KAZI 5 ZA SADAKA KIROHO.

 

Na Mwl Peter Mabula,  Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

Bwana YESU KRISTO  atukuzwe ndugu yangu. 

Karibu tujifunze Neno la MUNGU . 


Moja ya kitu muhimu na chenye kazi kubwa katika ulimwengu wa roho ni pamoja na Sadaka.


 Biblia inamtaka kila mteule wa KRISTO  kufanya kila jambo jema likiwemo la kutoa sadaka, kufanya jambo hilo jema   katika tu  jina la Bwana YESU KRISTO.


Wakolosai 3:17 "Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye."


■Sadaka inaweza kufanya mambo mengi katika ulimwengu wa roho kulingana na maelekezo ya mtoaji wa sadaka hiyo na kulingana na maombi yatayayoambatana na sadaka hiyo.  


Sio sadaka zote hufanya kazi kubwa ila moyo mweupe wa mtoaji, kusudi la MUNGU na maombi huifanya sadaka husika kufanya kazi kubwa sana katika ulimwengu wa roho  na udhihirisho wake katika  ulimwengu wa mwili. 


■Kutoa ni kupanda ili upokee ila uwe ni utoaji sahihi kulingana na mbingu. 


2 Wakorintho 9:6-7 "Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana MUNGU humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu."


Baadhi ya kazi za sadaka kiroho ni hizi. 


Mimi Peter Mabula leo nazungumzia tu sadaka ambayo unamtolea MUNGU kwa upendo na kwa imani katika KRISTO YESU Mwokozi 


1. Sadaka kiroho inaweza kuiweka wakfu madhabahu ya MUNGU. 


Hesabu 7:10 "Kisha wale wakuu wakatoa matoleo kwa ajili ya kuiweka wakfu madhabahu, katika siku hiyo iliyotiwa mafuta, wakuu wakayatoa matoleo yao mbele ya madhabahu."


Kuiweka wakfu madhabahu ya MUNGU  ina maana ya kuifanya madhababu iwe kamili,  maalumu iliyotengwa kwa ajili ya kazi ya MUNGU katika KRISTO YESU. 


Kuiweka wakfu madhabahu ina pia ya kuifanya madhabahu kuwa na thamani kiroho. 


Ndio maana madhabahu ya kiroho ya  MUNGU katika KRISTO YESU ni madhabahu moja tu lakini utendaji wake ni tofauti kati ya madhabahu ya eneo moja na madhabahu ya eneo lingine  japokuwa imani moja, ubatizo mmoja, Bwana YESU KRISTO ni yule yule, ROHO MTAKATIFU ni yule yule na MUNGU ni yule yule lakini nguvu zinazidiana. 


Sababu ya nguvu kiroho kuzidiana zinatokana na Mtumishi husika,  maombi, Imani na sadaka. 


Kama ulikuwa hujui kazi  ya sadaka basi moja wapo ya kazi ya sadaka ni kuifanya madhabahu kuwa na nguvu, sadaka huiweka wakfu madhabahu ili madhabahu husika iwe tayari kuwahudumia watu wa MUNGU. 


Ndio maana katika  maandiko maeneo mengi yaliyotaja madhabahu basi na sadaka ilitajwa pia.


Lakini pia ni muhimu kujua kwamba sadaka njema haipimwi kwa wingi wake tu bali utakatifu,  kumtii ROHO MTAKATIFU,  kutoa kwa upendo na kuishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU Mwokozi. 


Sadaka kazi yake mojawapo ni kuiweka wakfu madhabahu. 


Hakikisha unamtolea MUNGU sadaka safi na takatifu kama unamtolea MUNGU katika kipengele cha kuiweka wakfu madhabahu.


2.   Kazi ya sadaka kiroho ni kumpendeza MUNGU. 


Mwanzo 4:4 "Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake;"


Ukisoma andiko hilo katika tafsiri  ya BHN Biblia inasema "naye Abeli akamtolea MUNGU sadaka ya wazawa wa kwanza wa kondoo wake na nyama nono. Mwenyezi-Mungu akapendezwa na Abeli na sadaka yake,"


Kumbe MUNGU alipendezwa na sadaka ya Habili. 


Hata wewe unaweza kumtolea MUNGU sadaka na hiyo sadaka njema ikampendeza MUNGU. 


