MAMBO 7 YALIYOMLETA BWANA YESU DUNIANI.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU 


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni sana tujifunze Neno la MUNGU.

Naamini unafahamu Bwana YESU alikuja Duniani mara ya kwanza na atarudi tena mara ya pili.

Bwana YESU alipokuja mara ya kwanza alikuja kwa ajili ya majukumu mbalimbali na baadhi ndio nayaeleza leo.

■Bwana YESU alikuja Duniani kwa njia ya kuzaliwa kama Mwanadamu wa kawaida ingawa sio mwanadamu kwa asili.
Luka 1:31  ''Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita YESU.''

■Alipokuja Duniani alikuwa na Mamlaka kuu yaani alikuwa juu ya yote Duniani.
Yohana 3:31  'Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote.''

■■Ulishawahi kujiuliza huyu aliye juu ya yote alikuja kufanya nini Duniani?

Mambo saba ambayo yalimleta Bwana YESU KRISTO duniani ni haya;

1. Bwana YESU alikuja Duniani kuitimiliza Torati.

Mathayo 5:17  ''Msidhani ya kuwa NALIKUJA kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.''

Kabla ya Bwana YESU KRISTO kuja duniani Mwongozo wa kiroho kwa watu wa MUNGU duniani  ulikuwa torati.
Yoshua 1:8  ''Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.''

Anapokuja Bwana YESU anasema amekuja kuitimiliza hiyo Torati.
Biblia ya kiingeleza Neno ''Kuitimiliza'' limetumika Neno ''Fulfil''
Mathayo 5:17 ''Think not that I am come to destroy the law, or the prophets: I am not come to destroy, but to fulfil.''

●●Kutimiliza(Fulfil) maana yake ni kufanya kama ilivyotakiwa au ilivyopangwa.

■Kwa hiyo mambo ambayo Bwana YESU aliyaleta kuhusu torati ni ili  kuitimiliza.

■YESU hakuja kufuta maandiko ya torati  bali kuifanya imara  zaidi.

●●Maana yake kubwa ni kwamba Bwana YESU hakuja kufuta torati bali alikuja kujazia kilichopungua kwenye torati.
Waebrania 8:7 '' Maana kama lile la kwanza lingalikuwa halina upungufu, nafasi isingalitafutwa kwa lile la pili.''

●●Bwana YESU alikuja kuboresha torati ili kufikia utoshelevu.

●●Mtu ambaye bado hajaelewa maana yake ni kwamba Bwana YESU alikuja kutimiza kwenye usahihi wake kile kilichoandikwa kwenye torati hivyo inakupasa sasa kumfuata Bwana YESU na sio torati.

Ufafanuzi wake kwa baadhi  ya  maeneo ni hivi

■Amri 10 za MUNGU kwenye torati YESU anaelezea hivi
Mathayo 22:36-40 ''Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu?  Akamwambia, Mpende Bwana MUNGU wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza.  Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako.  Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.''

■Amri ya Usiue YESU anaielezea hivi
Mathayo 5:21-22 '' Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto.''

Maana yake dhambi ni kuua na dhambi pia ni kumuonea mtu hasira ya kumuua.
Huku ndio kuitimiliza Torati.

■Amrii ya Usizini YESU anaifafanua kwenye usahihi wake hivi.
Mathayo 5:27-28 ''Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.''

Kumbe kuzini ni dhambi lakini hata kutamani kuzini na Mtu fulani nayo ni dhambi mbaya, huko ndiko kuitimiliza torati, naamini sasa umeelewa nini maana ya Bwana YESU kuitimiliza torati.
Hii ni mifano hai michache sana kati ya mingi sana ya Bwana YESU  kuitmiliza torati, hivyo mfuate KRISTO kuanzia leo.


2. Bwana YESU alikuja duniani ili wanadamu watakaoupokea Wokovu wake wapate uzima wa milele.

Yohana 10:10 ''.......   mimi NALIKUJA ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.''

■■Bwana YESU alikuja ili wanadamu waupate uzima wa milele, ni jukumu lako tu ndugu yangu kama unautaka uzima wa milele basi mpokee YESU KRISTO kama Mwokozi wako na anza sasa kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wake.

■■Hakikisha Bwana YESU KRISTO anakuwa Mwokozi wako milele, usimwache hata sekunde moja maishani mwako  mwote.

■■Hakuna njia nyingine yeyote ile nje na KRISTO inayoweza kumpeleka Mwanadamu yeyote yule uzima wa milele.
Hivyo ndugu dini yako haiwezi kukupeleka uzima wa milele kama huna YESU.
Ukimkataa YESU KRISTO umeukataa Uzima wa milele hivyo ni heri tu kumpokea kama Mwokozi wako.

