NAMNA YA KUJITENGA NA MIZIMU YA FAMILIA YENU AU UKOO WENU.

 


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni tujifunze Neno la MUNGU.
Natamani kila mtu asome somo hili hadi mwisho,  somo hili pia kuna wakati nitaliweka katika kitabu ili watu wengi zaidi wajitenge na mizimu.

Kabla sijaendelea sana ngoja nianze na maandiko haya ya Isaya 8  Kutoka Biblia ya kiswahili ya kisasa ambayo ni BHN Version ili ujue madhara ya mizimu.

 Isaya 8:19-22  BHN 

"Baadhi watawaambieni: “Nendeni mkatake shauri kwa mizimu na mizuka iliayo kama ndege; kwani ni kawaida watu kutaka shauri kwa miungu yao, na kutaka shauri kwa wafu kwa ajili ya walio hai.
Hakika anayesema hivyo hajapata kuona mwanga. Lakini nyinyi shikilieni lile agizo na fundisho la MUNGU. Watu watatangatanga nchini wamefadhaika sana na wenye njaa. Na wakiwa na njaa, hasira zitawawaka na kumlaani mfalme wao kadhalika na Mungu wao. Watatazama juu mbinguni
na kuiangalia dunia, lakini wataona tu taabu, giza na mauzauza ya shida. Hakuna atakayeliepa giza hilo kuu." 

Hii maana yake mizimu ni miungu na wanaoifuata Nuru ya MUNGU wa Mbinguni haiko kwao.

✓✓Kwa mujibu wa maandiko hayo ni kwamba wanaofuata mizimu watakuwa na sifa zifutazo.
1. Watu wanaofuata mizimu watakuwa watu wa kutangatanga Duniani.

2. Watu wanaofuata mizimu maisha yao yataambatana na kufadhaika.

3. Watu wanaofuata mizimu maisha yao yataambatana na njaa.

4. Watu wanaofuata mizimu Shida, dhiki na taabu zitaambatana nao.

5. Watu wote wanaofuata mizimu hadi mwisho wa Maisha yao mwishoni kila mmoja wao ataingia katika giza kuu, hili giza lina maana ya kuwa upande wa Shetani na kuwa kuzimu, hii ni hatari sana.

Sasa ni mara nyingi tumeona watu fulani wakihangaika kishetani ili tu kuhakikisha mizimu haiwasumbui.

 Kuna wengine walipopatwa na mabaya wakala wa shetani aitwaye mganga wa kienyeji aliwashauri wakaiombe msamaha mizimu na kutoa kafara.

Katika jamii nyingi  ni kawaida sana kusikia watu wakisema wana mizimu ya ukoo wao.
Lakini ukweli wa ni Neno la MUNGU kuna mashetani hujifanya kama Malaika wema lakini ni mashetani, mashetani hayo ni pamoja na mizimu.

2 Wakorintho 11:14
“Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru”.

Siku Moja Mimi Peter Mabula nilifundisha somo hili kwa wazee kazaa wa kabila langu(Wasukuma) wakawa wakali sana na kuniona kama Sina adabu na nimepotoka kuisema vibaya mizimu ila baadae baadhi yao walinielewa maana hawakuwahi kusikia katazo la kutokujihusisha na mizimu na hawakujua kwa usahihi mizimu ni Nini.

Inawezekana wewe umewahi kusikia jambo hili au hujawahi kusikia lakini ukweli ni kwamba familia nyingi  na koo nyingi na makabila mengi walijikuta wana mizimu yao, nitakupa ushuhuda wangu binafsi ndani ya somo hili.

Mizimu ni nini?

✓Mizimu ni aina fulani ya maroho wa kuzimu walio wakuu wa giza ambao wanajimilikisha familia, ukoo au eneo ili watu wa eneo hilo wawe chini ya utawala wao na maelekezo yao na kwa njia hiyo ukoo huo wanakuwa wanamwabudu Shetani bila kujua au kwa kujua.


✓Mizimu ni aina fulani ya  majini wanaojifanya kuwa ndugu, mababu au watu walioishi siku za nyuma na hivyo kushawishi  au kuwalazimisha Wana ukoo au  wana familia kuhusu mambo  ya kimaisha ili watembee katika hayo na kumkosa MUNGU wa Mbinguni.

✓Mizimu ni mashetani yanayojifanya binadamu walioishi siku za kale.

