BAADA YA KUMPOKEA YESU UNATAKIWA UJITAMBUE.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni 



Bwana YESU atukuwe ndugu yangu!


Karibu tujifunze Neno la MUNGU kuhusu kuukulia wokovu.


Mteule wa KRISTO uliyeokoka sasa  inakupasa sana kujitambua, kwamba wewe ni nani katika  MUNGU na ujitambue wajibu wako kwa MUNGU na kwa wanadamu.



Bwana YESU alituletea Neno lake ili tujitambue na tumtambue MUNGU Muumba wetu, na tutambue haki zetu na nafasi zetu.



■Yapo mengi unayotakiwa kujitambua lakini jambo kuu na muhimu sana ni kujitambua kwamba wewe ni mpitaji, mgeni na msafiri tu duniani maana wenyeji wako ni mbinguni.



Siku moja Bwana YESU alikuwa anazungumza na MUNGU Baba yake  na katika maombi yake hayo alijulisha kwamba sisi wateule wake sio wa dunia hii.


Bwana YESU alisema Yohana


"Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.-Yohana 17:14-17"



Kama mteule hutaishi kama mgeni, msafiri na mpitaji duniani hakika utaishi kama mwenyeji wa dunia hii unayeipendeza dunia na maovu yake.



Siku zote msafiri yuko makini ili asiachwe na basi muda wa kusafiri ukifika.



Mpitaji hawezi kuwekeza pasipo kwao maana yeye anapita tu.



Mgeni hawezi kufuata mila za taratibu za ugenini Bali atafuata taratibu za kwao.



Tu wapitaji duniani na wenyeji wetu ni mbinguni kwa MUNGU maana tumechagua huko kupitia kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi, kutubu na kuacha dhambi.


Ndugu mteule wa MUNGU hakikisha unaishi kama mpitaji, mgeni na msafiri uliye tayari kwa safari muda wowote.



1 Petro 2:11-12 " Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho. Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze MUNGU siku ya kujiliwa."



 MUNGU hajakuita bure, Ukilijua hilo hakika utamtumikia Bwana YESU kwa uaminifu na juhudi sana.



Baada ya mtu kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wake anatakiwa mtu huyo ajitambue.



Warumi 12:1-2 " Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake MUNGU, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza MUNGU, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya MUNGU yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu."



Biblia katika kumjulisha mtu aliyeokoka ili ajitambue inamsaidia kwa kusema yafuatayo;



●Kwa sababu sasa umeokoka basi Usifuatishe namna ya machukizo ya dunia hii.



●Kwa sababu umeokoka basi geuza nia yako kutoka kuwaza mabaya na sasa nia yako igeuzwe kwa kufanywa upya kwa jinsi ya KRISTO.


 


Nia yako itageuzwa kutoka katika mabaya kwa kufanya yafuatayo;



■Kulisoma Neno la MUNGU, kulitafakari na kulitendea kazi katika ROHO MTAKATIFU.



■Yajue mapenzi ya MUNGU ya kumpendeza kwa ukamilifu.


Mapenzi ya MUNGU ni mambo ambayo MUNGU anataka ufanye.



Waefeso 5:8-11 " Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana(YESU); enendeni kama watoto wa nuru, kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli; mkihakiki ni nini impendezayo Bwana. Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee;"



Kumbuka Neno hili ya kwamba waliojitambua kwa kuokolewa na Bwana YESU na wakaishi maisha matakatifu ya Wokovu wake hakika yeye Bwana YESU atakuja kuwachukua.



●Katika kujitambua unahitaji sana utakatifu na kuongozwa na ROHO MTAKATIFU.



●Wanaojitambua humwabudu MUNGU Baba katika Roho na kweli.



●Wanaojitambua wameacha dhambi zote na sasa wanamtumikia MUNGU katika kweli ya injili.



●Wanaojitambua ni watauwa, wacha MUNGU na wamefanyika viumbe wapya waliosamehewa dhambi zao zote.



2 Wakorintho 5:17 "Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya."



Ndugu Yangu, kama kweli umezaliwa mara ya pili, umeokoka, umetubu dhambi zote na kuziacha hakika wewe ni mteule wa KRISTO unayejitambua.



■Kuokoka ni kumwamini Bwana YESU na na kumpokea rohoni


mwako kama Mwokozi wako na kuanza kuishi maisha matakatifu katika Wokovu wake.


Kuokoka ni kuchagua kumtumikia Bwana YESU.


Kuokoka ni kuchagua ROHO MTAKATIFU akae ndani yako ili akutumie katika kazi ya MUNGU.


