MIRIAMU ALIZUIA SAFARI YA WAISRAELI KUTOKANA NA MAKOSA YAKE.


Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO 

Bwana YESU KRISTO atukuzwe Ndugu zangu wote.
Karibuni tujifunze Neno la MUNGU.
Ukisoma Hesabu 12:15 kuna kitu Biblia inazungumza, Biblia inasema ''Kwa hiyo Miriamu akafungiwa nje ya kambi kwa siku saba. Watu hawakusafiri mpaka aliporudi kambini.''

Biblia inasema WATU HAWAKUSAFIRI MPAKA ALIPORUDI MIRIAMU.
Kwa nini ilikuwa hivyo?
Miriamu alifanya makosa yaliyopelekea adhabu ya kupata ukoma na kutengwa nje ya kundi la Waisraeli kwa siku 7.

Kumbuka wakati huu Waisraeli walikuwa wanasafiri, lakini kwa sababu ya kosa la Miriamu hawakusafiri siku 7 hadi Miriamu apone na kurejea kundini.
Kosa la Miriamu lilikuwa ni kuungana na Haruni kumsema vibaya Musa kwa sababu Musa alioa Mke Mwafrika yaani Mkushi.
Hesabu 12:1 ''Kisha Miriamu na Haruni wakasema kinyume na Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi ambaye alikuwa amemwoa.''

Kwenye ujumbe huu nimetumia zaidi mfano wa Miriamu kwa sababu Mtu mmoja alisababisha taifa zima lisiendelee na safari.

Nini nataka kusema kwa mifano zaidi?

■Kosa  baya mbele za MUNGU la Mama  au Baba kwenye familia linaweza kuwaweka matatani hadi watoto wakajikuta wanapata adhabu mbele za MUNGU bila kujua tatizo.
Kumbe kosa ni la mzazi lakini anayeteseka sasa ni mtoto

Maombolezo 5:7  "Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na sisi tumeyachukua maovu yao."

Mfano mzazi kujihusisha na mizimu au kuingia maagano ya damu au kuingia maagano ya kipepo.

■Kosa baya la kiongozi wa Nchi linaweza kusababisha mapigo ya MUNGU kwa nchi hiyo.

1 Wafalme 14:15-16 "Kwa kuwa BWANA atawapiga Israeli kama manyasi yatikiswavyo majini; naye atawang'oa Israeli katika nchi hii njema, aliyowapa baba zao, naye atawatawanya ng'ambo ya Mto; kwa sababu wamejifanyia maashera yao, wakimkasirisha BWANA.  Naye atawatoa Israeli KWA AJILI YA MAKOSA YA Yeroboamu, aliyoyakosa, AMBAYO KWA hayo AMEWAKOSESHA ISRAELI."

■Kosa baya la Kiongozi wa Kiroho linaweza kusababisha madhara kwa kundi  analoliongoza.

Isaya 9:16  "Kwa maana wawaongozao watu hawa ndio wawakoseshao, na hao walioongozwa na watu hao wameangamia."

Sasa kama iliwezekana Mtu mmoja kama Miriamu kuzuia safari ya taifa zima inawezekana kabisa Kiongozi mmoja Kanisani kuzuia kundi zima kupata baraka fulani ya Ki MUNGU. 

■Ujumbe huu lengo lake ni kwamba wewe uliye Kiongozi usifanye kosa linaloleta tatizo kwa wengine wasiohusika.

■Baba au Mama wa familia usifanye ushetani wowote maana ushetani huo unaweza kuja kuwaathiri hata watoto wako na wajukuu.

■Wewe ambaye unajijua kabisa kwamba kuna kosa la wazazi wako au Babu yako ambalo limesababisha wakati huu unateseka nakupa dawa leo, dawa hiyo ni moja tu kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na kuanza kuishi maisha matakatifu na ya Maombi  utakuwa sasa umetoka katika kifungo kilichotengenezwa na wazazi wako.

Ngoja nikupe mifano zaidi

1. Njaa kubwa iliwapata Israeli kipindi cha Daudi kwa sababu ya Makosa ya Sauli aliyekuwa kiongozi mkuu wa Nchi kabla ya Daudi.

2 Samweli 21:1  ''Kulikuwa na njaa siku za Daudi muda wa miaka mitatu, mwaka kwa mwaka; naye Daudi akautafuta uso wa BWANA. BWANA akasema, Ni kwa ajili ya Sauli, na kwa nyumba yake yenye damu, kwa kuwa aliwaua hao Wagibeoni.''

Kwanini kosa lako la sasa lilete madhara kwa watu wengine baadae wasiohusika?
Ni heri sana kila Mwanadamu akamcha MUNGU katika KRISTO YESU ili kuzuia adhabu kwake na kwa watu wasiohusika baadae.

2. Ahazia aliwakosesha Israeli kwa sababu ya kufuata Matendo mabaya ya Baba yake alitwae Ahabu na matendo ya Mama yake Aitwaye Yezebeli.