✓Mizimu ni miungu kwa jina lingine inayowamiliki watu wa familia fulani au ukoo fulani au eneo fulani au jamii fulani. 

Kwanini mizimu ndio miungu? 
Ni kwa sababu humiliki nchi fulani tu au ukoo fulani tu au eneo fulani tu au kabila fulani tu.
✓✓MUNGU wa Mbinguni anakataza Mtu yeyote kufuata miungu.

Kumbu 6:14 "Msifuate miungu mingine katika miungu ya mataifa wawazungukao;"

Maana yake kila taifa lina miungu yake,  taifa kibiblia ina maana jumuia ya watu wenye historia moja na utamaduni mmoja, hivyo hata ukoo au kabila au nchi au watu wa eneo moja wanaweza wakawa na miungu yao yaani mizimu, ni hatari sana. 
Ndio maana ukisoma maandiko utaona mataifa wasio mcha MUNGU walikuwa na miungu yao,  utaona miungu ya Waamori, miungu ya wakaldayo,  miungu ya Wamisri n.k

Yoshua 24:15 "Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia BWANA, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA."

✓✓MUNGU anatukataza sisi wateule wake katika KRISTO YESU,  anatukataza  kunyenyekea kwa mizimu wala kuitumikia mizimu. 

Kutoka 23:24 "Usiisujudie miungu yao, wala kuitumikia; wala usitende mfano wa matendo yao; bali utaiangamiza kabisa, na nguzo zao utazivunja vipande vipande."

✓✓MUNGU anataka tuangamize mizimu. 

Mizimu ni watendakazi wa shetani ili kuhakikisha wewe unayehusika unamilikiwa na shetani na kufanya mambo ya kishetani.

Mizimu ni miungu inayoshikilia familia au ukoo au jamii fulani.
MUNGU hataki wateule wake wahusike na mizimu yaani miungu. 

Mfano Misri Walikuwa na mizimu yao ambayo ilikuwa inawamiliki Wamisri lakini MUNGU alipokuja kuadhibu Misri aliadhibu hadi miungu ya Misri yaani MUNGU aliiadhibu hadi  mizimu inayowamiliki Wamisri. 

Kutoka 12:12 "Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi BWANA."

Watu wengi hudhani mizimu ni jambo zuri tu wakati haimpasi kamwe mteule wa KRISTO hujihusisha na mizimu maana mizimu ni watenda kazi wa shetani.

✓✓Ukishirikiana na mizimu  hakika wewe huitaki mbingu maana mizimu chanzo chake ni kuzimu.

Wanaojihusisha na mizimu ya ukoo  au kabila lao wanajuaje kuhusu hiyo mizimu yao?
Jambo la kwanza wanajua kwamba mzimu ni eneo la kufanyia tambiko linalosadikiwa kuwa  hapo ni makazi ya wazee wao waliofariki zamani(Angalia kamuzi ya kiswahili sanifu)

Lakini ukweli ni kwamba hawa wamepotoshwa na shetani mwenyewe maana  hakuna makazi ya roho za  waliokufa kwenye ardhi yeyote duniani, kumbuka mwanadamu ni roho hivyo roho ya mwanadamu baada ya kufa  haikai kwenye ardhi au mti au nyumba, badala yake maroho wa kuzimu kwa uongo uongo ndio wanakaa eneo hilo na kuliendesha katika kiwango ambacho watu hudhani ni roho za wazee wao waliokufa zamani na kumbe ni majini ndio yako hapo na yanatoa maelekezo katika sura za wazee wao.

Jambo la pili watu wanaojishughulisha na mizimu wanafahamu ni kwamba mzimu ni eneo kubwa ambalo husadikiwa kuwa ni makao ya pepo wakubwa wa wenyeji wa eneo hilo(Angalia kamusi ya kishwahili)
Lakini ukweli ni kwamba hao pepo wakubwa ni majini wenye vyeo vikubwa  yaani miungu  ambao huwamiliki watu hao na kuwafanya wawe chini ya ratiba ya kishetani.

Jambo la tatu ni kwamba maana ya mzimu kulingana na tafasiri ya kiswahili ni kwamba mzimu ni kivuli cha mtu aliyekufa zamani anayemtokea mtu ndotoni.

