OMBA MUNGU AKULINDE KILA UENDAKO.

 

Mwl Peter Mabula akiwa Biharamulo



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Kama kuna kitu muhimu mimi na wewe tunahitaji basi ni ulinzi wa MUNGU.

Kama kuna kitu muhimu familia yako na watu wa nyumba yako wanahitaji basi ni ulinzi wa MUNGU.

Ahadi ya MUNGU ni kwamba tukiomba lolote katika jina la YESU KRISTO atalifanya.

Yohana 14:14 "Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya."

Inawezekana una mahitaji mengi unayotamani MUNGU katika KRISTO YESU akutendee, ni vyema lakini kama ulinzi wa MUNGU hautakuwa kwako basi hata ukijibiwa mahitaji yako haitakusaidia, kama majibu hayo hayataambatana na ulinzi, ndio maana leo nakuambia kwamba omba MUNGU akulinde kila uendako.

MUNGU alimwahidi Yakobo kwamba atamlinda kila aendako.

Mwanzo 28:15 "Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia."

Yakobo wa leo ni mimi na wewe, omba MUNGU akulinde kila uendako.

MUNGU alimlinda Yakobo hivyo atakulinda na wewe pia kama ukihitaji ulinzi wake kwa maombi.

Wakati mwingine tunaishi na maadui wengi kuliko tunavyodhani.

Zaburi 69:4 "Wanaonichukia bure ni wengi Kuliko nywele za kichwa changu. Watakao kunikatilia mbali wamekuwa hodari, Adui zangu kwa sababu isiyo kweli. Hata mimi nalilipishwa kwa nguvu Vitu nisivyovichukua."

Inawezekana kabisa unaishi lakini kuna watu wanajiuliza utakufa lini.

Inawezekana unawindwa na mawakala wa shetani.

Inawezekana kuna watu Wanaitamani nafasi yako kazini au kwenye ndoa yako au uchumba wako hivyo wanatafuta nafasi ya kukuua ili wachukue nafasi hiyo, leo omba MUNGU Baba akulinde dhidi ya maadui zako kiroho na kimwili.

Sio watu wote wanakupenda, sio watu wote wanakuwazia mema, omba MUNGU akulinde ndugu yangu.

Daudi hakujua mwanzo kama anatafutwa na Sauli ili auawe bila hata kosa, hata wewe unaweza ukawindwa na wachawi, majini, wakuu wa giza na kila wanadamu wanaotumika kishetani, leo omba MUNGU katika KRISTO YESU akulinde, omba MUNGU akulinde kila uendako, haijalishi uko kama Daudi anayetafutwa na Sauli ili auawe bila kosa.

1 Samweli 26:20 "Basi sasa, isianguke damu yangu chini mbali na uso wa BWANA; maana mfalme wa Israeli ametoka ili kutafuta uhai wangu, kama vile mtu awindavyo kware mlimani."

Lakini Ashukuriwe MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi maana ukimuomba akulinde dhidi ya maadui hakika atakulinda.

Hakika leo baada ya maombi yako utakuwa hivi.

Zaburi 124:7-8 " Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokoka. Msaada wetu u katika jina la BWANA, Aliyezifanya mbingu na nchi."

✓✓Ukiomba MUNGU akulinde ujue mitego ya maadui zako wote itavunjika.

✓✓Ukiomba MUNGU ailinde ndoa yako au uchumba wako au familia yako ujue mitego ya maadui zako itavunjika.

Naipenda Biblia maana inasema " Mitego imevunjika,na sisi tumeokoka kwa msaada wa MUNGU "

MUNGU akulinde na uwe salama kila uendako na uwe salama kila siku.

Omba leo katika jina la YESU KRISTO na utakuwa salama.

✓✓Kazi yako iombee ulinzi.

✓✓Watoto wako waombee ulinzi.

✓✓ Mwenzi wako wa ndoa Muombee ulinzi na MUNGU katika KRISTO YESU atamlinda.

Nini ufanye katika Maombi leo?

1. Tubia dhambi, maovu na makosa kisha omba MUNGU akulinde.

Zaburi 51:1-2 " Ee MUNGU, unirehemu, Sawasawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu. Unioshe kabisa na uovu wangu, Unitakase dhambi zangu."

Kama unataka kumuombea mtu au watu basi tubu kwa ajili ya huyo unayetaka kumuombea kisha Muombee ulinzi.

2. Omba MUNGU akulinde kila uendako au kila uliko.

Mwanzo 28:15 "Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia."

3. Omba huku ukimwamini MUNGU na atakulinda.

Isaya 26:3-4 " Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini. Mtumainini BWANA siku zote Maana Bwana YEHOVA ni mwamba wa milele."

4. Omba MUNGU akulinde usiku na mchana.

Zaburi 121:7-8 "BWANA atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako. BWANA atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele."

Ndugu yangu omba katika jina la YESU KRISTO na MUNGU atakulinda.
Omba kwa Imani na utamuona MUNGU.
MUNGU akubariki.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292
Ubarikiwe

Comments