Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni tujifunze Neno la MUNGU.
Hata wakati umesingiziwa mtumaini MUNGU.
Mithali 3:5-6 '' Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako."
✓Kusingiziwa ni kusemewa uongo na mtu ili udharaulike au ili uadhibiwe bila kosa.
✓Kusingiziwa ni kutolewa sababu ya uongo kuhusu wewe ili uingie matatani.
Ngoja niweke wazi mapema kabisa juu ya hili kwamba sifa za msingiziaji kibiblia ni mpumbavu,Yaani wasingiziaji wote ni wapumbavu. Wasingiziaji hawana sifa nyingine yeyote nje na upumbavu.
Mithali 10:18 "Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo, Na yeye asingiziaye ni mpumbavu."
Wako watu wengi wamesingiziwa na na kupelekea kuharibiwa maisha au kusababishiwa kuchelewa kwa baraka zao fulani.
Ndugu tambua jambo hili, Mtu kukusingizia hakutaharibu hatima Yako njema kama una YESU KRISTO.
Msingiziaje ni mtu wa hila na hila hiyo inaweza kuleta madhara makubwa.
Zaburi 52:2-4 " Ulimi wako watunga madhara, Kama wembe mkali, Ewe mwenye hila. Umependa mabaya kuliko mema, Na uongo kuliko kusema kweli. Umependa maneno yote ya kupoteza watu, Ewe ulimi wenye hila."
Ngoja tuone baadhi ya mifano ya watu katika Biblia waliosingiziwa.
1. Yusufu alisingiziwa kwamba ametaka kumbaka mke wa mkuu wa jeshi.
Mwanzo 39: 6-20 utasoma yote lakini mstari wa 19 na 20 Biblia inasema " Ikawa bwana wake aliposikia maneno ya mkewe aliyomwambia, akisema, Mtumwa wako amenitendea mambo kama haya, hasira yake ikawaka. Bwana wake akamtwaa Yusufu, akamtia gerezani, mahali walipofungwa wafungwa wa mfalme, naye akawamo humo gerezani."
✓✓Madhara ya Yusufu kusingiziwa yalisababisha kufungwa gerezani miaka mingi bila hatia, usingiziaji ni jambo baya sana.
2. Mwanamke aliyesingizia ili aibe mtoto wa mwenzake.
1 Wafalme 3:17-28 utasoma yote ila mstari wa 26 Biblia inasema " Ndipo mwanamke yule, ambaye mtoto aliye hai ni wake, akamwambia mfalme kwa maana moyoni mwake alimwonea mtoto wake huruma, akasema, Ee bwana wangu, mpe huyu mtoto aliye hai, wala usimwue kamwe. Lakini yule mwingine akasema, Asiwe wangu wala wako; na akatwe."
✓Ilikuwa kidogo mtoto auawe na chanzo ni usingiziaji, ila hekima za Mfalme Suleimani na huruma za mzazi wa mtoto husika viliokoa maisha ya mtoto huyo.
Inawezekana wewe umesingiziwa uongo kwenye ukoo wenu ndio maana wewe umebaki kuwa mnyonge mbele za wana ukoo wenzako.
Inawezekana unasingiziwa uongo kazini ndio maana huna raha wala amani kazini maana muda wowote unaweza kufukuzwa kazi bila kosa.
Dada mmoja alisingiziwa kwa kuzushiwa kwamba ana miaka mingi sana hivyo kila kijana akitaka kumuoa anaambiwa "Huyu ni mzee sana, anakuzidi miaka zaidi ya kumi "
Hali ile ilipelekea vijana wote Kanisani kwao kudhani binti huyo ni mkubwa mno kiumri hivyo alichelewa kuolewa kwa miaka mingi sana sana. Chanzo ni uzushi yaani mtu wa miaka 20 na kidogo watu wameaminishwa kwamba ana miaka zaidi ya 40, ni hatari sana.
Inawezekana wewe ulisingiziwa kwenye ndoa yako au kwenye uchumba ndio maana ndoa yako ikafa au uchumba wako ukavunjika na kukuachia maumivu makubwa sana.
