MASWALI NA MAJIBU(sehemu ya 1)

 

 

 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.

Haya ni maswali ambayo baadhi ya marafiki zangu waliniuliza baada ya wao kusoma masomo yangu na mimi nikawajibu, inawezekana kuna kitu utajifunza hivyo fuatilia hadi Mwisho.

1. Swali la kwanza.

Mtumishi Mabula umetumia andiko la

Yeremia 33:8 "Nami nitawasafisha na uovu wao wote, ambao kwa huo wamenitenda dhambi; nami nitawasamehe maovu yao yote, ambayo kwayo wamenitenda dhambi, na kukosa juu yangu."

Naomba kujua, Baada ya mtu kuokoka umesamehewa dhambi zako zote.

Kwa nini bado mtu amekiri wokovu tena hata nyendo na maisha yake unaona kabisa yamebadilika na kumgeukia Mungu lakini bado yapo magonjwa na vifungo vinamfuata?

MAJIBU YA MTUMISHI PETER MABULA.

Kuna tofauti ya kusamehewa na kutakaswa.

Watu wengi wamesamehewa ila hawajatakaswa.

Mfano mtu mwenye mapepo anaweza kuongozwa sala ya toba au akatubu na kusamehewa na jina lake likaandikwa katika kitabu cha uzima lakini mtu huyo mapepo bado yako mwilini wake maana hajatakaswa.

✓✓Kutakaswa ni kuondolewa uchafu wa kiroho hivyo mtu akiishia tu kutubu na anasamehewa ila anakuwa bado anahitaji utakaso, inawezekana utakaso wake ni kwenye laana, magonjwa, vifungo n. K

Hivyo ni muhimu sana pia kusamehewa na kutakaswa.

Watu inawapasa kuomba kama hivi yaani kutubu na kutakaswa.

Zaburi 51:1-2 " Ee MUNGU, UNIREHEMU, Sawasawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu. UNIOSHE kabisa na uovu wangu, UNITAKASE dhambi zangu."

Huyu katika maombi yake hakuhitaji tu kuomba kusamehewa dhambi bali alihitaji na kutakaswa pia.

Kwa hiyo mkristo anahitaji kusamehewa na kutakaswa.

Watu wengi walipotubu watumishi waliwaambia wametakaswa pia lakini kama hayakufanyika maombi ya utakaso basi wanakuwa hawajatakaswa.

2. Swali la pili.

Mtumishi Mabula hivi kama mtu umeokoka na unaishi na mume bila kufunga ndoa kanisani je ni sawa au biblia inasema nini kuhusu hili?

MAJIBU YA MTUMISHI PETER MABULA.

Watu hawa kama waliamua kuchukuana ndani ya wokovu hao wanahitaji kutubu sana na kusaidiwa kiroho na wachungaji wao maana jambo walilolifanya ni baya sana.

✓✓Kama mtu uliolewa au kuoa ukiwa mpagani basi inahitajika toba kisha kubariki ndoa

Biblia inasema, kwa neno au kwa tendo fanyeni katika KRISTO, hivyo watu walioamua kuchukiana tu hawakufunga ndoa hiyo katika MUNGU hivyo ni dhambi

Wakolosai 3:17 "Na kila6 mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye."

Kama watu wa MUNGU inatupasa hata tendo na kuoa au kuolewa tulifanye katika MUNGU na sio katika shetani.

3. Swali la tatu.

Mtumishi, unapokuwa ni mzima na ni binti unaisubiri ahadi ya ndoa ni kweli tunasoma Mungu hachelewi anajibu kwa wakati lakini inafika mahali unakata tamaa na mwili ni dhaifu katika hili unamtiaje moyo mtu huyu, asante kaka kama utanipa ufafanuzi na Mungu akubariki.

MAJIBU YA MTUMISHI PETER MABULA.

Mtu wa namna hii namtia moyo kwa kumwambia amngoje MUNGU .

Zaburi 27:14 "Umngoje BWANA, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje BWANA."

Hakuna haja ya kuusikiliza mwili , jitenge na kuiga mabaya, jitenge na marafiki wabaya, jitenge na picha za ngono au video za ngono, wewe mche MUNGU, usiwashe tamaa za mwili wako

Warumi 13:14 "Bali mvaeni Bwana YESU Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake."