Kuokoka ndio mwanzo wa kumwabudu MUNGU katika kweli yake.


Kuokoka ni kumpokea YESU KRISTO huku ukijitenga na shetani na kila kazi ya giza.


Kuokoka ni kuchagua kufanyika mtoto wa MUNGU.


Kuokoka ni kufanyika mwenyeji wa mbinguni unayesubiri tu muda wa kuondoka hapa ili uende huko.


Kuokoka ni Kufanyika mrithi wa uzima wa milele.


Kuokoka ni kuchagua kuacha dhambi zote na sasa unamcha MUNGU na kumtumikia na kumwabudu katika Roho na kweli.


Kuokoka ni kuchagua uzima wa milele.


Kuokoka ni kuzaliwa mara ya pili kwa maji na kwa Roho.



Yohana 3:5-7 ''YESU akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa ROHO, hawezi kuuingia ufalme wa MUNGU. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa ROHO ni roho. Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili. ''



Hongera sana ndugu kwa kuokoka.


Na wewe ndugu ambaye hujaokoka napenda kukuambia kwamba YESU KRISTO anaokoa, ukimpokea leo hakika unaokoka.


Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.


Bwana YESU KRISTO Amekaribia Kurudi.


Je, Umejiandaaje?


Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?


Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.


Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.


Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.


Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU KRISTO Kwako.


By Peter Mabula.


Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.


+255714252292.













 






MAMBO MATATU(3) YA KUFANYA ILI UKUE KIROHO.



Bwana YESU KRISTO Mwokozi apewe sifa ndugu yangu.



Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU.



Kukua kiroho ni maamuzi binafsi anayotakiwa kuyachukua kila Mteule wa KRISTO.



Biblia haitaki uwe mtoto mchanga kiroho bali inataka ukue kiroho.



1 Petro 2:1-5 ''Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote.  Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;  ikiwa mmeonja ya kwamba Bwana(YESU) ni mwenye fadhili.  Mmwendee yeye(YESU), jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa MUNGU ni teule, lenye heshima.  Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya ROHO, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na MUNGU, kwa njia ya YESU KRISTO. ''



Biblia inasema ''Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu  ''



Kila mtu anapompokea YESU KRISTO kama Mwokozi, mtu huyu anazaliwa kiroho na MUNGU na kwasababu hiyo mtu huyo kwa wakati huo anakuwa mchanga kiroho na siku zote watoto wachanga inawapasa kukua. Katika hali ya kawaida kama katika ndoa yenu mtapata mtoto kisha ikapita miaka mitano hawezi kuongea wala kusimama wala kutembea mwenyewe hakika mtashtuka sana, kama mtashtuka basi kukua ni jambo la muhimu sana. Vivyo hivyo na kiroho mtu anapompokea YESU inampasa kukua kiroho na sio kuendelea kuwa mtoto mchanga, inampasa kukua kiroho na sio kudumaa kiroho. Biblia iko wazi sana kwamba kinachoweza kumfanya mtu akue kiroho ni ''maziwa ya akili yasiyoghoshiwa'', maziwa hayo yasiyoghoshiwa ni Neno la MUNGU la uzima, ni fundisho la KRISTO, ni  maandiko matakatifu ya Neno la MUNGU yaitwayo Biblia takatifu, hayo ndiyo maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, maziwa hayo safi hayatakiwi kugoshiwa kwa sababu anayeyaleta ni ROHO MTAKATIFU ndani ya watumishi wa KRISTO walio waaminifu.



Maana yake mambo yanayohusika na Neno la MUNGU ni ya muhimu sana ili kukua kiroho.



Hivyo kukua kiroho ni hatua ambayo kila mmoja anaitamani na inatakiwa kuifikia, lakini pia kukua kiroho sio jambo ambalo unakuwa kiroho na kugota bali kukua kiroho ni jambo endelevu, inawezekana wewe sio mtoto mchanga kiroho lakini hata wewe unatakiwa kuendelea kukua maana hakuna anayezaliwa harafu kwa sababu amefikisha miaka 40 basi sio mtoto mchanga lakini je huyo agande hapo kwenye 40 siku zote?  Hapana ni lazima aendelee kukua hata kufikia miaka ya mwisho wa kuwa kwake duniani, hata kukua kiroho ni jambo endelevu.  Ukomo  wa kukua kiroho haupo duniani hadi  unapoenda aliko KRISTO yaani baada ya kumaliza kazi yako duniani ukiwa kama Mteule safi wa MUNGU kwa njia ya KRISTO YESU.



