MAOMBI YA KUONDOA VIFUNGO VYA KIPEPO VYA AINA MBALIMBALI KWENYE MAISHA YAKO.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU 


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote. 
Karibuni tujifunze Neno la MUNGU kisha tuombe Maombi  ya ushindi yanayotuacha tukiwa tumefunguliwa vifungo vya giza.

Kifungo cha giza ni nini?

●Kifungo cha giza ni adhabu ya kuzuiliwa kiroho katika eneo fulani baya la kiroho.

Vifungo vya kipepo  huelekezwa kwenye eneo fulani la maisha ya mtu kulingana na mawakala wa shetani waliotoa vifungo hivyo vya giza walivyopanga.

Zaburi 107:10 "Waliokaa katika giza na uvuli wa mauti, Wamefungwa katika taabu na chuma,"

Kulingana na andiko hili tuliloanza nalo ni kwamba wapo watu wapo katika kifungo cha taabu na wapo pia wengine wako katika kifungo cha chuma, jifunze kwa makini somo hili lote na utatoka na maarifa ya maombi ambayo ukiyafanyia kazi kwa maombi hutabaki na kifungo cha kiroho chochote. 

Mtu aliye katika kifungo cha kiroho kwa jina lingine anaitwa mfungwa.
Hivyo wapo watu ni wafungwa wa kiroho yaani wana vifungo vya giza au wako kifungoni.

Mwingine kifungo chake ni utasa ili asizae, mwingine kifungo chake ni ugonjwa ili asipone, Mwingine ndoa yake ndio iko kifungoni ili isiwe na amani, Mwingine kifungo chake ni mapepo ili yamfanye kutokufanikiwa.

Wako watu vifungo vyao ni katika mwili, wengine vifungo vyao ni katika afya, wengine vifungo vyao ni katika uchumi, wengine vifungo vyao ni katika uzao na wengine vifungo vyao ni katika kibali, na wengine vifungo vyao ni katika ndoa yaani adui amemzuia kuingia katika ndoa au yuko kwenye ndoa ila ndoa imefungwa kwa vifungo vibaya.
Leo tunashughulikia vifungo vya giza na kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO kila aliye kifungoni anaenda kutoka.

Baadhi ya vifungo vya kipepo. 

1. Kifungo cha ulimi.

Marko 7:35 "Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri."

Bwana YESU KRISTO alipokuwa anamfanyia huduma ya maombi mtu huyu katika andiko hili alijua ana kifungo cha kiroho cha ulimi ndio maana Biblia inaonyesha baada ya Maombi kifungo hicho cha ulimi kikaondoka na mtu yule akapona tatizo lake.

Wako watu wamefungwa vifungo vya ulimi kiroho kiasi kwamba hata kwenye haki zao hawawezi kusema kwa sababu wamefungwa kiroho.
Mfano hai ni kama yule mheshimiwa aliyeshindwa kuapa mbele ya Rais ili awe nadhani naibu Waziri,  kifungo cha kiroho cha ulimi cha muda mfupi kiliondoa baraka yake ya cheo ambayo MUNGU alimpa kupitia Mamlaka kuu ya nchi.
Naamini baada ya hapo alifunguliwa kifungo hivyo na anaendelea na majukumu yake kama kawaida.

Sasa kama una kifungo cha giza cha ulimi leo omba katika jina la YESU KRISTO ukiamuru kifungo hicho kiondoke na kitaondoka.

2. Kifungo cha uovu.

Matendo 8:23 "Kwa maana nakuona u katika uchungu kama nyongo, na tena u katika kifungo cha uovu."

Katika andiko hili tunamuona mtu ambaye watu wote wa jamii yake walimuona yuko sawa tu lakini kwa ufunuo Mtume Petro akagundua kwamba mtu yule ana kifungo cha kiroho cha uovu.
Hiyo inajulisha ya kwamba wapo watu pia wamefungwa kiroho kifungo cha uovu.
Katika Hiyo Matendo 8 kuna andiko Mtume Petro anamwambia mtu huyo atubie uovu wake mbele za MUNGU maana alikuwa mwovu kwa sababu ya kifungo cha uovu alichokuwa nacho.
Leo katika maombi omba katika jina la YESU KRISTO uking'oa vifungo vya giza vya uovu vinavyokutesa au vinavyowatesa unaowaombea katika maombi haya ya kufunga.