Sadaka yako ikimpendeza MUNGU ujue atakubariki na baraka zilizo ndani ya sadaka hizo zitakufuata. 


Kama ulikuwa hujui kazi hii ya sadaka basi tambua leo kwamba kazi mojawapo ya sadaka ni kumpendeza MUNGU. 


Sadaka kumpendeza MUNGU ni nini? 


Sadaka kumpendeza MUNGU maana yake sadaka kumfurahisha na kumridhisha MUNGU,  kumfaa na kumvutia.


Na kama sadaka yako ikiwa katika kiwango hiki ujue MUNGU ataitazama sadaka yako na kuyaona maombi yaliyoambatana na sadaka hiyo na kukujibu. 


Inategemea sadaka yako inaambatana na maombi gani, maombi yako mtoaji  au maombi ya Mtumishi uliyempa akaiombea sadaka hiyo, maombi hayo yataonekana na kujibiwa mbele za MUNGU maana sadaka yako imempendeza MUNGU. 


Sadaka ya Nuhu ilimpendeza MUNGU na kumridhisha hivyo MUNGU akasema hatawaua tena kwa ghalika Wanadamu wote.


Mwanzo 8:20-21 "Nuhu akamjengea BWANA madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu.  BWANA akasikia harufu ya kumridhisha; BWANA akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya."


Vipi wewe ukipata neema kwa kutoa sadaka nzuri, njema na sadaka yako hiyo  ikamridhisha MUNGU na kumfurahisha  kisha akasema na wewe  kwamba "Kuanzia sasa hautakuwa tasa tena,  hautafungwa vifungo tena,  hautarogwa tena , hautateswa tena n.k"


Ndugu kazi mojawapo ya sadaka ni kumpendeza MUNGU katika KRISTO YESU,  kama ulikuwa hujui basi tambua leo hilo na hakikisha unakuwa mtu unayetoa sadaka inayompendeza  MUNGU. 


3.  Kazi ya sadaka kiroho ni  mlango wa baraka kwa mtoaji. 


Kutoka 20:24 "Utanifanyia madhabahu ya udongo, nawe utatoa dhabihu zako juu yake; sadaka za kuteketezwa, na sadaka za amani, kondoo zako, na ng'ombe zako, kila mahali nitakapotia ukumbusho wa jina langu, hapo ndipo nitakapokujilia na kukubarikia."


Mahitaji yako yote yanatokana na makundi matano ya baraka ambazo MUNGU hutoa, hivyo kazi ya sadaka kiroho ni ufunguo wa kubarikiwa. 


Baraka tano za MUNGU ni baraka za kiafya, baraka za uchumi,  baraka za ndoa,  baraka za uzao na baraka za kibali. 


Na mahitaji yako yote yako katika hizo baraka tano atoazo MUNGU. 


Sasa kazi mojawapo ya sadaka ni mlango wa kupokea baraka kutoka kwa MUNGU. 


Ni kanuni ya kupokea. 


Luka 6:38 "Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa."


Sadaka ni muhimu sana na  kuwe pia na maombi yanayoambatana na sadaka hizo ili kujulisha mtoaji anahitaji baraka gani.


Kama ulikuwa hujui basi tambua leo kwamba kuna sadaka kazi yake ni kufungulia baraka zako. 


■Baraka na utoaji ni mapacha ambao huwezi kuwatenganisha.


Ndugu hakikisha unakuwa mtoaji wa sadaka ya namna hii inayoambatanishwa na maombi katika jina la YESU KRISTO na utapokea. 


●Usitoe sadaka tu kama ratiba ya kutoa au  ibada bali toa ukijua unatoa kwa ajili ya nini na hitaji maombi kulingana na muono wako wa kutoa sadaka hiyo. 


Sadaka ni chanzo cha kuongezeka kiuchumi na kimafanikio. 


Wakati mwingine kutoa sadaka ni kama kutawanya tu lakini watawanyaji hao ndio huongezewa. 


Mithali 11:24 "Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi; Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji."


4. Kazi ya sadaka ni kufanya agano na MUNGU. 


Zaburi 50:5 "Nikusanyieni wacha MUNGU wangu Waliofanya agano nami kwa dhabihu."