Jifunze kwa waliovumilia kisha wakaingia katika ndoa njema zenye ushuhuda.

Unaweza kukimbilia kuolewa kwa njia za kipepo ambazo shetani amepanda mapando na baada ya muda mfupi unaachwa kwa maumivu.

Kumbuka kwamba wewe uliletwa duniani na MUNGU hivyo ratiba yako ya duniani ina MUNGU kama unamcha MUNGU katika KRISTO YESU ujue MUNGU ndio anaijua ratiba yako hivyo hakika hatakupita kamwe utafunga ndoa na hakuna kitakachopungua.

Nakuomba mngoje MUNGU na atakupa baraka ya ndoa.

Zaburi 37:7 "Ukae kimya mbele za BWANA, Nawe umngojee kwa saburi; Usimkasirikie yeye afanikiwaye katika njia yake, Wala mtu afanyaye hila."

Kumbuka pia ukifanya uasherati kwa sababu ya tamaa zako ujue kuna jehanamu kwa watu wa namna hao wasipopata neema ya kutubu.

1 Kor 6:9 ''Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,''

Hivyo katika maisha yako epuka sana uasherati.

Vumilia hadi ufunge ndoa maana hutapata madhara yeyote.

Endelea na maombi na MUNGU atakupa mwenzi wako.

1 Kor 6:18 ''Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. ''

4. swali la nne.

Samahani mwalimu naomba unieleze maana ya mstari huu

Isaya 23:17 "Hata itakuwa mwisho wa miaka sabini, Bwana ataizuru nchi ya Tiro, naye atarudi apate ujira wake, atafanya ukahaba pamoja na falme zote za ulimwengu juu ya uso wa dunia."

MAJIBU YA MTUMISHI PETER MABULA.

Andiko hilo lina maana kwamba MUNGU atazuru nchi ya Tiro na kuona kinachofanyika huko Tiro, Moja ya ambavyo MUNGU atavikuta Tiro ni kumkuta mfalme wa Tiro amefanya ukahaba na wafalme wengine.

Na maana ya hilo neno "Ukahaba" hapo lina maana ya mapatano ya kishetani au mikataba ya kishetani.

Andiko hilo halina maana ya MUNGU kufanya ukahaba/mikataba mibaya na wafalme, hayo ni maneno ya wapinga Kristo

Andiko hilo katika tafsiriya BHN linasema hivi.

Isaya :23:17 BHN"

Baada ya miaka hiyo sabini, Mwenyezi-Mungu atauadhibu mji wa Tiro, nao utarudia kufanya uzinzi kwa kujiuza kwa mataifa yote ya dunia."

Hivyo ukahaba hapo unamhusu mfalme wa Tiro.

ushauri wangu ni kwamba hakuna andiko limekosewa ndani ya Biblia hivyo kama kuna andiko hujalielewa liangalie kwenye lugha zingine kama kiingereza utaelewa vyema, au kuangalia andiko hilo katika tafsiri zingine utalielewa vyema.

Usipolielewa andiko omba ufafanuliwe.

Usikubali kuwa sehemu ya wapotoshaji wa maandiko.

5. Swali la tano.

Mtumishi naomba kujua jambo hili.

Je kama mwanaume na mwanamke mlichukuana kienyeji mkiwa wapagani na baadae mke ndiyo akamjua Mungu, lakini Mungu awezaje kumtumia huyu na vipawa vyake hali yu mzinifu maana hajafunga ndoa, na je Mungu aweza kukaa na mtu huyo. Na je kama mume hayupo Tayari kubariki ndoa twaweza zidi kumuombea tu hadi Mungu atakaporuhusu

MAJIBU YA MTUMISHI PETER MABULA.

Hapa inatakiwa tu kubariki ndoa, lakini mume huyo anaweza kutakaswa kupitia mkewe pia, wabariki tu ndoa yao.

1 Wakorintho 7:13-14 " Na mwanamke, ambaye ana mume asiyeamini, na mume huyo anakubali kukaa naye, asimwache mumewe. Kwa maana yule mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe; na wangekuwa si safi; bali sasa ni watakatifu."

Hapa ni kuendelea kuomba tu ili mume akubali kubariki ndoa.

Barikiwa.

By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

Comments