Hata MUNGU Baba anatutaka katika Maombi ya kufunga tuwe tunashughulikia pia vifungo vya uovu ili watu wafunguliwe na kuwa huru.

Isaya 58:6 "Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?"

3. Kifungo cha shaba.

Waamuzi 16:21 "Wafilisti wakamkamata, wakamng'oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza."

Shamba ni ngumu ila haifikii chuma, wako watu wamefungwa vifungo vya shamba katika ulimwengu wa roho. 
Inategemea tu kifungo hicho cha shaba kimeelekezwa kwenye nini.
Samson kifungo chake cha kipepo cha

shaba kilielekezwa kwenye mwili wake.
Wengine wana vifungo vya shaba kwenye afya zao au kwenye uchumi, wengine wana vifungo vya shaba kwenye uzao wengine kwenye kufaulu au kwenye kuolewa au kwenye kuoa n.k
Leo kwa Mamlaka ya jina la YESU KRISTO fungua kila kifungo cha shaba popote ulipofungwa kwacho kwenye ulimwengu wa roho katika eneo lolote la maisha yako.

4. Kifungo cha shingo.

Isaya 52:2 "Jikung'ute mavumbi; uondoke, Uketi, Ee Yerusalemu; Jifungulie vifungo vya shingo yako, Ee binti Sayuni uliyefungwa."

Katika andiko hili wanaambiwa wajifungulie vifungo vya shingo, hiyo inaonyesha huwa pia kuna vifungo vya kipepo vya shingo.
Inategemea na kazi za shingo, wengine shingo zao hugeukia tu maovu maana kwa njia ya kipepo shingo hizo zimezuiliwa kugeukia mema.
Leo kwa Maombi katika jina la YESU KRISTO fungua kifungo hicho kwako na kwa unaowaombea.

5. Vifungo vya utumwa.

Yeremia 30:8 "Na itakuwa katika siku ile, asema BWANA wa majeshi, nitaivunja nira yake itoke shingoni mwako, nami nitavipasua vifungo vyako; wala wageni hawatamtumikisha tena;"

Kifungo cha kiroho cha utumwa ni kifungo ambacho kinamfanya mtu kuwa mtumwa kwa watu.

Wako watu ni watumwa wa kiroho na wapo watu ni watumwa wa kimwili. 
Leo kwa Maombi katika jina la YESU KRISTO ondoa kifungo cha kiroho cha utumwa kwako.
Okoka kama hujaokoka na tafuta haki zako kwa maombi maana MUNGU ametununua kwa damu ya YESU KRISTO ya thamani sana ili tusiwe watumwa wa wanadamu. 

1 Wakorintho 6:20 "maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu."

 6. Kifungo cha kiroho cha nafsi.

Zaburi 142:7 "Uitoe nafsi yangu kifungoni. Nipate kulishukuru jina lako. Wenye haki watanizunguka, Kwa kuwa Wewe unanikirimu."

Huyu alikuwa kwenye maombi akimweleza MUNGU Baba aitoe nafsi yake kwenye kifungo.
Hiyo inaonyesha nafsi ya mtu inaweza ikawa katika kifungo cha giza.
Mimi Peter Mabula kazi yangu ni kukueleza ili wewe uombe na kufunguliwa uwe huru.

Kuna sababu nyingi za nafsi ya mtu kufungwa kiroho, moja ya sababu hizo ni ili mtu husika asiamue vyema mambo yatakayomsaidia katika maisha yake.

Wengine kwa sababu ya nafsi zao kufungwa kichawi wamejikuta siku zote ni watu wa kuwaza mambo ya kishetani tu, ni hatari sana.
Ndugu, leo kwa Maombi katika jina la YESU KRISTO itoe nafsi yako katika kifungo chochote cha kipepo.

7. Kifungo cha tumbo la Uzazi. 

Ayubu 3:10 "Kwa sababu haukuifunga milango ya tumbo la mamangu. Wala kunifichia taabu machoni."

Kumbe tumbo la uzazi lina milango.
Na kama tumbo la Uzazi lina milango maana halina mlango mmoja kama andiko lisemavyo, hivyo mlango kazi yake ni kufungwa au kufunguliwa.  Sasa mawakala wa shetani nao hupambana sana na Wanawake kwenye tumbo la Uzazi maana shetani siku zote ana vita na uzao wa Mwanamke yeyote.
Mwanzo 3:15 "nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino."

