WAKATI UKIPITIA WAKATI MGUMU SANA.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu yangu.

Ulishawahi kuwa kwenye wakati mgumu?


Kuna kipindi fulani Mimi nilikuwa kwenye wakati mgumu sana.

Wakati huo nilichoka kila kitu na nilikuwa katika hitaji Muhimu sana sana na la lazima.


Kwa sababu ya hitaji hili na mazingira nikiyokuwepo nilibaki kuomba Maombi 4 tu.


Niliomba hivi

 1. MUNGU wangu nisamehe.

2. Bwana YESU  nisaidie  

3. MUNGU wangu niokoe

4. MUNGU wangu niponye.


Karibia siku nzima nilishindwa kuomba kwa kirefu zaidi ya kutamka tu hayo maneno 4 yaani MUNGU wangu nisamehe, Bwana YESU nisaidie, MUNGU wangu niokoe na MUNGU wangu niponye.


Maombi mengine yote yalikata ndani yangu  nikabakiwa na hayo Maombi 4 tu.


Ilikuwa katika maamuzi magumu sana na nikihitaji msaada wa MUNGU ulio mkubwa sana.

Namshukuru MUNGU kwa Neema yake ya ajabu alinisaidia nikafanikiwa katika yote kwa Jina la YESU KRISTO.


◼️Inawezekana na Wewe uko kwenye wakati mgumu sana kama ilivyokuwa kwangu Mimi Peter Mabula au uko kwenye wakati mgumu zaidi yangu.


Maombi yamekataa  umebakiwa na kulia tu, ndugu omba hata hayo Maombi 4 yamkini au Maombi Yale utakayoweza na YESU KRISTO atakuonekania.


Mimi nilipokuwa kwenye wakati mgumu wangu kichwa kilikuwa kinaumwa karibia siku nzima.

Moyo unaenda mbio, mawazo mengi yaliyovuka akili zangu, hofu na mashaka na wasiwasi Mwingi mno, ni nani atanisaidia?

Ni MUNGU wa Mbinguni tu anayeweza kunisaidia, na ni kweli Bwana YESU KRISTO akanisaidia.


Ndugu, Nini nataka niseme?

◼️Omba katika Jina la YESU KRISTO hata kwa maneno machache tu uliyonayo wakati huo.


◼️◼️Kumbuka kwenye Biblia hakuna Mtu hata mmoja alimfuata YESU KRISTO kwa ajili ya uponyaji asipone, na Wewe utapona.


Kumbuka kwa mfano nikichoomba Mimi Kiko kwenye Biblia, ingawa wakati naomba hata sikujua imeandikwa wapi.


◼️✓✓Kwa habari ya MUNGU wa Mbinguni kusamehe 


imeandikwa katika Ezekieli 16:63 kwamba " upate kukumbuka, na kufadhaika, usifumbue kinywa chako tena, kwa sababu ya aibu yako; hapo nitakapokusamehe yote uliyoyatenda, asema Bwana MUNGU." 


Pia imeandikwa katika 

 Hesabu 14:20 kwamba  "BWANA akasema, Mimi nimewasamehe kama neno lako lilivyokuwa;"


✓✓Ndugu mabaya mengi yanayotupata ni kwa sababu ya makosa yetu hivyo usisahau kutubu kama unahitaji msaada wa MUNGU katika KRISTO YESU.


◼️✓✓MUNGU anaweza kusaidia katika jambo lako lolote.


Imeandikwa katika Isaya 41:13 kwamba "Kwa maana mimi, BWANA, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia."


Imeandikwa pia katika 

 2 Mambo ya Nyakati 26:7 kwamba " MUNGU akamsaidia juu ya Wafilisti, na juu ya Waarabu waliokaa Gur-baali, na juu ya Wameuni."


✓✓Hata Wewe Bwana YESU KRISTO anaweza kukusaidia dhidi ya maadui wengi hata kama Wana Nguvu kiasi gani.


Kama Mtu alisaidiwa dhidi ya waarabu  na wafilisti wengi waliokuwa tayari kummaliza, hata Wewe kwa Jina la YESU KRISTO utasaidiwa.


◼️✓✓MUNGU anaweza kukuokoa


 imeandikwa katika Ayubu 5:19 kwamba "Yeye(MUNGU) atakuokoa na mateso sita; Naam, hata katika saba hapana uovu utakaokugusa.


Imeandikwa pia katika 

 Kutoka 14:30 kwamba  kwamba "Ndivyo BWANA alivyowaokoa Israeli siku ile mikononi mwa Wamisri; Waisraeli wakawaona Wamisri ufuoni kwa bahari, wamekufa."


✓✓Utawaona adui zako wameshindwa na wale adui wakutoka kuzimu ving'ang'anizi utawaona wamekufa, amua Kuokoka na kuomba katika Jina la YESU KRISTO.

Hata kama upo katika wakati mgumu sana omba hata kwa maneno machache.


◼️✓✓MUNGU wa Mbinguni anaweza kukuponya


 imeandikwa katika  

Yeremia 30:17 kwamba " Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako, asema BWANA, kwa sababu wamekuita, mwenye kutupwa, wakisema, Ni Sayuni, ambao hapana mtu autakaye."


Imeandikwa pia katika 

Mathayo 4:23 "Naye(YESU)  alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu."


✓✓Bwana YESU aliponya magonjwa yote na kila udhaifu kwa Mwanadamu yeyote, anaweza kukuponya hata Wewe katika jambo lolote.


MUNGU anaweza yote ndugu, omba hata kwa maneno machache kama huwezi kuomba mengi.

Ila kama unaweza kuomba mengi omba sana na utamuona MUNGU wa Miujiza.

Hakikisha pia umeokolewa na Bwana YESU KRISTO na unaishi Maisha matakatifu ya Wokovu wake wa thamani sana.

By Mwl Peter Mabula 

Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele.

+255714252292

Ubarikiwe

Comments