Sasa nisikilize vyema hapa itakusaidia.
Jambo hili ndilo ambalo jamii nyingi wamefundishwa na kuamini, yaani mtu anapokufa kisha baadae kwa sura yake anawatokea ndotoni wao hudhani ni mzimu wake hivyo wanaweza kufuata hata maelekezo ya mzimu huo wanaouona ndotoni.

Mfano kuna watu walitoa sadaka watoto wao kwa maelekezo ya mashetani yaani miungu/mizimu 

Zaburi 106:3738 " Naam, walitoa wana wao na binti zao Kuwa dhabihu kwa mashetani. Wakamwaga damu isiyo na hatia, Damu ya wana wao na binti zao, Waliowatoa dhabihu kwa sanamu za Kanaani; Nchi ikatiwa unajisi kwa damu."

Nisikilize ndugu, kuna aina tatu za ndoto, kuna ndoto za MUNGU, kuna ndoto za shetani na kuna ndoto zinazotokana na yale uliyoyaona na kuyawaza kwa muda mrefu.
Kichwa cha mwanadamu ni kama Memory card ya simu ambayo hutunza kila kitu ambacho mwenye hiyo simu ana-save, hivyo  Mwanadamu anachokiona au kukiwaza sana au kukizingatia sana wakati mwingine hujikuta anakiona ndotoni, hizo ni ndoto ambazo hazina maana yeyote kwa mtu huyo.

Mfano ni binti  amuwazie sana mchana kijana fulani kwamba ingependeza wafunge ndoa, binti yule usiku anaweza kuota ndoto hata mara tano akijiona anafunga ndoa na kijana yule yule, binti huyu anaweza hata akadhani ni MUNGU amemjulisha na kumbe  aliyoyawaza sana mchana au kuyaona au kuyatafakari ndio hayo yanajirudia usiku kupitia utu wa ndani maana kichwa cha binti huyu ni kama memory card ambayo ilihifanyi mchana ili aje atumie usiku kupitia kuona ndotoni.

Mtu mmoja siku moja aliniambia kwamba amemuona YESU ndotoni nikamuuliza Bwana YESU alikuwaje? Akasema ''Si yule wa kwenye filamu'' nikamuuliza mara ya mwisho hiyo filamu ya Yesu uliiona lini? akasema ''jana mchana na usiku wake ndio nikaota''  nikajua kwamba hii ni ndoto inayotokana na uliyoyawaza sana mchana au kuyaangalia kwa muda mrefu ndio yanajirudia usiku kwa ndoto, hiyo ni ndoto isiyo na maana , sio ndoto ya kweli yaani sio ndoto yenye ujumbe.

Sasa ni kawaida sana mtu akifiwa na mtu wake muhimu anaweza kumuona ndotoni  hata kila siku kwa mwezi mzima, hiyo ni ndoto inayotokana na kumuwazia mtu kwa muda mrefu, ni ndoto isiyo na maana, lakini pia kwanini watu ndoto za hivyo wanaita kutokewa na mzimu wa marehemu?
 ni kwa sababu majini huitumia nafasi hiyo kuvaa sura ya aliyekufa ili kutoa maelekezo ya kipepo na kujikuta unamilikiwa na shetani na sio kumilikiwa na MUNGU katika KRISTO YESU.

Ndugu, kama ulikuwa hujui ni kwamba mizimu ni wafanya kazi wa shetani ambao wapo kulitimiza kusudi la shetani katika familia  au ukoo au eneo.

Mizimu ni maajenti wa kuzimu kama ilivyo kwa majini mengine.
Mizimu ni maroho wa kuzimu wanaomiliki jamii fulani, ukoo fulani au familia fulani na kushinikiza watu hao kufanya mambo ya kishetani au yanayompa shetani faida.

Hujawahi kuona ukoo mzima ni walevi au watumia sigara na ugoro? 
Hujawahi kuona ukoo mzima ili uwe tajiri lazima utoe kafara mtoto wako au kafara ya mume au mke? 
Hujawahi kuona ukoo mzima ni wazinzi na waasherati? 
Wengine hujikuta katika maovu hayo kwa sababu wanamilikiwa na mizimu inayowaelekeza katika hayo, maana mizimu ni miungu yaani watenda kazi wa shetani wanaoabudiwa na wapinga KRISTO .