Hivyo sehemu kubwa zaidi ya shetani kupambana  na uzao wa Mwanamke ni mahali ambako uzao huo hutunzwa.
Na tumbo la Uzazi kwa sababu lina milango ulimwengu wa roho wa giza wanaweza kuifunga milango hiyo ya uzazi ili uzao wa Mwanamke usitokee.

Leo kwa Maombi katika jina la YESU KRISTO fungua mlango wako wa uzazi uliokuwa umefungwa na wachawi au waganga au mizimu au majini na sasa ukazae katika jina la YESU KRISTO. 

Tuliombea maombi ya uzao mwaka jana kwa siku 7 na MUNGU aliwapa kuzaa watu wengi, hivyo wewe unayehusika au unayemuombea mtu omba kwa juhudi ili kuifungua milango ya tumbo lako la uzao ili uzae katika ndoa yako, kwa jina la YESU KRISTO inaenda kuwezekana.
Ndugu usiende kwa waganga kamwe ili kusaka uzao, MUNGU hakika anaweza.
Imeandikwa hivi katika Zaburi 113:9  kwamba MUNGU  "Huweka nyumbani mwanamke aliye tasa, Awe mama ya watoto mwenye furaha."

Ni saa yako ya kufunguliwa ili ukazae na unaenda kuzaa hakika.

8. Kifungo cha kiroho cha  chuma.

Zaburi 107:10 "Waliokaa katika giza na uvuli wa mauti, Wamefungwa katika taabu na chuma,"

Hiki ni aina ya kifungo cha kiroho ambacho kinaweza kumng'ang'ania mtu maisha yake yote asifanikiwe katika eneo fulani la m

aisha yake.
Mtu mwenye kifungo cha kiroho aina ya chuma kila akijaribu kutoka katika kifungo vita ndio inaongezeka kwake, kama ni mtu wa kukata tamaa anakata tamaa hivyo anaendelea kuteswa na nguvu za giza.
Akifanya juhudi kujiondoa katika kifungo latizo linaongezeka hivyo kama hana imani kubwa anaweza hata kukata tamaa na kuendelea kuteswa na kifungo hicho, mtu uliye na YESU KRISTO hutakiwi kamwe kuwa mtu wa kukata tamaa.

Luka 18:1 "Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba MUNGU sikuzote, wala wasikate tamaa."

Ashukuriwe MUNGU Baba maana katika KRISTO YESU  tukimwita MUNGU  anaweza kututoa katika kila kifungo haijalishi ni kifungo cha chuma au cha shaba.

Zekaria 9:11 "Na kwa habari zako wewe, kwa sababu ya damu ya agano lako, nimewatoa wafungwa wako katika shimo lile lisilo na maji."

Haijalishi umefungwa katika shimo la kiroho au gereza la kiroho lenye ulinzi mkali wa majini, leo kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi unatoka katika kifungo hicho.

Haijalishi umefungwa kifungo cha ulimi au cha shingo au cha chuma au cha tumbo la Uzazi,  katika jina la YESU KRISTO kuna kutoka haraka sana katika vifungo hivyo maana Bwana YESU alikuja duniani ili watu watakaomwamini watoke katika vifungo hivyo.

Luka 4:18 "Roho wa BWANA yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa,"

 Haijalishi umefungwa kifungo cha  namna gani, leo katika jina la YESU KRISTO ukiomba kutoka katika kifungo hicho unatoka.

Zaburi 146:7 "Huwafanyia hukumu walioonewa, Huwapa wenye njaa chakula; BWANA hufungua waliofungwa;"

Haijalishi umefungwa kifungo cha uzao au kifungo cha kukuzuia kufunga ndoa,  leo omba katika jina la YESU KRISTO  utatoka katika kifungo hicho.

 Nini ufanye katika Maombi?

1. Mpokee YESU KRISTO kama hujampokea na jitakase  kwa maombi ya toba katika yeye.

Mathayo 11:28 "Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha."

2. Omba MUNGU akutoe katika kifungo hicho ulichonacho.

Zaburi 107:14 "Aliwatoa katika giza na uvuli wa mauti, Akayavunja mafungo yao."

3. Omba MUNGU akufungue kifungo ulichofungwa na nguvu za giza.

Zaburi 102:20 "Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa, Na kuwafungua walioandikiwa kufa."