Ndugu hakikisha unakua kiroho.



Waefeso 4:13-15 '' hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa MUNGU, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, KRISTO. ''



Sasa kwa ujumla wa haraka Ili Mtu wa MUNGU akue kiroho ni lazima yahusike mambo yafuatayo.



●Kujifunza Neno la MUNGU na kulitendea kazi.



●Kuenenda katika ROHO MTAKATIFU na kuongozwa na yeye.



●Kuwa mtu wa maombi kila siku.



●Kuwa mtoaji matoleo kwa MUNGU, huku ukitoa matoleo yako kwa moyo wa upendo na imani na uaminifu.



●Kumtumikia Bwana YESU.


Maana katika utumishi huo Bwana YESU atatenda mengi na wewe kupitia hayo utaongezeka ki imani na kuwa na msimamo mzuri wa kiroho.



1 Wakorintho 15:58 "Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA."



Kila kitu chema duniani kina matumizi yake.


Moja ya kitu chema sana ni ''Imani ya Mkristo''


Ninachotaka kusema ni hiki ''Imani ya Mkristo'' nayo ina matumizi yake kama ambavyo kila kitu chema duniani kina matumizi yake.


Imani y


ako Mteule ni lazima itumike vyema, na katika Imani unatakiwa kukua kiroho.


Sio mambo yote yanahitaji Imani lakini mambo yote unayoyahitaji kupitia maombi yako yanahitaji Imani ndipo utapokea.


Kuna imani ya kuomba na imani ya kupokea.


Wakristo wengi sana wana imani ya kuomba lakini hawana imani ya kupokea.


Ngoja nikupe mfano huu.


Dada mmoja alikuwa amefunga na kuomba kwa imani kabisa kwamba MUNGU ampe Mchumba. Baada ya kumaliza maombi yake zilipita siku kama tatu hivi akaja rafiki yake na kumuuliza swali hili ''Je inawezekana Mwakani ukaolewa?'' Yule Dada muombaji aliyeulizwa swali hilo akasema '' Wakuolewa niwe mimi?''


Maana yake huyo hataki kuolewa hata kama amelia sana mbele za MUNGU kwamba anataka mume. Huyo ana imani ya kuomba ila hana imani ya kupokea, huyo hajakua kiroho  hata kuelewa vyema jinsi ya kuenenda.


Huo ni mfano usio na mambo makubwa ya kiimani. 



Ndugu mmoja baada ya kuombewa aliambiwa kwamba inampasa kutoa sadaka ya shukrani kwamba MUNGU kwa imani amempa hitaji lake, lakini yule ndugu akaondoka saa ile ile akisema kwamba MUNGU hawezi kusema hivyo. Kama Neno hilo lilitoka kwa mtumishi tu na sio kwa MUNGU ni sawa kabisa alivyosema, lakini kama alisema MUNGU hakika ndugu huyo alipishana na baraka yake maana alikuwa tu na imani ya kuomba na sio ya kupokea, kuna mambo yanaweza kutokea kwako kama kipimo cha kukujulisha kama umekuwa kiroho. Ibrahimu ili awe amekuwa kiroho na awe Baba wa imani alipewa mtihani mgumu sana wa kutoa sadaka lakini akaushinda ndipo akawa Baba wa Imani.


Rafiki za Ayubu  MUNGU aliwaambia waende na sadaka nzuri kwa Ayubu ili Ayubu awaombee ndipo MUNGU atawasemehe na kuwabariki.


Ayubu 42:7-8 ''BWANA akamwambia huyo Elifazi Mtemani, Hasira zangu zinawaka juu yako, na juu ya hao rafiki zako wawili; kwa kuwa ninyi hamkunena yaliyo sawa katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.


Basi sasa, jitwalieni ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba, mkamwendee mtumishi wangu Ayubu, mjisongezee sadaka ya kuteketezwa; na huyo mtumishi wangu Ayubu atawaombea ninyi; kwa kuwa nitamridhia yeye, nisiwatende sawasawa na upumbavu wenu; kwani ninyi hamkunena maneno yaliyonyoka katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu ''


Mtihani huu angepewa mtu mmoja hapa kwamba atoe sadaka ya ng'ombe saba ndipo atapata baraka yake hakika mtu huyo anaweza sio tu akahama kanisa bali akahama mji au nchi kabisa. Imani ya kupokea wakati mwingine huwa inaambatana na mambo mengi sana ya kiimani, kama hayo yametoka kwa MUNGU hakika ni faida ila kama yametoka kwa mwanadamu kwa sababu ya tamaa zake basi hakuna jibu la MUNGU hapo.