Yupo ndugu mmoja aliota ndoto Babu yake akimwambia aende porini na kukata miti fulani ili awe mganga wa kienyeji, akikataa wanamuadhibu, mtu yule akajikuta amegeuka mganga wa kienyeji, yaani mzimu inamfanya awe wakala wa shetani anayetambika na kuroga.
Hao ni wasio na YESU lakini sisi wateule wa MUNGU katika KRISTO YESU Biblia inasema kuhusu sisi hivi;
Kumbu 18:10-13 " Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri, wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa BWANA; kisha ni kwa sababu ya hayo BWANA, Mungu wako, anawafukuza mbele yako.  Uwe mkamilifu kwa BWANA, Mungu wako."

MUNGU wetu anatukataza hayo kwa sababu hayo yote ni kazi za mizimu au  huratibiwa na mizimu yaani miungu. 

Ndio maana hakuna mganga wa kienyeji bila kuwa na mizimu au kuhusika na mizimu.
Watu wengi wamekuwa wakitii mizimu na kujikuta siku zote wako kinyume na MUNGU Baba.
Ndugu uliye Kanisa hai la KRISTO hakikisha hufanyi patano lolote na mizimu ya ukoo au ya familia au ya kabila au ya eneo au ya Taifa. 

Kutoka 23:32 "Usifanye maagano pamoja nao, wala pamoja na miungu yao."

Ni vigumu  hata kumhubiria injili mtu aliyeshikiliwa vyema na mizimu/miungu.
2 Wakorintho 4:3-4 " Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake KRISTO aliye sura yake MUNGU."

 Watu wengine hata akiwa mtu wa kanisa anakuwa mkristo baridi au vuguvugu maana hajafunguliwa kwa maombi.

Kuna watu wengine akishika Biblia tu kusoma kichwa kinakuwa kizito na anasinzia hapo hapo hata kama ni saa moja tu iliyopita ameamka kutoka usingizi wa usiku mzima, lakini ukimpa gazeti au kitabu cha riwaya au tamthilia atasoma bila usingizi na anaweza kusoma kitabu kizima kwa masaa matatu lakini hawezi kusoma kurasa mbili za Biblia, ndugu huko ni kumilikiwa na mizimu, mizimu ni watenda kazi wa shetani kuhakikisha hujifunzi vyema habari za YESU KRISTO hata ukatii na kufanyika mwana wa MUNGU.

Kuna watu kila akiwa ibadani wakati wa Neno la MUNGU lazima asinzie, mizimu kama inakumiliki inaweza kukuzuilia kuisikia kweli ya MUNGU na kuielewa, ni hatari sana.

Mizimu iliingiaje kwenye familia yenu au ukoo wenu? 

 Mizimu huingia katika familia kwa kafara, Matambiko, Mazindiko, maagano ya kishetani au mikataba ya kishetani ya kiongozi wa familia na nguvu za giza.
Mfano kama Baba wa familia sasa anaenda kwa mganga  ili kuweka ulinzi wa kipepo kwake na kwa familia yake, na huko kwa mganga anatoa kafara labda ya mbuzi, kwenye ulimwengu wa roho wa giza wanateua mkuu wa giza mmoja ambaye ndiye mzimu/miungu ili kutekeleza matakwa ya kipepo ya familia hiyo, sasa baada ya miaka mingi baba huyu atakuwa ukoo maana alizaa watoto na watoto wake wakazaa na wajukuu zake wakazaa na kadri miaka inavyokwenda wanajikuta wanakuwa ukoo mkubwa.
 Na tukumbuke kwamba Baba yule hata kama alishafariki siku nyingi lakini aliukabidhi familia yake kwa nguvu za giza, na kwa sababu familia ile ilitengeneza ukoo basi aliukabidhi na ukoo  wake kwa shetani, hivyo ndivyo mizimu ilivyopata uhalali katika familia kisha ukoo kisha kabila au eneo na watu wa huko kujikuta wakimilikiwa na mashetani.

Mfano mama anapoamua kwenda kwa mganga wa kienyeji na kuingia mikataba ya kishetani ili apate watoto ujue watoto wote watakaotokana na tumbo lake watakuwa wameingia kwenye utawala wa mizimu aliyoenda kuitafuta kwa mganga.
Mizimu au miungu huingia sehemu kwa uhalali kupitia kafara iliyotolewa  hivyo hata vita ya kuiondoa hiyo miungu sio vita ndogo,  wakati mwingine omba maombi ya vita,  shirikisha watumishi wa MUNGU kama msuli wako wa maombi ni mdogo,  tumia sadaka kwenye  maombi yako ili kutengeneza agano la MUNGU(Zaburi 50:5), agano na MUNGU likisimama ujue maagano ya miungu /Mizimu yanatoweka na wanakuwa hawana uhalali tena wa kumtesa mtu huyo. 

