![]() |
| Na Mwl Peter Marco Mabula Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni |
Leo ni maombi ya toba.
Kipengele tunachoshughulika nacho ni FAIDA ZINAZOTOKANA NA TOBA YA KWELI.
✓Kutubu ni nini?
◼️Kutubu ni kuomba msamaha kwa MUNGU kwa sababu ya makosa uliyofanya kisha kuacha kuyafanya hayo makosa.
◼️Kutubu ni kujutia uovu wako kisha unaomba msamaha na kujitenga na uovu huo.
✓Toba ni nini?
◼️Toba ni kujutia matendo uliyotenda kinyume na MUNGU na kisha unaomba msamaha na unayaacha mabaya hayo kwa kuanza kutenda mema ayatakayo MUNGU.
Zaburi 51:1 "Ee MUNGU, unirehemu, Sawasawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu. Unioshe kabisa na uovu wangu, Unitakase dhambi zangu."
Zingatia unapotubu usiseme tu "natubu" bali itaje dhambi husika umwambie MUNGU akusamehe.
✓✓Kutubu huambatana na kuungama.
◼️Kuungama ni kukubali kwamba umekosea hivyo unahitaji kusamehewa.
Kama utatubu bila kukubali kama umekosea hutasamehewa.
Na katika maombi ya toba kumbuka inayoondoa dhambi ni damu ya YESU KRISTO.
Waefeso 1:7 "Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake."
Faida saba(7) zinazotokana na toba ya kweli.
1. Toba huleta kupona magonjwa.
Zaburi 103:3-4 " Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote, Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema,"
2. Kutubu hukufanya uiepuke adhabu ya MUNGU iliyopangwa ije kwa sababu ya dhambi.
Yona 3:6-10 " Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie MUNGU kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba MUNGU hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe? MUNGU akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi MUNGU akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende."
Unaweza kutubu wewe hata kwa ajili ya watoto wako, mke/mume wako, ofisi yako n.k na adhabu iliyopangwa ikafutwa.
Mfano ni huu kwa Waisraeli baada ya Amosi kutubu kwa ajili yao adhabu ilifutwa.
Amosi 7:1-3 " Haya ndiyo aliyonionyesha Bwana MUNGU; tazama, aliumba nzige mwanzo wa kuchipuka kwake mimea wakati wa vuli; na tazama, ilikuwa mimea ya wakati wa vuli baada ya mavuno ya mfalme. Ikawa, nzige walipokwisha kula majani ya nchi, ndipo nikasema, Ee Bwana MUNGU, samehe, nakusihi; Yakobo atasimamaje? Kwa maana ni mdogo. BWANA akaghairi katika jambo hili. Jambo hili halitakuwa, asema BWANA."
3. Kutubu huleta furaha ya MUNGU ndani ya mtu.
Matendo 3:19 "Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;"
Mfano mtu alikuwa ana mapepo yaliyoleta ugonjwa, anatubu na nguvu za giza zinaondoka kisha anapona ugonjwa, kinachofuata hapo ni furaha na kuishi bila hofu, huko ndiko kuburudishwa yaani kuwa na furaha.
4. Kutubu kutaifanya ardhi yako kuponywa na kustawishwa.
2 Nyakati 7:14 " ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao."
Neno "nchi" lina maana ya sehemu ya ardhi isiyofunikwa na maji.
Kwa hiyo Biblia inaposema nchi maana yake ardhi na ndio maana Biblia ya kiingeleza Katika 2 Nyakati 7:14 inatumia neno "Land" katika maana ya Ardhi. Sasa toba ya kweli inaweza kuifanya ardhi yako kuponywa na kustawishwa hata na wewe ufanikiwe.
5. Kutubu kutakufanya usamehewe na kuachiliwa.
Mithali 28:13 "Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema."
◼️Rehema maana yake kusamehe na kuachilia, hivyo MUNGU akikurehemu maana yake amekusamehe na kukuachilia, yaani kukufutia hatia.
Ili usamehewe na kuachiliwa inakupasa utubu dhambi na kuziacha.
6. Kutubu kutakufanya uhesabiwe haki.
Luka 18:13-14 " Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee MUNGU, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa."
7. Kutubu humpa mtu kuishi.
Zaburi 119:77 " Rehema zako zinijie nipate kuishi, Maana sheria yako ni furaha yangu."
Rehema zako maana yake msamaha wako, sasa msamaha wa MUNGU unaotokana na toba yako unaweza kukufanya uishi.
Ninawi ilikuwa wafe ila walipotubu waliishi, tumejifunza hapo juu kuhusu watu wa Niwawi.
Kutubu hufuta uharibifu hivyo hivyo kutubu huleta uhai, huleta kuishi.
Ayubu 33:24 "Ndipo amwoneapo rehema, na kusema, Mwokoe asishuke shimoni; Mimi nimeuona ukombozi."
Je unataka Bwana YESU KRISTO akurehemu ili usishuke kuzimu?
Basi tubu leo toba ya kweli.
MUNGU akubariki sana.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 (Whatsapp, ushauri na Sadaka ya kuipeleka Injili mbele)
Ubarikiwe

Comments