Nimekupa mifano miwili juu ya umuhimu wa kukua kiroho.



 Sasa  kiini cha somo la leo ni hiki hapa.



Ili ukue kiroho zingatia haya.



1. Ili ukue kiroho unahitaji sana kulisoma sana na kulitafakari Neno  la MUNGU.



Wakolosai 3:16-17 ''Neno la KRISTO na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia MUNGU kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye.''



Neno la MUNGU lina ujumbe wa namna nyingi kulingana na nyakati na lakini wakati huu tuliopo ni wakati wa injili ya KRISTO, hivyo injili ya KRISTO  ndio msingi wa sasa Wokovu.



Lakini pia ili mtu akue  tunafahamu kwamba anahitaji vyakula  mbalimbali, hata kukua kiroho unahitaji vyakula mbalimbali vya kiroho.



Kuna aina 4 za vyakula vya kiroho na vyakula hivyo wachungaji na wahubiri wote wanatakiwa kuhusika navyo katika kuwalisha watu wa MUNGU ili watu wa MUNGU wakue kiroho.



  A.Vyakula vya kulinda mwili; Mfano kufundisha watu wa MUNGU kujiepusha na dhambi na kuwafundisha hila za shetani ambazo wanatakiwa kuziepuka, wakiziepuka hila hizo za mawakala wa shetani hakika hapo unakuwa  umeulinda Mwili wa KRISTO ambao ndio Kanisa. Kuwafundisha watu wajitenge na mafundisho ya uongo, hapo hakika unakuwa unawalinda watu hao ambao ni kanisa la MUNGU. Kanisa lazima lilindwe ili shetani asipate nafasi katika Kanisa, mafundisho ya namna hiyo mimi


nayaita vyakula vya kiroho vya kuulinda mwili, yapo mengi na sio hayo tu ila kwa mifano miwili ni hiyo.



Matendo 20:28 ''Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo ROHO MTAKATIFU amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake MUNGU, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.''



  B. Vyakula vya kujenga mwili; Mfano wa vyakula vya kiroho vya kuwajenga watu ni kuwafundisha imani, kuwafundisha jinsi ya kutembea na MUNGU, kuwafundisha kazi za ROHO MTAKATIFU ndani yao n.k



Waefeso 2:20-22 ''Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye KRISTO YESU mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika BWANA. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya MUNGU katika ROHO.'' 



Kujengwa juu ya msingi wa mitume na manabii maana yake Neno la MUNGU walilofundisha mitume na manabii wa ndani ya Biblia linatujenga, Neno la KRISTO linatujenga kiroho na linatuunganisha hadi tunakuwa hekalu la MUNGU na tunakuwa makazi ya ROHO MTAKATIFU. Vyakula vya kuwajenga watu kiroho ni lazima viwepo.



  C. Vyakula vya kutoa uchafu(dhambi) mwili: Vyakula hivi vya kiroho navyo ni muhimu sana. Mfano ya vyakula hivi ni Neno la kuwafungua watu waliokuwa wamefungwa na nguvu za giza. Mapepo ni uchafu, dhambi ni uchafu, mila za kipepo ni uchafu, kujitegemea pasipo MUNGU ni uchafu n.k 



Ziko sumu nyingi za kishetani ambazo watu walimezeshwa kipindi hawajampokea YESU, sumu hizo za kipepo ni lazima ziondoke ndani ya watu wa MUNGU. Yako masomo mengi anayofunua ROHO MTAKATIFU ili watu wafunguliwe.



Kumbuka kazi mojawapo ya Bwana YESU iliyomfanya aje duniani ni ''Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. -1 Yohana 3:8b ''



  D. Vyakula vya kuupa mwili nguvu:  Vipo vyakula vingi sana vya kiroho vya kuupa mwili wa KRISTO nguvu, mfano mmoja wapo ni kufundisha sana juu ya maombi maana maombi huambatana na nguvu za MUNGU na nguvu hizo zikiwa ndani ya mwili wa KRISTO ambao ni mteule basi hakika mteule huyo atakuwa na nguvu daima. 



1 Nyakati 16:11 '' Mtakeni BWANA na nguvu zake; Utafuteni uso wake siku zote.   ''



Mwili wa KRISTO lazima ule chakula cha kiroho cha kuupa nguvu.



Chakula cha kiroho ni Neno LA MUNGU.



Wakristo ni kanisa na kanisa ni mwili wa KRISTO.


Mkristo ni mwili wa KRISTO.


