KATIKA KANISA KUNA.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni 


Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze kitu kupitia Neno hili la MUNGU wa Mbinguni.

Katika Kanisa Kuna watu wa aina nyingi.

1. Katika Kanisa wapo Wana wa Isakari, hawa ni Wateule wa KRISTO wanaojua nyakati.

“Na wa wana wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende; vichwa vyao walikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao.
  — 1 Mambo ya Nyakati 12:32 (Biblia Takatifu)


✓✓Watu wa aina hii ni watu ambao MUNGU amewapa akili ya kujua nyakati na kujua Nini Watu wa MUNGU wafanye kwa wakati huo kinapasacho mbele za MUNGU.

Mfano hai ni akina Danieli ambao walijua mambo kutoka ulimwengu wa roho.

Danieli 1:17 "Basi, kwa habari za hao vijana wanne, MUNGU aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima; Danielii naye alikuwa na ufahamu katika maono yote, na ndoto."

✓✓Mkristo aina ya Mwana wa Isakari anajua Siri nyingi za kiroho ambazo ROHO MTAKATIFU humjalia kujua kwa faida ya Kanisa.

Zaburi 25:14" Siri ya BWANA iko kwao wamchao, Naye atawajulisha agano lake."

✓✓Ushauri wangu, kama kweli Wewe ni Mkristo aina ya Mwana wa Isakari fuata kile ROHO MTAKATIFU anakujulisha ili uliponye Kanisa na Taifa ili Kanisa libaki katika KRISTO kwa ubora ule ule ambao Bwana YESU KRISTO Mwokozi anautaka.

2. Katika Kanisa Kuna Wakristo aina ya Wana wa kora.

Ukisoma Matendo 7:38 unagundua Waisraeli walikuwa Kanisa la MUNGU wakati wanatoka Misri. Lakini ndani yao kulikuwa na watu wenye tabia mbalimbali zingine mbaya na zingine nzuri, Wana wa kora walikuwa na tabia mbaya.
Nawaita Wana wa Kora kwa sababu Wana tabia kama za Kora.

Hesabu 16:1-3 " BASI KORA, mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, AKATWAA WATU, pamoja na Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi, waliokuwa wana wa Reubeni; nao, pamoja na watu kadha wa kadha wa wana wa Israeli, watu mia mbili na hamsini, Wakuu wa mkutano, waliokuwa wateule wa mkutano, WATU WENYE SIFA, WAKAINUKA MBELE YA MUSA; nao WAKAKUSANYIKA KINYUME CHA MUSA NA HARUNI, na kuwaambia, Ninyi inawatosha, kwa kuwa mkutano wote ni mtakatifu, kila mmoja miongoni mwao, BWANA naye yu kati yao; n'nini basi kujitukuza juu ya mkutano wa BWANA?"

✓✓Watu aina ya Kora huwa ni Walawi kama Kora alivyokuwa Mlawi, hawa wanaweza kuwa baadhi ya viongozi Kanisani, watu wenye karama na vipawa mbalimbali, Wana Maombi au Wa Mama Watumishi mfano Mama Mchungaji, akina Kora huwa  hawatoki katika kundi la Waumini wa Kawaida.

✓✓Hawa ni wapinzani kazi ya MUNGU na wapinzani wa kuzuia kusudi la MUNGU.
Mnaweza hata kupanga mipango ya mwaka kwamba "Mwakani Vijana Kanisani tutaanza kuhubiri mitaani na kuwaleta watu kwa YESU"  Mkristo aina ya Mwana wa Kora atapinga na kushawishi wengine kukataa jambo hilo kwa sababu ndani yake ana roho ya upinzani kwa kazi ya MUNGU.

Wakristo wa aina hiyo wenye kupinga kusudi la MUNGU hupelekea MUNGU kuwaadhibu vibaya na wengine wasipopata Neema ya KRISTO huwa na mwisho mbaya.
Hawa Makanisani wapo ila naomba usiwe Wewe unayesoma ujumbe huu.

3. Kanisani kunaweza kuwa na watu wenye Imani haba.

Mathayo 14:31" Mara YESU akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka?"