1 Wafalme 22:51-53 ''Ahazia mwana wa Ahabu alianza kutawala juu ya Israeli huko Samaria, katika mwaka wa kumi na saba wa Yehoshafati mfalme wa Yuda, akatawala miaka miwili juu ya Israeli.  Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, akaiendea njia ya babaye, na njia ya mamaye, na njia ya Yeroboamu mwana wa Nebati, aliyewakosesha Israeli. Akamtumikia Baali, akamwabudu, akamghadhibisha BWANA, MUNGU wa Israeli, kwa mfano wa mambo yote aliyoyafanya baba yake. ''

Kama kosa la Mtu mmoja kama Miriamu na Ahabu lilileta madhara kwa taifa zima unadhani kosa lako baya haliwezi kuleta madhara kwa watoto wako?

■■Wako Watu leo wanaingia mikataba ya kishetani wanadhani ni sawa tu lakini kumbe mikataba hiyo itaumiza ndugu zao na watoto wao.

■■Kuna watu kwenye ukoo au familia yao mnaweza mkashangaa wanapukutika tu kwa vifo vya ajabu na kumbe chanzo ni Kiongozi wa familia hiyo zamani aliingia mikataba ya kishetani. 

■■Ndugu jitahidi sana wewe usifanye kosa litakaloathiri kizazi chako au kundi unaloliongoza.

Nini ufanye?

1. Usifuate mabaya ambayo wazazi wako au viongozi wako waliyafanya.

Zaburi 34:14  "Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie."

2. Fuata mema hata kama wazazi wako au viongozi wako  hawakuwahi kuyafuata.

1 Petro 3:13  "Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema?"

Maana yake hutapata madhara ukiwa na juhudi kutenda mema.

Maana yake hutasababisha madhara ukitenda mema.

3. Tafuta Mtu mwema  wa mfano  ili ufuate nyayo zake.
Mfano ni huu
2 Wafalme 22:1-2" Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; akatawala miaka thelathini na mmoja katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Yedida, binti Adaya wa Bozkathi.  Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, AKAENDA KATIKA NJIA YOTE YA DAUDI BABA YAKE, WALA HAKUGEUKA UPANDE WA KUUME WALA WA KUSHOTO."

Yosia akamchagua Daudi kama Mtu wa mfano aliyetenda mema, akafuata mema ya Daudi akampendeza MUNGU. 
Wala Daudi hakuwa Baba mzazi wa Yosia ila ni Babu wa mbali sana ila akafuata mema yake.


4. Tubu kwa ajili ya makosa hayo na usiyatende wewe hutahusika na adhabu iliyo ndani ya mabaya hayo.

Yeremia 14:20-21" Ee Bwana, tunakiri uovu wetu, na ubaya wa baba zetu; maana tumekutenda dhambi. Usituchukie, kwa ajili ya jina lako; usikifedheheshe kiti cha enzi cha utukufu wako, kumbuka, usilivunje agano ulilofanya nasi."


5.  Mche MUNGU katika KRISTO YESU na shikamana naye daima.

Kumbu 11:22  "Kwa kuwa kwamba mtayashika kwa bidii maagizo haya yote niwaagizayo, kuyafanya; kumpenda BWANA, Mungu wenu, na kutembea katika njia zake zote, na kushikamana naye;"

Kumcha MUNGU katika KRISTO YESU kutakuweka mbali na adhabu za kipepo. Na hata kama adhabu hizo zitajaribu kukularibia ukifanya Maombi zinakufa rasmi.

Shikamana na Bwana YESU huku kwani ni kwa faida yako ya milele.

Yoshua 23:8  "bali shikamaneni na BWANA, Mungu wenu, kama mlivyotenda hata hivi leo."

Asante rafiki yangu kwa kujifunza Neno hili la MUNGU leo.
Kabla sijahitimisha leo ninalo Neno la mwisho kwa ajili yako.
Je umeokoka? 
Kama umeokoka endelea na Wokovu wa Bwana YESU KRISTO hadi mwisho wa maisha yako.
Na wewe ambaye hujaokoka nakuomba okoka leo maana tunaishi siku  za Mwisho. 
Ni YESU tu ndio anayeweza kuliandiika jina lako kwenye kitabu cha uzima hata upate Uzima wa milele, nakuomba sana mpokee YESU KRISTO leo kwa ajili ya Wokovu. 
Huko huko uliko tafuta Kanisa la kiroho wanaohubiri Wokovu Wa KRISTO ukamweleze Mchungaji atakuongoza sala ya toba na utakuwa umeokoka.
Fanya hivyo kwa faida ya roho yako milele
MUNGU akubariki. 
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU. 
+255714252292(Sadaka ya kupeleka Injili, Maombi na ushauri)
Ubarikiwe sana 



Comments