3. Bwana YESU alikuja ili aziharibu na kuzivunja kazi zote za shetani.

1 Yohana 3:8  ''atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU ALIDHIHIRISHWA, ili azivunje kazi za Ibilisi.''

Ndio maana katika KRISTO YESU mapepo, mizimu, vifungo vya giza na vyote vya shetani huondoka kwa Maombi katika jina lake Bwana YESU. 

Luka 4:18  'Roho wa BWANA yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa,''

■■Kama unasumbuliwa na nguvu za giza wafuate watumishi waaminifu wa Bwana YESU watakuombea na hizo nguvu  za giza zitakuachia utakuwa huru kabisa.

4. Bwana YESU KRISTO alikuja kwa ajili ya ondoleo la dhambi kwa watakaotubu katika yeye.

Luka 24:46-47 ''Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba KRISTO atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu.''

KRISTO ili ateswe na kufufuka kwa ajili ya ondoleo la dhambi lazima aje ili hao yatokee, ndio maana alikuja.

■■Ni ni wakati wako sasa kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako kutubu na kuacha dhambi utasamehewa.

■■Ni jukumu lako ndugu Kuokoka na kuongozwa sala ya toba na dhambi zako zote zitafutwa na kuondolewa kabisa.
Haijalishi ni dhambi gani umewahi kufanya, ukiamua leo kuokoka na kuongozwa sala ya toba dhambi hizo zinaondoka.

■■Ukitubu katika KRISTO YESU unasamehewa hakika.

5. Bwana YESU alikuja kutupa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU.

Yohana 1:12-13 ''Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU.''

■■Kufanyika Mtoto wa MUNGU ni kuwa na uhusiano na MUNGU, uhusiano wa Baba na mtoto wake.

Waefeso 2:13  ''Lakini sasa, katika KRISTO YESU, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake KRISTO.''

■■Kuwa mtoto wa MUNGU katika KRISTO YESU kutakufanya utambulike Mbinguni na uwe familia ya MUNGU.

2 Wakorintho 6:17-18 ''Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema BWANA, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,''

Je unataka kufanyika Mtoto wa MUNGU?
Mpokee leo YESU KRISTO kama Mwokozi wako na anza kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wake  kuanzia sasa.

6. Bwana YESU alikuja kutafuta na kuokoa kila mwanadamu aliyekuwa amepotea.

Luka 19:10  ''Kwa kuwa Mwana wa Adamu ALIKUJA kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.''

■Wanadamu wote dunia nzima kabla hawajampokea YESU kama Mwokozi wao, hao wanadamu wakati huo wanakuwa wamepotea.

■■Mtu yeyote kabla hajaokoka ni mtu aliyepotea.

YESU alikuja kutafuta watu ambao hawajampokea maana wamepotea hivyo inawapasa kumpokea sasa kama Mwokozi waoo.
Hata mimi Peter Mabula kabla sijampokea YESU KRISTO kama Mwokozi wangu nilikuwa nimepotea hivyo Wokovu Bwana YESU ndio uliondoa kupotea na sasa ni Mwana wa MUNGU niliyeokolewa na Bwana YESU KRISTO.
Hata wewe ndugu hakikisha unampokea Bwana YESU KRISTO awe Mwokozi wako.

7. Bwana YESU alikuja kutupatia mamlaka ya kumshinda shetani na mawakala zake.

Luka 10:19  ''Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.''

■Mamlaka hii ya kuzishinda nguvu za giza iko katika KRISTO YESU tu hivyo ukiokoka na kufanyika Mtumishi wake mamlaka hiyo utaiona maana itafanya kazi kwako.
Hakikisha tuu uko ndani ya KRISTO unaishi maisha matakatifu na ni muombaji.
Asante rafiki yangu kwa kujifunza Neno hili la MUNGU leo.
Kabla sijahitimisha leo ninalo Neno la mwisho kwa ajili yako.
Je umeokoka? 
Kama umeokoka endelea na Wokovu wa Bwana YESU KRISTO hadi mwisho wa maisha yako.
Na wewe ambaye hujaokoka nakuomba okoka leo maana tunaishi siku  za Mwisho. 
Ni YESU tu ndio anayeweza kuliandiika jina lako kwenye kitabu cha uzima hata upate Uzima wa milele, nakuomba sana mpokee YESU KRISTO leo kwa ajili ya Wokovu. 
Huko huko uliko tafuta Kanisa la kiroho wanaohubiri Wokovu Wa KRISTO ukamweleze Mchungaji atakuongoza sala ya toba na utakuwa umeokoka.
Fanya hivyo kwa faida ya roho yako milele
MUNGU akubariki. 
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU. 
+255714252292(Sadaka ya kupeleka Injili, Maombi na ushauri)
Ubarikiwe sana

Comments