Hawa  viwango vyao vya Imani hubaki vidogo hata kama Kanisani wapo zaidi ya Miaka 30, hiyo ni kwa sababu hawajaamua kupandisha viwango vyao kwa kuwa waombaji, watoaji zaka, wenye muda wa kumtumikia MUNGU n.k
Hawa anaweza akasikia tu paka usiku anasema "nyauuuuuuuu nyauuuuuuu" yeye anapiga simu kwa Mchungaji amuombee.
Wengi wa hawa hukimbilia visaidizi vya mambo ya kiroho kwa sababu wao hawajiamini, yaani huyu anaweza hata kuwa anatembea na picha ya Mtumishi kwenye mkoba wake akiamini picha itamlinda, hubeba maji ya upako na n.k akidhani ndio atakaa salama.
Kama Wewe unajifahamu una Imani hapa katika Wokovu wa KRISTO hakikisha kuanzia leo una muda wa kufundisha, kushuhudia mitaani, kuombea wagonjwa ili uone MUNGU akiwaponya kupitia Wewe ili Imani iongezeke, Anza kuwa mwaminifu katika kutoa zaka na ishi Maisha matakatifu ya Wokovu yasiyo na michanganyo.

4. Katika Kanisa wapo wasiojulikana.

Ufunuo  3:15-16 " Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu."

Maneno ya maandiko haya waliambia Kanisa la Laodokia, ni Kanisa hata Leo wapo Watu wa aina hii, ni watu wasiojulikana.
Hawa hawajulikani kama Wameokoka au hawajaokoka, hawajulikani kama Wana YESU au hawana.
Kuwaelezea hawa ni Rahisi sana maana kwa YESU wapo na kwa Shetani wapo, Kanisani wapo na kwenye dhambi wapo, Ibadani wapo na kwa Waganga usishangae kuwakuta.
Hii ni mbaya sana.
Hawa ukikutana nao unaweza kudhani wako hai kiroho kumbe wamekufa kiroho.
Ufunuo 3:1 "Na kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na hizo ROHO saba za MUNGU, na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa."

Kama Wewe uko kundi hili badilika Leo kwa Jina la YESU KRISTO.
Amua kumfuata YESU na utamuona MUNGU wa Mbinguni.

Kwa ujumla Makanisani wapo Watu wa aina nyingi, wenye sifa njema na mbaya, lengo la ujumbe wako mwenye sifa njema aendelee na mwenye sifa mbaya aziache.
Kwa ufupi tu baadhi ya wengine walio Kanisani wenye sifa mbaya ni pamoja na hawa.

5. Watu wasiokubali kuponywa.

Waebrania 3:13 ''Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi."

Waebrania 3:15 "hapo inenwapo, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha."

6. Watu wapenda Mashindano na Manung'uniko na wenye kulalamika tu.

Wafilipi 2:14 "Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano,"

Yuda 1:16 "Watu hawa ni wenye kunung'unika, wenye kulalamika, waendao kwa tamaa zao, na vinywa vyao vyanena maneno makuu mno ya kiburi, wakipendelea watu wenye cheo kwa ajili ya faida."

7. Watu wenye Kunia makuu.

Warumi 12:3 "Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama MUNGU alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani."

Mtu anayenia makuu ni Mtu anayejiona ni Bora zaidi kuliko anavyotakiwa kuwa.

Ushauri wangu wa mwisho kwa Kanisa katika somo hili ni huu
Ukiwa na maarifa kidogo ya Neno la MUNGU unaweza kudanganywa kirahisi sana na wapinga KRISTO au wapinga Wokovu.
Ushawishi unaweza kukufanya unase kwenye ukengeufu.
Hivyo jifunze sana Neno la MUNGU.
Mtii sana ROHO MTAKATIFU.
Ishi sana Maisha Matakatifu na MUNGU wa Mbinguni atakuonekania.
Asante rafiki yangu kwa kujifunza Neno hili la MUNGU leo.
Kabla sijahitimisha leo ninalo Neno la mwisho kwa ajili yako.
Je umeokoka? 
Kama umeokoka endelea na Wokovu wa Bwana YESU KRISTO hadi mwisho wa maisha yako.
Na wewe ambaye hujaokoka nakuomba okoka leo maana tunaishi siku  za Mwisho. 
Ni YESU tu ndio anayeweza kuliandiika jina lako kwenye kitabu cha uzima hata upate Uzima wa milele, nakuomba sana mpokee YESU KRISTO leo kwa ajili ya Wokovu. 
Huko huko uliko tafuta Kanisa la kiroho wanaohubiri Wokovu Wa KRISTO ukamweleze Mchungaji atakuongoza sala ya toba na utakuwa umeokoka.
Fanya hivyo kwa faida ya roho yako milele
MUNGU akubariki. 
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU. 
+255714252292(Sadaka ya kupeleka Injili, Maombi na ushauri)
Ubarikiwe sana

Comments