Inawezekana umesingiziwa kwenye eneo lako la biashara ndio maana wateja wamekukimbia bila kosa.
Inawezekana ulisingiziwa uongo Kanisani kiasi kwamba wanakanisa karibu wote wanakunyooshea vidole wakati umesingiziwa na mbingu zinajua unaonewa.
Inawezekana ulisingiziwa kwenye familia yenu na sasa ndugu zako wamekutenga.
Biblia inawataka watu wote kutokuwa wasingiziaji, mfano hapa wanawake hasa wake za watumishi wanasisitizwa kutokusingizia watu.
1 Timotheo 3:11 "Vivyo hivyo wake zao na wawe wastahivu; si wasingiziaji; watu wa kiasi, waaminifu katika mambo yote."
Mama mmoja ambaye ni rafiki yangu siku moja aliniambia kwamba aliwahi kusingiziwa kwa hila na watu wake wa karibu kwamba amekuwa kichaa, hivyo akapelekwa kwa nguvu hospitalini sehemu ya vichaa, akiwa kule alijaribu kuwaambia madaktari kwamba yeye sio kichaa lakini kwa sababu ya maelekezo ya hila ya watu wenye nguvu hakuna aliyemsikiliza bali alikaa huko muda mrefu huku muda wote akilia tu.
Kisha akiwa hiyo sehemu ya vichaa wakati yeye ni mzima alichukua simu yake na ku-search Google masomo ya maombi hivyo akakutana na somo langu moja akasoma na kuomba kwa sauti maombi ya ndani ya somo hilo hadi madaktari wakaamua kumwachia maana alikuwa sio kichaa ila kaletwa kwa nguvu na watu wa karibu ili wamkomeshe na kuharibu maisha yake.
Dada mmoja akiwa shuleni alisingiziwa kwamba ni mchawi, kumbe aliyeanzisha huo uzushi/usingiziaji ndiye mchawi. Aliyesingiziwa alikosa tumaini na wanafunzi wote walimuogopa na kumchukia na kumbe wala hajui chochote kuhusu uchawi.
Ndugu, wasingiziaji wapo lakini hata ikitokea umesingiziwa lolote kwenye maisha yako wewe mtumaini MUNGU.
✓✓Kumbuka kisasi cha MUNGU ni kikali sana hivyo usijitetee bali mwache YESU akushindie, ukijitetea kimwili MUNGU anakuacha hivyo heri kumtegemea MUNGU hata katika wakati wako huo mgumu sana.
✓✓Kama una YESU KRISTO ni kwamba usingiziaji wanaokufanyia watu hautabadili hatima Yako na baraka za MUNGU kwako.
Kuna ushindi ukimtegemea MUNGU katika KRISTO YESU, tena MUNGU atawashusha maadui zako na wewe utakuwa ni mshindi.
2 Wafalme 18:5-8 " Alimtumaini BWANA, Mungu wa Israeli; hata baada yake hapakuwa na mfano wake katika wafalme wote wa Yuda, wala katika hao waliomtangulia. Maana alishikamana na BWANA, hakuacha kumfuata, bali alizishika amri zake BWANA alizomwamuru Musa. Naye BWANA akawa pamoja naye, kila alikokwenda alifanikiwa; tena alimwasi mfalme wa Ashuru, wala hakumtumikia. Akawapiga Wafilisti mpaka Gaza na mipaka yake, tangu mnara wa walinzi hata mji wenye boma."
Ni kwanini umtumaini MUNGU wakati umesingiziwa?
1. Ni kwa sababu wakati huo ni rahisi kurudi nyuma kiroho kama waliokusingizia ni mnaoshirikiana kwenye mambo ya kiroho.
2. Ni kwa sababu wakati huo ni rahisi kukata tamaa hata ukapoteza haki zako mbele za MUNGU.
3. Ni kwa sababu wakati huo ni rahisi kutekwa na shetani maana utakuwa umevurugwa.
4. Ni kwa sababu wakati huo ni rahisi kujitetea kimwili hivyo MUNGU anakuacha na unapata madhara zaidi.
Ngoja nikujulishe baadhi ya sababu zinazopelekea watu kukusingizia.
