KIJANA KUHUBIRI INJILI LIFANYE KUWA JUKUMU LAKO.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni 


Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu yangu.

Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.


Kuhubiri Injili lifanye kuwa jukumu lako kijana.


Ngoja nianze na mifano.


✓✓Wakati Samweli anawahubiri Israeli maneno haya hapa chini hakuwa Mzee bali Kijana.


1 Samweli 7:3-4 " Basi Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, akasema, Ikiwa mnamrudia BWANA kwa mioyo yenu yote, basi, iondoleeni mbali miungu migeni, nayo Maashtorethi yatoke kwenu, mkamtengenezee BWANA mioyo yenu, mkamtumikie yeye peke yake; naye atawaokoa katika mikono ya Wafilisti. Ndipo wana wa Israeli wakayaondoa Mabaali na Maashtorethi, wakamtumikia BWANA peke yake."


Waisraeli walipomsikiliza Kijana Samweli, Mhubiri asiye na mawaa waliacha kuabudu miungu na kumpendeza MUNGU wa Mbinguni.


✓✓Daudi akiwa Kijana Biblia inasema hivi juu yake 


1 Samweli 18:14 "Naye Daudi akatenda kwa busara katika njia zake zote naye BWANA alikuwa pamoja naye."


Je na Wewe katika ujana wako unatenda kwa busara na MUNGU Yuko pamoja na Wewe? Au umeshamwacha MUNGU muda.

Ndugu, tenda kwa busara kwa kumtumikia Bwana YESU KRISTO Mwokozi.


✓✓Yeremia aliitwa katika utumishi akiwa Kijana Mdogo na hadi akaanza kutoa udhuru ili asimtumikie MUNGU.


Yeremia 1:6-8 " Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto. Lakini BWANA akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema BWANA."


Lakini alimtii MUNGU wa Mbinguni na katika utumishi wake huyo huyo Kijana aliwahi kuhubiri Maneno haya hapa chini ambayo ni faida kwa kila Mwanadamu hadi Siku ya mwisho.


Yeremia 2:19 "Uovu wako mwenyewe utakurudi, maasi yako yatakukaripia; ujue, basi, ukaone, ya kuwa ni jambo baya sana na uchungu, kuwa umemwacha BWANA, Mungu wako, na ya kuwa moyoni mwako hamna kunihofu, asema BWANA, BWANA wa majeshi."


Hata Wewe Kijana okoka na ishi Maisha matakatifu Kisha wakumbushe Ndugu na marafiki kwamba wasije wakamwacha kamwe BWANA YESU KRISTO.


Vipi Wewe Kijana unayesoma somo hili ambalo Mimi Peter Mabula nimekuletea Wewe? Kwanini usiwahubiri ukoo wako ili waache uchawi, waache kwenda kwa waganga wa kienyeji, waache pombe ili waokoke?

Kijana nakuomba fanyia kazi ujumbe huu.


◼️Kijana hubiri injili ya KRISTO kwa kila mwanadamu.


Marko 16:15 "Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe."


◼️MUNGU anawatumia vijana kwenye kazi yake kwa sababu vijana wana nguvu za kufika popote.


1 Yohana 2:14 " ........... Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la MUNGU linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu."


Sijui wewe kijana unautumiaje ujana wako katika kazi ya MUNGU.


◼️Inakupasa kuifanya kazi ya MUNGU kwa juhudi sana maana kipindi cha ujana ndicho kipindi chako ambacho una nguvu nyingi za mwili.


Mithali 20:29 "Fahari ya vijana ni nguvu zao, ....."


✓[Kuna maelfu ya watu wanasubiria kuokoka ila hakuna mtenda kazi wa KRISTO wa kuwahubiria injili ya KRISTO na kuwaongoza katika kweli yote ya Neno la MUNGU.


✓✓Kama kijana unapotumia muda wako kwa mambo mema kumbuka pia kuutumia na muda wako kumtumikia MUNGU Baba katika KRISTO YESU mwokozi.

MUNGU akubariki.

By Peter Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele.

+255714252292

Ubarikiwe sana

Comments