Tangu mimi  Peter binafsi nilipofunuliwa ufunuo wa kuombea sadaka ili kufanya agano na MUNGU sijawahi kusahau kuombea hitaji hilo, kama Nilisahau basi ni mara chache sana sana. 


Watu wengi wanateswa sana na maagano ya giza lakini kwa sadaka ukiomba maombi kwa kutumia damu ya YESU KRISTO na jina la YESU KRISTO unaweza kusimamisha agano na MUNGU,  na agano na MUNGU likisimama tu ujue maagano yote ya giza katika eneo hilo ambalo umesimamisha agano na MUNGU,  hayo maagano ya giza hapo yanatoweka.


Najua sio sadaka zote zinaweza kufanya agano na MUNGU  lakini sadaka yako ikiambatana na maombi ya kusimamisha agano na MUNGU ujue nguvu za giza katika eneo hilo ulilosimamisha agano,  hizo nguvu za giza hapo hazitakuwa na uhalali tena. 


Nina shuhuda juu ya hili.


Sadaka yako ikitengeneza agano na MUNGU katika eneo lako fulani ujue hata kama nguvu za giza zilimiliki hapo miaka mingi basi zitaachia. 


Muhimu tu ni sadaka njema inaayoambatana na maombi ya kulisimamisha  agano na MUNGU kupitia sadaka. 


Inawezekana ni kwenye eneo fulani la mwili wako, inawezekana ni kwenye eneo yaani ardhi yako,  inawezekana ni kwenye ofisi,  au familia au nyumba au ndoa au uchumba  mtakatifu n.k


Ndugu hii ni moja ya kazi muhimu sana ya sadaka kiro


ho,  ukilisimamisha agano na MUNGU  kwa sadaka yako na maombi ujue nguvu za giza hazitakuwa na uhalali hapo hivyo zitaondoka.


Sio kila sadaka inatengeneza agano na MUNGU hivyo ni wajibu wako kutambua katika ROHO MTAKATIFU juu ya hili. 


Kumbuka pia kuna sadaka hufanya ukumbusho mbele za MUNGU,  ukitoa sadaka ya aina hiyo utasababisha hiyo  sadaka  ikuletee faida nyingine  kutoka ulimwengu wa roho wa nuru. 


5. Kazi nyingi ya sadaka kiroho ni kutengeneza hazina ya mtoaji kwenye ulimwengu wa roho. 


Mathayo 6:19-21 " Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako."


Baada ya kukuletea kazi za sadaka kiroho ngoja pia nikujulishe baadhi ya kazi za sadaka kimwili. 


1. Kuwawezesha wahubiri injili ili waipeleke injili mbali zaidi au  kwa watu wengi zaidi. 


Warumi 10:15 "Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!"


2. Matumizi ya watumishi wa MUNGU. 


Hesabu 18:21" Na wana wa Lawi, nimewapa zaka yote katika Israeli kuwa urithi wao, badala ya huo utumishi wautumikao, maana, ni huo utumishi wa hema ya kukutania."


Hii pia ni kutokana na taratibu za kanisa la mahali  au taratibu za huduma husika. 


 Pia ni muhimu kujua kwamba ni MUNGU aliagiza watumishi wake wapate riziki zao na za huduma kutoka kwenye matoleo. 


1 Wakorintho 9:11-14 " Ikiwa sisi tuliwapandia ninyi vitu vya rohoni, je! Ni neno kubwa tukivuna vitu vyenu vya mwilini? Ikiwa wengine wanashiriki uwezo huu juu yenu, sisi si zaidi? Lakini hatukuutumia uwezo huo; bali twayavumilia mambo yote tusije tukaizuia Habari Njema ya Kristo. Hamjui ya kuwa wale wazifanyao kazi za hekaluni hula katika vitu vya hekalu, na wale waihudumiao madhabahu huwa na fungu lao katika vitu vya madhabahu? Na Bwana vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waihubirio Injili wapate riziki kwa hiyo Injili."


3. Kuhudumia wahitaji. 


Yakobo 1:27 "Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa."


Wahitaji mfano yatima na wajane. 

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU KRISTO Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU KRISTO Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.

Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.

Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.

Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.

MUNGU akubariki sana. 

By Peter Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai

+255714252292(whatsapp).

MUNGU akubariki sana.

Comments