndani ya Biblia kwa lugha ya Kiswahili ni Kutoka 20:13 ambao pia unapatikana katika Kumbu 5:17 ikisema kwamba "Usiue."

Na mstari mrefu zaidi ndani ya Biblia katika lugha ya kiswahili tunaweza kusema ni

Esta 8:9 ambapo Biblia inasema "Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa pale pale, siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa tatu, ndio mwezi wa Siwani; na kama vile Mordekai alivyoamuru, Wayahudi wakaandikiwa, pamoja na maakida na maliwali, na wakuu wa majimbo toka Bara Hindi mpaka Kushi, majimbo mia na ishirini na saba, kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; na Wayahudi kwa mwandiko wao na kwa lugha yao."

5. Swali la tano.

Mtumishi Mabula naomba unisaidie Ubatizo ni nini?

Majibu ya Mtumishi Mabula.

Neno ''ubatizo'' linatokana na Neno la kigiriki ''Baptizo'' ambalo katika kiingeleza ni ''Baptism'' Lenye maana ya Zamisha kwenye maji.

A. KUBATIZWA NI KUITIMIZA HAKI YOTE YA MUNGU .

Mathayo 3:14-15 '' Lakini Yohana alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu? YESU akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali.''

-Inatupasa kuitimiza Haki yote ya MUNGU kupitia ubatizo kama BWANA YESU aliposema hapo juu.

-Ukikataa kubatizwa maana yake unampinga MUNGU.

B. KUBATIZWA NI ISHARA YA KUFA NA KUFUFUKA NA YESU KRISTO.

Wakolosai 2:12 '' Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za MUNGU aliyemfufua katika wafu. ''

-Lazima tuzike matendo yetu mabaya na tufufuke pamoja na KRISTO tukiwa safi, jambo hilo linafanyika tukiwa hapa hapa duniani sio baada ya kufa.

-Tukifa tutakufa lakini kwasababu tumekufa na KRISTO tutafufuka naye vile vile.

C. KUBATIZWA NI KUTII USHAURI WA MUNGU.

Luka 7:29-30 '' Na watu wote na watoza ushuru waliposikia hayo, waliikiri haki ya MUNGU, kwa kuwa wamebatizwa kwa ubatizo wa Yohana. Lakini, Mafarisayo na wana-sheria walilipinga shauri la Mungu juu yao, kwa kuwa hawakubatizwa naye. ''

-Mafalisayo walilipinga shauri ya MUNGU yaani ubatizo.

-Kumbe kupinga ubatizo au kukataa kubatizwa ni kulikataa shauri la MUNGU.

-Kubatizwa ni kulitii shauri la MUNGU. Ni kuutii ushauri wa MUNGU.

Warumi 6:3-4 '' Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika KRISTO YESU tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama KRISTO alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa BABA, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima. ''

Kwa kifupi ubatizo wa maji ni ishara ya nje inayoonyesha badiliko la ndani.

6. Swali la sita.

Mtumishi Mabula naomba unisaidie, ili mtu abatizwe anatakiwa awe na umri gani?

Majibu ya Mtumishi Mabula.

Anayebatizwa lazima amwamini kwanza YESU KRISTO ya Kuwa ni BWANA na Mwokozi wake na atubu ndipo anabatizwa.

Marko 16:16 '' Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.''

Biblia hapa inathibitisha kwamba mtu anamwamini kwanza YESU ndio anabatizwa. hivyo kumbe kuwabatiza watoto ni matokeo ya kushindwa kuijua na kuielewa Biblia inavyotaka yenyewe.

Yohana hakumbatiza mtu ambaye hajatubu, ndio maana aliwahubiria kwanza wakatubu ndipo akawabatiza.

Matendo 2:38 ''Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake YESU KRISTO, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha ROHO MTAKATIFU.''

Hata hapo Biblia inathibitisha kwamba mtu anamwamini kwanza YESU na kutubu ndipo anabatizwa. kwa andiko hili mtoto mchanga hana sifa za kubatizwa maana mtoto hawezi kutubu na hajui atubu nini.

Tuone mfano mwingine huu.

Matendo 8:12 '' Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa MUNGU, na jina lake YESU KRISTO, wakabatizwa, wanaume na wanawake. ''

Kwa hiyo umri wa kubatizwa ni umri anaojitambua, anatambua mema na mabaya na anajua thamani ya kuokoka hivyo hakuna umri maalumu ila awe ana akili za kufuata hayo niliyoyaeleza juu.

7. Swali la saba.

Mtumishi Mabula naomba unisaidie.

Kuabudu ni nini?

Majibu ya Mtumishi Mabula.

Maana ya kuabudu ni kumsujudia na kumtumikia unayemwabudu.

Neno kusujudu halina maana tu ya kuinamisha mgongo Bali Neno Kusujudu maana yake ni kushuka, kunyenyekea kwa heshima za kiroho.

Kushuka huku sio kuinama tu Bali ni kukubali kuwa chini ya unayemwabudu.

Kwanini nasema unayemwabudu?

Ni kwa sababu sio wote wanaofanya ibada basi ni ibada kwa MUNGU Baba wa mbinguni.

Sio wote wanaoabudu humwabudu JEHOVAH MUNGU pekee wa kweli.

Lakini kwa Kanisa la KRISTO ibada ni jambo la muhimu sana.

Waebrania 10:25 "wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia."

Neno kuabudu linatokana na neno ibada hivyo ni maneno yenye maana moja .

Mbarikiwa sana wote mliojifunza kitu katika maswali na majibu.

By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

Comments