AINA 5 YA WASOMAJI WA BIBLIA.

 

Na Mwl Peter Mabula. 
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele 


Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe ndugu zangu wote. 
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Naamini wewe ni Msomaji wa Biblia, kama ni hivyo  unafanya vyema sana maana Biblia ndio Neno pekee la MUNGU wa kweli aliyeumba Mbingu na Dunia, ni Neno hai ambalo lina kila kitu anachokihitaji Mwanadamu kwa ajili ya uzima wa milele,  ushindi, Baraka, Namna na kumpendeza MUNGU, utakatifu, Njia ya Wokovu n.k
Biblia ni Neno hai kweli kweli.
Waebrania 4:12 "Maana Neno la MUNGU li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo."

Sasa Mimi  lengo langu leo ni ili wewe rafiki yangu ujifunze kitu kuhusu wewe mwenyewe na watu wengine unaowaona wanasoma Biblia takatifu au wanafundisha maandiko ya Biblia. 

Aina hizi 6 za wasomaji Biblia ni hizi.

1. Mtu anayesoma Biblia ila haelewi hivyo anahitaji Mtumishi wa KRISTO ili amsaidie kuelewa.

Mfano hai ni Towashi Mwethiopia ambaye alikuwa anasoma maandiko ya Biblia ila haelewi hivyo Filipo Mtumishi wa MUNGU ndiye aliyemsaidia kuelewa.

Matendo ya Mitume 8:27-35 " Naye akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu,  akawa akirejea, ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya.  ROHO akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo. Basi Filipo akaenda mbio, AKAMSIKIA ANASOMA CHUO CHA NABII ISAYA; akanena, Je! YAMEKUELEA HAYA UNAYOSOMA? Akasema, NITAWEZAJE KUELEWA, MTU ASIPONIONGOZA? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye.  Na fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, Na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya, Vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake.  Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika nchi.  Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine?  Filipo akafunua kinywa chake, naye, AKIANZA KWA ANDIKO LILO HILO, AKAMHUBIRI HABARI NJEMA ZA YESU. "

Leo wapo Watu wengi sana wanaosoma Biblia kama huyu Mwethiopia ila hawaelewi hivyo wanamhitaji Mtumishi mwaminifu wa Bwana YESU KRISTO ili awafafanulie kuelewa Maandiko hayo na maana yake kwetu. Ndio maana ni muhimu sana kuhudhuria ibada za Mafundisho ya Neno la MUNGU Kanisani, kwenye Semina za Neno la MUNGU au kwenye Mikutano ya Injili.

2. Mtu anayesoma Biblia na kuelewa Maandiko ila hajui kilichobebwa ndani ya maandiko hayo.

Kutoka 24:7 "Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena BWANA tutayatenda, nasi tutatii. "

Hawa ni Waisraeli na huu unaowahusu ni mfano hai wa watu waliosikia Neno la MUNGU likielezewa kwao na wakaelewa na wakaahidi kufanya yote yaliyosemwa na MUNGU kupitia Neno lake hilo lakini kwa sababu hawakuelewa kilichobebwa ndani ya Neno hilo walitii kwa muda tu Neno la MUNGU kisha wakaliacha na kumkosea MUNGU. 

Kabla ya siku 40 baada ya kuelezwa Neno la MUNGU na wakaapa watatii, kabla ya hizo siku 40 hazijaisha watu wale wale wakaabudu miungu.

Kutoka 32:1 "Hata watu walipoona ya kuwa Musa amekawia kushuka katika mlima, wakakusanyana wakamwendea Haruni, wakamwambia, Haya! Katufanyizie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo aliyetutoa katika nchi ya Misri hatujui  yaliyompata." 

 Ndani ya hizo siku chache watu wale walikuwa wamejiharibu nafsi zao.

Kutoka 32:7-8 "BWANA akamwambia Musa, Haya! Shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao,  wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri. "

Huu ni mfano tu, leo kuna watu anapohubiriwa Neno la MUNGU anaelewa na anasema "Amina" nyingi sana lakini muda mfupi baadae analiasi Neno hilo la YESU KRISTO. 
Alielewa ila hakujua kwa uzito kile kilichobebwa ndani ya Neno hilo.