Kwa sadaka na maombi  ikabidhi familia yako kwa MUNGU katika KRISTO YESU. 
Kwa sadaka na maombi hamisha uzao wako kutoka kumilikiwa au madhabahu za giza na sasa waanze kufuatiliwa na madhabahu ya MUNGU. 
 
Tumia jina la YESU KRISTO  na damu ya YESU KRISTO katika maombi yako.   

Lakini pia inawezekana wewe unatishwa na mizimu hata unataka kuua mtu wa karibu ili utoe kafara kwa miungu,  inawezekana mganga wa kienyeji au ndugu zako wamekutisha ili utekeleze matakwa ya mizimu. 
Ndugu nakuomba hakikisha unampokea YESU KRISTO kama Mwokozi na tambua kwamba MUNGU katika KRISTO YESU ana nguvu kuliko miungu hiyo yaani mizimu hiyo hivyo usiogope. 
Kutoka 18:11 "Sasa najua ya kuwa BWANA ni mkuu kuliko miungu yote; naam, katika jambo hilo walilowatenda kwa unyeti."

Siku moja kwa ufunuo nilifunuliwa baadhi ya watu ambao wanateswa na mizimu hivyo wanatakiwa kuvunja muunganiko huo kati yao na mizimu, makundi ya watu hao baadhi ni hawa. 

1. Ukiwa kwenye uwepo wa MUNGU kisha unaona kero au unatamani uondoke eneo hilo.

Mfano Kanisa zima mko katika maombi  na nguvu za MUNGU zimeshuka lakini wewe hujisikii vizuri  kuwepo hapo muda huo tu wa nguvu za MUNGU kushuka, unatamni kwenda nje ya Kanisa, yaani unaona kero kuwepo katika uwepo wa nguvu za MUNGU, ndugu, wakati mwingine ni kwa sababu unamilikiwa na mizimu hivyo vunja connection kati yako na mizimu.

2. Ukianza kusoma Biblia kichwa chako kinakuwa kizito au wakati mwingine kichwa chako kinaanza kuuma au unapata usingizi ghafla ili tu usiendelee kusoma Biblia na kutafakari Neno la MUNGU.

Ndugu, kama ni hivyo futa connection kati yako na nguvu za giza zikiwemo mizimu ya ukoo au familia.

3. Unapokuwa unaombewaa unasikia kichwa chako ni kizito sana na unajisikia vibaya isivyo kawaida.

Ndugu, wakati mwingine unamilikiwa na mizimu hivyo waeleze watumishi wanaokuombea juu ya unavyojisikia ili wakuombee na kufuta muunganiko kati yako na mizimu ya uko au familia au kabila.

4. Ukiwa kila mara ibadani wakati tu wa Neno na maombi unasinzia.

Tena inawezekana umeamka saa kumi na mbili asubuhi baada ya kulala masaa 8 kisha saa  moja asubuhi ukafika kanisani lakini saa  moja na nusu asubuhi wakati wa Neno la MUNGU unapata usingizi mzito na kusinzia lakini Neno likiisha tu unaamka na huna usingizi hata kidogo.

Ndugu, hapo ni nguvu za giza zinakuzuilia kuijua kweli ya MUNGU, mizimu inakuzuilia kufunguliwa vifungo vya giza walivyokufunga, ni mizimu inayomiliki familia yako au ukoo inajaribu kukufanya usiijue kweli ya KRISTO hata ukawa huru.
Hakikisha unaombewa ili kuvunja muunganiko kati yako na maroho hao wa kuzimu.

5. Wewe binafsi au kundi kubwa la watu katika ukoo wenu au familia yenu mnateswa na tabia chafu za aina moja.

Mfano kwenye ukoo wenu watu wengi ni watu wa pombe, wizi, uongo, ndoa za wake wengi, kuoa na kuacha, kuzalia nyumbani, ukahaba,sigara, uzinzi n.k
Ndugu, hiyo maana yake nyie mnamilikiwa na madhabahu moja ya kipepo inayosimamiwa na mizimu.
Nyie mnateswa na madhabahu moja ya kishetani ambayo inamilikiwa na mizimu ya ukoo wenu na mizimu hiyo ndio inawamiliki ninyi na kuwaendesha katika hayo.
Mizimu pia inaweza kuleta hali fulani inayofanana kwa watu wengi wa familia husika au ukoo, mfano umasikini, madeni, kuonewa, kukataliwa n.k
Ndugu chunguza kama kuna hali ya namna hiyo kwa kundi kubwa la wana ukoo au familia basi kama chanzo ni mizimu hakikisha unavunja muunganiko kati yako na mizimu ili uwe huru, mpokee YESU KRISTO awe Mwokozi wako na ukomboe ukoo wako kwa maombi kupitia jina kuu la YESU KRISTO Mwokozi.

Yohana 14:13 "Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu(YESU KRISTO) , hilo nitalifanya, ili Baba(MUNGU) atukuzwe ndani ya Mwana."

6. Miguu kuuma kwa ndani au kuwa kama inawaka moto kwa ndani.

Yaani mtu ni mzima lakini kuna muda miguu yake inakuwa inauma na kuwa kama inawaka moto.
Ndugu, kama ni muunganiko na mizimu basi hakikisha leo unajikomboa kwa maombi katika jina la YESU KRISTO.
Ukiligundua tatizo basi wafuate Wachungaji katika maeneo ya karibu na huko uliko uwaeleze kwa uwazi na watakuombea na utafunguliwa kutoka kumilikiwa na mizimu, kisha okoka na utakaa salama maana utakuwa katika YESU KRISTO Mwokozi.

7. Kuota mara kwa mara  wanyama hasa sana nyoka mkubwa  au ng'ombe akikufukuza au akikulinda.

Ukiona nyoka mara kwa mara akikufukuza maana yake huyo nyoka ni nguvu za giza hasa majini au mizimu.
Nyoka wakubwa ni mizimu au wakuu wa giza, nyoka wadogo ni majini, lakini pia unaweza ukaona nyoka akipambana na maadui zako au wanayama wengine ili kukuokoa wewe
 bado usidhani uko salama maana hiyo ni mizimu ya ukoo inajaribu kukulinda kipepo maana ndio inakumiliki kipepo, kumbuka shetani ni shetani tu hivyo baada ya muda yule yule nyoka atakumeza wewe na unaweza kujikuta unakosa mbingu, hivyo leo kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO uvunje muunganiko kati yako na mizimu ya ukoo.
Ng'ombe pia kwenye ulimwengu wa roho ni maroho wa kuzimu wa ukoo wanaowashikilia ukoo huo, uwe makini sana na omba sana ili kuuharibu muuganiko kati yako na nguvu za giza.

8. Kuota  watu waliokufa wakikupa maelekezo ya kipepo.

Hii ni niia nyingine ya mizimu kufanya kazi, hivyo vunja muunganiko kati yako na hizo nguvu za giza.
Wanaotumia mizimu husema mzimu ni kivuli cha  aliyekufa, ni roho ya aliyekufa inapokuja tena kwao lakini Biblia inasema  kwamba waliokufa  hawajui lolote linaloendelea duniani.
Mhubiri 9:5 "kwa sababu walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote, wala hawana ijara tena; maana kumbukumbu lao limesahauliwa."

Hivyo ukiona 'Mzimu'' wa mtu yeyote ujue umeona mashetani ambayo ni maroho ya kuzimu wanaovaa sura za marehemu ili kulaghai watu wa MUNGU.

Mimi  Peter Michael  Mabula, binafsi niliokoka December 2008  nikiwa mjini Magharibi unguja Zanzibar, niliokoka kwa muujiza wa MUNGU maana nilisikia sauti inikiniambia ''Nenda Kanisani maana usipoenda utakufa'' nilitii na kwenda Kanisani, mchakato wake nimeshawahi kuutoa katika masomo yangu kadhaa maana haikuwa kazi nyepesi, lakini mwisho siku hiyo hiyo nilijikuta niko Kanisa la Pentecostal Assemblies of God (P A G) Chukwani kwa Mchungaji Amos Lukanula  ambaye ndiye Baba yangu wa kiroho. Sasa miaka kadhaa baada ya mimi kuokoka nilijikuta kwenye wakati mgumu sana maana nilikuwa katika vita kubwa sana ya kiroho dhidi ya nguvu za giza,   nilifanya maombi lakini bado vita ile ilikuwa kubwa japokuwa mbingu za MUNGU zilinihakikisha kwamba nitakuwa salama, Sasa katika maombi hayo niliwiwa kuwashirikisha kuniombea watumishi wa MUNGU kumi ambao nawaamini, niliwaandikia meseji na mmoja kati yao alifunga siku saba ili kuniombea. Wakati ananiombea alishangaa kuona maono kadhaa baadhi ni haya kulingana na somo la hili ninalokufundisha. 
Alijikuta kwenye ulimwengu wa roho akiona kikao cha wakuu wa giza ambao ni mizimu, alisikia wakisema mambo haya kuhusu mimi walisema hivi ''Huyu Peter ni kijana mdogo tu kwanini anamtambulisha Mungu mwingine katika ukoo wakati sisi ndio miungu ya ukoo wake. Huyu amezuia kafara zetu nyingi sana lazima tumuwinde, sisi tuko kihalali katika ukoo wake na jamii nzima maana ni wao walitukaribisha kupitia kafara na matambiko, kwanini atusumbue na kutaka kutuondosha huyu Kijana mdogo katika ukoo?''

Nilishangaa sana baada ya maono hayo lakini nilijua nini nifanye katika maombi ili si tu kuwafukuza hao mizimu bali kuwatowesha kabisa.
Kumbe ninapohubiria ndugu zangu ili waokoke mizimu ya ukoo haitaki ndio maana ina vita na mimi, kumbe ninapoombea ndugu zangu na ukoo nakuwa nazuia kafara za kichawi nyingi hivyo mizimu wanakuwa wana hasira na mimi, nilifunuliwa juu ya namna ya kuomba na kuambatanisha na sadaka na najua katika KRISTO YESU kuna ushindi mkuu dhidi ya kila nguvu za giza, tunayo mamlaka kuu sana ambayo hakuna mzimu wala mchawi anaweza kushindana na mamlaka hiyo tuliyopewa na Bwana wetu YESU KRISTO Mwokozi wetu.

Luka 10:19 "Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru."

Sasa ngoja nikujulishe jinsi ya kujitenga na mizimu ya ukoo wenu au familia.

1. Mpokee YESU KRISTO kama Mwokozi wako, yaani okoka 

Yohana 1:12-13 " Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake;  waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU."

2. Usifanye ibada ya kishetani ya namna yeyote ile.
Ikimbieni ibada ya sanamu

1 Wakorintho 10:14 "Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu."

3. Usifanyie kazi maelekezo ya aina yeyote ya kishetani au ya mizimu.

Mfano ni huyu alienda kuuliza kwa mizimu akaishia kufa maana MUNGU alimwadhibu kwa kosa hilo. 
2 Wafalme 1:3-4, 17"Lakini malaika wa BWANA akamwambia Eliya Mtishbi, Ondoka, uende ukaonane na wale wajumbe wa mfalme wa Samaria, ukawaambie, Je! Ni kwa sababu hapana MUNGU katika Israeli, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni?  Basi sasa, BWANA asema hivi, Hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Eliya akaondoka. .......  Basi akafa, sawasawa na neno la BWANA alilolinena Eliya.  ......"

4. Haribu madhabahu za giza na choma moto vitu vyote ulivyonavyo vinavyotokana na mizimu ulivyopewa na waganga au ulivyoelekeza na waganga, kama huwezi wapelekee watumishi wa MUNGU watavichoma.

Kutoka 34:13 "Bali utabomoa madhabahu zao, na kuvunja-vunja nguzo zao, na kuyakata-kata maashera yao."

Kwenye ulimwengu wa roho mara  nyingi mizimu huonekana kama nyoka au watu waliokufa zamani wakitoa maelekezo.
Mizimu huwafanya watu wafanye ibada makaburini na kufanya ibada ya wafu.
Mtu mmoja aliota ndoto akimuona bibi yake ambaye alishafariki zamani, huyo bibi  marehemu akisema 'Mbona hupalilii kaburi langu?''
Bibi yule alikuwa jini/mzimu maana alimwambia pia kwamba akapalilie kaburi hilo na  na aweke damu ya mbuzi aliyemchinja na asipofanya hivyo atampiga mapigo mabaya.
Swali , marehemu  anaweza kumuadhibu mtu aliye hai? 
 Jibu ni kwamba haiwezekani kamwe,  huyo marehemu anayesema ataadhibu huyo sio marehemu halisi ila ni nguvu za giza katika umbo la mtu aliyekufa.
Mtu yule alijikuta anatekeleza maagizo ya mashetani yaani mizimu, na damu hiyo ilikuwa ya kuimalisha agano la kishetani la familia hiyo, ni hatari sana.