4. Tangaza kutoka katika kila kifungo unachokifahamu.

Isaya 49:9 "kuwaambia waliofungwa, Haya, tokeni; na hao walio katika giza, Jionyesheni. Watajilisha katika njia, na juu ya majabali watapata malisho."

5. Kwa Maombi ya Mamlaka katika jina la YESU KRISTO Pasua vifungo vya giza vyote vinavyotakiwa kupasuliwa ili viondoke.

Zaburi 2:3 "Na tuvipasue vifungo vyao, Na kuzitupia mbali nasi kamba zao."

6. Omba MUNGU ayapasue mafungo ya giza uliyofungwa wewe au unaowaombea.

Nahumu 1:13 "Na sasa nitakuvunjia nira yake, nami nitakupasulia mafungo yako."

7. Fungua kila kifungo cha giza popote kilipo, tumia Mamlaka ya jina la YESU KRISTO kufungua kifungo hicho iwe ni kwenye ndoa au uchumi au uzao au kibali au mwili au afya yako au eneo au familia n.k
Unayo mamlaka katika jina la YESU KRISTO hivyo omba.

Mathayo 16:19 "Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni."

 Ndugu omba na utamuona MUNGU. 
Baada ya toba omba kwa imani katika jina la YESU KRISTO na utamuona MUNGU wa Mbinguni. 

Ndugu omba na utamuona MUNGU.

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kueleea naamini  ameelewa .

Hapa chini ni MAOMBI YA KUONDOA VIFUNGO VYA KIPEPO VYA AINA MBALIMBALI KWENYE MAISHA YAKO. 
Maombi haya ni kwa ajili ya mtu ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba.

Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua anaombea nini

MAOMBI YA KUONDOA VIFUNGO VYA KIPEPO VYA AINA MBALIMBALI KWENYE MAISHA YAKO. 

Baba MUNGU wa Mbinguni, niko mbele zako nikiomba unisam

ehe dhambi zangu zote. 
Nisamehe pia Baba maovu yangu yote na makosa yangu yote. 

Ninatubia dhambi ninazokumbuka na dhambi zote ambazo sikumbuki, ninaomba BWANA MUNGU unisamehe.

Eee MUNGU Baba wa Mbinguni ninaomba unitakase roho yangu, mwili wangu na nafsi yangu.

Nakushukuru maana umenisamehe na kunipa neema mpya.

Sasa Eee MUNGU wangu niko mbele zako kwa ajili ya maombi siku ya leo nikiomba nitoke katika kila kifungo cha kiroho, Baba MUNGU naomba unitoe katika kila kifungo cha kiroho. 

 Neno lako MUNGU linasema katika Zaburi 107:14 kwamba  "Aliwatoa katika giza na uvuli wa mauti, Akayavunja mafungo yao."

Eee MUNGU Baba ninaomba unitoe katika giza na katika uvuli wa mauti kama Neno lako linavyosema.
Ninakusihi MUNGU Baba uvunje kila vifungo vya giza nilivyofungwa ili nami mtoto wako niwe huru.

Eee BWANA ninakusihi uvivunje vifungo vya kiroho vilivyofungwa katika afya, uzao na uchumi wangu. 

Ninakusihi pia Eee Bwana MUNGU  uvunje na kuondoa kila kifungo cha giza nilichofungwa katika ndoa yangu au katika mwili wangu, katika jina la YESU KRISTO ninaamini kimevunjika.

Neno lako pia BWANA linasema katika Zaburi 102:20  kwamba "Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa, Na kuwafungua walioandikiwa kufa."

Kumbe wewe MUNGU unaweza kumfungua aliyekuwa amefungwa na unaweza kumpa kuishi mtu ambaye nguvu za giza walitaka asiishi.

Eee MUNGU Baba ninaomba unitoe katika kila kifungo cha kichawi, kifungo cha kiganga au kifungo cha laana yeyote.

Neno lako MUNGU linanitaka katika Isaya 49:9 kwamba nitoke katika kifungo.
Neno lako linasema katika  Isaya 49:9  kwamba "kuwaambia waliofungwa, Haya, tokeni; na hao walio katika giza, Jionyesheni. Watajilisha katika njia, na juu ya majabali watapata malisho."

Kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninatangaza kutoka leo katika kila kifungo cha siri cha kichawi. 

Ninatangaza kutoka katika kifungo cha magonjwa au kifungo cha kiafya, ninatoka katika kifungo hicho kwa jina la YESU KRISTO. 

Ninatangaza kutoka katika kifungo cha utasa au ugumba, ninatoka katika kifungo hicho kwa jina la YESU KRISTO. 

Ninatangaza kutoka katika kifungo cha laana au kifungo cha uzazi, ninatoka katika kifungo hicho kwa jina la YESU KRISTO. 

Ninatangaza kutoka katika kifungo cha matatizo na majanga, ninatoka katika kifungo hicho kwa jina la YESU KRISTO. 

Ninatangaza kutoka katika kifungo cha kufeli  au umasikini, ninatoka katika kifungo hicho kwa jina la YESU KRISTO. 

Ninatangaza kutoka kwenye kila kifungo  cha chuma kwenye ulimwengu wa roho au kifungo cha shaba, ninatoka katika kifungo hicho kwa jina la YESU KRISTO. 

Ninatangaza kutoka katika kifungo cha nafsi au kifungo cha ulimi au kifungo cha shingo, ninatoka katika kifungo hicho kwa jina la YESU KRISTO. 

Ninatangaza kutoka katika kifungo cha mwili au kifungo cha ufahamu, ninatoka katika kifungo hicho kwa jina la YESU KRISTO. 

Kwa  Mamlaka katika jina la YESU KRISTO napasua vifungo vya giza vyote vinavyotakiwa kupasuliwa ili viondoke.
Neno la BWANA linasema katika Zaburi 2:3 kwamba "Na tuvipasue vifungo vyao, Na kuzitupia mbali nasi kamba zao."

Hivyo ninapasua kila kifungo cha majini mahaba, katika jina la YESU KRISTO kimepasuka na sitafungwa na majini mahaba tena.

Katika jina la YESU KRISTO ninapasua mafundo yote ya wachawi juu ya mwili wangu, afya yangu, uzao wako, ndoa yangu na uchumi wangu, katika jina la YESU KRISTO kifungo hicho kimepasuka.

Kila kifungo cha kiroho cha mwanadamu asiyenipenda au kifungo cha mwanadamu aliye wakala wa shetani, kifungo hicho cha kipepo ninakifungua katika maisha yangu na ninakiondoa kwangu kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai. 

Natangaza kufunguliwa kwangu kutoka kila kifungo cha kiroho cha chuma au cha shaba au cha mwili, katika jina la YESU KRISTO  na
tangaza kufunguliwa leo.
Nina kibali cha MUNGU cha kufunguliwa kutoka vifungo vyote vya mawakala wa kuzimu, kibali hicho kinatokana na Neno la MUNGU ambapo Biblia katika Nahumu 1:13  inasema "Na sasa nitakuvunjia nira yake, nami nitakupasulia mafungo yako."

Hivyo kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu vifungo vyote vya kishetani au vya wanadamu vi

ondoke leo katika maisha yangu.

Eee MUNGU Baba ninaomba Malaika wako waende kwenye kila eneo ambalo nimefungwa ili waondoke kifungo hicho kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu. 

Kila kifungo cha mchawi au mizimu au majini, hicho kifungo nakiharibu na kukivunja na kukiondoa katika jina la YESU KRISTO. 

Naachilia mapigo katika kila wakala wa shetani aliyekuwa amenifunga, sasa nimefunguliwa kwa jina la YESU KRISTO na mapigo ya MUNGU yamfuate sasa huyo aliyekuwa amenifunga.

Katika jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu natangaza kufunguliwa kutoka kila kifungo cha siri au kifungo cha wazi. 

Naifungua milango ya tumbo langu ya uzazi iliyokuwa imefungwa,  na sasa kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO nafunguliwa kutoka vifungo vyote vya kutoka ulimwengu wa roho wa giza. 

Nakushukuru MUNGU Baba kwa kunishindia leo na kuniweka huru.
Nakushukuru Bwana YESU KRISTO kwa kwa Miujiza hii ya kunifungua kutoka nguvu za giza.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kushukuru kwa MUNGU. 
Amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen. 

Ndugu, ni hakika moja kwamba wewe umefunguliwa kwa jina la YESU KRISTO. 
Omba kwa imani na omba katika jina la YESU KRISTO. 
Mwamini MUNGU maana anatenda.
Mwamini Bwana YESU KRISTO maana yeye hutenda. 
MUNGU akubariki sana. 
By Peter Mabula. 
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi. 
+255714252292.
Ndugu, omba na utamuona MUNGU.
Ndugu endelea kuomba na utamuona MUNGU.

Comments