JIFUNZE KUHUSU MTI WA UZIMA.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU 




Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Je unafahamu nini kuhusu Mti wa Uzima?
Karibuni tujifunze Neno la MUNGU.
Naamini unafahamu kuhusu  Bustani ya Edeni na habari za Mti wa uzima.

Sasa ni kwamba katika Bustani hiyo ya Edeni kulikuwa na miti mingi lakini  katikati ya bustani hiyo ya Eden  kulikuwa na Miti miwili ambayo ni MTI WA UZIMA na mti mwingiine uitwao MTI WA UJUZI WA MEMA NA MABAYA.
Mti wa ujuzi wa mema na mabaya ndio mti ambayo Eva alitoa matunda akala na tunda lingine akampelekea Adamu mmewe na wote wakakosa mbele za MUNGU.

Mwanzo 3:6-7 ''Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala. Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo.''

Baada ya kula matunda hayo kutoka katika katika mti wa ujuzi wa mema na mabaya na adhabu ya MUNGU ikatolewa  ililazimika waondolewe Edeni maana kama wangekula tena matunda ya Mti wa uzima wangeishi milele. 

Mwanzo 3:22-24 '' Bwana MUNGU akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele;  kwa hiyo Bwana MUNGU akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa. Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.''

Leo nazungumzia Mti wa uzima.

■Huu ni mti uliozungumzwa kwenye kitabu cha kwanza kwenye Mtiririko wa vitabu vya Biblia yaani kitabu cha Mwanzo na pia mti huu wa uzima umezungumziwa kwenye kitabu cha mwisho kwenye  mtiririko  wa vitabu vya Biblia yaani kitabu cha Ufunuo. 
Hivyo Mti wa uzima umezungumzwa katika Kitabu  cha Mwanzo na Kitabu cha ufunuo tu.

■Mti wa uzima ni Mti kama ilivyo miti mingine ila wenyewe ni Mti wa Uzima.

Mwanzo 2:9  ''Bwana MUNGU akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.''

■Sifa kuu ya Mti huu wa uzima ni kwamba ukila matunda yake utaishi milele.

Mwanzo 3:22  ''Bwana MUNGU akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele;''

Baada ya makosa ya akina Adamu na Eva mti huo ulianza kulindwa na Malaika, hata njia tu za kuuendea mti huo zililindwa hivyo  isingewezekana Mwanadamu yeyote kuufikia.

Mwanzo 3:24  ''Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.''

■■Mti wa uzima kwa sasa uko wapi?

●Mti wa uzima kwa sasa uko Mbinguni.

Ufunuo 22:1-2 '' Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung'aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha MUNGU, na cha Mwana-Kondoo, katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo MTI WA UZIMA, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa.''

Mtume Yohana kwa ufunuo aliona kiti cha Enzi cha MUNGU na mbele ya pale aliona njia, mojawapo aliona Mti wa uzima.
Kama Mti wa Uzima uko karibu na kiti cha enzi cha MUNGU je huo mti uko wapi?
Jibu ni Mbinguni maana Biblia inaonyesha kiti cha Enzi cha MUNGU kiko Mbinguni.
Mathayo 5:34 '' lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha MUNGU;''

■■Mambo gani yatafanyika baadae kuhusu Mti wa Uzima?

1. Mwanadamu yeyote anayempokea YESU KRISTO kama Mwokozi wake na akashinda ya dunia akiingia Uzima wa Milele atapewa kula matunda ya Mti wa Uzima.

Ufunuo  2:7  ''Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya MUNGU.''

2. Majani ya Mti wa Uzima yanaweza kuponya watu.

Ufunuo  22:2  ''katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa.''

3. Watakatifu tu katika KRISTO YESU ndio watakaoweza kwenda ulipo Mti wa Uzima.

Ufunuo  22:14  ''Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake.''

4. Kila Mtu kwa asili anayo sehemu yake katika Mti wa Uzima.

Kila Mtu anayo sehemu yake katika Mti wa Uzima ila kumkataa YESU na kuondoa lolote kwenye Biblia sehemu yako katika Mti wa Uzima huondolewa.

Ufunuo 22:19  ''Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, MUNGU atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.''

Biblia inasema ''MUNGU atamwondolea sehemu yake katika ule Mti wa uzima'' hii maana yake Mtu huyo alikuwa na sehemu yake katika huo Mti wa uzima ila akiondoa lolote kwenye Biblia ndio sehemu yake kwenye Mti wa Uzima itaondolewa.

5. Kila atakayebadili kweli ya Biblia na kuwapotosha watu kuhusu ukweli wa MUNGU katika KRISTO YESU, Mtu huyo sehemu yake katika Mti wa Uzima inaondolewa.

Ufunuo 22:19  ''Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, MUNGU atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.''

Asante rafiki yangu kwa kujifunza Neno hili la MUNGU leo.
Kabla sijahitimisha leo ninalo Neno la mwisho kwa ajili yako.
Je umeokoka? 
Kama umeokoka endelea na Wokovu wa Bwana YESU KRISTO hadi mwisho wa maisha yako.
Na wewe ambaye hujaokoka nakuomba okoka leo maana tunaishi siku  za Mwisho. 
Ni YESU tu ndio anayeweza kuliandiika jina lako kwenye kitabu cha uzima hata upate Uzima wa milele, nakuomba sana mpokee YESU KRISTO leo kwa ajili ya Wokovu. 
Huko huko uliko tafuta Kanisa la kiroho wanaohubiri Wokovu Wa KRISTO ukamweleze Mchungaji atakuongoza sala ya toba na utakuwa umeokoka.
Fanya hivyo kwa faida ya roho yako milele
MUNGU akubariki. 
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU. 
+255714252292(Sadaka ya kupeleka Injili, Maombi na ushauri)
Ubarikiwe sana

Comments