Siku chache zilizopita tulikuwa kwenye Maombi ya kufunga, Ndugu mmoja kati ya wengi tuliofunga nao maombi wakati wa maombi aliniandikia jumbe nyingi za kubarikiwa Na Neno nililofundisha na kubarikiwa sana na muongozo wa maombi niliotoa, Maombi yakaisha salama na ndugu huyu akikiri ushindi mkuu lakini siku 3 baada ya Maombi aniniandikia ujumbe ambao ukiusoma kwa mara ya kwanza unaweza kudhani mtu huyu hamwamini MUNGU,  hana imani hata kidogo, hajawahi kufanya Maombi au ndio ana wiki moja tangu aokoke lakini ukweli ni kwamba yuko katika Wokovu miaka mingi sana na huwa anafunga mara kwa mara. Yaani ni kama huwa anafunga harafu  akimaliza tu kufunga yale maombi yake ya kufunga anayafuta kwa maneno ya kinywa chake. Huyu hajui kwa ukubwa kilichobebwa ndani ya Neno la MUNGU. 


3. Mtu anayesoma Biblia na kuelewa ujumbe Binafsi anaopewa na MUNGU kupitia andiko husika.

Au tunaweza kusema Mtu anayesoma Biblia na kuelewa  na kuelewa kilochobebwa  ndani ya maandiko husika.

Mfano hai ya Mtu aliyesoma Biblia na kuelewa kilichobebwa ndani ya Neno hilo la MUNGU ni Danieli.

Danieli 9:2-4 " katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danieli, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la BWANA lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini.  Nikamwelekezea BWANA Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu.  Nikamwomba BWANA, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee BWANA, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; "

Huyu ni mfano hai wa mtu aliyesoma Biblia na kuelewa kilichobebwa ndani ya maandiko husika.

■Danieli baada tu ya kusoma Biblia aligundua muda wa kutoka utumwani umefika, wewe ukisoma Biblia unagundua nini sawasawa na kusudi la MUNGU katika Wokovu  wa KRISTO?

■Danieli aliposoma Biblia aligundua kilichobebwa ndani ya maandiko husika akaamua kuchukua hatua kwa maombi ya kufunga,  wewe ukisoma Biblia huwa unachukua hatua gani sawasawa na kusudi la MUNGU katika KRISTO YESU?

■Danieli aliposoma Biblia na kuelewa Neno la MUNGU alilihamishia kwenye vitendo kwa kufunga na kuomba na kudai haki zake sawasawa na Neno la MUNGU,  hiyo ndio sifa kuu ya watu wanaosoma Biblia na kuelewa kilichobebwa ndani ya maandiko husika yaani huwa wanachukua hatua za kuliishi Neno la MUNGU au kulifanyia kazi kama linavyotaka ili wafanikiwe jambo fulani maishani mwao. Hakikisha unakuwa na wewe hivyo wewe ambaye huwa unasoma Masomo yangu mimi Peter Mabula pamoja na watumishi wengine waaminifu wa Bwana YESU KRISTO Mwokozi. 

4. Mtu anayesoma Biblia na kuelewa ila anapotoa maandiko kwa tamaa zake Binafsi. 

Hili ni kundi baya sana la watu yaani anasoma Biblia na kuielewa kisha anapotoa maandiko kwa hila zake.
Mfano ni watu waliokuwa wanayapotoa maandiko ya Neno hai la MUNGU aliyopewa Mtume Paulo.

2 Petro 3:16 "vile vile kama katika nyaraka zake zote pia, akitoa humo habari za mambo hayo; katika nyaraka hizo yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na maandiko mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe."

●Leo kuna Madhehebu ni zao la wapotoa maandiko.

●Leo kuna mpaka mwanzilishi wa dhehebu anajiita Mungu na watu walioathiriwa na upotofu wake wanamfuata, huo ni ujinga wa kiwango cha mwisho kabisa kwenye akili.

●Leo kuna mpaka madhehebu ya waabudu sanamu, mashoga, waabudu shetani n.k, hicho ni kiwango cha mwisho kabisa cha akili ndogo duniani. 

■Leo kuna watu wanakataa Wokovu wa Bwana YESU KRISTO na wanatumia Biblia,  hao wamedanganywa na wakala wa shetani aliyepotoa maandiko.

■Leo kuna watu Wanamkataa ROHO MTAKATIFU na wanapinga kunena kwa Lugha katika ROHO MTAKATIFU,  hao wamedanganywa na mwanzilishi wa dhehebu lao asiye na YESU KRISTO. 

Leo kuna watu wengi wanatumia Biblia na kuisoma kisha wanapotoa maandiko na kuwapotosha wengi hasa kwa ajili ya kujitafutia umaarufu na kwa ajili ya kujipatia kipato kikubwa, ni hatari sana

Tito 1:11 "Hao wanapindua watu wa nyumba nzima, wakifundisha yasiyowapasa kwa ajili ya mapato ya aibu." 

■■Ndugu, katika hili kundi la watu wanaopotoa maandiko naomba usiwe wewe,  narudia tena Naomba usiwe wewe unayesoma somo hili, mara ya tatu na ya mwisho naomba usiwe wewe ndugu.


5. Mtu anayesoma maandiko na kuyalazimisha maandiko yakubaliane tu na msimamo wake au dini yake au dhehebu lake na kumbe haiwezekani. 

2 Petro 2:1 "Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana(YESU)aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia."

●Hawa wameathiriwa na udhehebu au udini hivyo wako tayari kulazimisha baadhi ya maandiko ili yawe tu upande wa dhehebu lao, baadhi ya maandiko hawasomi kabisa na mengine wanaamua kuyageuza.
Mfano mmoja kuna dhehebu Biblia yao andiko la Yohana 1:1 wameligeuza lengo lao hawataki kusikia YESU ni MUNGU,  wakikusikia unasoma Isaya 9:6 inayosema kwamba YESU ni MUNGU mwenye nguvu wanachukia.
Huo ni mfano mmoja tu kati ya mingi.
Wengine wanasema hakuna siku ya hukumu, wengine bila kuwa dhehebu lao MUNGU hatakukubali, hawa wote Biblia inawaita Mitume wa uongo maana wanapotosha maandiko kwa misimamo yao na tamaa zao Binafsi.
Mfano mmoja nimemsikia mtu  mmoja leo mtandaoni amekataza wanafunzi kwenda shule kwa sababu YESU anarudi, huko ni kupotoa maandiko maana Biblia kwa hapa duniani inasema hakuna mwanadamu ajuaye siku wala saa.

 Ni kweli kabisa dalili zote kimaandiko za kurudi kwa Bwana YESU KRISTO zimeshatimia na wahubiri injili wengi sana nikiwemo mimi Peter Mabula tunafundisha watu kujiweka tayari yaani kuishi maisha matakatifu ya wokovu maana tunaishi siku za mwisho kimaandiko,  Lakini siwezi kufundisha kwamba usiende shule au usifanye biashara au usifanye kazi au usioe au usiolewe kwa sababu hakuna haja maana YESU anarudi, nikikufundisha hivyo nakuwa nakupotosha maana Biblia haijipingi, Biblia katika Mathayo 24:40-41 inaonyesha siku ya unyakuo itakuja huku watu wakiendelea na majukumu yao kila mmoja lakini aliye mtakatifu atanyakuliwa ila mtenda dhambi ataachwa. Nikiwafundisha watu kuacha  kufanya yawapasayo ya kimaisha yaliyo mema kwa kigezo cha kurudi kwa YESU nakuwa napotosha.
Biblia inatutaka tu tuwe tayari yaani tuishi maisha matakatifu ya wokovu wa KRISTO baada ya kumpokea kama Mwokozi wetu.

Mathayo 24:42 "Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. "

Sasa mitume wa uongo au wapotoshaji ni wengi sana hivyo ndugu uwe makini sana.

2 Wakorintho 11:13 "Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa KRISTO. "

Ndugu, ukitaka uielewe Biblia isome kwa jinsi ya KRISTO na sio kuisoma kwa jinsi ya dhehebu lako au kwa jinsi ya dini yako au kwa jinsi ya msimamo wako binafsi. 

■Kuisoma Biblia kwa jinsi ya KRISTO ni kujua huu ni wakati wa Wokovu wa KRISTO hivyo Okoka kwanza kisha utampokea ROHO MTAKATIFU atakayekusaidia kuelewa maandiko vizuri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU KRISTO Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO.
+255714252292(Whatsapp)
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments