KWA IMANI MUSA ALIPOKUWA MTU MZIMA ALIKATAA KUWA MTOTO WA BINTI FARAO.

 

Ma Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU 


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni sana tujifunze Neno la MUNGU.

Kwanza imani ni nini?

■Imani ni kuwa na uhakika wa mambo unayoyatarajia.

■Imani ni kuyaona mambo mazuri ya baadae kwa jicho la leo.

■Imani ni kuyaona mambo ya baadae kwa kutumia wakati wa sasa.

Leo nazungumzia kuwa mtu mzima kiimani.

Mambo mazuri yote ya baadae yako katika MUNGU kupitia KRISTO YESU.

Waefeso 1:18  ''macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo;''

■■Imani katika KRISTO YESU ndio imani ya Waenda Mbinguni.

Unapoipokea imani hii ya Wokovu katika KRISTO YESU unakuwa umetokea katika imani zingine ambazo sio za MUNGU.
Imani katika KRISTO YESU unapokuwa nayo inakupasa sasa usiwe mchanga katika imani bali uwe mtu mzima  katika imani.
Leo nazungumzia Mtu mzima kiimani.

1 Wakorintho 13:11 '' Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto.''

Sasa somo la leo linasema Musa alipokuwa Mtu mzima  kwa imani yake katika MUNGU akakataa kuitwa Mtoto wa Binti Farao.

Waebrania 11:24  ''Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao;''

■Na wewe unapokuwa Mtu mzima katika imani kwa KRISTO inakupasa kuacha baadhi ya mambo au kuachana na baadhi ya Mambo yasiyofaa.

Kuna siri kubwa Musa kukataa kuitwa mtoto wa Binti Farao.

Unajua nini?

Musa angeendelea kuwa Mtoto wa Binti Farao maana yake Musa angeendelea kuwa mtoto wa ukoo wa Farao.
Musa angeendelea kuwa mtoto wa Kifarao, hiyo ingemfanya kuendelea kufuatiliwa na tabia mbaya za Kimisri.

Musa kuendelea kuwa mtoto wa Binti farao kungemfanya Musa Mizimu au miungu ya Farao iendelee kuwa na uhalali naye.
Kumbuka kuendelea kuwa Mtoto wa Farao ni kukubali kumilimikiwa na ufalme wa shetani kiroho maana Farao ni joka kubwa aoteaye.

Ezekieli 29:3  ''nena, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ewe Farao, mfalme wa Misri, joka kubwa aoteaye kati ya mito yake, aliyesema, Mto wangu ni wangu mwenyewe, nami nimeufanya kwa ajili ya nafsi yangu.''

Farao hapa anaitwa Joka, Sasa Musa alipokuwa Mtu mzima alikataa kuwa mtu wa kutoka  uzao wa shetani.

Nazungumza sasa na Mtu ambaye ni Mtu mzima katika imani ya Wokovu wa KRISTO.

Yakobo 2:22  ''Waona kwamba imani ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na ya kwamba imani ile ilikamilishwa kwa njia ya matendo yale.''

■■Walio watu wazima kiimani hawawezi kushiriki katika mambo ya kishetani kama kutambika, kukeketa watoto kama jamii zao zinavyofanya.
Kwa imani Musa alipokuwa Mtu mzima alibadilika katika maamuzi na mitazamo.

■Leo wapo Wakristo lakini kamba inayowaunganisha wao na shetani hawajaikata ndio maana wanamiliki bar, wanafanya kazi kwenye makampuni ya sigara na pombe huku wakijua mambo hayo ni kamba ya shetani.
Ndugu, Umekuwa mtu mzima kiimani sasa kwanini unaendelea kuyafanya yale yalikuwa yanakutenga  mbali na MUNGU kabla hujaokoka?

1 Petro 1:14  ''Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu;''

■■Ndugu, kama kweli wewe ni Mtu mzima kiimani usifanye machukizo kwa MUNGU.

Waefeso 5:11  ''[Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee;''

Hakikisha tu ndugu unakuwa Mtu Mzima kiimani kama Musa ambaye alipokuwa tuu Mtu mzima alikataa kuitwa Mtoto wa Binti Farao, na wewe kama kweli ni Mtu mzima kiimani kataa mambo yote yaliyo kinyume na Kusudi la MUNGU katika KRISTO.

Kama unahitaji kukua kiimani ngoja nikuambie mambo muhimu kuhusu Imani.

Mambo muhimu kuhusu Imani.

1. Usipokuwa na Imani thabiti MUNGU anaweza kuuficha uso wake kwako.

Kumbu  32:20 '' Akasema, NITAWAFICHA USO WANGU, Nitaona mwisho wao utakuwaje; Maana, ni kizazi cha ukaidi mwingi, Watoto WASIO IMANI NDANI YAO.''

■■MUNGU akiuficha uso wake kwako mambo mengi hutafanikiwa, hakikisha sasa una imani thabiti katika MUNGU kupitia KRISTO YESU.

2. Imani yako katika KRISTO YESU inaweza kukuokoa.

 Luka 17:19  ''Akamwambia, Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa.''

Hivyo ongeza Imani kwa YESU KRISTO.

3. Imani thabiti katika KRISTO YESU inakufanya uushinde ulimwengu.

1 Yohana 5:4  ''Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na MUNGU huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu.''

4. Imani yako kwa YESU wakati mwingine  inaweza ikajaribiwa, ukishinda itakuletea heshima hivyo Usiogope.

1 Petro 1:7  ''ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake YESU KRISTO .''

5. Hakikisha Imani yako inaambatana na matendo yanayoonyesha umekua Kiimani.

Yakobo 2:26  ''Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa.''

■■Musa alipokua kiakili kuna mambo yasiyo ya Ki  MUNGU aliyakataa, hivyo na wewe unakupokua kiimani kataa mambo yasiyo ya MUNGU. kukataa huko hayo ndio matendo yanayoambatana na imani iliyo hai.

6. Imani inaweza kusababisha mambo makubwa sana, ona mifano hii

●●Kuta za Yeriko zilianguka kwa Imani.

Waebrania 11:30  ''Kwa imani kuta za Yeriko zikaanguka, zilipokwisha kuzungukwa siku saba.''

●●Ukiamini kwa imani unaweza kupona.

Luka 8:50  ''Lakini YESU aliposikia hayo, alimjibu, Usiwe na hofu, amini tu, naye ataponywa.''

●●Ukimuombea Mtu kwa imani katika KRISTO YESU mtu huyo anapona kwa imani yako iliyoambatana na Maombi.

Yakobo 5:15  ''Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na BWANA atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa.mba kwa Imani kunaweza kuleta matokeo makubwa.''

●●Kwa imani Isaka aliwabariki Wanaye na wakabarikiwa kweli.

Waebrania 11:20  ''Kwa imani Isaka akawabariki Yakobo na Esau, hata katika habari ya mambo yatakayokuwa baadaye.''

●●Kwa imani Sarah akapokea uwezo wa kuzaa uzeeni na akazaa.

Waebrania 11:11 '' Kwa imani hata Sara mwenyewe alipokea uwezo wa kuwa na mimba; alipokuwa amepita wakati wake; kwa kuwa alimhesabu yeye aliyeahidi kuwa mwaminifu.'

7. Imani inaweza kukuponya.

Luka 18:42''  YESU akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya.''

Ndugu yangu uliyefuatilia ujumbe huu tangu mwanzo ushauri wangu kwako  hakikisha unakuwa Mtu mzima kiimani kama Musa.

Tito 1:13  ''Ushuhuda huo ni kweli. Kwa sababu hiyo uwakemee kwa ukali, ili wapate kuwa wazima katika imani;''
Asante rafiki yangu kwa kujifunza Neno hili la MUNGU leo.
Kabla sijahitimisha leo ninalo Neno la mwisho kwa ajili yako.
Je umeokoka? 
Kama umeokoka endelea na Wokovu wa Bwana YESU KRISTO hadi mwisho wa maisha yako.
Na wewe ambaye hujaokoka nakuomba okoka leo maana tunaishi siku  za Mwisho. 
Ni YESU tu ndio anayeweza kuliandiika jina lako kwenye kitabu cha uzima hata upate Uzima wa milele, nakuomba sana mpokee YESU KRISTO leo kwa ajili ya Wokovu. 
Huko huko uliko tafuta Kanisa la kiroho wanaohubiri Wokovu Wa KRISTO ukamweleze Mchungaji atakuongoza sala ya toba na utakuwa umeokoka.
Fanya hivyo kwa faida ya roho yako milele
MUNGU akubariki. 
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU. 
+255714252292(Sadaka ya kupeleka Injili, Maombi na ushauri)
Ubarikiwe sana

Comments