NISALIMIENI WATU HAWA WAFUATAO.




Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU na ninayekuletea somo hili naitwa Mwl Peter Mabula.

Ukisoma Warumi 16:3-16 utakutana na watu mbalimbali wa Kanisa wakisamiliwa na Mtumishi wa MUNGU ambaye ni Mtume Paulo aliyekuwa mbali na wao.

Ni watu gani walisalimiwa katika salama hizo?

Ni Hawa hapa.

1. Nisalimieni watenda kazi katika KRISTO.

Warumi 16:3,9 " Nisalimieni Priska na Akila, watenda kazi pamoja nami katika KRISTO YESU; ........ Nisalimieni Urbano, mtenda kazi pamoja nami katika KRISTO, na Stakisi, mpenzi wangu.

2. Nisalimieni wapendwa walio malimbuko kwa ajili ya KRISTO.

Warumi 16:5 "Nisalimieni Epaineto, mpenzi wangu, aliye malimbuko ya Asia kwa KRISTO."

Hawa ni walioungana na KRISTO kupitia kumpokea na kufanya kazi yake.

Warumi 16:8 "Nisalimieni Ampliato, mpenzi wangu katika Bwana(YESU)."

3. Nisalimieni waliojitaabisha kwa ajili ya kazi ya MUNGU.

Warumi 16:6-7 " Nisalimieni Mariamu, aliyejitaabisha sana kwa ajili yenu. Nisalimieni Androniko na Yunia, jamaa zangu, waliofungwa pamoja nami, ambao ni maarufu miongoni mwa mitume; nao walikuwa katika KRISTO kabla yangu."

4. Nisalimieni wenye kukubaliwa katika KRISTO.

Warumi 16:10 "Nisalimieni Apele, mwenye kukubaliwa katika KRISTO. Nisalimieni watu wa nyumbani mwa Aristobulo."

5. Nisalimieni walio katika Bwana YESU KRISTO.

Warumi 16:11 "Nisalimieni Herodioni, jamaa yangu. Nisalimieni watu wa nyumbani mwa Narkiso, walio katika Bwana(YESU)."

6. Nisalimieni wenye bidii katika KRISTO.

Warumi 16:12 "Nisalimieni Trifaina na Trifosa, wenye bidii katika Bwana(YESU). Nisalimieni Persisi, mpenzi aliyejitahidi sana katika Bwana."

7. Nisalimieni wateule wa Bwana YESU KRISTO.

Warumi 16:13 "Nisalimieni Rufo, mteule katika Bwana(YESU), na mamaye, aliye mama yangu pia."

8. Nisalimieni watakatifu.

Warumi 16:15 "Nisalimieni Filologo na Yulia, Nerea na dada yake, na Olimpa, na watakatifu wote walio pamoja nao."

Kiini Cha somo langu hili ni hiki.

✓✓Kama salamu hizi zitaelekezwa kanisani kwenu unadhani zitawahusu wangapi?

✓✓Kama salama hizi zitaelekezwa kwako binafsi je ni salamu ngapi zitakuhusu kati ya hizi salama 8?

✓✓Kama salamu hizi hazikuhusu hata moja, je ni kwanini?

✓✓Je uko katika makundi haya 8 hata usitahili kupewa salamu hizi njema?

✓✓Je salamu hizi zikitolewa leo utahusika?

✓✓Je una sifa za kusalimiwa salamu hizi?

✓✓✓Je wewe ni mtenda kazi katika kazi ya MUNGU hata usitahili salamu hii njema inayowahusu tu watenda kazi katika kazi ya MUNGU?

✓✓✓Je wewe ni mpendwa katika wokovu wa Bwana YESU na unatimiza wajibu wako kwa MUNGU hata usitahili salamu hii njema inayowahusu tu waaminifu katika KRISTO?

✓✓✓Je wewe unajitaabisha kwa ajili ya kazi ya MUNGU, yaani unafanya kazi ya MUNGU au unatoa pesa yako ili kazi ya MUNGU iende mbele, je una muda wa kuombea kazi ya MUNGU na watumishi wa MUNGU hata salamu hii njema inayowahusu tu wanaojitaabisha katika kazi ya MUNGU, una sifa za kuipokea salamu hii?

✓✓✓Je unaishi maisha ya haki hata uwe mwenye kukubaliwa katika KRISTO ili salamu hii njema inayowahusu tu wanaoishi maisha ya haki katika KRISTO ikuhusu?

✓✓Je umeokoka kwelikweli na YESU KRISTO ni Bwana na Mwokozi wa maisha yako hata usitahili salamu hii njema inayowahusu tu waliokoka?

✓✓Je una bidii katika mambo ya MUNGU hata salamu hii njema inayowahusu tu wenye bidii katika kazi ya MUNGU, una sifa ya kupokea salamu hii?

✓✓Je wewe ni Mteule wa MUNGU hata usitahili salamu hii njema inayowahusu tu wateule wa Bwana YESU KRISTO?

✓✓Je wewe unaishi maisha matakatifu hata usitahili salamu hii njema inayowahusu tu watakatifu katika KRISTO?
Majibu sahihi yako moyoni mwako.
Lakini Biblia inakutaka yafuatayo.

✓✓ Ishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO.

1 Petro 1:14-16 " Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu."

✓✓Timiza wajibu wako kwa KRISTO.

Wakolosai 1:10 "mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya MUNGU;"

✓✓Usiache kuipeleka kazi ya MUNGU kwa pesa yako, na toa kwa moyo na upendo sio kwa kujilazimisha .

2 Wakorintho 9:6-7 " Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu."

✓✓Husika tu na yaliyo mema ya kumpendeza MUNGU.

Wafilipi 4:8 "Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo."

Nini nataka kusema zaidi?

Katika maisha yako ya Wokovu zingatia mambo yafuatayo.

1. Katika maisha yako ya Wokovu fanyika mtenda kazi katika kazi ya MUNGU.

2. Katika maisha yako ya Wokovu jitaabishe kwa ajili ya kazi ya MUNGU ili kazi ya MUNGU iende mbele, hubiri Neno la MUNGU kama umepewa kuhubiri, toa pesa yako kwa kazi ya MUNGU, hubiri injili hata kama ni kwa gharama, toa fungu la kumi na sadaka ili kazi ya MUNGU ifanyike vyema.

3. Katika maisha yako ya Wokovu hakikisha unakubaliwa katika KRISTO.

4. Katika maisha yako yote kaa katika KRISTO Siku zote.

5. Katika maisha yako ya Wokovu hakikisha una bidii katika kazi ya MUNGU siku zote.

6. Katika maisha yako Siku zote hakikisha wewe ni Mteule wa Bwana YESU KRISTO.

7. Katika maisha yako ya Wokovu hakikisha jina lako liko daima katika kitabu cha uzima mbinguni.

8. Katika maisha yako ya Wokovu hakikisha Siku zote wewe ni mtakatifu unayeishi maisha ya haki.

Kama ni hivyo umestahili Sana kupewa salamu hizi za watu wa MUNGU, salamu za waenda mbinguni.
Ndugu yangu nakuomba fanyia kazi Neno hili hai la MUNGU kipengele kwa kipengele.
Namshukuru Sana ROHO MTAKATIFU kwa ufunuo huu alionipa, naamini ndugu yangu utaufanyia kazi pia.
MUNGU akubariki Sana Sana ukifanyia kazi.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, meseji, whatsapp, Sadaka, Ushauri, Maombezi n.k).
Ubarikiwe

Comments