1. Wanakusingizia na kukuzushia uongo kwa sababu ya wivu.
Matendo 5:17-19 "Akaondoka Kuhani Mkuu na wote waliokuwa pamoja naye, (hao ndio walio wa madhehebu ya Masadukayo), wamejaa wivu, wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza; lakini malaika wa BWANA akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema,"
2. Wanakusingizia kwa sababu kuna kitu kizuri umewazidi na wao hawana.
Matendo 7:9 "Wale wazee wetu wakimwonea wivu Yusufu, wakamwuza aende Misri. MUNGU akawa pamoja naye,"
Yusufu aliiona kesho yake njema kwa ndoto hivyo ndugu zake kwa sababu hawakuona kesho zao wakamchukia na kumuuza Misri huku mbele za Baba yao wakisingizia Kwa kusema amekufa kwa kuliwa na mnyama mkali.
3. Wanakusingizia kwa sababu wewe una kibali Kwa MUNGU kuliko wao maana hawajaokolewa na YESU KRISTO.
1 Petro 4:14 "Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la KRISTO ni heri yenu; kwa kuwa ROHO wa utukufu na wa MUNGU anawakalia."
4. Wanakusingizia kwa sababu hufanyi maovu kama wao.
Mwanzo 39:9 "Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu cho chote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose MUNGU?"
Yusufu alikuwa hatendi dhambi ndio maana walipotaka kumwingiza dhambini alikataa hadi akasingiziwa kwamba alitaka kubaka.
5. Wanakusingizia kwa sababu una msimamo thabiti kwa YESU KRISTO.
Mathayo 5:11-12 " Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu."
6. Wanakusingizia ili wewe uharibikiwe na wao wafanikiwe.
Yaani ili wakushushe wewe na wao wawe juu yako.
Yeremia 18:18" Hapo ndipo waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yo yote."
Hawa walianza vita ya kumpiga Yeremia kwa vivywa vyao hivyo walijaa uongo, uzushi na usingiziaji kwa Yeremia ili wamshushe kisha wao wawe juu yake, ila hawakufanikiwa.
7. Wanakusingizia kwa sababu unatishia nafasi zao.
1 Samweli 18:8-9 "Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile."
Ndugu, hata kama umesingiziwa na kudhalilishwa nakuomba mtumaini MUNGU katika KRISTO YESU maana MUNGU atakuinua wewe na kuwashusha wao.
Yeremia 17:7 "Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake."
Nini MUNGU anaweza kufanya ikiwa umesingiziwa na unamtegemea yeye MUNGU bila kulipa kisasi?
1. MUNGU atakulipizia kisasi kama kisasi cha MUNGU kinahitajika.
Kumbu 32:35 " Kisasi ni changu mimi, na kulipa, Wakati itakapoteleza miguu yao; Maana siku ya msiba wao imekaribia, Na mambo yatakayowapata yatafanya haraka."
MUNGU atakulipizia kisasi hivyo usilipe kisasi wewe.
Warumi 12:19 "Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya MUNGU; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena BWANA."
2. MUNGU atamharibu huyo aliyekusingizia.
Zaburi 101:5 "Amsingiziaye jirani yake kwa siri, Huyo nitamharibu. Mwenye macho ya kiburi na moyo wa majivuno, Huyo sitavumilia naye."
3. Aliyekusingizia atakuwa ni mtu wa kutetereka katika nchi
Zaburi 140:11 "Msingiziaji hatawekwa imara katika nchi, Mtu wa jeuri, uovu humwinda kumwangamiza."
4. Msingiziaji atakataliwa na MUNGU.
Zaburi 5:6 "Utawaharibu wasemao uongo; BWANA humzira mwuaji na mwenye hila"
Ndugu kuna faida kwako ukimtegemea MUNGU wakati wote, hata wakati umesingiziwa.
Ndugu kuna faida ukibaki na YESU KRISTO wakati wote, hata wakati wa magumu na kusingiziwa.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai
+255714252292( whatsapp).
Ukipenda ku-share kwa marafiki zako ujumbe huu Share kama ulivyo, usibadili chochote, Ubarikiwe
Comments