Ili mwili utimilike ni lazima mwili huo upokee vyakula vya aina hiyo 4 niliyoitaja.



Chakula ni neno La MUNGU.


Kuna watu hupenda vyakula vya kujenga mwili tu lakini chakula cha kulinda mwili hawahitaji ndio maana afya zao za kiroho zinazorota maana wamekosa chakula cha kulinda mwili.


Kuna watu hupenda tu chakula cha kulinda mwili lakini chakula cha kutoa uchafu hawakitaki wakati uchafu huo mwilini hadi utoke ndio watakuwa na afya nzuri ya kiroho.



Chakula cha kulinda mwili ni maombi.


Chakula cha kutoa uchafu mwilini ni neno la maonyo ili watu watubu na kukimbilia toba kwa BWANA YESU ndio uchafu(dhambi) wao utaondoka.



2. Ili ukue kiroho unatakiwa kuliweka Neno la MUNGU kwenye vitendo.



Kuongezeka kiroho hutokana na mambo yafuatayo.



■Maisha ya maombi, baada ya kujifunza Neno la MUNGU ambalo linakuelekeza maombi na kisha ukaingia katika maombi na ukawa unatembea katika maombi siku zote, basi  hapo neno la MUNGU ulilojifunza umeliweka katika vitendo, hiyo hukufanya ukue kiroho.



■Maisha ya ibada, ulilisikia Neno la MUNGU linalokuelekeza umuhimu wa kuhudhuria ibada kila mara na umezingatia Neno hilo, hapo unakuwa umeliweka Neno katika vitendo.



■Maisha ya kushuhudia wengine injili ya KRISTO, Umejifunza Neno la MUNGU juu ya umuhimu wa kuwashuhudia wengine injili ya KRISTO, unaposhuhudia hakika umeliweka Neno la MUNGU katika vitendo, na hiyo ni njiia moja wapo ya kukua kiroho maana MUNGU atakutumia hata huko kwenye kushuhudia.



  ■Kuenenda kwa ROHO MTAKATIFU, Umejifunza kuhusu ROHO MTAKATIFU na umeamua kumtii na kumsikiliza kila siku, hiyo itakupa faida na zaidi ya faida katika kukua kiroho.



  ■Maisha matakatifu, unapoanza kuishi maisha matakatifu baada ya Neno la MUNGU kukujulisha basi hapo unakuwa umehamishia Neno ka


tika matendo na ndivyo Biblia inavyotaka.



■Mfano umefundishwa FAIDA ZA MAOMBI na MAOMBI YA KUFUNGA, vitendo vinavyotokana na Neno hilo ni wewe kuwa muombaji, kuhudhuria mikesha ya maombi na kutenga muda wa kuwa na maombi ya kufunga.



Kumbuka ili ukue kiroho Biblia inasema yafuatayo.


Yakobo 1:22-25 " Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo. Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake."


Mfano umefundishwa JINSI YA KUISHI MAISHA MATAKATIFU , vitendo ni kuhakikisha unaishi maisha matakatifu katika mienendo yako yote.


Umefundishwa FAIDA ZA MATOLEO, vitendo hakikisha unakuwa mtoaji na toa kwa moyo wa upendo.


Mfano umefundishwa MAADUI WA IMANI, vitendo ni hakikisha unajiepusha na maadui wa imani.



3. Ili ukue kiroho unatakiwa kuzaa matunda.



Bwana YESU anasema juu yako Mteule kwamba " Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo BABA kwa jina langu awapeni.-Yohana 15:16"



Uzaeje matunda?


Ukiwashuhudia watu injili unazaa matunda. Ukiwaombea watu na nguvu za Giza zikawatoka umezaa matunda, na kuzaa matunda ni njia mojawapo ya kukua kiroho kwa haraka.


Kuzaa matunda katika KRISTO ndio matokeo ya kukua kiroho.


Ukifanya huduma mfano uinjilisti, uimbaji n.k unakuwa unazaa matunda katika ufalme wa MUNGU na hatua hiyo ni ukuaji wa kiroho.


Hivyo ili ukue kiroho hakikisha unazaa matunda.



Ndugu Fanya juhudi za kukua kiroho ukizingatia maelekezo hapo juu.


' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa.-Ufunuo 3:22 ''


Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.


MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu.


Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.


Bwana YESU KRISTO Amekaribia Kurudi.


Je, Umejiandaaje?


Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?


Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU KRISTO Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.


Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.


Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.


Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.


By Peter  Mabula.


Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO.


+255714252292( Chochote na hadi whatsapp).


Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments