SAMAKI BAHARINI WANAKUSUBIRI.

 

Na Mwl Peter Mabula 


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Ziwani kuna samaki wengi sana wanatangatanga lakini wavuvi hakuna.

Baharini kuna samaki wengi sana lakini wavuvi hakuna.

Kiroho ziwani na baharini ni duniani, ni kwenye maeneo unayokaa na kwenye maeneo ya mbali na huko uliko, huko kote kuna samaki wengi lakini wavuvi hakuna.

✓✓Bwana YESU KRISTO anataka uwe mvuvi wa watu.
Marko 1:17 "YESU akawaambia, Njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu."

✓✓Kwenye familia yako, wewe uliye na YESU KRISTO unatakiwa kuwa mvuvi wa watu ili nao waokoke.

✓✓Mtaani kwako,kazini kwako na kokote uliko kuna samaki wengi sana wanaosubiri tu kuvuliwa na mvuvi hata waingie katika ghala la Bwana YESU kujiandaa na uzima wa milele.

Najua rafiki yangu umejiwekea Malengo yako mengi ya Mwaka huu, nakuomba ongeza na lengo hili la kuhakikisha angalau watu kumi wanampokea YESU KRISTO kuwa Bwana na Mwokozi wao, ukifanya hivyo utakuwa Mtu mwenye thamani sana mbele za MUNGU Baba wa Mbinguni.

Paulo ni mfano hai kwetu, aliwavuta watu ili wamwabudu MUNGU katika KRISTO YESU hadi watu walio kinyume na Wokovu wakalalamika.
Matendo  18:12-13 " Hata Galio alipokuwa liwali wa Akaya, Wayahudi wakamwinukia Paulo kwa nia moja, wakamleta mbele ya kiti cha hukumu wakisema MTU HUYU HUWAVUTA WATU ILI WAMWABUDU MUNGU kinyume cha sheria."

Ndugu yangu, kwa mwaka huu jitahidi kuwavuta watu ili waje kwa YESU hadi mawakala wa shetani walalamike.
Jiwekee Malengo hata ya kuwaalika watu 4 kila jumapili ili waje Kanisani Kuokoka.

Ndugu Mteule wa KRISTO naamini kabisa kila siku unapishana na samaki wengi wanaotangatanga maana wavuvi hakuna, wewe fanyika mvuvi sasa.
Usiogope kuvua samaki hawa ili waingie kwenye chombo cha Bwana YESU kwa ajili ya uzima wa milele, hata akina Petro na akina Yohana na Yakobo, YESU KRISTO aliwaambia wasiogope kuwa wavuvi wa watu, hata wewe usiogope kuwa mvuvi wa watu kwa ajili ya ufalme wa MUNGU.
Luka 5:10 "na kadhalika Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. YESU akamwambia Simoni, Usiogope, TANGU SASA UTAKUWA UKIVUA WATU."

✓✓Kuna marafiki zako wengi ni samaki wanaotangatanga kwa waganga wa kienyeji, unatakiwa uwavue ili waingie katika ghala la Bwana YESU KRISTO.

✓✓Kuna ndugu zako wengi ni samaki wanaotangatanga vilabu vya pombe  na kwenye  bar kulewa, unatakiwa uwavue ili waingie katika ghala la Bwana YESU KRISTO.

✓✓Kuna watu wako wa karibu wengi ni samaki wanaotangatanga kwenye uzinzi na uasherati, unatakiwa uwavue ili waingie katika ghala la Bwana YESU KRISTO.

✓✓Kuna wafanyakazi wenzako au watu wako wa karibu ni samaki wanaotangatanga kwenye machukizo ya kila namna, unatakiwa uwavue ili waingie katika ghala la Bwana YESU KRISTO.

✓✓Ndugu, kumbuka kwamba siku ulipookoka ulifanyika pia siku hiyo hiyo kuwa mvuvi wa watu.
Siku YESU KRISTO alipokuokoa hakika ni siku hiyo hiyo MUNGU alikufanya uwe mvuvi wa watu.
Marko 16:15-18 " Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya."

Ndugu kama ambavyo wewe ulivuliwa ziwani au baharini basi na wewe fanyika sasa fanyika mvuvi wa watu.

✓✓Hata kwa pesa zako yaani sadaka zako za hiari hakikisha samaki wanavuliwa na kuingia katika ghala la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
Warumi 10:15 "Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!"

✓✓Hata kwa maombi yako hakikisha unawaombea samaki wakubwa na wadogo ili wapate neema ya kuvuliwa ili waingie katika ghala la Bwana YESU KRISTO Mwokozi, ombea mchakato wote wa uvuvi, ombea wavuvi na vyombo vya kuvulia.
Mathayo 9:37-39 " Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni BWANA wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake."

✓✓Mimi Peter Mabula ni mvuvi wa watu ili waingie katika ghala la Bwana YESU Mwokozi, wewe je ni mvuvi wa nini?

Nakuomba ndugu fanyika mvuvi wa watu kwa ajili ya uzima wa milele katika KRISTO YESU.

✓✓Ukianza kuvua watu ndipo utaona miujiza mikubwa zaidi ya MUNGU.
Marko 16:20 "Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, BWANA akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.]"

Ndugu wala hujachelewa kufanyika mvuvi wa watu, anza leo na MUNGU atakuwa pamoja na wewe.

✓✓Usihubiri dhehebu maana dhehebu halimpeleki mtu mbinguni bali hubiri Wokovu wa KRISTO ambao humfanya mtu kuingia Uzima wa milele.
MUNGU akukumbuke na kukubariki.
Ni mimi ndugu yako Peter Mabula 
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili, meseji na whatsapp n.k).
Usifanye mchezo na Neno la MUNGU, hilo litadumu daima, hakuna atakayeshinda.
Isaya 40:8 "Majani yakauka, ua lanyauka; Bali neno la MUNGU wetu litasimama milele."

Comments