TUWE KANISA LENYE NGUVU.

 

Peter na Jemimah Mabula



Bwana YESU KRISTO alipoondoka duniani aliacha Kanisa lenye washirika 120.

Matendo 1:15 "Siku zile akasimama Petro kati ya hao ndugu (jumla ya majina ilipata mia na ishirini), akasema,"

Kanisa hili lenye washirika 120 lilikuwa na umoja wa ajabu sana, Kanisa hili walikuwa wamejaa ROHO MTAKATIFU, Kanisa hilo walikuwa watoaji na wanaoishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO.

Japokuwa Kanisa hili walikuwa watu 120 tu lakini ndio hao waliupindua ulimwengu hata ulimwengu ukamgeukia YESU KRISTO Mwokozi.

Ni Kanisa hili lenye washirika 120 ndilo lilipeleka injili Asia, Afrika, ulaya na Amerika.

Nini nataka niseme kwa Kanisa hai la KRISTO leo?

Ni kwamba, tukitaka tuwe Kanisa lenye nguvu lazima tuwe tunaokolewa na Bwana YESU KRISTO Mwokozi, lazima tuwe na nguvu za ROHO MTAKATIFU, lazima tuwe na umoja.

Zaburi 133:1 "Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja."

Tukitaka tuwe Kanisa lenye nguvu lazima tuhubiri injili ya kweli KRISTO YESU, tena tuhubiri bila kuogopa wanadamu au mazingira.

Isaya 58:1" Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao."

Tukitaka tuwe Kanisa la MUNGU lenye nguvu lazima tufuate nyayo za Kanisa la kwanza.

Matendo 2:41-42 "Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu. Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali."

Ni ajabu watu 120 walipindua ulimwengu wote, lakini kwa sasa kuna wateule wa KRISTO kila taifa wengi sana, maelfu au mamilioni lakini wameshindwa kulifanya taifa lao kufanyika wateule wa KRISTO YESU Mwokozi.

Tatizo kubwa kwa Kanisa la sasa ni kukosekana kwa umoja, kuwa walegevu katika kazi ya MUNGU, kutokuwa watoaji ili kupeleka wahubiri kila pahali, kuwa watu wa mashindano, mbwa mwitu kujiingiza kwenye uongozi wa kundi la watu wa MUNGU, kukumbatia dhehebu huku umemwacha YESU KRISTO Mwokozi n.k

Inatupasa sana kama Kanisa hai la KRISTO duniani kuwa na umoja kwanza.

Mambo 5 ambayo huambatana na umoja wa watu wa MUNGU ni haya;

1. Kila mtu kutembelea kwenye wito alioitiwa na MUNGU.

2. Unyenyekevu na Upole.

4. Kuwa na uvumilivu.

4. Kuchukuliana kwa upendo wa ki MUNGU.

5. Kuhifadhi umoja wa ROHO MTAKATIFU.

Mambo hayo matano yanapatikana katika Waefeso 4:1-3 ambapo Biblia inasema " Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani."

Ndugu, Mimi binafsi natamani wewe uwe Kanisa lenye nguvu.
MUNGU akubariki sana.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU.
+255714252292.
Ubarikiwe

Comments