Ndugu, hakikisha una YESU KRISTO ili ukae salama. 

Watu wengi sana wamekuwa watumwa wa shetani kupitia mizimu kwa sababu wanaipenda mizimu na wanaitii na kuitumikia, ni hatari sana.
Kuna watu wanateswa na nguvu za giza kwa sababu wako katika adhabu ya hizo nguvu za giza ambazo ni mizimu, leo katika jina la YESU KRISTO omba na hizo nguvu za giza zitakuachia na utakuwa huru.
Ndugu, ukimkimbilia Bwana YESU KKRISTO hakika utakuwa huru mbali na nguvu za giza , mbali na mizimu ya ukoo.
Kuna watu mnaambiwa mmekosea masharti ya mizimu hivyo  kila mwaka mnazika au kuna matatizo makubwa sana kwenu, ndugu, mkimbilie YESU KRISTO na utakuwa salama hakika.

Bwana YESU anasema  katika Mathayo 11:28  kwamba "Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha."

Ndugu, ni YESU KRISTO pekee ndiye anayeweza  kukuweka huru milele, achana na mizimu , ikatae mizimu na usikubali kushiriki jambo lolote la kiukoo au kifamilia linalotokana na mizimu.

Nini ufanye katika maombi ili ujitenge mbali na mizimu ya ukoo au familia.

1. Baada ya kumpokea YESU KRISTO tubu kwa pale uliposhirikiana na mizimu au ulipofanyia kazi jambo ambalo chanzo chake ni mizimu.

Isaya 59:1-2 " Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia."

2. Kwa Maombi na kwa vitendo Jitenge na mizimu  kwa njia ya kuukataa na kuuvunja muunganiko uliopo kati yako na mizimu.

Kumbu 7:5-6 " Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga. Kwa maana wewe u taifa takatifu kwa BWANA, Mungu wako; BWANA Mungu wako, amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi."

3. Kwa Maombi Wafukuze mizimu na watakuachia,  wafukuze pia kwa watoto wako,  familia yako au ukoo wako.

Kumbu 3:22 "Msiwache, kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, ndiye awapiganiaye."

4. Kwa Maombi Futa agano lolote kati yako na mizimu, kati ya mama hadi bibi yako na mizimu, kati ya baba hadi babu yako na mizimu.

Maombolezo 5:7 "Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na sisi tumeyachukua maovu yao."

5. Haribu Ivunje kimaombi madhabahu ya giza iliyoshikilia ukoo wenu au familia yenu.

Kumbu 12:2-3 " Vunjeni kabisa mahali pote walipokuwa wakiitumikia miungu yao mataifa mtakayoyamiliki, juu ya milima mirefu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi; nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo."

6. Kwa Maombi Komboa vitu vyako au baraka zako kwa damu ya YESU KRISTO.

1 Yohana 1:7,9 " bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na KUTUSAFISHA NA UDHALIMU WOTE."

7. Kwa Maombi Ifute adhabu ya kipepo, kalenda ya kipepo na kila ratiba ya kishetani  iliyopangwa na mizimu.

Ayubu 5:12 "Yeye(MUNGU) huyatangua mashauri ya wadanganyifu, Mikono yao isipate kuyatimiza makusudi yao."

8. Kwa Maombi Wafungue familia yako na ukoo wako na wewe mwenyewe, wafungue kutoka katika ushirika na mizimu, wafungue kwa jina la YESU KRISTO.

Yohana 14:14 "Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya."

9. Omba MUNGU Baba akulinde siku zote.

Zaburi 121:7-8 " BWANA atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako.  BWANA atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele."

10. Iombee familia yako na ukoo wako neema ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO.

2 Wakorintho 13:14 "Neema ya Bwana YESU KRISTO, na pendo la Mungu, na ushirika wa ROHO MTAKATIFU ukae nanyi nyote."
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele.
+255714252292(Ni namba hii  kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili, meseji na whatsapp).

Uki-share kwa marafiki zako ujumbe  huu naomba share  kama ulivyo,usibadili jina wala chochote.

Comments